The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

‘Askari Wangu Wamefanya Kitu Kibaya Sana’: Ya Nanjing 1937, Tiananmen Square 1989 na Oktoba 29, 2025 Tanzania

Nyerere na CCM waliitaka China kutoa ufafanuzi wa kilichotokea Juni 4, 1989, pale Tiananmen Square. Sijui kama Chama cha Kikomunisti cha China kitataka maelezo kutoka kwa chama-dada CCM juu ya Oktoba 29.

subscribe to our newsletter!

Siku kadhaa zimepita tangu nisome makala ya jarida la The Economist yakifananisha maandamano na matukio ya Oktoba 29, 2025, nchini Tanzania na yale ya Tiananmen Square kule Jamhuri ya Watu wa China. Nimeona pia makala ya Zitto Kabwe yenye kichwa cha habari “Our Tiananmen Moment: Tanzania’s Cry for Justice Amid October Massacres.” 

Kama mtafiti wa mahusiano ya Afrika na China, nilipatwa na shauku ya kujua ni kwa namna gani naweza kuandika makala juu ya Oktoba 29 lakini kwa kuitazama China. Utafiti wangu kwenye mahusiano ya Afrika na China umejikita kwenye masuala mtambuka, lakini moja kati ya hayo ni “Chinese soft power” – ama kwa Kiswahili tunaweza kusema nguvu laini.  

Nguvu laini, kwa muktadha huu, ni namna ambavyo nchi za Kiafrika huitazama China kama nchi ya kupigiwa mfano kiasi cha kujikuta zinatamani kuiga utamaduni na siasa yao. Ni nguvu ambayo huleta ushawishi, tofauti na nguvu ngumu ambayo huleta shuruti. 

Pamoja na makala hizo mbili kujaribu kufananisha kilichotokea Oktoba 29 na kile cha Tiananmen, nimeamua kuanzia na Nanjing. 

Nanjing, 1937

“Askari wangu wamefanya kitu kibaya sana. Ni majuto.”

Hayo ni maneno ya Jenerali Matsui Iwane, kamanda wa vikosi vya Japan vilivyovamia na kutwaa mji mkuu wa China wakati huo, Nanjing, Disemba 4, 1937. Nanjing (au Nanking) ilianguka Disemba 13, 1937, baada ya vikosi vya China kushindwa kuhimili umahiri wa vikosi vya Japan kwenye vita ya pili ya dunia. 

Siku 14 baadaye, Disemba 18, Jenerali Matsui alifika Nanjing huku akiwa na wasiwasi wa atakachokiona. Tayari alishapata taarifa za awali za ukatili wa wanajeshi wake kwa watu wa Nanjing, na kwa mateka wa kivita wa Kichina. Licha ya amri kwa vikosi vyake kabla ya uvamizi akiwataka wasifanye ushenzi, Matsui alitilia shaka nidhamu ya askari hao ambao wengi walikuwa ni wa vikosi vya akiba, au reservists kwa kimombo. Hakukosea. 

Baada ya kuingia Nanjing, Matsui alishikwa na butwaa baada ya kujionea ukatili wa vikosi vyake. Raia na askari mateka wa China waliteswa na kuuawa kwa namna ya kikatili ambayo baadhi ya wataalamu wa vita wanasema haikuwahi kutokea. 

SOMA ZAIDI: Tanzania Baada ya Oktoba 29, 2025: Tunarejeshaje Kisiwa cha Amani? 

Makamanda wawili wa Kijapan walithubutu hadi kucheza mchezo wa kuua, wakishindana nani kati yao angeweza kuua watu 100 kwa haraka kuliko mwingine. Wanawake wajawazito walitobolewa matumbo yao, wengine walibakwa; mateka walikatwa vichwa na kuteswa, wengine walizikwa hai, wengine wakiuawa kwa kuchomwa moto au kuchomwa na sime kidogo kidogo hadi walipokata roho. 

Tukio hili la kihistoria linaitwa Nanjing Massacre (Mauaji ya Nanjing). Inakadiriwa kwamba watu wapatao 300,000 waliuawa na vikosi vya Japan. Simulizi ya kina unaweza kuipata kwenye kitabu kiitwacho The Rape of Nanking kilichoandikwa na Iris Chang. 

Iris alijiua mwaka 2004 akiwa na umri mdogo wa miaka 36 tu baada ya kuathirika na msongo wa mawazo. Wazazi wake na watu wengine wa karibu wanaamini msongo huo wa mawazo ulitokana na tafiti alizokuwa anafanya, ikiwemo utafiti uliopelekea kuandika kitabu tajwa hapo juu. 

Simulizi za manusura pamoja na mashuhuda wa ukatili wa vikosi vya Japan ni baadhi ya mambo ambayo yalimtesa sana Iris hadi kupata nervous breakdown. Ukipata nafasi ya kufika Nanjing, jitahidi sana utembelee makumbusho ya Mauaji Nanjing. Utapata simanzi lakini kubwa zaidi utajifunza kitu. 

