The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Vijana Wabuni Mfumo wa Kidijitali Kudhibiti Taka Dar es Salaam

Wabunifu hawa wameunda mfumo unaolenga kuwaunganisha wananchi, wakandarasi na mamlaka za Serikali za Mitaa kwenye jukwaa moja la kushughulika na uondoshaji taka kwenye mazingira.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam – Kila siku, wakazi wa Dar es Salaam huzalisha maelfu ya tani za taka. Baadhi hukusanywa na kupelekwa kwenye dampo, lakini kiasi kikubwa hubaki kwenye mitaa, pembezoni mwa barabara na kwenye mifereji, kikisubiri siku ambayo gari la taka litapita.

Katika baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es Salaam, tatizo hilo limekuwa sehemu ya maisha ya kila siku. Taka zinapochelewa kuondolewa, harufu huongezeka, mifereji huziba na mazingira yanabadilika kutoka kuwa sehemu ya makazi na biashara hadi kuwa eneo la mrundikano wa taka.

Tatizo hili limefikia hatua ambayo limekuwa likitajwa hata katika ngazi ya juu ya Serikali. Hivi karibuni, Rais Samia Suluhu Hassan alieleza kutoridhishwa na hali ya usafi katika miji mbalimbali nchini, akitolea mfano Dar es Salaam na kusema hali ya jiji hilo haijaridhisha.

Lakini nyuma ya tatizo hilo kubwa la mazingira kuna swali jingine: Je, teknolojia inaweza kusaidia jiji kujua ni wapi taka zimejaa kabla hazijaanza kuzagaa mitaani?

Kwa kundi la vijana watatu waliohitimu Shahada ya Uhandisi wa Usafi wa Mazingira kutoka Chuo cha Maji jijini Dar es Salaam mwaka 2026, jibu la swali hilo limekuwa chanzo cha wazo waliloliita “Smart Dar.”

Kwao, mrundikano wa taka haukuwa tu changamoto ya mazingira. Ulikuwa pia fursa ya kutumia maarifa waliyoyapata chuoni kutafuta njia tofauti ya kusimamia taka.

Isdory Walter Denis, mmoja wa wabunifu wa mfumo huo, pamoja na Evelina Amon Mlungu na Josephine Godfrey Alfred, walianza kutengeneza wazo hilo baada ya kuona kwa karibu changamoto zinazotokana na mfumo wa kawaida wa ukusanyaji wa taka.

Mbunifu wa mfumo, Isdory Dennis, akitoa maelezo ya kina kuhusu muundo wa kidijitali wa Smart Dar na namna unavyofanya kazi. PICHA | THE CHANZO

“Tatizo kubwa ambalo tunalenga kutatua ni kuzagaa kwa taka jijini Dar es Salaam,” anasema Isdory.

“Lengo la mradi huu ni kuhakikisha tunaenda kupunguza kiwango cha taka kinachozagaa mtaani kutoka tani 700 kwa siku katika eneo la Ilala mpaka angalau tani 200 kwa siku.”

Jiji linalozalisha taka kuliko uwezo wa kukusanya

Dar es Salaam ni moja ya miji inayokua kwa kasi nchini Tanzania. Kadiri watu wanavyohamia jijini kutafuta ajira, biashara na fursa nyingine za kiuchumi, ndivyo mahitaji ya huduma za msingi yanavyoongezeka.

Moja ya huduma hizo ni usimamizi wa taka.

Takwimu za Benki ya Dunia zinaonyesha kuwa Dar es Salaam huzalisha takribani tani 4,600 za taka kwa siku. Hata hivyo, chini ya asilimia 40 ya taka hizo ndizo hukusanywa na kufikishwa kwenye maeneo rasmi ya utupaji taka, kama Pugu Kinyamwezi.

SOMA ZAIDI: Mhitimu wa NIT Alivyobadili Changamoto ya Taka Kuwa Fursa Wilayani Mafia

Hii ina maana kuwa sehemu kubwa ya taka hubaki nje ya mfumo rasmi wa ukusanyaji, hali inayoongeza uwezekano wa kutupwa kiholela mitaani, kwenye maeneo wazi na kwenye mifereji.

Ripoti ya UNEP Hotspot nayo inaonyesha changamoto hiyo, ikibainisha kuwa takribani asilimia 40 hadi 50 ya taka pekee ndizo hukusanywa na kufikishwa kwenye maeneo ya kutupa taka, huku kiasi kikubwa kikibaki katika mazingira ya makazi.

