Kumekuwa na gumzo kubwa nchini kutokana na kauli za wananchi, hasa vijana wa Gen Z, za kujitenga na kuweka mgomo wa kutazama kazi za wasanii wa muziki kutokana na ukimya wao hasa baada ya mauaji yaliyotokea Oktoba 29, 2025, na siku chache baadae.
Huu ni mjadala muhimu ambao unapaswa kutazamwa kwa undani na kugusa kiini cha haya yanayotokea leo. Kabla na hata baada ya uhuru, sanaa nchini Tanzania, hasa muziki, nyimbo, mashairi na sanaa za maonesho zimekuwa sehemu muhimu ya mjadala wa kijamii.
Katika nyakati tofauti, sanaa imecheza nafasi ya kuhamasisha, kuelimisha, kuburudisha na wakati mwingine kuwa chombo cha mapambano ya jamii. Makala hii inaangazia mabadiliko ya sanaa chini ya awamu mbalimbali, na kuchambua kwa nini wasanii wengi wa sasa wamejiondoa katika mavuguvugu ya umma.
Je, huu ni ukimya wa wasanii au ukimya wa sanaa kwa maumivu ya umma? Je, kwa sasa sanaa ni chombo cha Ukombozi wa jamii au chombo cha kupumbaza jamii? Mgomo wa Gen Z ni adhabu kwa wasanii au wito wa mabadiliko ya sanaa?
Sanaa baada ya Uhuru
Katika miaka ya awali baada ya Uhuru, na hasa chini ya falsafa ya Ujamaa na Kujitegemea, sanaa ilipewa wajibu wa kutafsri mwelekeo huo, kutoa matumaini na ujenzi wa taifa. Serikali mpya ya Tanganyika, na baadae Tanzania, ilitumia sanaa kama nyenzo ya kujenga utambulisho wa kitaifa kwa kuhamasisha umoja, kazi, usawa, mshikamano na uzalendo.
Ingawa sanaa iliratibiwa na dola, taasisi za umma, kama vikundi vya sanaa vya taifa na redio ya Serikali, vilitoa jukwaa kwa sanaa inayounga mkono malengo ya Serikali ya chama kimoja. Kulikuwepo wasanii walioibua maswali kuhusu haki, usawa, ushiriki wa wananchi na kuikosoa Serikali.
SOMA ZAIDI: Barua Kwa Wasanii wa Tanzania: Huwezi Kujiunga na Wawindaji na Kujidai Uko Upande wa Wawindwaji
Ukosoaji ulionekana kama tishio. Wasanii waliokosoa Serikali, kama ilivyo ada, walikumbana na vikwazo. Hata hivyo, sanaa ya mapambano haikukoma; ilibadilika umbo. Ilijificha kwenye lugha ya sitiari, muziki wa mtaani na mashairi ya mafumbo. Sanaa haikuwa anasa, au kuhalalisha vitendo vya watawala, bali sehemu ya maisha na harakati ya kujenga jamii mpya.
Mageuzi ya soko huria
Kuanzia miaka ya 1990 na 2000, mabadiliko ya kiuchumi na kisiasa yalibadilisha kwa kiasi kikubwa mazingira ya sanaa. Mageuzi ya soko huria, kuporomoka kwa mifumo ya Serikali kufadhili sanaa na kuibuka kwa vyombo binafsi vya habari, na studio binafsi kulisukuma wasanii kwenye mantiki ya soko.
Kampuni za kurekodi, vyombo vya habari na mapromota walipendelea kazi zinazouzwa kwa haraka, zisizo na hatari ya kisiasa. Msanii alianza kufikiria zaidi mauzo, taswira, umaarufu na uwezo wa kuvutia matangazo.
Katika kipindi hiki, muziki wa dansi na baadaye Bongo Flava ulipata nafasi kubwa, lakini pia ulianza kuachana taratibu na wajibu kombozi wa kijamii, ukielekea zaidi kwenye simulizi binafsi, mikasa ya kimapenzi na burudani.
Ninakiri, katika hatua za mwanzo za Bongo Flava, kulikuwepo na wasanii walioikosoa Serekali, kudadisi masuala ya umaskini, ukosefu wa ajira, rushwa na maisha ya vijana wa mitaani. Nyimbo hizi ziliakisi maisha halisi ya vijana wa mijini na zilikuwa aina ya ukosoaji wa kijamii.
Kadri tasnia ilivyokua na kuingiliwa zaidi na mapromota, matangazo na mitandao ya kijamii, mwelekeo huo ulipungua. Muziki ukawa zaidi juu ya anasa (consumering), mapenzi na ndoto za umaarufu (celebrity), na si tena juu ya mapambano ya umma.
SOMA ZAIDI:Tukiruhusu Ukatili Utawale Tanzania, Tutawezaje Kuwa na Nchi ya Amani?
Katika muktadha wa sasa, ukosoaji unaoelekezwa kwa wasanii kwamba hawasimami pamoja na wananchi kulaani dhuluma au mauaji ya Oktoba 29, 2025, au kupaza sauti ya watu waliopotea, kuuawa na kubambikiwa kesi, ni ukosoaji halali.
