Nianze kwa kutoa pole kwa familia zote zilizopoteza wapendwa wao. Kuna waliowapata wapendwa wao na kuwapa heshima za mwisho. Kuna ambao bado wanalia, wakiwa hawajui wapendwa wao wako wapi. Kuna picha za kina mama wanaolia wakiwa wameshikilia bendera ya taifa kama ishara ya miili ya watoto wao.
Nimetizama leo mtandaoni, kuna mama kamuona mwanae kati ya mahabusu walioletwa mahakamani. Anaandika, mwanangu nimekutafuta mochwari zote, nimetembea kila mahali, leo nakuona unashushwa kwenye gari, sijui uko gereza gani, lakini nakupenda.
Huhitaji kuwa mama, mwanamke, au mzazi kusikia maumivu aliyo nayo huyo mama. Huhitaji kuwa chochote. Unachohitaji ni kuwa mtu. Binadamu mwenye utu.
Kuna chapisho linalosambaa mtandaoni likimuonyesha kaka akiwalilia ndugu zake mapacha waliouwawa. Mama kabaki na mtoto mmoja. Ameshindwa kulia. Anamkataza mwanae asitoke asije akakosa wa kumzika.
Hiyo ni sauti ambayo huhitaji kuwa chochote kuisikia hadi tumboni kwako, unahitaji tu kuwa mtu. Binadamu mwenye utu. Na hao ni wachache, hadithi ni nyingi, vilio ni vingi sana, sana.
Kila nikiongea na marafiki, ndugu, jamaa, na hata watu baki tu, kitu kimoja kila mmoja anakipitia, imekua ngumu kupata usingizi, nafsi hazitulii. Mie binafsi, kama marafiki wengine nilioongea nao, napitia kipindi cha hasira, huzuni, baridi ambayo siielewi nafsini, nikiwa sina hisia zozote bali kutoa macho bila mwelekeo. Tunajua wapi tulipoangukia. Unajiuliza, kulikua na ugumu gani kuparekebisha?
Watanzania na hasa vijana, hawakuomba vitu vigumu ambavyo ilibidi watu wasafiri kwenda sayari nyingine kuvipata. Vyote walivyoviomba vimo ndani ya uwezo wa watawala.
SOMA ZAIDI: Tanzania Baada ya Oktoba 29, 2025: Tunarejeshaje Kisiwa cha Amani?
Watawala, kwa bahati mbaya, wakachagua tunda lisilo bora, kutosikiliza, wakaweka pamba masikioni. Watanzania wamezoea viongozi kuweka pamba masikioni, na huwa hawana taabu wakishaona hivyo “wanajisoti” kivyaovyao, maisha yanaendelea.
Pamba masikioni, kejeli
Kipindi hiki ilikua tofauti, sio tu pamba ziliwekwa masikioni, kejeli kutoka kwa watawala zilikuwa nyingi, wengi hawakutaka kushusha sauti ili watafakari nini kinafaa kufanyika kwa maslahi mapana ya nchi yetu. Kila walipokumbushwa kushusha sauti waliongeza ukubwa wa sauti, “volume” ili na wa nyuma wasikie.
Kitu ambacho hawakujua ni kwamba, vijana wa sasa sio wa enzi ya zamani, wana taarifa na wanajua wajibu na haki zao. Vijana hawa wanapodai haki hawaanzii patupu, wameshawasoma wenzao ndani na nje ya Afrika. Kitu ambacho watawala wetu walijisahaulisha ni kusoma upepo.
Walidhani upepo utaelekea kule walipoupangia kama ilivyokuwa siku zote. Zamu hii upepo ulichagua mwelekeo tofauti, na kuna ishara nyingi zinazobainisha kuwa dalili zilikuwepo. Kilichotokea si kitendawili. Tusiendelee kutafuta mchawi. Mchawi yuko miongoni mwetu, ni sisi.
