Wakati Watanzania wakisherekea sikukuu ya Eid, tarehe 21 Machi 2026, Serikali, kupitia Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana, ilitoa tangazo rasmi la fursa ya mkopo wa mfuko wa maendeleo ya vijana.
Kupitia tangazo hilo, serikali iliwatangazia “vijana wote nchini kuwa dirisha la kupokea maombi ya mkopo kupitia programu ya Shilingi Bilioni 200… limefunguliwa rasmi.” Kupitia tangazo hilo, Serikali imetoa wito kwa vijana wote wenye miradi au mawazo ya miradi kutuma maombi.
Kama ilivyo kawaida, pamoja na jumbe za kutakiana heri ya Eid, mitandao ya kijamii, makundi sogozi na jumbe binafsi zilitumwa na wazazi, walezi, ndugu, jamaa na marafiki, zikihamasisha vijana kuchangamkia “fursa” ya mabilioni lelelele – kama wasemavyo vijana wenzangu.
Programu hii imeibua hisia na ari ya matumaini kwa baadhi ya watu katika jamii. Wazazi wanahimiza vijana kuitikia wito huo na baadhi ya vijana wameanza kujadiliana na kuhamasishana kushiriki kwenye kinyang’anyiro hiki cha “mchongo pesa” wa bilioni 200, kwa kusuka “mikeka”, ambayo kwa muktadha huu inaitwa “miradi”.
Wakati huo huo pia, lipo kundi la vijana na wanajamii, wengi tu, ambao wana mashaka makubwa na “fursa” hii. Makala hii inalenga kufanya tathmini ya kina kuhusu programu na mfuko huu.
Serikali, Oktoba 29 na Vijana
Baada ya mauaji ya kisiasa yaliyotokea Oktoba 29, 2026, na tarehe zilizizojiri; Serikali ilianzisha Wizara ya Maendeleo ya Vijana, ikielezwa kuwa ngao na jukwaa muhimu katika kusimamia masuala na mustakabali wa vijana.
Katika jitihada za kuwa daraja la kuiunganisha na kuisafisha Serikali kwa vijana, Ndugu Joel Nanauka, Waziri husika, akaamua kuandaa majukwaa “huru” kwa ajili ya vijana kutema nyongo na kuzungumza kuhusu yaliyotokea tarehe 29 Oktoba na masuala mengine ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Majukwaa haya yalidhihirisha chuki ya wananchi kwa mambo yanayoendelea na hivyo Serikali ikajidhihirishia kwa dhahiri kuliko nyakati nyingine zozote kuwa imekosa uungwaji mkono kwa sehemu kubwa miongoni mwa vijana na wananchi.\
SOMA ZAIDI: Uchaguzi Mkuu 2025: Fursa ya Kubadili Maisha ya Vijana Tanzania
Katika hali ya kutapatapa na kujikomba, ikilenga kujisafisha na kujenga upya mahusiano yake na umma wa Watanzania na hususani vijana, serikali ikaamua kutangaza kutenga haraka bilioni 200 kwa ajili ya maendeleo ya vijana.
Taarifa zaidi zinaeleza kwamba, pesa hizo zimetengwa na kutolewa na Rais Samia Suluhu Hassan. Hata hivyo, taarifa za msingi kuhusiana na fedha hizo hazipo na hatuambiwi. Mfano, fedha hizo Rais kazitolea wapi? Kazitoaje? Kazitoa huko alikozitoa lini? Alipozitoa zitarudishwa? Kama ndio, zitarudishwaje? Zitarudishwa lini? Zitarudishwa na nani?
Yote haya na mengine mengi hatuambiwi, cha msingi tunasisitiziwa kwamba hii ni hisani ya “mkuu” na hisani haihojiwi; sisi tunapaswa kusema hewala na kushukuru kwa yote!\
Bilioni 200 na Vijana
Tarehe 05 Februari 2026, jijini Dodoma, tulishuhudia hafla ya kukabidhiwa kwa hundi ya Bilioni 200, iliyotolewa na kukabidhiwa na Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba, kwenda kwa Waziri ya Maendeleo ya Vijana.
