The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Buriani Mzee Mtei: Tusisubiri Msiba Mwingine Ndiyo Tupate Nafasi ya Kusema Ukweli

Maneno msibani kwa Mzee Mtei yalikuwa makali kwa sababu maumivu ya watu bado ni makali, na hayawezi kupoozwa na wito wa kusahau yaliyopita.

subscribe to our newsletter!

Ni jambo la ajabu na la kusikitisha kwamba sehemu pekee ambapo watu wote wanaweza kutoa maoni yao kikamilifu bila kuwa na wasiwasi wa kukamatwa, au kutekwa, ni kwenye mazishi. 

Enzi zile za kupambana na mfumo wa kikatili wa kibaguzi, apartheid, kwa kimombo, wanaharakati wasanii walitumia mazishi kama sehemu ya kutoa mashairi ya kupambana na mfumo ule wa kikandamizi hadi mashairi ya mazishi yaligeuka kuwa fani maalum ya kuomboleza, na kuungana dhidi ya mfumo huo.  

Wasanii walifanya hivyo kwa sababu mazishi yalikuwa sehemu moja katika sehemu chache ambapo kulikuwa na uwezekano angalau kidogo wa kukutana kisiasa, na kutoa yaliyo moyoni. Ilikuwa ni fursa ya kipekee.

Bila shaka, sisi hapa Tanzania hatujafikia hali hiyo, lakini narudia kwamba ni jambo la ajabu na la kusikitisha kwamba sehemu pekee ambapo watu wa itikadi, vyama, maoni mbalimbali kisiasa waliweza kukutana na kutoa maoni yao kikamilifu bila uoga, au tishio, la kuvamiwa na mfumo usiopenda mawazo mbadala. Kweli ni jambo la kufikirisha pia. 

Naamini mtu yeyote aliyehudhuria alifaidi sana kuelewa mambo mengi kwa upana, si tu maisha ya Hayati Mzee Edwin Mtei – maana watu waliongea kwa kirefu, walichambua, walilinganisha na matukio muhimu katika historia yetu. Yalikuwa mazishi, lakini yalikuwa zaidi ya mazishi sana, yenye kugusa hapa tulipo na huko tunakotamani kwenda.

SOMA ZAIDI: Barua Kwa Wasanii wa Tanzania: Huwezi Kujiunga na Wawindaji na Kujidai Uko Upande wa Wawindwaji 

Ni dhahiri kwamba muktadha ni tofauti na muktadha wa huko kusini mwa Afrika. Katika mazishi ya hayati Mzee Mtei, tunamkumbuka mtu mzee, tofauti na wale vijana walio wengi waliopambana na mfumo kandamizi wa makaburu. Lakini yeye pia anafanana nao kwa mambo mengi.  

Uthubutu 

Kwanza alithubutu kusimama imara mbele ya bosi wake, mbele ya hasira za bosi wake, na kusimamia alichoamini. Sijui moyoni alijisikiaje maana si kazi rahisi, lakini nakumbuka msemo ule wa “sema ukweli hata kama sauti inatetemeka.”

Labda, kwa ujasiri wake, sauti yake haikutetemeka. Lakini sishangai kwamba, wakati wa mazishi, wengi walikumbuka kitendo chake hiki, kwanza kumpinga na kisha kujiuzulu. Na hakuishia hapo. Hata baada ya kujiuzulu, aliendelea kusimamia alichoamini hadi alipoanzisha chama cha siasa, CHADEMA.

Hiki nacho kilikuwa kitendo cha kijasiri sana maana ingawa kinadharia tuliingia katika mfumo wa vyama vingi, watawala walio wengi waliingia shingo upande hadi hata midomo yao ilipinda. Muktadha ulibaki wa chama kimoja na umebaki hivyo hadi leo.  

Hata jina la chama lilibeba kinagaubaga msimamo wake, yaani Demokrasia na Maendeleo ni kama pete na kidole. Na si hivyo tu. Ingawa, binafsi, sijakubaliana sana na ubepari uliokuwemo katika itikadi yao, bado alivyounganisha demokrasia na maendeleo, kama alivyosema msemaji mmoja katika hotuba kwenye mazishi, alionesha maono muhimu sana. 

SOMA ZAIDI: Tukiruhusu Ukatili Utawale Tanzania, Tutawezaje Kuwa na Nchi ya Amani? 

Bila demokrasia, ushiriki wa watu na maendeleo ya watu, ya watu wote, si maendeleo ya vitu, hayawezi kuwepo. Ndiyo maana duniani kumekuwa na viongozi ambao wameendeleza sana vitu, na hata huduma za jamii lakini waliishia kupinduliwa. 

Hii inatokana na ukweli kwamba kama watu hawajisikii huru, kama hawawezi kushiriki kama watendaji wa maendeleo yao, na wenye maamuzi juu ya maendeleo yao, maendeleo yanakuwa chapwa, licha ya takwimu zote za kutambia kujengeka kwa hiki, na kutolewa kwa kile. Buriani hayati Mtei!

