The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Dodoma Inayokua, Taka Zinavyoongezeka: Mitaa Yakumbana na Changamoto ya Utupaji Taka Holela

Utupaji holela wa taka umesababisha kuibuka kwa ‘madampo bubu’ kwa baadhi ya mitaa jijini Dodoma.

subscribe to our newsletter!

Dodoma. Pamoja na kuwepo kwa Mpango Kabambe wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira 2022-2032, utupaji wa taka katika maeneo mengi nchini umeendelea kufanyika kwa namna ambayo si rafiki kwa mazingira.

Kwa mfano, asilimia 30.7 ya utupaji wa taka nchini unahusisha utupaji holela kwenye maeneo yasiyotengwa kwa ajili ya utupaji wa taka. Asilimia 38.4 unahusisha utupaji wa taka katika maeneo yaliyotengwa, lakini yasiyo na miundombinu inayokidhi utupaji salama wa taka.

Kwenye Jiji la Dodoma linaloendelea kukua kwa kasi, tatizo la utupaji holela wa takataka katika maeneo yasiyo rasmi limeendelea kushamiri siku hadi siku. 

Abeid Ramadhani, 31, baba wa watoto wawili anayejishughulisha na ujasirimali Mtaa wa Ng’hong’hona anasema, utupaji holela wa taka katika mtaa wao unasababishwa na uhaba wa vyombo vya kukusanyia taka.

“Unakuta ana guta moja, haitoshi katika kukusanya taka kwa wakati katika mazingira ambayo watu wanatakiwa watupe taka,” anasema Abeid wakati akizungumza na The Chanzo.

Abeid anasema kwamba si hivyo tu, mkandarasi aliyechukua zabuni ya kuzoa taka ni mmoja katika mtaa huo, hali inayosababisha watu kuendelea kutupa taka kwenye maeneo yasiyo rasmi.

“Angepata gari ingemsaidia kutoa taka kwa wakati. Unaweza ukazunguka kwenye maeneo mbalimbali ukakutana na harufu mbaya, kutokana na taka zilivyotupwa hovyo. Pia hata muonekano wa mazingira unakuwa mbovu, kama hapo unaona kuna pempasi za watoto zingine zina kinyesi,” anasema Abeid.

Uchunguzi uliyofanywa na mwandishi wa habari wa The Chanzo umebaini kuwa baadhi ya watu hutupa taka hizo nyakati za usiku, kwa kukwepa kulipa ada za taka na pamoja na uwepo wa uhaba wa vifaa vya kukusanyia taka. Utupaji holela wa taka umesababisha kuibuka kwa ‘madampo bubu’ kwa baadhi ya mitaa jijini Dodoma.

Uchunguzi huo umefanyika katika mitaa mitatu ikiwemo Mtaa wa Sechelela uliopo katika Kata ya Tambukareli, Mtaa wa Ng’hong’hona uliopo katika Kata ya Ng’hong’hona, na Mtaa wa Chikole uliopo katika Kata ya Msalato.

Asna Mohamed ni mjasiriamali anayefanya shughuli zake katika Mtaa wa Ng’hong’hona anasema, hakuna mpangilio mzuri wa uzoaji taka katika mtaa huo kwa kuwa watu hutupa sehemu yoyote. 

“Huku hapapiti magari, Serikali ya Mtaa itusaidie kupitisha magari ya uzoaji taka. Gari la taka kama huku huwa halipiti, labda tuseme huku ‘center’ huwa lina pita mara moja moja sana,” anasema Asna.

Wanaogopa kulipa tozo

Odula Mwambigija ni mmoja wa wananchi ambao amejitolea kubeba taka katika Mtaa wa Ng’hong’hona, anakiri uwepo wa changamoto ya utupaji holela wa taka katika mtaa huo.

“Suala la usafi wa mazingira lina upana wake, kuna mwingine anatupa kwa kuogopa kutoa ile tozo kwa mujibu wa Sheria yuko tayari usiku wengine wamelala yeye akaenda porini kutupa taka,” anasema Odula.

