Soka, kabumbu, kandanda, au boli ni maneno maarufu sana katika vijiwe mbalimbali Tanzania. Maneno yote haya yanamaanisha kitu kimoja: mchezo wa mpira wa miguu, mchezo ambao pengine ni maarufu kuliko michezo yote mingine duniani kwa sasa.
Ukitoa Tanzania, umaarufu wa mchezo huu umekuwa ukitofautiana katika maeneo mbalimbali duniani kutokana na uwepo wa michezo mingine kwenye maeneo hayo, jambo ambalo bado haliondoi mchezo wa mpira wa miguu kuwa kati ya michezo mitatu mikubwa maarufu na inayopendwa duniani.
Kwa mujibu wa historia na machapisho mbalimbali, mpira wa miguu umekuwepo tangu karne ya 15, na umeendelea kufanyiwa maboresho mbalimbali mpaka kufikia ubora ulionao leo. Mpira wa miguu umekuwa bidhaa adimu inayotumika duniani kote kama kiunganishi cha kijamii katika kutoa burudani na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.
Kama zilivyo sehemu nyingine duniani, mchezo wa mpira wa miguu hapa nchini Tanzania una historia ndefu inayorudi hadi kipindi cha ukoloni. Duru za kihistoria zinaeleza kuwa mchezo huu ulitumika kama nyenzo ya kijamii iliyowezesha watu kukutana kwa urahisi na kujadili masuala ya harakati za kupinga ukoloni, hasa kupitia mikusanyiko ya michezo, ikiwemo soka.
Historia ya soka nchini ilianza kwa mara ya kwanza na wamisionari wa Kiingereza wa madhehebu ya Kikirsto ya The Universities’ Mission to Central Africa(UMCA) katika shule yao ya michezo iliyokuwa kiungani, Zanzibar miaka ya 1920, na ukaenezwa na wanafunzi waliomaliza masomo yao katika shule yao ya UMCA na baadae mwaka 1921 chama cha kwanza cha mpira wa miguu, Association Football League, kiliundwa, lakini kilikuja kuandikishwa rasmi mwaka 1932 kama chama cha mpira wa miguu.
Maboresho mbalimbali yaliyotekelezwa katika soka yameufanya mchezo huu kuwa na mifumo ya sheria inayoratibiwa na Shirkisho la Soka Duniani (FIFA) linalotekeleza baadhi ya sheria na kutoa miongozo inayoendana sambamba na sheria zingine za taasisi kubwa duniani za soka katika ngazi za mabara na katika ngazi za kitaifa ili kudhibiti namna mchezo wa soka unavyoendeshwa na kusimamiwa.
Uratibu wa Ligi
Moja ya maboresho makubwa duniani ni namna mashindano ya soka, au Ligi, yanayosimamiwa na kuratibiwa na vyama vya soka katika nchi zilizoendelea, au zenye mafanikio kisoka yalivyoweka vigezo na kanuni madhubuti ili kusimamia mapato na matumizi ya vilabu, kwa lengo la kupunguza, au kuondoa kabisa, uwezekano wa kuingizwa kwa “pesa chafu” katika mchezo wa mpira wa miguu.
Hili linalenga kuliondoa soka kuwa kimbilio la biashara haramu lakini kuhakikisha mizania sawa a ushindani kati ya timu shiriki katika mashindano husika.
Mashindano ya soka nchini Uingereza yanayounda Ligi Kuu nchini humo, yaani English Premier League, ni mfano bora wa namna usimamizi makini unavyoweza kuboresha uendeshaji wa michezo.
Ligi hii imekuwa miongoni mwa ligi bora barani Ulaya kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika katika miundombinu ya michezo, matangazo ya kibiashara, pamoja na ubora wa viwango vya wachezaji wanaoshiriki katika ligi hiyo.
Ubora huu umechangiwa kwa kiasi kikubwa na mfumo madhubuti wa usimamizi na uendeshaji unaoratibiwa kwa kufuata kanuni zilizowekwa na Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA), ambamo Chama cha Soka cha Uingereza (FA) ni mwanachama.