Baada ya Vita ya Pili ya Dunia, Jenerali Matsui alipatikana na hatia ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu, na akanyongwa hadi kufa. 

Tiananmen Square

Ni nini hiki, Tiananmen? 

Mnamo June 4, 1989, maelfu ya wanafunzi na watu wa kada nyingine waliokuwa wamekusanyika  katika eneo linaloitwa Tiananmen Square jijini Beijing walikutana na nguvu ya dola uso kwa uso. 

Waandamanaji walikuwa na madai kadhaa, kubwa ikiwa kudai mageuzi ya kidemokrasia katika nchi ambayo ilikuwa ikiendeshwa kwa siasa ya Ukomunisti. Kufuatia mkwamo uliodumu kwa muda wa siku 50 hivi, Serikali ya China iliamua kutumia nguvu “kusafisha” maandamano hayo. Kilichofuata ni vurugu na maafa. 

SOMA ZAIDI: Oktoba 29, 2025: Tulichoka Hekima na Busara, Tukajaribu Ujinga, Tumeona Matunda Yake

Ni ngumu kujua idadi kamili ya waliofariki, lakini taarifa mbalimbali zinaonesha kwamba idadi yake inafikia mamia kama sio maelfu. Damu ilimwagika. Nchi za magharibi ziliishutumu China, zikisema Beijing ilikiuka haki za binadamu kwa kiasi kikubwa. Shinikizo hili lilipelekea China kutengwa na kuwekewa vikwazo na nchi hizo. 

Oktoba 29, 2025, Tanzania

Nimeandika makala hii kwa zaidi ya juma moja. Nakosa maneno sahihi ya kuelezea kilichojiri siku hii. Hata hivyo, ni wazi kwamba historia ya nchi yetu imeongeza ukurasa mpya katika kitabu chake. Huu ni ukurasa wa giza. Maadamu Tanzania inaishi, Oktoba 29 itabaki kuwa rejea muhimu kwa watu wake. 

Sote tunakumbuka matukio ya Januari 27, 2001, kule Zanzibar ambayo yalipelekea watu kadhaa kupoteza maisha. Rais Mkapa aliitangazia dunia kwamba idadi yao ilikuwa 17, wakiwemo maafisa usalama watatu. Wapo wanaosema idadi ni kubwa zaidi. Mpaka mauti yanamfika, mauaji ya January 27 yalimtesa Mkapa. 

Tofauti na ya Januari 27, hadi sasa mamlaka husika bado hazijatoa idadi ya watu waliopoteza maisha kwa kuuawa na vyombo vya usalama. Tulichoona ni simanzi na vilio kutoka kwa wafiwa waliopoteza ndugu na jamaa zao. 

Misiba ikawa mingi. Kumbukumbu za Oktoba 29 zimechukuliwa na kuhifadhiwa na wananchi wenyewe kupitia simu za mkononi. Upo msemo wa Kiingereza usemao seeing is believing, yaani kuona ni kuamini kwa Kiswahili. 

Maswali

Nimefanya rejea ya Nanjing na Tiananmen ili kuona kama tunaweza kujifunza kitu kwa kujiuliza maswali kadhaa.

Je, yuko Matsui wa kwetu ambaye baada ya kilichotokea Oktoba 29 na siku zilizofuata, anaweza kuwatazama usoni wale waliofyatua risasi zilizoua Watanzania na kuhamaki, “Mama yangu, mmefanya nini?” Kama yupo, basi umma haujamsikia. 

SOMA ZAIDI: Tume Kuchunguza Matukio ya Oktoba 29, 2025: Serikali Iepuke Vishawishi vya Kutaka Kujistiri na Badala Yake Ijikite Kwenye Kuliponya Taifa

Je, yupo Matsui wa kwetu ambaye alitilia shaka nidhamu ya askari wake na vikosi vingine kabla ya kutoa amri ya kudhibiti maandamano kwa kutumia nguvu? 

Nani ni Iris Chang wetu, ambaye, kutokana na aliyoyaona na kusikia, anaweza kupata msongo wa mawazo? Hapa sizungumzii mtu mmoja. Watanzania hatujazoea kuona tulichokiona siku zile. 

Licha ya jitihada za kudogosha kilichotokea, wengi miongoni mwetu wamepata taharuki na tunahitaji msaada wa kisaikolojia. Watoto wa Kitanzania wameona ama ana kwa ana, au kwa kuona picha-mnato na picha za video za kikatili na kutisha, wamesikia simulizi zenye kutia simanzi na hofu. Hawatasahau. Wakisahau watakumbushwa na teknolojia.

Kutoka Tiananmen, tujikumbushe kwamba Agosti 1, 1989, ujumbe wa watu watatu kutoka Chama cha Kikomunsiti cha China uliwasili Tanzania, dhumuni lao likiwa kutoa maelezo kwa chama-dada CCM, juu ya kile kilichotokea. Ujumbe huo ulikutana na Kamati Kuu ya CCM, chini ya mwenyekiti wake, Mwalimu Julius Nyerere. 

