Watoto wetu wako likizo. Milango ya shule imefungwa, ratiba za kila siku zimebadilika, na nyumbani kuna muda mwingi zaidi wa pamoja. Katika kipindi hiki, ni rahisi sana sisi kama wazazi kuruhusu simu na runinga kuchukua nafasi kubwa ya siku, hasa tunapojaribu kupumzika, au kutekeleza majukumu mengine ya maisha.
Ni kweli simu na runinga zina nafasi yake. Tafiti zinaonyesha kuwa matumizi ya teknolojia kwa kiasi na kwa maudhui sahihi yanayozingatia umri yanaweza kuwa na manufaa makubwa kwa watoto.
Hata hivyo, wataalamu wa maendeleo ya watoto wanasisitiza kuwa watoto hujifunza vizuri zaidi kupitia uzoefu wa moja kwa moja kama vile kucheza, kuzungumza, kugusa, na kuingiliana na watu na mazingira yao.
Hivyo basi tufanye likizo hii kuwa fursa ya kipekee ya kuhakikisha watoto wanajifunza zaidi kupitia mazingira na watu wanaowazunguka kwa kuwasiliana kucheza na kudadisi.
Watoto wa miaka 0–3
Kwa watoto wadogo wa miaka ya awali (0–3), ubongo hukua kwa kasi kubwa sana. Kulingana na utafiti wa maendeleo ya ubongo, zaidi ya asilimia 80 ya ukuaji wa ubongo hutokea katika miaka mitatu ya kwanza ya maisha. Katika hatua hii, watoto hujifunza kupitia hisia, kusikiliza, kuona, kugusa na kuiga.
SOMA ZAIDI: Migogoro ya Watoto Wakati wa Likizo: Tunawasaidiaje?
Shughuli rahisi kama: kupanga vitu vya nyumbani, kuimba nyimbo, kusoma vitabu vya picha, kuchezea maji, mchanga au mpira chini ya uangalizi wetu, husaidia kukuza lugha, kumbukumbu, na kujenga afya ya mwili pia.
Tafiti pia zinaonyesha kuwa mazungumzo ya ana kwa ana kati ya mzazi na mtoto hujenga misingi imara ya lugha na uwezo wa kufikiri, kuliiza msawali na kujadili mambo, kuliko muda wa kuangalia TV na kutumia simu ambapo ubongo wa mtoto huganda bila kujishughulisha na ikizidi inasababisha madhara katika ukuaji wa lugha, uwezo wa kudadisi na ubunifu.
Kwa watoto hawa, sisi watu wazima ndiyo chachu ya kujifunza kwao.
Watoto wa miaka 4–6
Watoto wa umri wa kuanza shule (4–6) hujifunza sana kupitia michezo ya kubuni na kuigiza. Wanapochora, kupaka rangi, kusimulia hadithi au kuigiza kama walimu, madaktari au wazazi, wanakuwa wanajenga ubunifu, lugha na uwezo wa kutatua matatizo.
Likizo ni muda mzuri wa kuwahusisha katika kazi ndogo za nyumbani, kuwapa majukumu rahisi, na kucheza michezo ya kufikirika pamoja nao. Kisayansi, michezo ya aina hii huimarisha utendaji kazi wa ubongo (executive function) ikiwemo uwezo wa kupanga, kudhibiti hisia na kufuata maelekezo.
Watoto wa miaka 7–11
Kwa watoto wa umri wa kati (7–11), likizo inaweza kuwa zaidi ya mapumziko; inaweza kuwa kipindi cha kukuza ujuzi wa maisha. Kusoma vitabu kwa hiari, kucheza michezo ya nje kama kuruka kamba au kuendesha baiskeli.
SOMA ZAIDI:Mwalimu v Mzazi: Tunavyoweza Kushirikiana Kutatua Migogoro ya Watoto Bila Upendeleo
Tafiti zinaonyesha kuwa michezo ya nje husaidia kupunguza msongo wa mawazo, kuboresha usingizi na kuongeza umakini kwa watoto.
Huu pia ni wakati mzuri wa kuanzisha desturi kama: kuandika kumbukumbu za likizo, kujifunza kupika mapishi rahisi na kushiriki shughuli za kijamii au za kifamilia. Shughuli hizi hujenga uhuru na kuwasaidia watoto kujiona wana uwezo.
Vijana balehe (miaka 12–18)
Vijana balehe wanapokuwa likizo, mara nyingi changamoto si “wafanye nini,” bali “wafanye nini chenye maana.” Kipindi hiki cha maisha kinahusishwa na mabadiliko makubwa ya kihisia na kisaikolojia.
Tafiti za saikolojia zinaonyesha kuwa vijana hawa wanahitaji nafasi ya kujieleza, kusikilizwa, na kushiriki maamuzi ili kukuza afya njema ya akili.
Shughuli kama: mazungumzo ya wazi ya kifamilia, kushiriki maamuzi madogo ya nyumbani, kujifunza kupanga bajeti na kushiriki kazi za kijamii au kujitolea, huwajengea kujiamini na uwezo wa kufanya maamuzi.
SOMA ZAIDI:Tunawezaje Kuwasaidia Watoto Wetu Wanapohisi Hofu Katika Kipindi Hiki?
Tunapowahusisha badala ya kuwaamrisha, tunajenga uhusiano wa kuaminiana na kuwaandaa kwa maisha ya utu uzima.
Tukumbuke kwamba Watoto wetu hawahitaji ratiba ngumu, wala shughuli za gharama kubwa. Wanachohitaji zaidi ni sisi uwepo wetu, masikio yetu ya kusikiliza, na mioyo yetu ya kuelewa.
Kutakuwa na siku zenye kelele na siku zingine tulivu. Zote ni sehemu ya safari ya malezi. Likizo ni nafasi ya kupunguza kazi, kuimarisha uhusiano wetu na watoto, na kuwasaidia kukua siyo tu kimwili, bali pia kihisia, kijamii na kiakili.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.