Kipindi cha likizo na sikukuu huwa na mvuto wake wenyewe: vicheko, harufu za chakula, pilikapilika za wageni, na watoto kukimbizana kila upande. Ni msimu unaojaza nyumba furaha hadi pale tunaposikia.
“Mama! Amenichukulia kitu changu!”
“Baba! Amenisukuma!”
Hapo tunajua siku imechukua mwelekeo mwingine kabisa. Lakini kwa kweli, ugomvi wa watoto wakati wa sikukuu ni wa kawaida kabisa. Hawapigani kwa sababu hawapendani, hapana. Ni kwa sababu wako karibu muda mrefu kuliko ilivyo kawaida, wanagawana vitu, kila mmoja anahitaji uangalizi, na msisimko wa sikukuu unawafanya wawe na hisia kali zaidi.
Katika familia zetu, watoto wanapokutana na binamu zao, marafiki au ndugu ambao hawajawaona muda, kelele huongezeka, uchovu unawapata haraka, na hisia zao huwa juu kuliko kawaida. Ndipo malalamiko na migongano huanza. Na sisi wazazi mara nyingi tunajikuta tunakemea matendo yao haraka, tunawatenganisha au tunachukua upande wa mmoja bila kutafakari chanzo ya migogoro yao..
Lakini mara nyingi, kinachohitajika si ukali bali ni utulivu wetu.
Sasa tufanye nini wakati ugomvi unakuja kila baada ya dakika chache?
SOMA ZAIDI: Mwalimu v Mzazi: Tunavyoweza Kushirikiana Kutatua Migogoro ya Watoto Bila Upendeleo
Tuanze kwa kutuliza hisia zetu wenyewe. Tusikimbilie kukemea au kuwagombeza watoto. Tuwaongoze watulie kwanza. Kujipumzisha kwa dakika moja, kupumua kwa kina, au kunywa maji huwaweka sawa. Wakishatulia, mazungumzo huwa rahisi zaidi.
Tuwasaidie kuelezea hisia zao. Watoto wengi hupigana kwa sababu hawajui kutaja hisia zao. Tuwasaidie kutumia kauli kama: “Nilikasirika kwa sababu…” “Ningependa unirudishie…” “Sikufurahia ulivyofanya” Kadri wanavyozoea kueleza hisia zao, ndivyo migogoro inavyopungua.
Watoto wakikaa bila shughuli za kufanya, ugomvi huongezeka. Tujitahidi kuweka ratiba nyepesi kama muda wa kucheza nje, muda wa kusoma, au shughuli ndogo ndogo za ndani, inaweka siku katika utaratibu mzuri.
Tuwapongeze wanapofanikiwa. Wakigawana, wakielewana, au wakimaliza ugomvi kwa utulivu tuwatambue. Watoto wanastawi wanapojisikia kuthaminiwa.
Tuwasikilize wote bila kupendelea upande mmoja. Tusihukumu kabla hatujasikia maelezo ya kila mmoja. Hii huwasaidia wajisikie salama na kuheshimiwa.
SOMA ZAIDI: Tunawezaje Kuwasaidia Watoto Wetu Wanapohisi Hofu Katika Kipindi Hiki?
Tuwape nafasi ya kutengana kwa muda. Hata watoto wanaopendana huchoka kukaa pamoja kwa muda mrefu. Tuwape muda mfupi wa kila mmoja kufanya anachokipenda peke yake. Hii husaidia kurudisha amani haraka.
Tuwafundishe watoto kutatua changamoto zao wenyewe kabla ya kutuhusisha. Si lazima kila tatizo lije kwa mzazi. Tukiona wanakuja wakiwa wamechachamaa kwa hasira au kilio, tuwaulize tu: “Hebu niambieni, mlijaribu kuongea kwanza?” na kama jibu ni hapana basi tuongeze jinsi ya kuzungumza.
Pia, tuzungumze nao baada ya hali ya ugomvi kutulia. Tukiwa wote tumetulia, tunaweza kuwauliza, “Tukikutana na hali kama hii tena, tunaweza kufanya nini tofauti?” Mazungumzo mafupi kama haya huwafundisha sana.
Ni kweli, sikukuu huja na ugomvi wa watoto hapa na pale lakini pia huja na nafasi nzuri ya kuwasaidia watoto wetu kujifunza kusikilizana, kueleza hisia na kumaliza migogoro kwa amani. Wazazi tuchague utulivu na busara, ili kuwasaidia kujenga misingi ya mahusiano bora si tu wakati wa sikukuu, bali katika maisha yao yote.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.