The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Simulizi za Maisha ya Watoto Wanaoishi na Kisukari Zanzibar: Namna Kituo cha Tiba Chumbuni Kinavyowasaidia

Umaskini, lishe duni pamoja na imani za kishirikana sababu zinazopelekea wengi wao kugundulika katika hali ambayo dalili zimeanza kuleta madhara.

subscribe to our newsletter!

Zanzibar – Kwa Farda Issa, miaka mitatu ya mtoto wake haikuwa na maana ya kujua sindano, kliniki wala vipimo vya sukari. Alitarajia kuona mtoto wake akikimbia, kucheza na kukua kama watoto wengine wa umri wake. 

Lakini mwaka jana, maisha ya familia yake huko Mbuzini, Wilaya ya Magharibi A, yalibadilika baada ya mtoto wake wa kwanza kugundulika kuwa ana kisukari.

Mwanzoni, Farda hakuelewa kilichokuwa kikitokea.

“Mwanangu ana kisukari maana ni mdogo sana,” anasema, akikumbuka kipindi kabla ya vipimo vya hospitali. Mtoto huyo alikuwa akiugua homa mara kwa mara na kukojoa kupita kiasi.

Wakati mwingine, mkojo wake ulikuwa ukivutia sisimizi, hali iliyomfanya familia kutafuta huduma ya afya. Vipimo hospitalini ndivyo vilivyowapa jibu ambalo Farda hakulitarajia: mtoto alikuwa na kisukari.

Tangu siku hiyo, chakula kimekuwa chanzo cha hofu kwake.

“Kila ninachompa kula huwa nafikiria sana kama kinamfaa au kinaweza kumuathiri,” anasema Farda. Hofu yake kubwa ni kuona mtoto wake akitofautiana na watoto wengine au ugonjwa huo ukaathiri ukuaji wake.

Maisha ya familia sasa yamejikita katika kumfuatilia mtoto kwa karibu, kuhakikisha anapata dawa, sindano na kwenda kliniki mara kwa mara. Farda anasema akimpa chakula bila kuzingatia uwiano unaoshauriwa, huanza kuona mabadiliko: mtoto hudhoofika, hataki kucheza na wakati mwingine hulia sana.

Hadithi ya Farda ni moja kati ya simulizi zinazojitokeza Zanzibar kuhusu watoto na vijana wanaoishi na kisukari, ugonjwa unaohitaji ufuatiliaji wa karibu, matibabu na mabadiliko ya namna ya kula.

“Familia ilinipeleka kwa mganga”

Kwa Salama Abdallah, mwenye umri wa miaka 17, safari ya kuishi na kisukari ilianza kwa homa kali na mwili kukosa nguvu.

Salama Abdallah binti mwenye ugonjwa wa kisukari akiwa kwenye Hospitali ya Wilaya ya Chumbuni kwa ajili ya kuchukua dawa.Picha/ Najjat Omar

Mwaka 2022, alianza kuumwa ghafla. Hali yake ilipozidi kuwa mbaya, alikuwa akizimia. Familia ilimpeleka hospitalini, ambapo vipimo vilibaini kuwa ana kisukari.

Lakini utambuzi huo haukuishia hospitalini.

SOMA ZAIDI: Zanzibar Yaweka Walimu wa Saikolojia Shuleni Kusaidia Wanafunzi Wanaokabiliwa na Changamoto za Afya ya Akili

Baada ya familia ya upande wa mama yake kusikia hali hiyo, Salama alipelekwa Makunduchi, Wilaya ya Kusini Unguja, alikokuwa akiishi mama yake mdogo. Huko alipelekwa kwa mganga wa jadi kwa imani kwamba tatizo lake lingeweza kuhitaji tiba hiyo.

“Nilipewa dawa za miti shamba, lakini hali yangu haikubadilika,” anasema Salama. Homa na kizunguzungu viliendelea kumsumbua hadi aliporudi mjini.

Baadaye, Salama na mlezi wake waliamua kuanza tena kliniki na kufuata matibabu ya hospitali. Sasa, anasema, ni takribani miaka minne tangu aanze kufuatiliwa kliniki na anaendelea vizuri.

Simulizi yake inaonyesha changamoto nyingine inayowakabili baadhi ya watoto na familia zao: namna imani na uelewa wa ugonjwa unavyoweza kuathiri uamuzi wa kutafuta matibabu.

Usiku uliogeuka kuwa ishara ya ugonjwa

Kwa Asha Omar Mustafa, sasa mwenye miaka 23, ishara ya kwanza ilikuwa kwenda haja ndogo mara kwa mara, hasa usiku.