Ukimya wa wasanii katika nyakati za maumivu ya jamii unaacha pengo kubwa. Hata hivyo, tatizo kubwa zaidi si tu ukimya wao wa sasa, bali ni mwelekeo wa muda mrefu wa maudhui ya sanaa yao ambayo tayari yalikuwa yamejitenga na maisha halisi ya wananchi kabla hata ya matukio ya sasa.
Burudani pendwa
Kwa muda mrefu, muziki wa Tanzania—hasa ule unaotawala vyombo vya habari—umefanywa kuwa burudani pendwa, au aestheticized entertainment kwa kimombo. Unavutia masikioni, ukiutazama kideoni lakini hauna ujumbe wa maana.
Hauhoji mifumo ya kitabaka, umiliki wa rasilimali, wala maamuzi ya Serikali. Badala yake, zinasherehekea anasa, mafanikio binafsi, mahusiano ya kingono na ndoto za umaarufu. Hii imewatenga wasanii na jamii, na jamii ikaachwa bila lugha ya kisanii ya kuelezea maumivu yake.
Chambilecho Vitali Maembe, hali hii imezalisha kizazi cha wasanii kinachojiona kama “maarufu” na wengine wasanii “marufuku.” Wasanii marufuku ni wale wasio kubali kuacha wajibu jamii wa kiukombozi ili kupata umaarufu, kuwaburudisha vibwenyenye uchawara na wamekataa kuipumbuza jamii kuacha kupambana, kujiona ipo katika Firdaus – hali ya starehe na raha ya hali ya juu – wakati mtaani kuna mazonge, udhalili na ni jahanamu ya walio wengi – mateso na adhabu.
Maoni yangu ni kuwa ukosoaji wa wasanii bila kuyachambua maudhui yao unakuwa dhaifu. Msanii aliyefundishwa na soko kupima thamani yake kwa idadi ya watazamaji (viewers), wafuasi (followers), maonesho na mikataba ya matangazo hawezi ghafla kuwa sauti ya mapambano bila kuvunja msingi mzima wa kazi yake.
SOMA ZAIDI: Kama Tanzania Ingekuwa Timu ya Mpira Unayoshabikia, Bado Ungeipongeza Hata Kama Inakosea?
Hapa lawama hazipaswi kuelekezwa kwa wasanii peke yao, bali pia kwa jamii iliyokubali kugeuza sanaa kuwa bidhaa na wasanii kuwa chapa. Ndio maana hata walivyosikia mgomo huo wapo waliojitokeza na kutoa hoja ya uhuru wa kuchagua.
Lakini, hawakwenda mbali na kuhoji kuchagua nini? Dhulma au haki? Matokeo yake walichepusha mjadala na kufanya kama wanalazimishwa kuchagua aidha vyama vya upinzani au chama tawala, iingawa ukweli wa mambo ni kuwa chaguo lililopo ni moja tu: mapambano (kudai mabidliko, kukataa dhulma) au mapambio (kukubali, kufurahia au kutetea hali iliyopo).
Na sanaa haina upande wa kati, au neutrality kwa kimombo; ni aidha iwe upande wa watesi au upande wa wanyonge.
Funzo la kihistoria
Hata hivyo, msisitizo ni kuwa historia inatukumbusha kuwa sanaa ya mapambano haikuwahi kuwa salama. Ina gharama na hatari. Kilichowatofautisha wasanii wa nyakati zilizopita si ujasiri pekee, bali mwelekeo wa maudhui yao—maudhui yaliyotokana na maisha ya wananchi.
Kama sanaa ya leo itarejesha nafasi yake kama chombo cha ukombozi, lazima ivunje minyororo ya anasa, burudani tupu na umaarufu wa juu juu, na ijiweke tena upande wa wananchi. Je, hicho ndio wanachi wanachotaka? Binafsi, sina jibu.
Kwa hitimisho, mjadala wa wasanii na ukimya wao haupaswi kuishia katika lawama binafsi, au kuishia kuuliza kwa nini wasanii hawapo kwenye upande wa wananchi. Swali la msingi kwa Gen Z na Watanzania: ni sanaa ya aina gani tunaikuza na kuithamini? Sanaa inayotenganishwa na maisha ya wananchi haiwezi kuwa chombo cha ukombozi. Sanaa inayolea ndoto za mtu mmoja haiwezi kuzaa mapambano ya wengi.
SOMA ZAIDI: Watawala Tanzania Wana cha Kujifunza Kwenye Kisa cha Mfalme Henry II wa Uingereza na Askofu Thomas Becket
Hata hivyo, kama ilivyokuwa katika historia ya Tanzania, sanaa ya mapambano haijapotea kabisa. Ipo katika pembezoni: tuna Hip Hop Handaki, mashairi huru, sanaa ya mitaani (KINASA) na majukwaa mbadala ya kidijitali.
Wapo wasanii waliosimama imara kupaza sauti kama vile Roma, Vitali Maembe, Rosa Ree, Ney wa Mitego, Nash MC Zuzu na wengine wengi. Changamoto ni kuipa nafasi na uhalali sanaa hiyo, na kurejesha mjadala wa maudhui kama kiini cha sanaa, si mapambo yake.
Idrisa Kweweta ni mtafiti na mchambuzi wa sera, siasa na masuala ya kijamii, na
Katibu Mkuu Kiongozi wa Baraza Kivuli la Mawaziri la ACT Wazalendo. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia Idrisakweweta34@gmail.com au X kama @idrisa_kweweta. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Je, ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.