Je, umewahi kupokea taarifa kwamba mtoto wako amehusika kwenye mgogoro shuleni, ukajikuta moyo ukikurupuka kabla hata hujasikia upande wa pili?
Ni kawaida kabisa, wazazi na walimu sote tunawapenda watoto na tunataka kuwalinda, lakini kwenye haraka ya kufanya hivyo, mara nyingi tunaishia kupendelea upande mmoja bila kukusudia. Na hapo ndipo kupata suluhisho kunakua kugumu.
Lakini tukiangalia kwa undani, migogoro ya watoto ni fursa nzuri ya kuwafundisha maisha: uadilifu, mawasiliano, na kutatua tofauti zao kwa utulivu. Ili hayo yawezekane, tunahitaji kusimama pamoja kama wazazi na walimu bila hasira, bila ushabiki, na bila upendeleo.
Kwa nini ni muhimu kutokupendelea upande mmoja? Kwa sababu watoto hujifunza haki wanapoona sisi tunachunguza tukio kwa usawa. Tunazuia ugomvi mdogo kugeuka chuki ya muda mrefu. Tunajenga uaminifu kati ya mzazi, mwalimu, na mtoto. Isitoshe, tunawasaidia watoto kujifunza kusuluhisha changamoto badala ya kulaumiana.
Tuwape watoto nafasi waeleze kilichotokea, hisia zao, na walichotamani kingetokea.
Tujitahidi kuepuka kauli kama “Najua wewe huwezi kufanya hivyo.” Badala yake tuulize maswali yanayofungua mazungumzo kama: Ulihisi nini kilipotokea? Ungependa tukusaidieje?
SOMA ZAIDI: Tunawezaje Kuwasaidia Watoto Wetu Wanapohisi Hofu Katika Kipindi Hiki?
Tunapaswa kueleza mahali na muda tukio lilipotokea, watoto waliohusika, kauli na matendo yaliyotokea na hatua zilizochukuliwa na uongozi wa shule. Hii humsaidia mzazi kupata taswira pana, si simulizi ya upande mmoja.
Wazazi na walimu wote kwa pamoja tunapaswa kufanya mazungumzo ya pamoja yenye heshima na lengo liwe kusuluhisha mgogoro wa haki kwa ajili ya ustawi wa watoto. Mazungumzo ya mzazi na mwalimu yasigeuke kuwa mashindano. Lengo liwe moja: maslahi mazuri ya mtoto na kurejesha amani.
Katika mazungumzo hayo tujitahidi kutambua hisia za kila mtoto, kuepuka kulaumiana, na kukubaliana hatua za mara moja na za kufuatilia
Tuwafundishe kwamba wao si watazamaji kwenye mgogoro wao. Tuwasaidie wajieleze, watambue walipokosea au walipokosewa, na wajifunze kuwajibika. Tuwaulize maswali kama: Mnahisi mnaweza kusameheana? Ungependa mwenzako afanye nini tofauti? Wewe unaweza kubadilisha nini ili hili jambo lisijirudie?
SOMA ZAIDI: Hizi Hapa Tabia Tunazojua Zinawaumiza Watoto Wetu Lakini Tunaendelea Kuzifanya
Hii inawafundisha umuhimu wa msamaha, kuweka mipaka, na kujenga mauhusiano mazuri.
Tukumbuke kuwa lengo sio kupata mshindi, bali kujenga tabia njema ya watoto. Katika migogoro ya watoto, ushindi si muhimu. Tunachotafuta ni ukuaji wa tabia, uadilifu, na uwezo wa kujidhibiti.
Tukionyesha usawa kwa watoto wote wawili tunawafundisha watoto kwamba sauti yao ina thamani, hisia zao zinaheshimiwa, kwamba wanaweza kukosea na bado wakajirekebisha na pia kwamba migogoro haipaswi kututenganisha, bali kutusaidia kukua.
Watoto hujenga mtazamo wao wa dunia kupitia sisi. Wanapotushuhudia tukisimama pamoja kwa utulivu, usawa, na busara wanajifunza kwamba migogoro ni sehemu ya maisha na suluhusho hupatikana kupitia mazungumzo, si upendeleo.
Hapo ndipo safari ya kulea kizazi kinachojitambua, kinachoheshimu wengine, na kinachoweza kutatua changamoto zake kwa busara inaanza.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.