Hundi husika iliandikwa na kuelezwa kuwa ni kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Vijana. Zaidi, Serikali ilieleza kwamba Bilioni 200 hizo zitagawanywa kwa usawa katika sekta za uvuvi, madini, kilimo, biashara na teknolojia, kupitia wizara husika.
Mwezi mmoja baadae, Serikali imetoa tangazo na wito rasmi kwa vijana kuwasilisha maombi ya ufadhili kwa miradi na mawazo ya miradi. Huku ikieleza lengo lake ni kuongeza ajira kwa vijana, kukuza ujasiriamali na kuchochea maendeleo ya uchumi wa taifa.
Maneno haya ya Bilioni 200 na miradi kwa ajili ya vijana si mageni sana nchini… labda kwa watu wageni nchini. Yalikuja mabilioni ya Kikwete… yakatikisa wee… yakaenda na kupotelea wapi, ni kizungumkuti. Mabilioni hayo yalikuja kwa Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya na yakapotezwa na watu “wasiojulikana” kwa Ari Zaidi, Nguvu Zaidi na Kasi Zaidi.
Pia, kwa mbwembwe na nderemo nyingi, ikaja programu ya mfuko wa maendeleo wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu (4-4-2); nayo vijana wakaelezwa kujiunga kwenye vikundi. Hata hivyo, kwa miaka na miaka, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ametueleza juu ya ubadhirifu, uozo na changamoto luluki juu ya fedha hizo kupelekea Serikali kutafuta namna mbadala ya kuendelea na mikopo hiyo.
Tathmini ya kina inaonesha kuwa takribani ya bilioni 200 na zaidi, ambazo leo hii zinaahidiwa tena kwa vijana, zimepotea na kupotezwa kwa namna moja au nyingine. Tathmini na uchambuzi wa dhati unaonesha kwamba fedha hizo zimekuwa kwa kiasi kikubwa mtaji wa kisiasa wa Chama cha Mapinduzi – na sio kuendeleza vijana.
Bilioni 200 kwa ajili ya nani haswa?
Katika mradi na mpango huu “mpya” unaoelezwa na Serikali ni muhimu kujiuliza kuwa hizi bilioni 200 ni kwa ajili ya nani haswa? Ili kuweza kulibaini hili, ni muhimu kuzichambua na kuzitathmini kauli na matamko ya serikali.
Mosi, tangazo rasmi la Serikali linasema kwamba, “Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana (OR-MV) inapenda kuwatangazia vijana wote nchini…” Pia, kauli za Waziri Mkuu na Waziri wa Maendeleo ya Vijana zinaeleza na kuonesha kwamba fedha hizi ni kwa ajili ya vijana wote.
Hata hivyo, je, ni kweli na halisia kwamba fedha hizi ni kwa ajili ya vijana wote? Swali hili linatokana na uhalisia wa kwamba, vijana sio kundi moja tu linaloshabihiana katika kila namna na hali. Kubwa kuliko, yapo makundi ya vijana walio na ajira rasmi, wasio na ajira rasmi na wasio na ajira kabisa.
Kwa mujibu wa taarifa ya Utafiti wa Nguvu Kazi uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mwaka 2024, inaelezwa kwamba takriban watu milioni 2.3 nchini Tanzania, waliokuwa ni nguvu kazi, hawana ajira. Utafiti huo huo pia unaeleza asilimia 94.6 (sawa na takribani milioni 28) ya ajira zote ni ajira zisizo rasmi, hususani katika sekta ya kilimo, huduma na viwanda.
Kwa maana hii, uhalisia wa mienendo na utaratibu wa uendeshaji wa shughuli na maisha, kwa zaidi ya milioni 30 (wasio na ajira na walio kwenye ajira zisizo rasmi), ni utaratibu usio rasmi. Kwa maana kwamba, kundi hili, kwa kiasi kikubwa, halina taarifa rasmi za kibiashara, kiutendaji na hata isivyo bahati kimaisha.
SOMA ZAIDI: Je, Tuwatazame Vijana Kama Kundi Maalumu Tanzania?
Kwa kueleza haya, inastaajabisha kwamba Waziri na Serikali inatamba kwamba Bilioni hizi 200 ni kwa ajili ya vijana wote, huku ikiweka sifa/ vigezo vya kuomba na kupata fedha hizo, ambazo sio halisia kwa mazingira na maisha ya vijana wa kawaida kabisa, ambao wako sehemu ya vijana milioni 30, kama walivyoelezwa hapo juu.