Miongoni mwa kanuni hizo ni Kanuni za Faida na Uendelevu, au Profit and Sustainability Regulations kwa kimombo, ambazo zinalenga kuhakikisha vilabu havitumii fedha kuzidi mapato yao halisi. Aidha, kanuni hizi huweka ukomo wa kiwango cha hasara kinachoruhusiwa ili kulinda uendelevu wa kifedha wa muda mrefu.
Kwa maneno mengine, Ligi Kuu ya England inasimamia falsafa kwamba kila mkulima ale na kutumia kile alichopanda, yaani, kila klabu iendeshe shughuli zake kwa mujibu wa uwezo wake wa kifedha. Mfumo huu unalenga kuimarisha uadilifu wa kiuchumi, uwajibikaji wa kifedha, na kuzuia “njaa” ya kifedha isiwe sehemu ya kawaida katika mchezo wa soka nchini humo.
Hali halisi Tanzania
Miaka ya hivi karibuni, mchezo wa soka Tanzania umeendelea kupiga hatua. Maendeleo yaliyoshuhudiwa ni pamoja na uwepo wa ligi tofauti ngazi za mkoa na kitaifa kama Ligi Kuu Tanzania na Ligi Daraja la Kwanza, Ligi Daraja la Pili, na kadhalika, mashindano yanayohusisha jinsi zote, wanaume na wanawake.
Maendeleo haya makubwa yamelifanya soka la Tanzania kupiga hatika katika ubora wa mchezo wa soka, uwekezaji wa miundombinu, udhamini, na ongezeko la mapato yatokanayo na soka jambo linaloashiria ukuaji wa mchezo huu nchini.
Kwa upande wa ubora wa mchezo, Ligi Kuu Tanzania imepanda kwa kasi kutoka nafasi za chini kwenye viwango vya ubora wa ligi bora Afrika. Kwa mujibu wa Shirikisho la Kimataifa la Historia na Takwimu za Mpira wa Miguu (IFFHS) Tanzania inashika nafasi ya nne ikiwa nyuma ya nchi kama Misri, Morocco na Algeria.
Hii ina maana kwamba, mbali na Ligi za nchi tajwa, hakuna ligi bora zaidi barani Afrika kwa sasa kuliko Ligi Kuu ya Tanzania. Kimaendeleo ya kiuchumi, ligi hii imeendelea kuvutia wawekezaji wakubwa wanaotoa ufadhili wa kifedha kama sehemu ya udhamini.
Mfano bora ni AZAM TV kupitia kampuni ya , ambayo ni mdhamini mwenye haki za kipekee za kurusha maudhui ya ligi kupitia televisheni na redio, pamoja na Benki ya Biashara ya Taifa (NBC) inayohudumu kama mdhamini mkuu wa ligi, au Title Sponsor, kama inavyojulikana kwa kimombo.
Vilevile, vilabu vinavyoshiriki ligi hiyo vimenufaika na ukuaji huu wa kiuchumi kupitia udhamini binafsi kutoka kwa makampuni mbalimbali yanayowekeza fedha kwa lengo la kupata manufaa ya kibiashara na kutangaza bidhaa zao.
Kwa sasa, Ligi Kuu ya Tanzania imejijengea hadhi kama moja ya platform bora zaidi za matangazo na uwekezaji wa michezo katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Kasoro za kurekebishwa
Waswahili wanasema, palipo na mazuri, mabaya pia hayakosekani. Pamoja na maendeleo makubwa yanayoonekana katika mpira wa miguu nchini kwetu, bado yapo mambo yanayoweza kutia doa mchakato mzima wa maendeleo haya.
Kwa mfano, ukiachana kuwa taswira ya soka letu inaonesha umiliki tofauti wa timu zetu, ikiwemo timu zinazomilikiwa na watu/kampuni binafsi, taasisi za Serikali kama majeshi, mamlaka za serikali za mitaa, na zile ambazo zinaaminika zinamilikiwa na wanachama, ila sehemu ya umiliki huo iko chini ya wawezekaji.