Mwaka 2021, akiwa na miaka 18, alianza kwenda haja ndogo kwa namna ambayo haikuwa kawaida kwake. Watu waliokuwa karibu na familia yake waliona mabadiliko hayo na kuwashauri wazazi wake wampeleke hospitalini.

Vipimo vilifanyika na jibu likawa wazi: alikuwa na kisukari.

Leo Asha anaendelea na matibabu na bado anatumia sindano. Amejifunza kujichoma mwenyewe na kujipima, huku akifuata masharti ya chakula anayopata kliniki.

Anasema baada ya kuanza matibabu, hali ya kwenda haja ndogo mara kwa mara imepungua.

“Watu wengi wanafikiri kisukari ni ugonjwa wa watu wazima, lakini mimi niligundulika nikiwa na miaka 18,” anasema Asha. Uzoefu wake, anasisitiza, unaonyesha umuhimu wa vijana na wazazi kutopuuza dalili zisizo za kawaida.

Kwa Anuwar, kisukari halikuwa jambo la kishirikina

Tofauti na Salama, Anuwar Faki Ali, sasa mwenye miaka 14, anasema tangu alipopata utambuzi akiwa na miaka sita, aliuchukulia kisukari kama ugonjwa wa kawaida unaohitaji matibabu.

Mwaka 2018, alianza kwenda haja ndogo mara kwa mara. Wazazi wake walimpeleka hospitalini na vipimo vikabaini kuwa ana kisukari.

“Nilipokea kama ugonjwa wa kawaida na sikuona kama ni jambo la kishirikina,” anasema Anuwar.

Anuwar Faki 17, akiwa nyumbani kwao Mfenesini anaugua ugonjwa wa kisukari kwa zaidi ya miaka 6 sasa.Picha /Najjat Omar

Miaka kadhaa baadaye, kliniki imekuwa sehemu ya maisha yake. Amejifunza kuhusu matumizi ya insulini na umuhimu wa kula kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu. Anasema katika familia yao pia kuna watu wanaoishi na kisukari, jambo linalomfanya aone umuhimu wa kufuatilia afya yake.

Mboga na vyakula vyenye protini ni miongoni mwa vyakula anavyosema amejifunza kuzingatia ili kupata nguvu na kuendelea na shughuli zake za kila siku, ikiwemo kwenda madrasa na skuli.

Ugonjwa unaohitaji utambuzi wa mapema

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo katika utafiti unaohusu kisukari aina ya kwanza kwa watoto nchini Tanzania, makadirio yanaonyesha takribani watoto 10 kati ya kila watoto 100,000 walio chini ya miaka 15 wana kisukari, huku makadirio hayo yakihusisha pia Zanzibar.

Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 zinaonyesha Zanzibar ina idadi kubwa ya watoto na vijana. Watoto wenye umri wa miaka 0 hadi 4 walikuwa zaidi ya 276,000, wakati kundi la miaka 5 hadi 9 lilikuwa na takribani 263,843. Wenye miaka 10 hadi 14 walikuwa zaidi ya 231,000.

SOMA ZAIDI: Gharama za Huduma za Afya Chanzo Kikuu cha Umasikini Afrika. Uhandisi Jeni kwa Afya Unaweza Kupunguza Tatizo Hili

Kuwa zaidi ya watoto na vijana 10,000 nchini Tanzania wanategemea insulini ili kuishi, huku Zanzibar ikikadiriwa kuwa na mamia ya watoto na vijana wanaohitaji huduma hiyo.

Takwimu za Wizara ya Afya Zanzibar za mwaka 2023 zinaonyesha kuwa kati ya wagonjwa 1,818 waliolazwa kwa kisukari, watoto na vijana walikuwa sehemu ya wagonjwa hao. Makadirio ya kitabibu yaliyotajwa yanaonyesha kuwa kati ya asilimia 5 na 7 ya wagonjwa wanaolazwa kwa kisukari ni walio chini ya miaka 18.

Madhara yanapoanza kuonekana

Hospitali ya Wilaya ya Chumbuni sasa ndiyo kituo ambacho watoto na vijana wenye kisukari kutoka Zanzibar nzima hupata huduma maalumu.

Kitengo hicho kilianzishwa mwaka 2000 na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Afya. Awali huduma zilitolewa katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja, lakini sasa huduma zinapatikana Chumbuni kwa watoto na vijana wenye umri wa miaka 4 hadi 25.

Kwa siku, kliniki huhudumia wagonjwa kati ya 10 na 15, idadi inayofikia takribani wagonjwa 75 hadi 105 kwa wiki.

