Katika siku za hivi karibuni, taifa letu limepita katika kipindi kigumu. Matukio yaliyotokea yameacha majeraha mioyoni mwa wengi, familia zimepoteza wapendwa wao, jamii zimetikisika, na watoto wetu wamehisi hofu ambayo hata sisi wazazi tumeihisi.
Maneno hayatoshi kuelezea maumivu, lakini jambo moja tunalojua ni kwamba, hofu hii imetuathiri wote: watoto, wazazi, na jamii nzima.
Watoto wetu hawahitaji kuelewa kila kitu ili kuhisi uzito wa yaliyotokea. Wanahisi kupitia sauti zetu, nyuso zetu, na hata kimya chetu. Na kama wazazi na walezi, jukumu letu sasa ni moja: kuwasaidia watoto wetu kurejesha hali ya usalama na utulivu.
Tunapobaki watulivu, watoto wetu huanza kutulia. Tunapowapa matumaini, mioyo yao huanza kupona. Na tunapowaonyesha upendo, wanajifunza kwamba hata baada ya maumivu, dunia bado ni mahali salama.
Tuone njia chache tunazoweza kutumia kuwasaidia watoto wetu kukabiliana na hali ya hofu katika kipindi hiki. Kwanza, watoto wanahitaji kusikia ukweli kwa lugha rahisi na yenye faraja.
SOMA ZAIDI: Hizi Hapa Tabia Tunazojua Zinawaumiza Watoto Wetu Lakini Tunaendelea Kuzifanya
Tusiwafiche ukweli, lakini tuzungumze nao kwa upole. Tunaweza kusema, “Ni kweli, jambo la kusikitisha limetokea, lakini kuna watu wengi wanaofanya kazi kuhakikisha wote tunakuwa salama.”
Watoto hupata utulivu wanapohisi mambo hayajabadilika sana. Tuendelee na ratiba za kawaida: kula pamoja, kucheza, kusali au kusoma hadithi kabla ya kulala. Mambo haya madogo huwapa ujumbe kwamba bado wapo kwenye mazingira salama na yenye upendo.
Tuwaulize watoto wetu wanavyohisi. Wanaweza kunyamaza, wengine watakuwa wakali, au wakibadilika kitabia, yote hayo ni njia zao za kueleza na kuonesha hofu yao. Tusiwahukumu. Tuwape nafasi ya kusema wanachohisi, na tuwasikilize kwa uvumilivu na tuwasaidie kuelewa hisia zao.
Watoto hujifunza jinsi ya kukabiliana na changamoto kwa kututazama sisi. Tunapovuta pumzi, kuzungumza kwa upole na kuonyesha huruma, tunawafundisha kwamba hata katika hofu, amani bado inawezekana.
Tunaweza kupata nguvu na msaada kupitia familia, walimu, taasisi za dini, au vikundi vya kijamii. Tuwaonyeshe watoto kwamba hatuko peke yetu, na kwamba kuna watu wengi wanaotujali.
SOMA ZAIDI: Fahamu Watoto Wanavyoomba Msaada Katika Kila Hatua ya Ukuaji Wao
Katika kila jicho la mtoto lenye hofu, kuna matumaini yanayosubiri kutulizwa. Na sisi, kama wazazi na walezi, tuna nafasi ya kuwa sauti ya utulivu na faraja hiyo. Tuwafundishe watoto wetu kwamba hata baada ya giza, nuru hurudi.
Kwa pamoja, tutaendelea kulinda mioyo yao na kujenga taifa lenye upendo na amani.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.