Upande wa pili wa shilingi

Lakini kwenye mazishi ya Mzee Mtei, watu waliongelea upande wa pili wa shilingi pia. Mtei alipambana na bosi wake, tena bosi ambaye alikuwa ameongoza miaka mingi, bosi maarufu, lakini pamoja na upinzani wake, hakutekwa, hakukamatwa. 

Badala yake aliruhusiwa kuendelea na maisha yake kama kawaida. Shamba lake kubwa halikuingiliwa na kuharibiwa kama shamba la aliyekuja kumrithi baadaye. Hadi alipoanzisha chama kingine. 

Ikanikumbusha jinsi mzee mwingine aliyekuwa Mwanasheria Mkuu, Mheshimiwa Joseph Warioba, alivyopingana na bosi wake na kuthubutu kumwambia kwamba amevunja katiba. 

SOMA ZAIDI: Karibu Katika Enzi za Mabavukrasia Ambapo Uhuru wa Kusema Hutegemea Nani Anasema

Maraisi jamani, si wanajiona kwamba wako juu ya katiba, au hata kwamba wao ndio katiba. Umwambie Rais hivyo? Na Rais kweli alikasirika na kumtimua huyu aliyethubutu.  Lakini kesho yake, Rais akamwita tena na kukiri kwamba alikosea na kubatilisha uamuzi wake uliovunja katiba!

Duh! Rais akubali kwamba alikosea? Akili gani hiyo? Inahitaji Rais anayejiamini, Rais asiyeogopa kukubali amekosea. Na hapo tunajifunza kwamba ujasiri wa upande mmoja unaendana na uwezo wa upande wa pili kusikiliza na ama kuvumilia ama kubadili.  

Na huo uwezo wa upande wa pili unaruhusu na kuchochea ujasiri. Vinajengana na huwezi kusema ipi ilitangulia, kuku au yai.

Sikatai kwamba Rais enzi zile hakufanya hivyo kila wakati, hasa miaka ya mwanzo wakati Tanzania ilikuwa inajengwa kama taifa. Najua wapo wengi waliotengwa enzi zake, hata mwasisi mwingine wa vyama vingine, Mheshimiwa James Mapalala. 

Lakini hii pia inanikumbusha ujasiri wa mahakama enzi zile. Mzee Mapalala alienda mahakamani na mahakama ilithibitisha uhuru na haki yake ya kufungua chama chake.  

SOMA ZAIDI: Kama Tanzania Ingekuwa Timu ya Mpira Unayoshabikia, Bado Ungeipongeza Hata Kama Inakosea?

Kwa kweli, enzi zile, ujasiri ulikuwa mkubwa zaidi na pia muktadha wa kuruhusu ujasiri ulikuwa mkubwa zaidi. Kinyume chake, muktadha mbovu utajenga uchawa na uchawa utaimarisha muktadha mbovu. Vinajengana.  

Najua wajasiri bado wapo, tena wajasiri zaidi mbele ya vitisho na utekaji na kukamatwa kwa wengi lakini yawezekana wamepungua kwa sabau

Nini kinafuata?

Ndiyo maana najiuliza sasa, baada ya yote yaliyosemwa, na kutangazwa, na kusikilizwa na kuahidiwa kupokelewa nini inafuata? Maneno yalikuwa makali kwa sababu maumivu ya watu bado ni makali na hayawezi kupoozwa na wito wa kusahau yaliyopita. 

Hayasahauliki, vifo haviwezi kusahaulika, vidonda vya mwili na roho haviponi kwa kujifanya, au kutangaza, kwamba havipo tena. Hapo naona kwamba mazishi ya Mzee Mtei yametuweka njia panda kwa mara nyingine.  

Tunaamua kufuata njia ya uwazi na ukweli, njia ya kuchambua yaliyotokea na kujirekebisha hata kama ina maana ya kuanza upya kabla ya matukio Oktoba 29, au tunaamua kuzidi kufunika vidonda hadi vioze zaidi, na mpasuko uzidi kuongezeka?  

SOMA ZAIDI: Watawala Tanzania Wana cha Kujifunza Kwenye Kisa cha Mfalme Henry II wa Uingereza na Askofu Thomas Becket 

Mzee Mtei alikuwa mfano bora kwa vitendo katika maisha yake, na sasa hata katika kufariki kwake anatuita kwa mara ya mwisho tujitambue na kufuata njia sahihi ya maendeleo juu ya misingi ya demokrasia. 

Hapo nasisitiza kwamba siongei kichama bali kihali halisi tu. Tusije tukasubiri mazishi mengine tupate nafasi ya kusema ukweli ili kujenga haki na amani ya kweli

Buriani Mzee Mtei!

Richard Mabala ni mdau wa masuala ya elimu, mshairi na mwandishi wa vitabu. Anapatikana kupitia rmabala@yahoo.com au X kama @MabalaMakengeza. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Je, ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi. 

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×