Daktari Tamara Said Alle, Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani na Mkuu wa Idara ya Kliniki ya Kisukari katika Hospitali ya Wilaya ya Chumbuni, anasema wengi wanaofika kliniki ni watoto wenye umri wa miaka 6 hadi 20.

Lakini baadhi yao hufika wakiwa tayari wameanza kupata madhara ya ugonjwa.

Anasema baadhi wameanza kupoteza nuru ya macho, wengine wameanza kupata dalili za figo kushindwa kufanya kazi, huku wengine wakifika wakiwa wamevimba mwili na miguu au kuwa na ganzi miguuni.

”Wagonjwa ambao wanakuja katika kliniki wengi walishawahi kupata huduma katika hospitali nyengine, na wengi tunaowapata tayari wameshaonekana na athari za matatizo ya viungo kama nuru ya macho kupungua, wengine wameshaanza kupata dalili za figo kuanza kufeli, wengine wamevimba mwili na kujaa miguu pamoja na miguu kuwa na ganzi,” anasema Daktari Tamara.

Kwa Daktari Tamara, changamoto mojawapo ni kuchelewa kwa wazazi kutafuta matibabu. Anasema baadhi ya wazazi bado wanaamini kuwa kisukari kinahusiana na masuala ya kishirikina, hali ambayo inaweza kuchelewesha kuanza kwa matibabu ya hospitali.

Chakula nacho ni sehemu ya matibabu

Mbali na dawa na insulini, chakula ni sehemu muhimu ya maisha ya mtoto mwenye kisukari.

Daktari Tamara anaeleza kuwa mlo wa mtoto unapaswa kuwa na makundi mbalimbali ya chakula kama wanga, protini, mboga, matunda na maziwa, kwa kiasi kinacholingana na umri na mahitaji yake.

Daktari Tamara Alle, Mkuu wa Idara ya Kliniki ya Kisukari iliyopo katika Hospitali ya Wilaya ya Chumbuni.Picha/Najjat Omar

Vinywaji vyenye sukari, pipi, biskuti, keki na vyakula vilivyosindikwa vyenye sukari nyingi vinapaswa kutumiwa kwa kiasi kidogo.

Lakini ushauri huo unakutana na hali halisi ya familia nyingi: umaskini.

Daktari Tamara anasema familia nyingi zinazofika kliniki zina hali za maisha ya chini. Kwa hiyo, wataalamu hujaribu kutoa ushauri unaozingatia kile ambacho familia inaweza kumudu.

Ikiwa familia haiwezi kupata mbogamboga za aina nyingi, anaeleza, hata vyakula vinavyopatikana kwa urahisi kama kitunguu maji na tungule vinaweza kutumiwa pamoja na chakula cha wanga.

Huduma bure, lakini safari inaendelea

Tanzania Diabetes Association, kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, imekuwa ikishiriki katika juhudi za kuzuia, kutambua mapema na kusaidia watu wanaoishi na kisukari, wakiwemo watoto.

Zanzibar, huduma za upimaji, utambuzi, matibabu na dawa kwa watoto wenye kisukari hutolewa bure. Kwa mujibu wa Daktari Tamara, msaada kutoka mashirika mbalimbali, ikiwemo katika upatikanaji wa insulini, umechangia watoto kupata matibabu kwa wakati.

Hata hivyo, nyuma ya takwimu na huduma hizo kuna watoto wenye maisha halisi.

Kuna Farda anayemwangalia mtoto wake kwa hofu kila anapoweka chakula mezani. Kuna Salama ambaye familia yake ilitafuta tiba ya jadi kabla ya kurejea hospitalini. Kuna Asha ambaye alijifunza kwamba kwenda haja ndogo mara kwa mara kunaweza kuwa ishara ya ugonjwa mkubwa. Na kuna Anuwar, ambaye tangu utotoni amejifunza kuishi na insulini, kliniki na mlo maalumu bila kuiona hali yake kama mwisho wa maisha ya kawaida.

Kwao, kisukari si takwimu tu.

Ni sindano wanazotumia, chakula wanachochagua, kliniki wanazohudhuria na hofu ambazo familia zao hubeba. Lakini pia ni safari ya kujifunza namna ya kuishi na kuendelea kukua, kusoma, kufanya shughuli za kila siku na kutazamia maisha yaliyo mbele yao.

Najjat Omar ni mhariri na mwandishi wa The Chanzo kutoka Zanzibar, unaweza kuwasiliana nae kwa email –najjatomar@gmail.com. 

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×