Sifa na vigezo ambavyo vinaibua maswali mengi kwa vijana ni pamoja na mahitaji ya vijana kuwa na namba ya mlipa kodi; awe kwenye eneo linalotambuliwa na mamlaka kwa ajili ya kufanya biashara; awe mtu mmoja, kampuni changa, kikundi cha kijamii, kilichosajiliwa kufanya shughuli; na, awe na leseni kwa biashara inayoendelea.
Tuanza na hili la Namba ya Mlipa Kodi. Mikopo hii bila shaka ni mikopo ya biashara, hivyo itamhitaji kijana kuwa na namba ya mlipa kodi ya biashara. Kwa mujibu wa taarifa za TRA, ni takribani watu na taasisi milioni saba, kwa ujumla, zenye usajili wa namba ya mlipa kodi. Hivyo, kwa takwimu hii, ni dhahiri kwamba sehemu kubwa ya vijana watapata kikwazo kwenye kipengele hiki kikuu na cha lazima.
Pengine ni rahisi kwa mtu kueleza kwamba ni jambo jepesi kwa mtu kujipatia namba ya mlipa kodi. Hata hivyo, huu sio ukweli. Zipo namba mbili za Mlipa Kodi: Namba ya Mlipa Kodi ya Kibiashara na Namba ya Mlipa Kodi isiyo ya Kibiashara. Kwa msingi wa fedha hizi, ni dhahiri vijana watahitajika kuwa na Namba ya Mlipa Kodi ya Kibiashara. Utaratibu wa upatikanaji wa namba hiyo unamhitaji kijana kujisajili kupitia mfumo wa mtandao wa TRA wa IDRAS.
Pamoja na changamoto mbalimbali zinazoweza kuwakabili vijana kuweza kufanya maombi hayo kwa ukamilifu kupitia mfumo huo; takwa la lazima la kwenye mfumo linalotaka na kuhitaji taarifa za eneo la biashara zitakuwa mwiba kwa vijana wengi.
Katika kipengele hiki, Mlipa Kodi (kijana, kampuni changa au kikundi) anatakiwa aeleze iwapo eneo lake la biashara amepangisha au ni lake. Miongoni mwa changamoto nyingine nyingi za kutambua ni wapi haswa ni eneo la kibiashara; kwa kiasi kikubwa vijana hawana maeneo yao ya biashara na hivyo wanakuwa wamepangishwa.
Endapo kijana atakuwa amepangishwa, kijana huyo anahitajika kujaza taarifa za Mlipa Kodi za mwenye nyumba/ mwenye eneo alilopangisha. Utaratibu huu si tu ni mpya kiasi katika jamii, lakini pia ni utaratibu rasmi sana, ambao katika mazingira ya sasa ni rafiki zaidi kwa wapangishaji wa majengo na nyumba kuu kuu.
Uhalisia watakaokumbana na vijana katika kipengele hiki ni kwamba, pale watakapodai namba za mlipa kodi za “mwenye nyumba/ eneo”, kwa kiasi kikubwa, uzoefu ni kwamba wataambiwa mwenye nyumba hana namba ya mlipa kodi.
Taarifa hiyo pengine inaweza kuwa ni ya kweli, kwamba mwenye nyumba/ shamba/ eneo hana kweli namba ya mlipa kodi (kumbuka juu nimeonesha namba hiyo ni ndogo sana kulinganisha na uhalisia). Ila pia, taarifa hiyo inaweza kuwa ni ya uongo, kwa hofu ya kwamba, endapo mwenye nyumba/ eneo atatoa namba yake ya mlipa kodi, na namba hiyo ikaingizwa kwenye mfumo, basi naye ataanza kumulikwa na kutazamwa kwa jicho la tofauti na mamlaka hiyo ya kodi na Serikali kwa ujumla. Hapo ndipo msemo, wasiwasi ni akili unapofanya kazi.
Akiwa kwenye hali kama hiyo, kijana anaweza kuamua kumdai mwenye eneo, na uzoefu, wenye eneo wengi huwatolea nje vijana; na hapo mtu anakuwa na chaguo ama abaki kwenye eneo afanye biashara au atafute eneo lengine atakaloweza kupata namba ya mlipa kodi ya mwenye eneo.