Kawaida huwa nikiwa na wasiwasi, au nataka nisali kwa utulivu, kuna nyimbo nitazisikiliza, mfano ule wa Yupo Mungu Mbinguni, Asikiaye Maombi Yetu na nyingine kadhaa. Tangu Oktoba 29, nyimbo hizo zinasikika tofauti masikioni kwangu. Hazinifanyi nafsi itulie, iwe nyenyekevu iongee, zinanifanya nijisikie niko msibani na kuanza kulia upya, zinanifanya nijiulize na kumuuliza Mungu kama upo mbinguni kwa nini hili hukulizuia?
Yeye anayeona hata yasiyoonwa, kwa nini hili ameliona na hakufanya mioyo ya walio na uwezo wa kuliepusha inyenyekee? Baadae najikumbusha Mungu alipotuumba alitupa utashi, alitujalia akili, weledi, busara, na hekima ili tuweze kujiongoza, na sio sawa kutotumia vyote alivyotujalia, tukamsubiri tena aje duniani kufanya kazi ambayo iko ndani ya uwezo wetu.
Siyo ya kushitukiza
Oktoba 29 haikua ya kushitukiza. Ilijulikana itakuja, hali ya itakujaje, na inaweza isije ilivyozoeleka, ilikuwepo, dalili zilikuwepo. Hiyo siku kikawaida ilitakiwa iwe siku Watanzania wanaamua nani awaongoze – ingawa, kwa hakika, sijui kama walishawahi kuamua nani awaongoze – kwa kipindi kingine cha miaka 5.
SOMA ZAIDI: Wananchi Dar Waeleza Matamanio Yao Binafsi Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025
Kabla ya siku yenyewe tayari kulishajaa matobo, na matobo hayo tulikuwa na uwezo wa kuyaziba, kuyashona, au kununua nguo mpya kabisa na yale tuyaweke kama sehemu ya historia yetu ya kujifunza. Hatukufanya hivyo. Tuliamua matobo yale tuongeze. Tuliamua kimakosa, kwa kiburi na tambo.
Oktoba 29 ikageuka siku ya simanzi, vilio, hofu, hasira, na wakati mwingine mioyo iliyoganda. Kwa wengine, hali hii imeanza hiyo siku. Wengine, kwa kuwa hawafuatilii yanayoendelea nchini, na wengine kwa kuwachukulia Watanzania poa na kusema Watanzania tunawajua.
Kabla ya Oktoba 29, miezi kadhaa vijana wamekuwa wakidai HAKI, wakieleza kutofurahishwa na mwenendo wa utekwaji, upoteaji wa watu, lugha za vitisho, rushwa, hali ngumu za maisha na mambo mengine mengi ambayo hayakuwapa furaha.
Wakati wananchi, na hasa vijana, wakiongea, bahati mbaya sana, hawakusikilizwa. Mie binafsi nilipokua napitia mitandaoni niliogopa, nilitizama nyuso za vijana, nikaona hawatanii, walijua nini wanataka, waliamua, na walikuwa tayari. Tumekosea na kuwasaliti watoto na vijana wetu.
Na baada ya kuwasaliti tukaona haitoshi, tukaruhusu uhai wao uchukuliwe, damu yao iliyomwagika ardhini itatusuta milele mpaka pale tutakaposema samahani tuliwakosea vijana, tuliwakosea Watanzania, tukae chini, tuwajibike, turudishe nchi nyumbani, tuijenge kwa pamoja, ikibidi tushone nguo mpya ya zamani tuitupe.
Najua kuna makundi mengi yenye wajibu, na hayo nitayarudia siku nyingine, ila kwa sasa watawala wajue wameshikilia makali na sio mpini, wakikosea tu nchi ndio itakayoumia
Kuna rafiki yangu nilikua naongea naye siku mvua inanyesha, huku akilia kwa uchungu kwenye simu akasema, “Mary, fikiria tumeshindwa hata kwenda kuwatoa watoto wetu barabarani, Mary tunashindwa kwenda kuikumbatia miili ya watoto wetu tuwaombe radhi, tuishike miili yao tuipapase, tuioshe, tuizike kwa heshima, picha zao zitawale nchi nzima kama wakombozi. Tumeshindwa hata kwenda “mochwari” tuombe kuwapaka mafuta watoto wetu hata kama itakua ni miguu tu. Mary, tumeshindwa hata kwenda kusafisha damu za watoto wetu barabarani, Mungu ameona bora alete mvua damu ya watoto wake isikaukie barabarani, ikageuka sehemu ya lami au majani.”
