Dar es Salaam – Mpaka sasa kunguru na nzi wamezuka eneo ambapo majirani nane wa mtaa wa Kanga-Kariakoo, Kinyerezi, jijini hapa, walipouwawa. Kabla ya mvua kunyesha Novemba 4, 2025, harufu ya kifo ilikua ndiyo alama ya eneo hilo. Mvua iliweza kusafisha baadhi ya mabaki ya viungo vya binadamu yaliyokuwa yamebaki, ikiwemo damu nzito.
Tukio hili lilitokea usiku wa kuamkia Novemba 3, 2025, majira ya saa tisa. Majirani hao waliuwawa zamu kwa zamu kwa kupigwa risasi. Hii ni baada ya kuambiwa wajilaze nyuso zao zikiangalia ardhi, na kuamrishwa kusali sala ya mwisho.
Majirani hao ambao nyumba zao zimefuatana katika mstari mmoja, walikuwa ni afisa polisi mstaafu, walimu wawili, dereva, wauza duka wawili, afisa wa benki na mfanyabiashara ndogondogo.
“Hapa kulikua hakufai kabla ya hii mvua kunyesha, wao walikuja wakamwagia mchanga, lakini kulikua hakufai, mvua imesafisha safisha, kidogo,” moja ya majirani alitueleza hali baada ya mauaji hayo.
Tukio hili lilianza baada ya duka la jumla lililopo katika mtaa huo kusikika kuwa limevamiwa na vibaka. Polisi mstaafu aliwaongoza majirani wenzake kwenda kuimarisha ulinzi katika eneo hilo, ambapo pia aliamua kupiga simu na kuita polisi.
Polisi wenye silaha walivyofika kwenye eneo hilo waliwaamrisha wote kulala chini. Licha ya kujitetea, hoja zao hazikuweza kufua dafu. Waligawanywa makundi mawili, wakitenganishwa na barabara ambayo imegawanya makazi yao, upande wa kulia na kushoto, wengine wakawekwa karibu na duka hilo la jumla, na wengine wakawekwa upande wa pili, pembeni ya nguzo ya umeme.

Afisa wa benki, ambaye duka la jumla limetazamana na nyumba yake, alikuwa wa mwisho kufika katika eneo hilo. Hii ni baada ya kuona polisi wamefika, akajitokeza kuungana na majirani zake. “Kuna usalama?” aliuliza afisa huyo, ambapo alihakikishiwa na polisi hao kwamba “usalama upo.”
Hata hivyo, tukio hilo liliwabadilikia na kuwa ndiyo safari yao ya mwisho. Mmoja wa marehemu aliyepewa pia jina la utani mtaani kama Ostaadh, ambaye kazi yake ni udereva, akawasihi watu hao kuwa tayari mke wake ameshafariki, na ana mtoto mdogo wa miezi sita, hivyo wasimuue, kilio ambacho hakikusikika.
Katikati ya kilio hicho, na baada ya wengine kuanza kuuwawa, wawili waliweza kukimbia kutoka katika eneo hilo, ambao ndio walioweza kuhadithia kilichojiri usiku huo, mpaka sasa wamebaki katika hali ya hamaki na hofu kubwa.
“Ukiongea naye, akinyamaza, usimsemeshe, muache atulie,” moja ya majirani anayeomboleza aliiambia The Chanzo wakati tukijiandaa kumhoji mmoja wa manusura.
“Hata sisi tunaogopa. Tunaogopa hata kuzungumzia. Hatuelewi kwa nini wametufanyia hivi. Tunaogopa,” jirani mwingine alieleza, huku hali ya unyonge na hofu zikionekana katika macho yao na matamshi yao, wengi wakiongea katika hali isiyo na uchangamfu, wakiongea kwa sauti ya chini kana kwamba kuna anayewasikiliza.
Toka siku ya tukio hilo, eneo hilo limekuwa likizungukwa na kunguru, waliofika na kuweka alama kwa sababu ya mabaki ya miili ya watu yaliyoachwa kwa makovu ya risasi, hasa ubongo uliomwagika.
Mpaka sasa hivi, miili minne bado haifahamiki ilipo, huku miili minne mingine ikiwa imepatikana baada ya ndugu na jamaa kuzunguka katika sehemu mbalimbali za Dar es Salaam.