SOMA ZAIDI: Uraibu wa Tramadol: Janga Linalonyemelea Familia za Kitanzania Kimya Kimya

Odula anasema pia changamoto ya miuundombinu inachangia magari ya kukusanya takataka kushindwa kufika kuchukua taka kwenye baadhi ya nyumba za watu. 

“Sehemu nyingine unakuta hizi barabara hamna kwa hiyo inasababisha vile vyombo ambavyo vinasaidia kukusanya taka haviwezi kufika kwenye eneo hilo,” anasisitiza Odulla 

Kwa upande wa uongozi wa Mtaa wa Ng’hong’hona unabainisha kwamba aliyepewa zabuni ya kuzoa taka katika mtaa huo anazidiwa kutokana na uhaba wa vifaa vya kuzolea taka.

Mtaa wa Ng’hong’hona kata ya Ng’hong’hona: Picha ilipigwa Mei 3, 2026

Akizungumza na The Chanzo, Mwenyekiti wa Ng’hong’hona Charles Mnyamazi anasema mzabuni huyo  anatumia guta kuzoa kukusanya taka jambo ambalo anaona halikidhi mahitaji ya uondoaji taka katika mtaa wake.

“Hakidhi kwa kweli kutokana na hali halisi ya mtaa wetu,” anasema Mnyamazi.

Kuhusu suala la wakazi kukwepa kulipa tozo ya ukusanyaji taka kwa upande wake Mnyamazi anasema linasababishwa na baadhi ya wananchi kuishi kwa mazoea kwa sababu wapo pembezoni mwa jiji maeneo ambayo awali yalionekana kama ni vijiji.

“Kuna maeneo mengine wamelima basi unakuta hiyo hela anayoitoa inampa kero, anaamua kutupata taka kwenye mashamba,” amesmea Mnyamazi.

Changamoto hiyo anasema wanaendelea kukabiliana nayo huku akisisitiza lazima mtaa wao wapate mzabuni mwenye vifaa vya kutosha ili kupunguza changamoto ya taka waliyonayo sasa.

Kwa mujibu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma linakisiwa kuzalisha tani 350 za taka ngumu kwa siku, taka za nje ya mji zinazozalishwa ni tani 114 na taka za ndani ya mji wake uzalishaji wake ni tani 236. 

Wastani wa tani 150 pekee ndizo ambazo huondoshwa mjini kwa siku. Hii ni sawa na asilimia 66 tu.

Taka hizo zinazokusanywa husafirishwa moja kwa moja hadi dampo la Kisasa la Chidaya, ambalo lina ukubwa wa hekari 48. Wastani wa tani 120 -150 za taka ngumu hutupwa katika dampo hilo kutoka katika vyanzo mbalimbali vya uzalishaji taka.

Katika Mtaa wa Sechelela uliopo katika Kata ya Tambukareli umezungukwa na hoteli nyingi, taasisi za kiserikali na biashara nyingi zinazofanyika hapo. Katika mtaa huu, upande wa kulia inaonekana reli ya kati Dodoma huku upande wa kushoto ukionekana uwanja wa mpira.

Majira ya saa saba mchana mwandishi wa The Chanzo anakutana na Mamvula Matonya ,64, aliyevalia dera la maua ya rangi ya Chungwa. Kwa muonekano ni mfupi wa kimo na mwenye rangi ya maji ya kunde anaonekana akipita katikati ya taka zilizotupwa na zina harufu kali.

“Kama wananchi tunakerwa,” Mamvula Matonya anasema akionesha kukunja sura na kuendelea kusema, “wanachafua mazingira wanatudhalilisha wakazi wa eneo hili, hautelewi taka wanatupa wakati gani. Kuna muda unakuta kusafi, baada ya siku mbili, tatu ukipita unakuta mizigo ya taka utafikiri wametengeneza dampo la kuweka taka.”

Kaimu Mwenyekiti wa Mtaa wa Sechelela, Baraka Pangaselo anaweka wazi kuwepo kwa baadhi ya vijana waliowakamata ambao walikuwa na tabia ya kutupa taka kwenye eneo lisilo rasmi.