Ilala ni miongoni mwa maeneo yanayokabiliwa na changamoto hiyo kwa kiwango kikubwa. Kwa wastani, wilaya hiyo huzalisha zaidi ya tani 1,500 za taka kwa siku. Kati ya hizo, takribani tani 800 ndizo hukusanywa na kuondolewa, huku karibu tani 700 zikibaki.

Kwa Isdory na wenzake, pengo hilo ndilo walilolenga kulifanyia kazi.

Badala ya kusubiri taka zijaze vizimba na kuanza kumwagika, walitaka kutengeneza mfumo ambao ungeweza kutoa taarifa kabla tatizo halijawa kubwa.

Kutoka mfumo wa kawaida hadi “Smart Dar”

Kwa mfumo wa kawaida, ukusanyaji wa taka hutegemea ratiba za magari, wafanyakazi na mawasiliano kati ya wananchi na wakusanyaji taka.

Mfumo wa Smart Dar unajaribu kubadilisha mtazamo huo kwa kutumia mifumo ya data.

Hatua hii ya mfano wa awali (prototype) ya Smart Dar inaonyesha namna teknolojia inavyoingia hadi kwenye miundombinu ya msingi ya makazi ikiwemo usimamizi wa mtandao wa maji taka. PICHA | THE CHANZO

Katika mfumo huo, vihisi au kwa kimombo ‘sensor’ vya kidijitali vinavyofahamika kama HRC Ultrasonic Sensors vitawekwa kwenye vizimba vya taka. Vizimba hivyo vinapendekezwa kujengwa kwa matumizi ya kaya takribani 10 hadi 20.

Sensor hizo zitafuatilia kiwango cha taka kilichopo ndani ya kizimba.

Kizimba kinapokaribia kujaa, taarifa itatumwa kwenye mfumo na kumfikia mkandarasi anayehusika na ukusanyaji wa taka katika eneo hilo.

Hivyo, badala ya mkandarasi kusubiri ratiba ya kawaida au wananchi kuanza kulalamika baada ya taka kufurika, mfumo unampa taarifa mapema kwamba kuna taka zinazohitaji kuondolewa.

“Sensors ambazo zinaitwa HRC Ultrasonic Sensors tunazifunga kwenye vizimba na lengo lake ni kukusanya data ya kiwango cha takataka katika vizimba,” anaeleza Isdory.

“Kwa hivyo, kizimba kinapokuwa kinajaa takataka, ile taarifa inakuwa inatumwa kwenye mfumo kutoka kwa mtumiaji kwenda kwa mkandarasi ambaye ana jukumu la kuja kukusanya hizo taka. Kwa hiyo, yeye anakuwa anapata taarifa, anakuja anakusanya hizo taka anaenda kuzimwaga dampo.”

Haya ni mabadiliko kutoka mfumo unaosubiri tatizo litokee kwenda mfumo unaojaribu kuliona kabla halijawa kubwa.

Wananchi hawabaki nje ya mfumo

Smart Dar haikulenga tu kuboresha mawasiliano kati ya vizimba vya taka na wakandarasi.

Wabunifu wake wameunda mfumo unaolenga kuwaunganisha wananchi, wakandarasi na mamlaka za Serikali za Mitaa kwenye jukwaa moja la kushughulika na uondoshaji taka kwenye mazingira.

Hii ina maana kuwa mwananchi anaweza kutumia mfumo huo kuomba huduma au kutoa taarifa kuhusu changamoto ya taka.

Ikiwa mkandarasi hatashughulikia taarifa hiyo, suala hilo linaweza kuonekana kwenye mfumo wa mamlaka husika ya Serikali za mitaa.

Kwa Isdory, hatua hiyo inalenga kuongeza uwajibikaji katika mfumo mzima wa ukusanyaji taka.

“Endapo kuna changamoto imetokea na mtumiaji ameomba usaidizi au ameomba huduma kutoka kwa mkandarasi na hajapata, tatizo lake halijatatuliwa, hilo tatizo linaonekana moja kwa moja kwa mamlaka husika ambayo ni Halmashauri ya Manispaa,” anasema.

SOMA ZAIDI: Dodoma Inayokua, Taka Zinavyoongezeka: Mitaa Yakumbana na Changamoto ya Utupaji Taka Holela

“Na hivyo basi, Halmashauri inaweza kulichukua jukumu na kumhimiza yule mkandarasi aje kushughulikia tatizo lako.”

Kwa mtazamo huo, teknolojia haitumiki tu kutambua ujazo wa taka. Inatumika pia kuunda mnyororo wa uwajibikaji kati ya anayezalisha taka, anayehusika kuzikusanya na mamlaka inayosimamia huduma hiyo.