Chaguo la kuhama sio chaguo lenye uhalisia sana, kwa kuwa hamna maeneo mengine mengi yenye wamiliki ambao wana namba ya mlipa kodi au wako tayari kuitoa. Hivyo basi, kwa kipengele hiki, vijana watashindwa kabisa kujipatia Namba ya Mlipa Kodi, kwa njia halali na inayozingatia taratibu za kisheria.
Kikwazo hiki maana yake ni kwamba vijana wengi watashindwa kujipatia Namba ya Mlipa Kodi, na hivyo kushindwa kuwasilisha maombi yao. Kwa hatua nyingine, vijana wanaweza, katika hali ya matamanio makali wanaweza kulazimika kutumia njia za magendo kwa kujaza Namba za Mlipa Kodi zisizo za kweli – kumaanisha, zisizo za wapangishaji wao halisi.
SOMA ZAIDI: Ushiriki wa Vijana katika Maendeleo: Tuache Kauli Mbiu, Tujikite kwenye Mifumo
Kwa kigezo hiki, bila shaka ni vijana walio kwenye utaratibu rasmi na biashara zenye hadhi fulani ndio wataweza kukidhi hiki kigezo.
Ukiachana na Namba ya Mlipa Kodi, kigezo kingine awe kwenye eneo linalotambuliwa na mamlaka kwa ajili ya kufanya biashara. Kigezo hiki ni sehemu ya utaratibu rasmi wa kisera na kisheria kwenye uendeshaji wa biashara nchini, ambapo mtu anahitajika/ anatakwa kuwa na sehemu mahususi ya biashara. Hata hivyo, sehemu hiyo si tu sehemu yeyote ile, bali ni sehemu ambayo inatambulika na inatambuliwa na mamlaka kwa ajili ya kufanya biashara.
Hata hivyo, kama nilivyoeleza hapo awali, vijana wengi wanafanya kazi kwenye sekta isiyo rasmi, na hivyo hata maeneo wanayofanya biashara kwa kiasi kikubwa katika maeneo “yasiyo rasmi” na kwa utaratibu “usio rasmi”.
Uzoefu wetu, kwenye mazingira kama haya, pale ambapo mamlaka imesisitiza kwamba maeneo sio rasmi na watu wanaendelea kufanya kazi na shughuli zao hapo; mamlaka hiyo hiyo huishia kukusanya kodi, tozo na ushuru, na hujitenga kabisa na jitihada za kurasmisha ufanyaji kazi wa watu katika maeneo hayo.
Msisitizo mkubwa wa mamlaka hizo husemwa kuwa, ‘wakizitambua biashara na wakawatambua wafanyabiashara husika, basi wanakuwa wanahalalisha na kwa namna moja au nyingine wana zirasmisha hata biashara hizo, na hivyo wanakuwa wamehalalisha “magendo” katika jicho la kisera, kisheria na kiutawala.
Kwa mantiki hii, kigezo hiki kinachoweka msisitizo kwenye maeneo yanayotambuliwa na mamlaka kinawaweka vijana wengi kwenye wakati mguu; na, kimsingi, kinawabania kabisa na kuwafanya vijana walio wengi washindwe kabisa kukidhi takwa na kigezo hiki.
Badala yake hata hivyo, kigezo na takwa hili, kama ilivyo kwa kigezo cha namba ya mlipa kodi, kinaonekana kuwa ni rafiki kwa aina fulani ya vijana ambao wanajimudu kifedha, kifamilia na kimahusiano katika jamii, kiasi cha kwamba wamefanikiwa kupata maeneo rasmi ya biashara yanayotambuliwa na mamlaka.
Kigezo kingine ni mtu awe mmoja, kampuni changa, kikundi cha kijamii, kilichosajiliwa kufanya shughuli. Kwa mara nyingine tena, kigezo na sifa hii inayotaka usajili wa shughuli inawalenga vijana ambao wako kwenye sekta rasmi au wanaojiendesha kwa utaratibu rasmi; ambao kwa mujibu wa takwimu nilizozitoa hapo awali ni takribani asilimia 5 – 7 tu.