“Tuliona ule uchafuzi wa mazingira tukaweka doria kuweza kugundua kwamba ni akina nani wanaenda kuzimwaga zile taka,” anasema Baraka huku akiendelea, ”Kweli tuliwapata baadhi ya vijana ambao ambao walikiri kwamba taka zile huwa wanazibeba kwenye toroli kutoka kwenye makazi ya watu.”

SOMA ZAIDI: Upande wa Pili Usiozungumzwa wa Michezo ya Kubashiri ‘Kubeti’ Tanzania

Baraka anasema kuwa kuna mgomo kwa baadhi ya wananchi kutokulipa taka kwa magari yanayopita kukusanya. Mgomo huo unatokana na wazoaji wa taka kukaa muda kuchukua takataka.

“Sasa wanaanza kujiuliza wale watu wanawalipa pesa kwa kazi gani. Lakini wale wazoa taka walikiri kuna wakati gari linashindwa kupita njia za ndani, jambo linalopelekea taka kukaa kwa muda mrefu,” anasema Baraka.

Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Tanzania inaeleza kuwa Tanzania huzalisha zaidi ya tani milioni 17 za taka ngumu kila mwaka, asilimia 60 hadi 75 ya taka hizo hazikusanywi ipasavyo, hali inayosababisha uchafuzi mkubwa wa mazingira.

Katika Mtaa wa Chikole kata Msalato kila siku ya Jumamosi hufanyika mnada pembezoni mwa mnada huo zipo taka zilizotupwa katika eneo ambalo si rasmi.

Laban John ni mkazi wa Mtaa wa Chikole Kata ya Msalato yeye anaishi karibu na mnada jijini Dodoma akijihusisha na kilimo anasema, utupaji wa taka umekuwa ni kero katika mtaa huo.

“Tunaomba ikiwezekana jiji waweze kuchukua hizi taka na kupeleka sehemu nyingine ambazo ni nje ya mji,” anasema John.

Gideon Malyampa ni mfanyabiashara anayeishi Mtaa wa Chikole Kata ya Msalato anasema, baada ya kuwekwa mnada walitarajia kungewekwa vifaa vya kuhifadhi taka, jambo ambalo limekuwa gumu kutekelezeka.


“Utupaji taka hapa umekuwa endelevu na utolewaji wake ni mdogo sana. Sasa sisi tulikuwa tunashauri jiji kama kuna uwezekano waweke vihifadhia taka zaidi ya viwili,” anasema Malyampa.

Sheria ndogondogo

Sheria ndogo ya jiji la Dodoma ya Mwaka 2020, imeweka utaratibu wa kulipa viwango vya kulipa ada ya takataka. Kaya hutakiwa hulipa Shilingi Shilingi 5,000 kwa mwezi. Kwenye biashara za kawaida ni Shilingi 10,000 na kwenye maduka makubwa ni Shilingi 20,000 kwa mwezi.

Mbali na hilo, Jiji la Dodoma limekuwa likitutumia mifumo mbalimbali ya kuondosha taka moja ni mfumo wa wakandarasi wa kukusanya taka. Mwingine ni mfumo wa vikundi vya kijamii, ambavyo hukusanya taka maeneo ya pembezoni, kisha kuziweka kwenye kontena la kuhifadhia taka na hatimaye kusafirishwa hadi dampo la Chidaya.

Licha ya kuwepo kwa mifumo hiyo, Mkuu wa Kitendo cha Usafi na Udhibiti wa Taka Ngumu, Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro anasema baada ya Serikali kuhamia Dodoma ongezeko la watu limekuwa ni kubwa na hivyo uzalishaji wa taka nao umeongezeka.

“Kuna maeneo kwa kweli vikundi vimeshindwa, kwa maana hiyo uzalishaji umekuwa mkubwa kuliko uwezo wa vikundi kuweza kuondosha taka kwenye hayo maeneo,” anasema Kimaro.

