Akizungumza katika kikao na wahariri, Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba amepinga takwimu zinazotajwa juu ya idadi ya watu waliofariki kufuatia matukio yaliyotokea baada ya maandamano ya Oktoba 29. Pamoja na Waziri Mkuu kukubali kuwa watu waliofariki, ameeleza kuwa namba zinazotajwa hazina uhalisia.
“Mlikuwa mnaona hata na nyie ameanguka mmoja pale, kaanguka hivi pale ka.. ndio tunakubali vurugu hii, imekuwa na upotevu wa maisha…..” ameeleza Nchemba.
“Hivi unajua inamaanisha nini watu kama wale wanaotajwa sisi tuliwahi kushuhudia mambo ya aina hiyo kwenye nchi moja ya jirani mnajua kwanza tu huwezi uka…huwezi …eh..eh..kwanza mji huu tu, harufu yake ingekuwa… hivi unajua damu ya binadamu ilivyo? Wanaongelea tu elfu ngapi, sijui laki ngapi,tuwe makini kuna vita ya kiuchumi,” aliendelea kufafanua.
Katika kuelezea zaidi, Waziri Mkuu Nchemba alitoa mfano wa meli ya MV Bukoba ambapo alitaja kuwa watu takribani watu 850 walifariki, ambapo Nchemba alieleza kuwa kwa idadi ile takribani kila nyumba ilikuwa na msiba.
Katika suala la kutoa takwimu juu ya vifo, Dk. Mwigulu amelipinga suala hilo akitoa sababu mbalimbali ikiwemo kuingia katika mtego wa watu ‘wanaosherehekea vifo’, pia ametaja kuheshimu familia zinazoomboleza msiba na mwisho akaeleza kuna kazi inayofanywa na tume iliyoundwa.