The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Kahawa ni Zao Lenye Thamani Kubwa Duniani. Lakini Mbona Wakulima wa Tanzania Hawanufaiki?

Faida kubwa ikiendelea kubaki kwenye mikono ya wafanyabiashara wakubwa, wakulima wataendelea kung’oa miti ya kahawa ili wapande migomba, na Serikali haiwezi kuwazuia.

subscribe to our newsletter!

Kwa siku tatu mfululizo, kuanzia Oktoba 3 hadi 5, hapa Moshi, mkoani Kilimanjaro, kulifanyika tamasha kubwa la kahawa, au Kahawa Festival, kama lilivyoitwa kwa kimombo. Sikuweza kuhudhuria kwa siku zote, lakini hata ule muda mfupi niliopata ulikuwa na maana kubwa kwangu.

Binafsi ninapenda kahawa. Napenda harufu yake, ladha yake, na hata simulizi iliyo ndani yake. Lakini zaidi ya yote, nina mapenzi makubwa na biashara yake. Hadi sasa sijaanza rasmi kuifanya, lakini ndoto hiyo ipo ndani yangu. Na siku hii ilikuwa sehemu nyingine ya kujifunza zaidi kuhusu zao hili linalotupa hadhi duniani.

Mkoa wa Kilimanjaro unazalisha kahawa aina ya Arabica, kahawa inayopendwa zaidi duniani. Ni laini, tamu na yenye harufu ya kipekee. Kila unapoinywa, unapata msisimko na kuhisi fahari ya jasho la wakulima wetu.

Nilipokuwa nimeketi nikinywa kikombe changu cha kahawa pale kwenye tamasha, nilijikuta nikitafakari sana kuhusu mustakabali wa zao hili. Siyo tu hapa Tanzania, bali duniani kote. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Shirikisho la Kahawa Duniani, ifikapo mwaka 2050 uzalishaji wa zao hilo unaweza kushuka kwa kiwango kikubwa kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Tanzania tumejipangaje?

SOMA ZAIDI: Tanzania Inaenda Kumuuzia Nani Kahawa Ndani ya AfCFTA?

Ukweli ni kwamba uzalishaji wa kahawa umeshaanza kushuka kwa kiwango kikubwa nchini kwetu, huku sababu ikiwa tofauti na mabadiliko ya tabianchi. Ndiyo, kwenye maeneo mengi ya mkoa wa Kilimanjaro wakulima wamebadilisha mazao. Wameng’oa mikahawa na kuotesha migomba kwa sababu wanaiona faida yake kwa haraka zaidi.

Nilimkumbuka Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, alipotoa maagizo kwa wakulima kutokukata mikahawa yao. Nikajiuliza, kama alitafuta sababu ya wao kutolitaka tena zao hili au aliongea kisiasa.

Wakulima hawaoni faida ya kahawa. Fedha wanazozipata kwenye zao hilo hazitoshi kuwadumu kwenye mahitaji yao ya Kila siku. Sasa, kama kahawa ni zao lenye thamani kubwa duniani, kwa nini basi wakulima wetu hawapati faida hiyo? 

Jibu ni kwamba faida kubwa inabaki kwa wafanyabiashara wakubwa. Sasa, kwa nini faida kubwa inaishia mikononi mwa wafanyabiashara na wauzaji wakubwa, huku wale wanaolima kwa jasho na kujinyima wakibaki na kidogo? Kwa nini wale waliowahi kuiamini kahawa kama mkombozi wao kiuchumi, leo wameikatia tamaa?

Hapa kuna tatizo kubwa ambalo haliwezi kutatuliwa kwa amri ya mkuu wa mkoa. Serikali itambue kwamba wakulima nao wanahitaji faida kama watu wengine. Huwezi kuwalazimisha kufanya Jambo Kwa maslahi ya watu wengine.

SOMA ZAIDI: Wakulima Mbozi Wagoma Kuuza Kahawa Yao Wakidai Bei Hairidhishi 

Ni lazima Serikali ikae chini na kutafakari upya. Iangalie sera zake za kilimo na biashara ya kahawa kwa jicho jipya. Vyama vya ushirika viboreshwe, maana hapa ndipo wakulima wanaruhusiwa kuuza kahawa yao. Uwazi uongezwe, na mfumo mzima wa biashara uangaliwe upya. 

Maana kama sera na mifumo tuliyonayo sasa inaendelea kuwanufaisha wafanyabiashara zaidi kuliko wakulima, basi tutaendelea kupoteza ari na nguvu ya wakulima wetu. Hali ikiendelea kuwa hivi, miaka michache ijayo kahawa inaweza kuwa historia katika maeneo mengi ya Kilimanjaro.

Binafsi bado ninaamini kuwa kahawa ina nguvu ya kubadilisha na kuinua maisha ya wakulima na vijana wa kanda ya kaskazini kama tutatengeneza mfumo wa haki, unaompa nafasi kila mtu ndani ya mnyororo wake wa thamani, hasa mkulima.

Ni wakati sasa wa wadau wote wa kahawa, yaani Serikali, vyama vya ushirika, wafanyabiashara, wakulima, na vijana, kukaa pamoja na kuzungumza kwa uwazi mustakabali wa kahawa. Tukiweka maslahi ya pamoja mbele, tutarudisha hadhi ya zao hili na nguvu yake kwa taifa letu.

Tukumbuke, kahawa siyo tu kinywaji, bali pia ni maisha, utamaduni na ni fahari yetu. 

Tusimame Kwa pamoja, tuilinde kahawa yetu!


Brayan Silayo ni mdau wa elimu kutoka Kilimanjaro, Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia brayansilayo14@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×