“Tumeanza kuchukua hatua moja wapo, tunataka kamati za maendeleo zikae tuwajadili. Halafu baada ya hapo tunaviondosha tunaweka watu wenye uwezo,” 

Kimaro amesisitiza kuwa kila mwananchi anapaswa kujua kwamba ni lazima achangie ada ya takataka ili kuwezesha ukusanyaji taka katika maeneo yao kufanyika kwa ufanisi.

“Lakini ukienda kwenye Sheria ya Mazingira kuna Kanuni husema yule anayewajibika kuchafua mazingira anawajibika kuondosha taka,” anasisitiza Kimaro.

“Pale ambapo kwa kweli inabainika kuna mwananchi ametupa taka makusudi, anachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria za halmashauri za mwaka 2022, ambazo zinakataza kabisa mwananchi kutojihusisha na utupaji wa takakata.”

Wadau wa Mazingira

Festo Mugongo Mkurugenzi wa Taasisi ya API-CARE INTERNATIONAL ambayo inahusika na utunzaji wa mazingira na nyuki anasema muitikio wa watu kutoa ushirikiano wa fedha za kukusanya taka ni mdogo ikilingana na gharama ambazo jiji limetaka wachangie. 

“Wananchi wenyewe hawako tayari kuchangia, wanaona kama gharama ni kubwa, kwa hiyo wanajificha labda muda wa usiku wanawapa bodaboda hizo takataka kwenda kuzitupa,” anasema Festo.

SOMA ZAIDI: Wazazi Walalamikia Wanafunzi Kwenda Shule Wakati wa Likizo: ‘Mtoto Ana Maisha Zaidi ya Shule’

Anasema Mugongo huku akibanisha kwamba hata wakandarasi ambao hupita kwenye makazi ya watu kukusanya taka, hujikuta wakitoa huduma kubwa tofauti na kiwango cha fedha wanachopata. 

“Ile mitaa ambayo wamefanikiwa kudhibiti takataka kwa kiwango fulani wengi wao wananchi hawafuati zile gharama za jiji, wanatoa zaidi ya ile gharama za jiji,”

Joan Itanisa ni Mkuu wa Idara ya Mawasiliano kutoka Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira Ulimwenguni WWF anasema, suala la utupaji wa taka katika maeneo yasiyo rasmi ni tatizo kubwa nchini Tanzania linalochangiwa na vitu mbalimbali.

“Wakati mwingine unafika pahala unakuta hakuna sehemu maalum iliyotengwa ya kutupa uchafu,” Joan anaiambia The Chanzo huku akiendelea kusema, “unakuta mtu anashindwa kukaa na zile taka anaamua tu azitupe sehemu yoyote.”

Katika hali hiyo Joana anasema utupaji huo wa taka husababisha kuwa na miji ambayo si misafi jambo ambalo linapelekea hata hatari ya magonjwa yanayotokana na hali mbaya ya usafi wa mazingira.

Serikali yafafanua juu ya utaratibu

Mkurugenzi Msaidizi anayesimamia udhibiti na uchafuzi wa mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Thomas Chali anasema, Serikali inatekeleza Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Taka 2025-2030, wenye lengo la kuhimiza usimamizi endelevu wa taka ili kulinda afya ya binadamu, mazingira na kupunguza uzalishaji wa gesi joto unaotokana na uzalishaji wa taka. 

Anasema Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura ya 191 imetoa jukumu la usimamizi wa taka ngumu kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa, ambapo zina jukumu la kusimamia ukusanyaji wa taka katika maeneo ya mijini na pembezoni mwa miji na kuanzisha mfumo wa usafirishaji na utupaji salama wa taka.

“Kwa Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC, pia linahusika moja kwa moja kwa taasisi na kampuni binafsi ambao wanaonekana wanafanya uchafuzi wa mazingira kwa makusudi kinyume cha Sheria NEMC inawawajibisha,” anasema Chali

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana mkoani Dodoma. Unaweza kumpata kupitia jaquelinevictor88@gmail.com 

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×