Kumekuwepo na matukio ambapo klabu hubadilishwa umiliki kiholela bila kuwepo taarifa za wazi kuhusu mchakato mzima wa uhamisho wa umiliki huo.
Umiliki huu unaenda sambamba na uwepo wa wanasiasa ambao ni sehemu ya umiliki wa timu hizi jambo linaloleta usawa kinzani wa kimaamuzi, hasa katika kuhakikisha masuala mazima ya usimamizi wa soka yanafanyika.
Mpaka kipindi hiki si ajabu kutafuta taarifa za kutosha juu ya uongozi wa timu husika, umiliki wake, vyanzo vya mapato na matumizi, ukiachana na kuwa si ajabu kwa timu kubadili jina, au umiliki bila kuweka wazi mchakato ulikuweje.
Miaka michache iliyopita, kuna klabu moja ya madaraja ya chini ilishushwa daraja kutokana na makosa ya upangaji wa matokeo, lakini baadaye wamiliki wake wakaachana nayo, wakainunua klabu nyingine na kuipa jina lilelile la klabu iliyoshushwa na kuendelea na “mwendo mdundo” kana kwamba hakuna lililotokea.
Kama kweli tuna dhamira ya dhati ya kuendeleza soka letu kufikia hadhi ya nafasi ya nne Afrika, ni lazima tuondoe umiliki holela wa timu na tuwe makini katika namna vilabu vyetu vinavyopata na kutumia fedha.
Uwajibikaji
Klabu za Ligi Kuu na ligi nyingine nchini zinapaswa kuweka wazi mapato na matumizi yake kama sehemu ya uwajibikaji kwa sheria za nchi na uwazi kwa wanachama wanaochangia fedha zao kupitia ada za uanachama.
Jitihada hizi zinapaswa kwenda sambamba na uwajibikaji wa vyombo vya mamlaka vinavyohusika katika kusimamia uanzishwaji, uendeshaji, ununuzi, na usimamizi wa soka nchini.
Uwepo wa taasisi za Serikali kama vile Benki Kuu, Tume ya Ushindani (FCC), Bodi ya Ligi, Baraza la Michezo, na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) unapaswa kuonekana wazi katika namna soka letu linaendeshwa kibiashara na kisoka ili kuzuia mianya ya biashara chafu au vitendo vinavyoweza kuharibu taswira ya mchezo huu nchini.
Aidha, kama ilivyoelezwa katika utangulizi, kuna uwezekano wa fedha zisizo na maelezo ya wazi kuingia katika mfumo wa uendeshaji wa ligi yetu, na hivyo kusababisha makosa ya kijinai yanayohusisha fedha, yaani financial crimes.
Swali muhimu la kujiuliza ni: ikitokea TFF na Bodi ya Ligi wakaamua kuweka mikakati madhubuti ya usimamizi wa timu zetu nchini na kudhibiti fedha chafu katika soka, ni klabu ngapi zitabaki zikiweza kujiendesha?
Na je, wapenzi na mashabiki wa soka nchini wako tayari kubeba gharama halisi za uendeshaji ili kuhakikisha vilabu vinatumia fedha zinazozalishwa kihalali?
Hili litawezekana endapo tu kila klabu itakuwa na vyanzo vya mapato vya kueleweka kama sehemu ya uendeshaji wake, badala ya kutegemea hisani, michango, au mahaba ya kisiasa.
Litakuwa jambo la kushangaza kwa ligi inayoshika nafasi ya nne barani Afrika kushindwa kujiendesha kwa uhuru wa kifedha, ukizingatia fursa kubwa zilizopo za kuijenga, kuiboresha, na kuifanya kuwa mfano wa uwazi na uwajibikaji katika michezo ya Afrika.
Moruo King ni mpenzi na shabiki mkubwa wa michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia mtandao wa X @Moruoking au baruapepe mklomayani@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.