The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Maridhiano Mapya Zanzibar – Mkataba wa Amani ama Funika Kombe?

Jambo muhimu zaidi litakuwa jitihada katika masuala ya haki, mageuzi ya kitaasisi, na utawala bora.

subscribe to our newsletter!

Baada ya miezi minane ya mazungumzo na majadiliano yaliyofanyika nyuma ya pazia, CCM na ACT Wazalendo Zanzibar wamesaini makubaliano mapya ya maridhiano yanayojulikana kama Tamko la Pamoja huko Zanzibar. 

Kwa mtazamo wa awali makubaliano haya ni hatua nzuri ya kisiasa. Zanzibar imekuwa na historia ya siasa yenye misukosuko, iliyotawaliwa na migogoro ya uchaguzi na siasa za utambulisho ambazo zimeathiri mahusiano ya vyama vya siasa na jamii kwa ujumla.

Kwa miaka mingi, mivutano hii ya kisiasa imesababisha vurugu, kufutwa kwa uchaguzi, na kususiwa kwa uchaguzi—kumbukumbu ambazo zinaendelea kuathiri Zanzibar. Hata hivyo, kumekuwepo na jitihada za kuleta amani na maridhiano, zikianza na Muafaka I wa mwaka 1999, uliosimamiwa na Jumuiya ya Madola kufuatia uchaguzi wa mwaka 1995 uliokuwa na utata. 

Tangu wakati huo, kila uchaguzi umekuja na makubaliano ya maridhiano yaliyolenga kufanya mageuzi katika mifumo ya uchaguzi na utawala, pamoja na kupunguza mivutano ya kisiasa. Kwa mfano, Muafaka II, uliofikiwa mwaka 2001, ulijengwa kwenye msingi wa mageuzi ya kitaasisi na uwajibikaji katika uchaguzi.

Uanzishwaji wa SUK

Makubaliano ya Maridhiano ya mwaka 2010 yalikuwa kilele cha jitihada za usuluhishi wa ndani zilizopelekea kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK). Kufuatia uchaguzi wa mwaka 2015, Maridhiano yalionekana kama yamekufa pale Chama cha Wananchi (CUF), wakati huo kikiongozwa na Maalim Seif Shariff Hamad, kiliposusia uchaguzi wa marudio wa mwaka 2016 baada ya kufutwa kwa uchaguzi wa mwaka 2015. 

Katika uchaguzi wa mwaka 2020, ambao uligubikwa na vurugu, Maalim Seif Hamad, sasa akiwa na chama kipya cha siasa, ACT Wazalendo, alijiunga na SUK baada ya majadiliano ya ambayo yaliyolenga madai yya fidia ya wahanga wa uchaguzi, mageuzi katika mfumo wa uchaguzi miongoni mwa mambo mengine.

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar Imefeli?

Kuelekea uchaguzi wa mwaka 2025, dhamira ya Maridhiano ilionekana kama haipo kabisa. Maalim Seif Shariff Hamad, aliyekuwa ishara kuu ya maridhiano, alifariki mwaka 2021, na Othman Masoud akachukua nafasi yake kama Makamu wa Kwanza wa Rais. CCM ilishinda uchaguzi wa mwaka 2025, lakini kwa mara nyingine, chama cha upinzani ACT Wazalendo kililalamikia matokeo hayo, kikisema kuwa uchaguzi haukuwa huru wala wa haki.

Licha ya kuwa na kiwango cha kura kinachostahili kikatiba kuiwezesha kujiunga na SUK, ACT Wazalendo iliamua kujitathmini kwa kina kuhusu mustakabali wake ndani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa. 

Makubaliano haya yaliyosainiwa tarehe 9 Julai 2026 yameelezwa kama jitihada za kuimarisha umoja, uvumilivu wa kisiasa, na amani ya kudumu Zanzibar. Uwepo wa Rais Samia Suluhu Hassan katika hafla ya utiaji saini ulikuwa na ishara ya kisiasa na ukiipa hafla hiyo uzito wa kitaifa ambao utatafsiriwa hata nje ya mipaka ya Zanzibar.

Kwa nini maridhiano hayadumu?

Zanzibar na watu wake wanastahili maelewano ya kisiasa baada ya miongo kadhaa ya uhasama na mivutano. Chaguzi za Zanzibar haziishii tu kwenye ushindani wa kura. Ni mahala ambapo malalamiko ya kihistoria, kumbukumbu za kisiasa, na mitanziko ya utambulisho hujitokeza kupitia vyama viwili vikuu vya siasa—CCM na ACT Wazalendo, na hapo awali CUF. 

Kwa hiyo, historia ya maridhiano ina uzito mkubwa wa kimaadili na kisiasa, kama ilivyoshuhudiwa wakati wa kusainiwa kwa makubaliano haya mapya. Kwa miaka mingi, makubaliano ya maridhiano yamekuwa njia za kuponya majeraha ya kitaifa.

Hata hivyo, funzo kutoka makubaliano ya maridhiano yaliyopita linatuonesha pia kwamba maridhiano hayaendi kwa mchakato ulionyooka. Kama Othman Masoud alivyobainisha katika hotuba yake wakati wa kusaini makubaliano hayo, kuna baadhi ya makundi katika maeneo fulani ambayo hayaungi mkono maridhiano. Makubaliano ya tarehe 9 Julai yanaibua swali lingine muhimu: kwa nini makubaliano ya maridhiano hayudumu?

