Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetabiri kuwa mvua za Vuli za Oktoba hadi Januari 2026 huenda zikaathiriwa na hali yenye nguvu sana ya El Niño.
Mvua zinatarajiwa kuwa juu ya wastani hadi wastani katika maeneo mengi ya Kanda ya Ziwa, Nyanda za Juu Kaskazini-Mashariki na Ukanda wa Pwani ya Kaskazini.
Mvua hizo zinatarajiwa kuanza kati ya mwishoni mwa Septemba na mwanzoni mwa Oktoba, kuongezeka zaidi Novemba na, katika baadhi ya maeneo, kuendelea hadi Januari 2027.
Hii si taarifa ya kututia hofu, bali ni onyo linalotupa nafasi ya kujiandaa. Tanzania imeanza kuchukua hatua, ikiwemo kusafisha mitaro na njia za maji kwenye baadhi ya barabara kuu zinazosimamiwa na Wakala wa Barabara (TANROADS).
Hata hivyo, maandalizi katika mitaa, vijiji na maeneo yaliyo chini ya halmashauri bado yanaonekana kuwa hafifu. Hapo ndipo hatari kubwa ilipo, kwa sababu mafuriko mengi huanzia katika mifereji midogo, makaravati yaliyozibwa na mikondo ya asili ya maji iliyovamiwa.
Mvua peke yake si janga. Mara nyingi janga hutokea pale maji yanapokosa njia kutokana na ujenzi holela, taka ngumu, mitaro iliyozibwa na udhaifu wa utekelezaji wa mipango ya matumizi bora ya ardhi. Maji yakizuiwa, hayaachi kutiririka; hutafuta njia nyingine kupitia kwenye nyumba, shule, hospitali, mashamba na barabara zetu.
READ MORE: ‘Mazao Yetu Yote Yamesombwa na Maji.’: Njaa Inavyowanyemelea Waathirika wa Mafuriko Mtwara
Tumeona gharama ya kutokuchukua hatua mapema. Mafuriko yaliyotokea Kisongo, Arusha, Aprili 2024 yaliharibu nyumba, barabara na shughuli za kiuchumi.
Kuziba kwa daraja la barabara ya Arusha – Minjingu kulilazimisha maji kubadili mkondo, kubomoa kuta na kuingia katika makazi ya watu. Kukarabati daraja baada ya uharibifu ni muhimu, lakini ni ghali zaidi kuliko kuzuia madhara kabla hayajatokea.
Gharama ya mafuriko hayaishi maji yanapopungua. Barabara zinapokatika, wafanyabiashara hushindwa kufika sokoni, watoto hukosa shule, wagonjwa huchelewa kupata matibabu na wafanyakazi hushindwa kufika kazini. Maji safi yanaweza kuchanganyika na maji taka na kusababisha kuenea kwa magonjwa, huku familia zikitumia akiba zao kukarabati nyumba na kununua upya mali zilizoharibika. Kwa hiyo, gharama ya kutochukua hatua mapema hubebwa na jamii nzima.
Mamlaka za Serikali za mitaa lazima zishuke hadi ngazi ya kaya. Watendaji wa halmashauri, kata, vijiji na mitaa waongoze ukaguzi wa maeneo hatarishi, nyumba kwa nyumba.
SOMA ZAIDI: Athari za Mabadiliko ya Tabianchi Huathiri Maisha, Uchumi wa Watanzania
Mikondo ya maji inayojulikana ifunguliwe mara moja, ikiwemo inayopita katika viwanja vya watu binafsi. Umiliki wa hati hauwezi kuwa kibali cha kuzuia mikondo wa maji na kuhatarisha maisha ya wengine.
Hatua zichukuliwe kwa haki, bila kuangalia tofauti za kipato, nafasi au ushawishi wa mhusika. Wanaokaidi maagizo ya kufungua njia za maji wawajibishwe kwa mujibu wa sheria.
Vivyo hivyo, maofisa wanaopuuza taarifa za wananchi au kushindwa kusimamia kanuni za mipango miji nao wawajibishwe. Halmashauri zitangaze hadharani maeneo yaliyokaguliwa, mitaro iliyofunguliwa, kaya zilizopewa maelekezo na mipango ya kuwasaidia watu wanaoishi katika mazingira hatarishi.
Miundombinu nayo inahitaji kuchunguzwa mapema. Makaravati, madaraja na mitaro isafishwe na uwezo wake wa kupitisha maji mengi uthibitishwe.
Maeneo yanayokumbwa na mafuriko mara kwa mara, yakiwemo Ngaramtoni ya chini, Mianzini, Ngorbob na Mateves mkoani Arusha, yanahitaji hatua za haraka. Barabara mbadala na njia za dharura zitambuliwe, zisafishwe na kuwekwa alama kabla barabara kuu hazijakatika.
Taka ngumu, hasa plastiki, ni tishio jingine. Halmashauri zipitie utendaji wa kampuni zilizopewa kandarasi za kukusanya taka na zichukue hatua dhidi ya zinazozembea. Ratiba za ukusanyaji ziwekwe wazi na maeneo ya kutupa taka yatambuliwe.
SOMA ZAIDI: Mtaalamu Apangua Hoja za Wanaopinga Uwepo wa Athari za Mabadiliko ya Tabianchi
Wananchi nao waache kutupa taka mitaroni, barabarani na kwenye mikondo ya maji. Plastiki tunayoitupa leo inaweza kuelekeza maji ndani ya nyumba zetu kesho.
Kila familia inapaswa kuwa na mpango wa dharura. Tufuatilie taarifa rasmi za TMA, tutambue njia salama za kutoka katika maeneo hatarishi na tuhifadhi nyaraka, dawa na vifaa muhimu mahali salama.
Watoto, wazee, wajawazito na watu wenye ulemavu wapewe kipaumbele. Tusitembee wala kuendesha magari katika maji yanayotiririka kwa kasi, na turipoti mapema mifereji iliyoziba, nyufa katika madaraja na dalili za maporomoko ya ardhi.
Maandalizi yasibaki katika vipeperushi, mikutano na maelekezo kutoka juu. Kamati za maafa katika ngazi za mikoa, wilaya, kata, vijiji na mitaa ziamshwe na kupewa majukumu yanayopimika.
Serikali, sekta binafsi, mashirika ya kiraia, viongozi wa dini, vyombo vya habari na wananchi washirikiane katika kutoa elimu, kusafisha mazingira na kuwafikia walio hatarini zaidi.
SOMA ZAIDI: Tunawezaje Kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Tabianchi?
TMA imetekeleza wajibu wake wa kutoa tahadhari. Kilichobaki ni sisi kuibadilisha tahadhari hiyo kuwa hatua. Tusisubiri nyumba zibomoke, barabara zikatike na maisha yapotee ndipo tutoe pole.
El Niño inaweza kuwa hali ya asili, lakini madhara mengi yanaweza kuzuilika. Tukijiandaa pamoja sasa – Serikali ikiwajibika na wananchi wakitimiza wajibu wao – tutaokoa maisha, mali na fedha ambazo zingetumika kurekebisha uharibifu unaoweza kuepukika.
Emmanuel Sulle ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Hali ya Hewa na Mazingira, Chuo Kikuu cha Aga Khan, Tawi Mama Arusha; anapatikana kupitia sulle.emmanuel@gmail.com. Epiphania Ngowi ni mtaalam wa sera ya afya; anapatikana kupitia epingowi@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Je, ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.