Tatizo la taka si suala la mwonekano pekee

Kwa Dar es Salaam, madhara ya taka zinaposhindwa kukusanywa kwa wakati yanaenda mbali zaidi ya kuonekana kwa jiji kuwa chafu.

Karibu asilimia 60 ya taka zinazozalishwa jijini ni taka za kikaboni, hasa mabaki ya chakula. Taka hizi zinapooza bila usimamizi mzuri zinaweza kuzalisha gesi ya methane, ambayo ina athari katika mabadiliko ya tabianchi.

Wakati huo huo, taka zinazotupwa kwenye mifereji zinaweza kuzuia mtiririko wa maji, kuongeza hatari ya mafuriko na kuunda mazingira yanayoweza kuchochea milipuko ya magonjwa, ikiwamo kipindupindu.

Hivyo, changamoto ya ukusanyaji taka inagusa kwa wakati mmoja mazingira, afya ya jamii na uwezo wa jiji kukabiliana na athari za mvua.

Kwa wabunifu wa Smart Dar, teknolojia ni sehemu moja tu ya jibu. Lakini wanachoamini ni kwamba taarifa sahihi na zinazopatikana kwa wakati zinaweza kusaidia mamlaka na wakandarasi kufanya maamuzi bora zaidi kuhusu mahali pa kupeleka magari na muda wa kuondoa taka.

Kutoka darasani kwenda maabara ya jiji

Kwa sasa, Smart Dar bado haijafikia hatua ya kutumika katika Jiji lote la Dar es Salaam.

Mfumo huo uko katika hatua ya awali ya prototype, huku timu hiyo ikiwa imeanza hatua inayofuata ya kufanya pilot project katika mazingira ya Chuo cha Maji.

Muonekano wa ndani wa mfumo wa kidijitali (web dashboard) unaotumika kuendesha na kusimamia mradi wa Smart Dar. PICHA | THE CHANZO

Majaribio hayo yanalenga kuona namna mfumo unavyofanya kazi katika mazingira halisi, kubaini changamoto zinazoweza kujitokeza na kuboresha teknolojia kabla ya kufikiria kuipeleka katika maeneo mengine.

Kwa vijana hao, hatua hii ni muhimu kwa sababu wazo lililo kwenye karatasi linahitaji kuthibitishwa katika mazingira halisi kabla ya kutumika kwa kiwango kikubwa.

Mfumo wa taka wa jiji unahusisha mamilioni ya wakazi, maeneo mengi ya makazi, wakandarasi, mamlaka za Serikali za mitaa, magari ya ukusanyaji, vituo vya taka na maeneo ya mwisho ya utupaji.

Kwa hiyo, Smart Dar itahitaji zaidi ya teknolojia kufanya kazi kwa kiwango cha jiji.

Itahitaji pia miundombinu, ushirikiano wa taasisi, uwekezaji na utayari wa watumiaji kuutumia.

Wito wa kuamini ubunifu wa vijana

Isdory anaamini kwamba changamoto kama ya taka zinaweza pia kuwa nafasi ya Tanzania kukuza suluhisho lake yenyewe kupitia vijana.

Anataka Serikali, wakandarasi na taasisi za elimu kuona ubunifu kama huo si wazo la wanafunzi pekee, bali kama sehemu ya jitihada pana za kutafuta majibu ya changamoto zinazolikabili taifa.

“Wito wangu kwa wadau ni kushirikiana. Naiomba Serikali, wakandarasi mbalimbali na taasisi za elimu kama Chuo cha Maji tuweze kushirikiana kuhakikisha wazo hili na mengine yenye nia njema yanapewa ushirikiano, nguvu na rasilimali zinazohitajika ili kujenga uchumi na kulinda afya zetu,” anasema.

Kwa Dar es Salaam, changamoto ya taka imekuwepo kwa muda mrefu na imekuwa ikikua sambamba na ukuaji wa jiji.

Lakini katika mazingira hayo hayo, kizazi kipya cha wahandisi kimeanza kutafuta majibu kwa kutumia teknolojia waliyojifunza.

Kwa vijana hao watatu, taka ambazo zimekuwa kero ya kila siku kwa wakazi wa Dar es Salaam zimekuwa pia darasa lao la ubunifu—na mwanzo wa jaribio la kuifanya huduma ya ukusanyaji taka kuwa ya kidijitali zaidi.

Ibrahim Mgaza ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam. Anapatikana kupitia ibrahimmgaza39@gmail.com.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×