SOMA ZAIDI: Mustakabali wa Maridhiano na Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar

Kama nilivyoeleza hapo awali, Zanzibar ishapitia katika hatua hii ya majadiliano ya maridhiano. Lugha ya Maridhiano imekuwa kiini cha mabadiliko ya kisiasa Zanzibar baada ya mwaka 1995. Kauli na lugha ya maridhiano imekuwa daima ikibeba matumaini ya amani ya kudumu. Hata hivyo, nje ya makubaliano ya viongozi wakuu wa kisiasa, maridhiano hayaonekani kutafsiriwa kikamilifu kuwa manufaa ya kijamii. 

Kila mara, maridhiano yamewasilishwa kama daraja la kuelekea amani na maelewano. Lakini kila mara, matatizo makubwa ya kimuundo wa kisiasa ya Zanzibar imeendelea kubaki bila kutatuliwa.

Jambo la kushangaza katika kuingalia michakato hii ni kwamba kwa kiasi kikubwa imebaki kuwa ya kugawana nafasi za kisiasa (position sharing), badala ya kugawana mamlaka ya kisiasa (power sharing). 

Michakato hii imezalisha makubaliano ya kisiasa ya ngazi ya juu (elite accomodation) ambayo hayajatafsiriwa kuwa mageuzi endelevu ya uchaguzi na utawala, wala uwajibikaji wa kidemokrasia. Mfumo wa SUK, kama ulivyokubaliwa mwaka 2010, unatoa nafasi ya kugawana madaraka. Chini ya mfumo huu, mshindi wa uchaguzi wa urais anakuwa na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. 

Nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais inaenda kwa chama kinachoshika nafasi ya pili katika uchaguzi, na nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais inaenda kwa chama kilichoshinda urais. Hata hivyo, Makamu wa Kwanza wa Rais kwa kiasi kikubwa amebaki kuwa nafasi ya kiishara na isiyo na mamlaka na nguvu kisiasa, na mara nyingi hutengwa na mfumo wa CCM.

Katika kazi yangu ya awali ya kisomi kuhusu Zanzibar, niliueleza mwenendo huu kama siasa za mwendelezo na ushirikiano na kimasilahi. Kwa maana hii, maridhiano hayaondoi kuhodhi kwa utawala wa CCM; bali yanaleta uimara na kutoyumba kwa mfumo. Hii inaleta taswira ya ujumuishi huku yakihifadhi muundo wa udhibiti wa chama tawala. Hii haimaanishi kwamba viongozi wa upinzani wanaoingia kwenye maridhiano bila ufahamu wa kisiasa. 

SOMA ZAIDI: Je, Matakwa ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar Yanakinzana na Yale ya Demokrasia ya Vyama Vingi?

Mara nyingi, hukabiliwa na maamuzi magumu yasiyokuwa na njia rahisi ya kupata ufumbuzi. Mara nyingi wanajikuta na mtanziko wa kuchagua kati ya kukataa kushiriki na kulaumiwa kwa kuhatarisha amani, au kuingia kwenye mazungumzo na kulaumiwa kwa kuhalalisha mfumo wa kisiasa usio wa haki.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini, Othman Masoud alisisitiza tena mtanziko huu. Kwa upande mmoja, anaelewa kuwa kuingia katika SUK kupitia makubaliano haya mapya kunatengeneza nafasi ya kisiasa, kunapunguza mivutano, kunalinda wafuasi wao, na kunaendeleza uwezekano wa mageuzi zaidi. Hata hivyo, Masoud na ACT Wazalendo pia wanaelewa kuwa hili limekuwa ni suala linalojirudia, linaloelezwa vyema na methali ya Kiswahili: funika kombe mwanaharamu apite.

Katika SUK iliyopita ya mwaka 2020 hadi 2025, akiwa Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud alijiweka katika nafasi ya kuwa mshiriki wa serikali na wakati huo huo mkosoaji. Hii haikua jambo rahisi. Katika siasa za Zanzibar, upinzani mara zote unahitaji kupima kati ya msimamo ambao unalenga kupinga kwa njia za kimaadili ama kubaki ndani ya mfumo na kupigania haki wakiwa ndani. Kukataa maridhiano moja kwa moja kunaweza kuwa na gharama ya kisiasa; kuyakumbatia kikamilifu kunaweza kuonekana kama usaliti.

Uaminifu wa CCM

Mafanikio ya Tamko hili la Pamoja yatategemea dhamira na uaminifu wa CCM. Rais Hussein Mwinyi, ambaye yuko katika muhula wake wa mwisho, ameahidi kujitolea na kuonesha nia njema. Hili linaweza tu kutafsiriwa kupitia mageuzi ya uchaguzi yenye kuaminika na uvumilivu wa kisiasa. Jambo muhimu zaidi litakuwa jitihada katika masuala ya haki, mageuzi ya kitaasisi, na utawala bora.

Uwepo wa Rais Samia katika hafla ya utiaji saini pia unaibua swali pana la kitaifa. Je, Zanzibar inaweza kuwa maabara ya siasa pana za maridhiano nchini Tanzania? Tangu aingie madarakani, Samia amezungumza lugha ya maridhiano, mageuzi, na uvumilivu wa kisiasa. 

Hata hivyo, Tanzania Bara inaendelea kushuhudia mkwamo na mivutano ya kisiasa. Kwa hiyo, makubaliano ya Zanzibar yanaweza kuwa zaidi ya suala la Visiwani pekee. Yanaweza kuwa ishara ya mkakati mpana wa utawala wa CCM kuanzisha mazungumzo ya maridhiano Tanzania Bara.

Nicodemus Minde ni mtafiti wa masuala ya siasa za muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Unaweza kumpata kupitia nminde96@gmail.com au kupitia X @decolanga. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi msimamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×