Wananchi wawili Innocent Paul Chuwa, anayefahamika pia kwa jina la Kiduku, na mwenzake Frida Mikoroti, wameachiwa kwa dhamana leo Jumatano Oktoba 1, 2025 baada ya kushikiliwa kwa takribani juma moja katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam. Chuwa alikamatwa Septemba 24, 2025 maeneo ya Kariakoo jijini humo, huku Frida akikamatwa Septemba 26, 2025 katika eneo la Marambamawili.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Tanzania Human Rights Defenders Coalition (THRDC) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), wananchi hao walikamatwa kutokana na shughuli zao za mtandaoni. Katika tamko lao la Septemba 29, 2025, taasisi hizo mbili ziliweka wazi kuwa walikuwa wakifuatilia kwa karibu mwenendo wa kesi na kuhakikisha kwamba haki na taratibu za kisheria zinazingatiwa.
Timu ya mawakili kutoka THRDC na LHRC ilitembelea Kituo Kikuu cha Polisi cha Kati Dar es Salaam kwa lengo la kupata taarifa sahihi kuhusu hali ya watuhumiwa. Polisi waliwaarifu kuwa upelelezi ulikuwa katika hatua za mwisho na kwamba wawili hao wangepatiwa dhamana ya polisi ifikapo Septemba 30, 2025.
Hatimaye, dhamana hiyo imetolewa leo, na ingawa wako huru kwa muda, masharti ya dhamana yanawataka Chuwa na Frida kuripoti kila siku asubuhi saa tatu kituoni hapo hadi pale watakapopelekwa mahakamani au kuarifiwa vinginevyo.
Mawakili watatu waliokuwa wakifuatilia dhamana za wawili hawa ni pamoja na Kulwa William Maduhu kutoka LHRC, Paul Kisabo kutoka THRDC na Fredrick Msaki kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).
“Tuhuma zao zilikuwa ni tuhuma za makosa ya mtandao kwa maana ya kuchapisha maandiko mbalimbali yanayoonyesha kuchochea, uchochezi kwenye mitandao ya kijamii,” alieleza Maduhu.
“Wengine walikuwa wanasambaza tu siyo maandiko yao, na nusu ya hayo maandiko tulionyeshwa ambayo walikuwa wanasambaza. Kwa hiyo tuhuma zao ni hizo tu za kimtandao,” aliongeza zaidi.
Kwa sasa, Chuwa na Frida wako nje kwa dhamana, wakisubiri matokeo ya uchunguzi na hatma ya iwapo watapelekwa mahakamani au la.