Utaratibu wa usajili wa mtu – kupitia mfumo wa usajili binafsi; kampuni; au, kikundi, ni mchakato ambao unagharimu pesa na umejaa urasimu mkubwa sana. Kwa ujumla na udogo wa kubana bajeti, kijana atahitaji 50,000 kwa ajili ya usajili wa jina la biashara; 100,000 kwa ajili ya usajili wa biashara binafsi; na, 50,000 kwa ajili ya ada ya biashara ndogo. Hapo ni 200,000 imeteketea; na hatujajumuisha gharama za pango, vifaa, bidhaa, uendeshaji n.k.
Hizi ni gharama kwa ajili ya kijana anayehitaji kusajili tu biashara yake. Hapo hajajishughulisha na usajili katika ngazi ya TRA, ambapo napo anagharama za kulipa kodi ya pango na ushuru wa stempu n.k.
SOMA ZAIDI: Tumezungumza na Vijana Kumi Waliojiajiri Kupata Uzoefu Wao. Hiki Hapa Ndicho Walichotuambia
Usajili wa biashara au shughuli sio jambo linalofanywa kwa hiyari tu ya nafsi. Hili ni suala linalohitaji maandalizi na kubwa kuliko pia linahitaji ushauri (consultation) ya kisheria na kikodi. Hizi nazo ni gharama, ambazo kimsingi vijana hawana, na hivyo wengi wao wanaamuaje? Kufanya biashara pasipo kuzisajili, hususani katika hatua za mwanzo; na yote haya si kwa sababu ya ukaidi dhidi ya sheria, bali ni kutokana na uhalisia wa hali zao.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (SBR, 2024) ni takribani biashara 257,000 tu ambazo zimesajiliwa na biashara ambazo hazijasajiliwa ni takribani milioni 3.6. Hivyo, kitendo cha kuamua kuisimamia na kusisitizia sifa na kigezo hiki cha usajili, hatua hii inawatenga vijana wengi zaidi na kutoa kipaumbele kwa vijana wachache sana katika jamii.
Katika tathmini hii ndogo ila ya kina, tunafanikiwa kupata jibu la swali letu, bilioni 200 ni kwa ajili ya nani haswa? Kwa sifa na vigezo hivi, bila shaka bilioni hizi 200 ni kwa ajili vijana walioko na wanaoishi hususani maeneo ya mijini; wanaojihusisha na shughuli rasmi; na, ambao kwa namna moja au nyengine wametoka au ni sehemu ya familia zenye ahueni kidogo kijamii na hata kisiasa.
Hivyo basi, tusidanganyane kwamba bilioni hizo 200, kama kweli zipo, ni kwa ajili ya vijana wote. Jambo hili halihitaji mtu kuwa Tomasa, hoja nilizozianisha hapa zinajielezea. Huu ni mchongo mwengine unaolenga kuwanufaisha sehemu ndogo sana ya vijana, lakini muda huo huo, vijana wote – mijini na vijijini – tutapaswa kuimba ngonjera za kusifu na kuabudu, tukizisujudu bilioni 200 hizi kana kwamba ni za kwetu sote.
Kwa leo niweke nukta hapa, hata hivyo ninajiahidi na kuwa ahidi vijana wenzangu na wasomaji kwa ujumla kurejea na makala nyingine mbili kwenye mada hii hii. Makala moja, inayofuata, itaendelea kuanika ulaghai wa hizi bilioni 200 na makala ya tatu italenga kuonesha ni namna tunapaswa kama taifa kushiriki kikamilifu kwenye maendeleo ya vijana.
Mpaka wakati mwengine, msidanganyike, hizi sio bilioni 200 za vijana, bali mradi mwengine unakusudia kuitakatisha taswira ya Chama cha Mapinduzi kwenye macho ya umma. Ilivyo bahati, hivi sasa CCM haisafishiki, si kwa jiki wa dodoki.
Ruqayya Nassir ni Naibu Katibu Ngome ya Vijana ACT Wazalendo Taifa, ameandika makala hii kwa kushirikiana na Ofisi ya Utafiti na Sera ya Chama cha ACT Wazalendo. Kwa mrejesho, mwandishi anapatikana kupitia ruqayyanassir95@gmail.com au X kama @RuqayyaNassir. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.