Katika kipindi cha sasa, mstaafu nchini Tanzania si maskini tena kutokana na kuanzishwa kwa dhana ya urekebishaji wa pensheni, inayojulikana kwa kimombo kama Pension Indexation, ambayo imerejesha heshima kwa waliolitumikia taifa kwa uaminifu.
Kwa miaka mingi, wastaafu nchini walikabiliwa na changamoto kubwa ya kupoteza thamani ya mafao yao kutokana na kupanda kwa bei za bidhaa na huduma, hali iliyofanya kipato chao cha kila mwezi kuwa kidogo mno kulinganisha na gharama halisi za maisha, na kuwafanya washindwe kumudu mahitaji ya msingi.
Ili kukabiliana na hali hii, Pensioner Indexation iliibuka kama suluhisho muhimu linalolenga kulinda ustawi wa wastaafu dhidi ya mfumuko wa bei kwa kurekebisha kiasi cha pensheni ya kila mwezi ili kuendana na mabadiliko ya gharama za maisha, au ongezeko la mishahara ya watumishi walioko kazini.
Lengo kuu ni kuhakikisha kuwa thamani halisi ya pensheni haipotei kadri muda unavyosonga mbele, hivyo kumwezesha mstaafu kuendelea kumudu maisha kwa kiwango kinachokubalika badala ya kuendelea kupokea kiasi kilekile licha ya kupungua kwa uwezo wa ununuzi.
Kwa mfano, iwapo mstaafu alianza kulipwa pensheni ya Sh300,000 mwaka 2010, na gharama za maisha zimeongezeka mara tatu, bila indexation ataendelea kupata kiasi kilekile licha ya kupungua kwa uwezo wa ununuzi. Indexation, kwa hiyo, huzuia hali hiyo kwa kuongeza pensheni kulingana na hali halisi ya uchumi.
Hatua madhubuti
Serikali imechukua hatua katika kutekeleza utaratibu huu kuanzia mwaka 2025 ili kuhakikisha maisha ya wastaafu yanalingana na hali halisi ya uchumi nchini.
SOMA ZAIDI: Je, Wafanyakazi Wanakumbuka Kuomba Fidia Pale Wanapopatwa na Majanga wakiwa Kazini?
Mabadiliko yalianza Januari 2025 ambapo pensheni ya kima cha chini iliongezeka kwa asilimia 50, kutoka Sh100,000 hadi Sh150,000 kwa mwezi, huku wastaafu waliokuwa wakilipwa zaidi ya kiasi hicho wakipata nyongeza ya asilimia mbili ya pensheni yao ya awali.
Maboresho zaidi yalifanyika Julai 2025, ambapo kima cha chini cha pensheni kwa wastaafu wanaolipwa kupitia Hazina kiliongezwa hadi Sh250,125.90, na kwa wale wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), kiasi hicho kilifikia Sh250,000.
Hatua hizi zinaonesha dhamira ya Serikali ya kuimarisha ustawi wa wazee na kujenga mfumo imara wa hifadhi ya jamii ambapo sasa kima cha chini cha pensheni nchini ni takribani Sh250,000 kwa mwezi.
Faida nyingine
Sambamba na maboresho ya pensheni, Serikali imeanzisha faida nyingine muhimu kwa wastaafu wa mifuko ya hifadhi ya jamii ili kuwapunguzia mizigo ya kijamii.
Kuanzia Januari 2025, endapo mstaafu atafariki dunia, familia yake inapata fao la msaada wa mazishi la Sh500,000 ndani ya siku 30 baada ya kuwasilisha ombi, hatua inayosaidia kugharamia mazishi kwa heshima bila kulazimika kukopa au kuuza mali.
SOMA ZAIDI:Mambo Muhimu ya Kuzingatia Usipoteze Mafao Yako Kutoka kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii
Aidha, wategemezi halali wa mstaafu aliyefariki, wakiwemo wajane na watoto walio chini ya umri wa miaka 18 au 21 kwa wale wanaoendelea na masomo, wanastahili kulipwa pensheni ya mkupuo inayolingana na malipo ya miezi 36 ya pensheni aliyokuwa akiipata mstaafu huyo.
Umuhimu wa Pensioner Indexation unaenda mbali zaidi ya kutoa fedha, kwani unasaidia kudumisha uwezo wa ununuzi wa wastaafu na kuhakikisha wanapata mahitaji muhimu kama chakula, makazi na afya.
Utaratibu huu unakuza haki na usawa kwa kutambua mchango wa wastaafu sawa na watumishi walioko kazini, huku ukiimarisha imani ya wanachama kwa mifuko ya hifadhi ya jamii wanaposhuhudia wazee wakitunzwa vizuri.
Kwa kulinda kipato dhidi ya mfumuko wa bei, indexation huongeza heshima na utu wa wazee na kupunguza utegemezi kwa ndugu au watoto. Ni dhahiri kuwa utaratibu huu si neema bali ni haki ya msingi, na hatua zilizochukuliwa mwaka 2025 ni mwelekeo chanya wa kujenga mfumo wa hifadhi ya jamii ulio imara, jumuishi na unaojali utu nchini Tanzania.
Thomas Ndipo Mwakibuja ni mtaalamu wa hifadhi ya jamii. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia thomasmwakibuja@gmail.comau +255 767 879 281.