Alhamisi ya Novemba 6, 2025, ibada ya mazishi ya mmoja ya aliyeuwawa, ambaye ni Askari Mstaafu, Joseph Igumba Mwakabana ilifanyika katika Kanisa Katoliki Kinyerezi. Familia, ndugu na jamaa wakihudhuria kabla ya mwili wa mzee huyo aliyezaliwa Julai 7, 1961, kusafirishwa kuelekea Mbeya kwa ajili ya maziko. Katika hali ya huzuni, mtoto wake aliyekuwa akisoma wasifu wa baba yake, alishindwa kujizuia na kujikuta machozi yakimdondoka na kukatisha hotuba hiyo ya wasifu.
Majirani zake Mwakabana wanamweleza kama mzee wa kutegemewa aliyekuwa mashauri wa karibu kwa vijana wengi na mwenye hulka ya upendo hata kwa watu asiowafahamu.

Ijumaa ya Novemba 7, 2025, ibada nyingine ya kuuga mwili wa Aloyce Leonard Soka, aliyekuwa mfanyakazi wa moja ya Benki ya kibiashara Tanzania, ambaye pia ni Baba wa watoto wawili, ilifanyika tena katika Parokia ya Kanisa Katoliki Kinyerezi na mwili ukasafirishwa kuelekea Moshi, Kilimanjaro ambapo mazishi yalifanyika mnamo Novemba 08, 2025.

Majirani zake wanamwelezea Aloyce Soka kama mtu ambaye hakuwa na hulka ya kupuuzia matatizo ya watu, na pale alipokuwa na uwezo aliweza kuwasaidia. Nje ya nyumba yake, gari yake aina Volkswagen Beetle maarufu kama Kobe limepaki, likiwa limefunikwa kwa turubai, huku majirani wakikumbushia namna alivyokuwa akipenda magari ya kizamani, na namna alivyokuwa akilitengenza gari hilo taratibu, majirani wakieleza kama jambo ambalo walikua wakitumia kumtania Aloyce.

Wengine katika msiba huu ni pamoja na Shabani,Ignas,Mustapher,Abuu, Shabani (Ostadh) na Mcheda. Kwa watu wanne ambao miili yao bado haijapatikana, misiba isiyokuwa na tarehe ya kuisha imewekwa katika makazi hayo. Ukifika katika mtaa huo utaona kina mama, na baadhi ya watu wakiwa wamekaa, wakisubiri taarifa zozote juu ya watu wanaozunguka kutafuta miili hiyo iliyobebwa na watu waliofanya mauaji hayo.
Kwa upande mwingine, vikao vya misiba vinaendelea kufanyika, familia zikikutana, kila mmoja akijaribu kutumia nguvu kubwa kujisahaulisha namna ndugu zao walivyo ondoka duniani, na hata katika ibada zikielezwa kuwa ni moja wa wanusurika wa matukio baada ya uchaguzi.
Wengi katika vikao wanaonekana kujaribu kuficha hofu, kuchanganyikiwa na huzuni yao, jambo ambalo hufichuka kila kunapokua na ukimya.
Changamoto nyingine zilizowakuta familia hizi ni kwamba majirani wote wamefiwa, hivyo kila mtu inabidi kutafuta msaada kwa ndugu wa mbali na eneo hilo, hasa katika kutafuta ghrama mbalimbali, ikiwemo usafiri na gharama za vyakula. Kwa ambao ambao bado hawajapata miili, wanaendelea kuwaza kama wafanye maziko bila miili hiyo.
Tukio hili linakuwa sehemu ya matukio ya vifo vya Watanzania ambao mpaka sasa idadi rasmi haijajulikana, huku kwa wengi picha zao zikisambaa mtandaoni, zikionesha majeraha ya risasi waliyokutana nayo kufuatia maandamano katika siku ya uchaguzi mkuu, Oktoba 29, 2025, yaliyofuatishwa na zuio na tahadhari ya kiusalama iliyotolewa jioni ya siku hiyo na kuendelea mpaka Novemba 3, 2025.
3 responses
I wish I raise that 6 month’s newborn. Nampataje?
Amina Sana the chanzo
Duh