Ujumbe wa China ulitoa maelezo kwamba maandamano yale yalilenga kuangusha Serikali, na kwamba walijaribu kutumia njia za kidiplomasia bila mafanikio. Ikumbukwe kwamba maandamano ya Tiananmen yalianza Aprili 15 had Juni 4 yalipozimwa kwa nguvu ya kijeshi. 

CCM ilipokea maelezo ya ujumbe huo, lakini ikasema imesononeshwa na ukweli kwamba damu ilimwagika. Kufuatia hali hiyo, Kamati Kuu ya CCM ilikiri kujifunza mambo mawili kutokana na tukio la Tiananmen.

La kwanza ni kwamba yaliyotokea Tiananmen yalitokana na chama na Serikali ya China kuwa mbali na wananchi, na pili ni kwamba CCM itazame hili kama funzo na kuchukua hatua kushugulika na kero na shida “ndogondogo” za wananchi ambazo zikiachwa zinaweza kuleta maafa kama ya Tiananmen. 

‘Mtambo ya uchaguzi’

Mwaka mmoja baadaye, Agosti 1990, Nyerere alionya juu ya mwenendo wa CCM kugeuka “mtambo ya uchaguzi” (electioneering) – yaani hali ambayo makada wake baada ya uchaguzi hawana tena mahusiano na chama, achilia mbali wananchi. Wao ni uchaguzi, uchaguzi na wao. 

SOMA ZAIDI: Hotuba Kamili ya Rais Samia Akizindua Tume ya Uchunguzi Matukio ya Oktoba 29, 2025: ‘Nina Matumaini Makubwa na Tume Hii’

Maelezo haya yapo kwenye kitabu cha wasifu wa Mwalimu Nyerere “Development as Rebellion: Rebellion without Rebels” kilichiandikwa na mwanazuoni nguli Issa Shivji. Swali, je, ni funzo gani CCM na serikali yake imejifunza sio tu kutokana na tukio la Tiananmen, bali pia Oktoba 29? 

Kwa upande mmoja, kama mwanafunzi wa Chinese soft power, unapata shauku ya kutaka kujua kama namna Serikali ilivyoshughulika na waandamanaji wa Oktoba 29 inatokana na kujifunza jinsi China ilivyoshughulika na waandamanaji wa Tiananmen Square. 

Kwa upande mwingine, ukimya wa mamlaka juu ya mauaji yaliyotokea unaleta shauku kama hiyo tena. Nchini China, mauaji ya Tiananmen hayazungumzwi. Ukiongea hadharani utakuwa matatani. Ikitokea kiongozi wa China akaongelea yale ya Tiananmen huwa inakuwa ni habari motomoto

Hata hivyo, miaka 36 baadaye, kilichotokea Tiananmen kimegoma kufutika kabisa. Hadi leo hii, serikali ya China hujikuta katika wakati mgumu kuelezea kilichojiri Tiananmen.

Dalili

Zipo dalili hapa kwetu za kutaka matukio ya Oktoba 29 na siku kadhaa zilizofuata yasizungumzwe kwa uwazi. Watu wayajadili chinichini kwa kificho kama ambavyo Wachina hufanya kwa Tiananmen. Tufunike kombe mwanaharamu apite. Hili sio somo la kujifunza kutoka Tiananmen. 

Mwalimu Nyerere na CCM yake waliitaka China kutoa ufafanuzi wa kilichotokea Juni 4, 1989, pale Tiananmen Square. Sijui kama Chama cha Kikomunisti cha China kitataka maelezo kutoka kwa chama-dada CCM juu ya Oktoba 29. Hata hivyo, wanaotaka maelezo hayo ni wengi. 

SOMA ZAIDI: Bila Ushirikishwaji Mpana na Uhalali wa Kijamii, Wananchi Lazima Waione Tume Kama Chombo cha Serikali Badala ya Taifa

Tayari tumeelezwa kile waandamanaji walifanya ambacho ni uharibifu wa mali binafsi, mali za CCM na miundombinu ya umma. Baadhi ya waandamanaji hao tayari wamefikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka yao, ikiwemo yale ya uhaini. 

Ambacho hatujaelezwa na mamlaka ni namna gani waandamanaji na wasio waandamanaji waliuawa kwa risasi kati ya Oktoba 29 na Novemba 4. Serikali tayari imekiri watu kupoteza maisha, lakini haijasema idadi yao na pengine muhimu zaidi walipoteza vipi maisha hayo, na nani anahusika. Ni ukweli tu utakaotusaidia kupona majeraha haya na sio uenezi kwa maana ya propaganda

Je, hili ni moja ya yale yatakayoainishwa na ripoti ya Tume ya Rais ya Uchunguzi iliyoundwa kuchunguza “matukio ya uvunjifu wa amani wakati na baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika 29 Oktoba 2025”?

Muhidin Shangwe ni mhadhiri kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Anapatikana kupitia barua pepe yake ambayo ni shangwez@yahoo.com au kupitia Twitter @ShangweliBeria. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Je, ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×