The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Hizi Hapa Tabia Tunazojua Zinawaumiza Watoto Wetu Lakini Tunaendelea Kuzifanya

Ukweli ni kwamba kujihisi vibaya haitusaidii. Kinachotubadilisha ni kujielewa na kutafuta njia bora zaidi za kushughulikia hisia zetu kabla hazijatuongoza vibaya.

subscribe to our newsletter!

Kuna nyakati tunajikuta tumepaza sauti, tumeongea kwa ukali, au tumenyamaza kimya kwa hasira tukiwa na watoto wetu. Huenda wanakua wamekosea, au hawakufanya tulichowaelekeza kama tulivyowaelekeza na mara nyingine wanakua hawajakosea kabisa.

Baada ya hapo huwa tunahisi vibaya, tunajilaumu, na kujiambia “Sikutaka kufanya hivyo. Ila ni hasira tu.”

Lakini siku zinavyozidi kwenda, tunajikuta tumerudia tena. Tunaumia ndani kwa ndani kwa sababu tunajua tabia hizi zinawaumiza watoto wetu.

Kwa nini tunaedelea kufanya hivyo? Sio kwa sababu sisi ni wazazi wabaya, bali kwa sababu mara nyingi tunakua tumechoka, tumezidiwa na kazi, au changamoto za maisha, na akili zetu hazina utulivu.

Wanasayansi wa ubongo wanasema pale tunapokuwa na msongo wa mawazo, sehemu ya ubongo iitwayo amygdala huchukua usukani. Sehemu hii hutuma ishara za hatari ili mwili utoe homoni za cortisol na adrenaline, zinazotufanya kuwa tayari “kupambana au kukimbia.”

SOMA ZAIDI: Fahamu Watoto Wanavyoomba Msaada Katika Kila Hatua ya Ukuaji Wao 

Katika hali hiyo, hatuwezi kufikiri kwa utulivu, na mara nyingi tunajikuta tumeitikia kihisia kabla hata ya kufikiri.

Kwa hiyo, tunapowagombeza watoto kwa ukali mara nyingi si kwa sababu tunataka, bali kwa sababu tumepoteza uwezo wa kutuliza hisia zetu kwa muda. Tatizo ni kwamba, kadri hali hii inavyojirudia, ndivyo inavyoumiza zaidi uhusiano wetu na watoto wetu.

Madhara kwa watoto

Tafiti mbalimbali, ikiwemo kutoka Chuo Kikuu cha Harvard na Pittsburgh, zinaonesha kuwa kufoka, au kuonesha hasira kali, huamsha katika ubongo wa mtoto athari sawa na adhabu ya kimwili.

Mapigo yake ya moyo huenda haraka, mwili wake hujaa homoni za hofu, na ubongo wake unaanza kufikiria kuwa hayuko salama.

Kwa maneno mengine, mwili wa mtoto hauwezi kutofautisha kati ya kupigwa na kufokewa au kugombezwa.

SOMA ZAIDI: Siku ya Mtoto wa Kike Duniani: Kijiji Kinachomlea Binti ni Kipi Hapa Tanzania? 

Na anapopitia hali hii mara kwa mara, anaanza kuamini ndani yake kwamba hana thamani na hayuko salama. Baadaye, imani hizi hubadilika na kuwa sauti yake ya ndani anayojisemea kila siku, sauti itakayomuongoza kadri anapokua.

Kila mmoja wetu anajua hisia zinazokuja na ule ukimya unaotokea baada ya kumfokea mtoto kwa hasira, haswa pale ambapo hajafanya kosa lolote.  

Ukweli ni kwamba kujihisi vibaya haitusaidii. Kinachotubadilisha ni kujielewa na kutafuta njia bora zaidi za kushughulikia hisia zetu kabla hazijatuongoza vibaya.

Hatua za kuchukua

Kitu cha kwanza, tukihisi hasira inatanda, tujipe sekunde chache kupumua, au kujitenga kidogo mbali na watoto. Huo muda mfupi husaidia ubongo wetu wa kufikiri, kurudi kazini kabla ya hisia zetu kututawala.

Cha pili, tujifunze kujirekebisha mara baada ya hisia zetu kututoka. Tujifunze kusema “Samahani, niliongea na wewe vibaya. Nilikuwa nimechoka, lakini si kosa lako.” Maneno kama haya yanafundisha watoto kwamba makosa hayavunji upendo bali yanaweza kuwa nafasi ya kujifunza.

SOMA ZAIDI: Vitu Tisa vya Kushangaza Kuhusu Watoto Ambavyo Hukuvijua

Kingine, tuonyeshe uvumilivu na utulivu. Watoto hujifunza kutuliza hisia zao kwa kututazama sisi. Tunapojituliza badala ya kulipuka, tunawafundisha jinsi ya kushughulikia hisia zao ikiwemo hasira, woga, na huzuni.

Pia, tuzungumze nao badala ya kuhukumu. Baadala ya kusema “Kwa nini umefanya hivi?” Tuseme, “Nieleze mwanangu, nini kilitokea?” Maswali ya huruma hufungua mioyo; maneno ya ukali hufunga mlango wa mazungumzo.

Mwisho kabisa, tutafute msaada kwa watu tunaowaamini, au hata kwa wataalamu wa kisaikolojia pale mambo yakitulemea.

Tukumbuke, watoto wetu hawahitaji wazazi kamili. Wanahitaji wazazi wanaoweza kusema:“Leo nilishindwa kuwa mtulivu, lakini kesho nitajaribu tena.”

Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×