SOMA ZAIDI: Wananchi Dar Waeleza Sifa za Mwakilishi Wanayemtaka Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025
Ni Watanzania wachache hawalii, wengi wanalia hata waliodhani hawatalia. Juzi nilipotazama video ya Njombe wakilia nilijiunga nao kulia japo siwafahamu. Niliangua kilio utadhani niko msibani pamoja nao hapo walipo. Watanzania siku zote tunaunganishwa na Umoja na Undugu wetu, bila kujali tofauti zetu za kikabila au dini.
Kwa sasa tunaunganishwa na majonzi ya mauaji ya halaiki na mioyo iliyopondeka. Wengi hatukumbuki tulicheka lini mara ya mwisho. Sasa hata kucheka unalazimisha, na hata wewe unajua hakitoki moyoni, amani ndani ya nafsi, au furaha ndani ya nafsi unalazimisha na bado imegoma na unajua haipo. Tumetawaliwa na mengi nafsini.
Watawala washushe sauti
Ili tutoke hapa lazima watawala washushe sauti. Muda upo, sababu ipo na kubwa zaidi sasa kuliko wakati mwingine wowote. Tanzania ni kubwa kuliko sisi wote kwa pamoja. Sitaki kujidanganya, au kujipa matumaini hewa, kwamba tutarudisha Tanzania ya zamani.
Hiyo Tanzania imekwenda, tumeruhusu damu ya Watanzania imwagike, tumeionyesha damu ardhi hii, tumewaliza wanawake wakafunga kanga matumboni wanagaragara, tumeliza kina baba, tumeliza watoto.
Kuna taarifa za watoto kushuhudia wazazi wao wakiuliwa kwa risasi mbele ya macho yao. Hawa watoto sijui tumejiandaaje kuwasaidia kisaikolojia.
Kwa watawala, ninyi ni watumishi wa watu. Kuomba radhi, kujishusha, na kukubali kuna makosa yalifanyika ni dalili ya ukomavu wa uongozi na sio udhaifu. Hii nchi inawadai. Wanawake wa nchi hii wanawadai. Wazazi wa nchi hii wanawadai. Watanzania kwa ujumla wanawadai.
Huu sio muda wa kupandisha mabega, bali kuyashusha yawe chini ikibidi usawa wa magoti. Uponyaji hauji kimiujiza, wala kwa kuzidisha jeuri. Unakuja kwa kutambua thamani ya utu, kujuta pale unapovuka mipaka ya utu, kuonesha utayari wa kuanza upya si kwa maneno tu, bali kwa vitendo.
Tumefikia hatua sasa raia unaomba ukutane na wanajeshi barabarani kuliko askari polisi? Ni juzi tu polisi walikua wanakusimamisha hata kama una kosa unapiga nao “stori,” na kuna wakati mnataniana unaendelea na maisha na wao wanaendelea na yao hata kama wamekuchukulia hatua.
Tumeporomoka mno kutoka kule tulipokuwa tukiinadi nchi yetu kuwa ni kisiwa cha amani, tujisahahishe!
Namalizia kwa maneno aliyoongea mama kutoka Njombe wakati wa mazishi ya wapendwa wao: “Tumeona hekima na busara tumechoka, tumejaribu ujinga na tumeona matunda ya ujinga na sasa tumevuna.”
Na pia padri mwingine ambaye maneno yake yalinukuliwa kwenye taarifa ya BBC News Hour: “Some people had already died, and others might have to die in order for this wrong to be righted.” Yaani, baadhi ya watu walishafariki, na wengine wanaweza kulazimika kufa kurekebisha kasoro hii.
Tusisubiri watu wengine wengi zaidi wafe ili kusahihisha makosa yaliyotufikisha hapa.
Mungu Ibariki Afrika,
Mungu Ibariki Tanzania,
Mungu wabariki vijana wote wa nchi hii.
Mary Fadei!
Mary Fadei ni mtaalamu na mwanaharakati wa masuala ya kijinsia. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia maryfadei05.mn@gmail.com au X @Mary_ndaro. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Je, ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.