The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Bongo Flava Miaka 30: Tulipotoka, Tulipo na Tunakoelekea

Kama maadhimisho haya yatafanyika kila mwaka, ni muhimu kuboresha namna kamati ya maandalizi inavyopanga na kutekeleza shughuli zake.

subscribe to our newsletter!

“Muziki asili yake wapi? Muziki ni wa nani?” aliwahi kuuliza marehemu Ramadhani Mtoro Ongala, maarufu kama Dk Remmy Ongala, mzaliwa wa Kindu, mashariki ya kati ya Kongo, sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, mwaka 1947. Yeye aliuliza maswali haya katika wimbo wake Muziki Asili Yake Wapi?, akiwa na bendi yake ya Orchestra Super Matimila. 

Wimbo huo ulirekodiwa kwa mara ya kwanza mwaka 1989 Radio Tanzania, Dar es Salaam au RTD, na baadae kurudiwa tena nchini Uingereza kwenye studio iitwayo Real World iliyopo katika mji wa Bristol, kijiji kinachoitwa Box. 

Walioshiriki ndani ya wimbo huo ni yeye mwenyewe Dk Remmy Ongala (Solo na Kuimba), Ayas Hassani (Rhythm), Haji Kisukari (Base), Lawrence Limbanga (Drums), Freddie Mwalasha (Sec Solo), na Kiniki Kieto (Vocal). 

Nimeyakumbuka maswali haya nilipokuwa nikitafakari kuhusu shamrashamra za miaka 30 ya Bongo Flava. Hii ni kwa sababu muziki wa dansi, au rhumba, ni sehemu ya chimbuko la muziki wa Bongo Flava kwani kabla ya hapo, muziki huo ulikuwa sehemu kubwa sana ya vijana wa wakati huo, hata watu wa umri wa kati ambao walihudhuria maonesho ya muziki wa bendi kama sehemu ya mapumziko, na starehe baada ya uchovu wa shughuli za kutwa nzima. 

Pamoja na wimbo huo kurekodiwa miaka zaidi ya 35 iliyopita, bado wimbo huu upo kwenye majukwaa ya kusikilizia muziki duniani na rekodi za watayarishaji na washiriki bado zipo. Hii ni tofauti na muziki wa Bongo Flava ambao bado uwekaji wa taarifa sahihi ni mgumu.

Bongo Flava

Muziki wa Bongo Flava ni mtindo wa muziki ulioanza kusikika mwishoni mwa miaka ya 1980 na mwanzoni mwa miaka ya 1990. Steji katika madisko mbalimbali hapa Dar es Salaam, Mbeya na Arusha na miji mingine mikubwa nchini ndipo mziki huu ulianzia, huku vijana wakirap kwa kukopi nyimbo za Marekani na baadaye kurekodi kwa lugha ya Kiswahili, nyimbo zilizotokana na utunzi wao wenyewe.

Taji George Liundi, maarufu kama Master  T, mtangazaji kijana aliyekuwa akihudumu Radio One Stereo wakati huo, ndiye mtangazaji kijana wa mwanzo kabisa miongoni mwa wanaotajwa kuubeba muziki huu. 

SOMA ZAIDI: Hadhi ya Ligi Yetu na Mizani ya Uadilifu: Tuendelee au Turekebishe?

Yeye alifanya hivyo kuupa nafasi kubwa ya kusikikika redioni, huku yeye akiwa DJ wa kipindi maarufu cha DJ Show ambacho kimsingi kilikuwa ni kipindi cha vijana kilichoteka nchi nzima, na pengine Afrika Mashariki, kilisikika pia online kupitia tovuti ya www.ippmedia.co.tz  

Liundi aliwahi kueleza katika mahojiano na Podcast ya #MezaHuru, nikiwa kati ya watu waliomuhoji, kwamba alianza kupiga nyimbo za wasanii wa muziki wa Bongo Flava mwaka 1994 wakati huo ukiitwa “muziki wa kizazi kipya,” ingawa alipewa dakika chache tu kufanya hivyo. Kwa hesabu yake, umri sahihi wa Bongo Flava ni zaidi ya miaka 32. 

Liundi amekaririwa mara kadhaa akisema kwamba enzi hizo muziki huu ulionekana kuwa ni wa kihuni, na ukabandikwa jina la “muziki wa kufokafoka.” Lakini upepo ulibadilika pale mtangazaji aliyepokea kijiti cha Taji “Master T” Liundi katika kipindi hicho cha DJ Show cha Radio One Stereo 99.6 FM wakati huo, Mike Pesambili Mhagama, aliyekuja na neno “Bongo Flava” akimaanisha “Ladha za Bongo.”  

Kwa sababu, kwa mujibu wa Mike, alikuwa katika kipindi chake akicheza nyimbo za maeneo mbalimbali duniani kama R&B, Hip Hop za Marekani au Reggae, na ilipofika zamu ya muziki huu wa kizazi kipya yeye aliipachika “session” hii ya muziki wa vijana wa Tanzania kama “Ladha za Bongo,” au kwa Kiingereza “Bongo Flavas,” kwani ulifanywa na wasanii wa hapahapa nyumbani Tanzania ambao ni vijana kwa kutumia lugha ya Kiswahili.

Safari ya Bongo Flava

Kabla Bongo Flava haijapata nafasi redioni na kuenea nchini, tasnia ya muziki ilitawaliwa na muziki wa bendi na Taarab zaidi kutoka maeneo ya mwambao. Vinara wa muziki huo walikuwa majirani zetu kutoka Kongo au Wakongo waishio nchini. 

Muziki kutoka nje ya nchi, hasa kutoka Ulaya na Marekani, nao ulikuwa maarufu sana kwa wakati huo kwani hata Radio One Stereo ilipoanza karibu asilimia 98 ilikuwa ikipiga muziki huo wa nje na huu muziki wa dansi, au wa nyumbani, ulipewa asilimia ndogo sana na huku muziki wa Taarabu kukatazwa kupigwa kabisa radioni.

Kazi kubwa ilifanyika kuhakikisha muziki huu wa Bongo Flava unapenya na kuenea nchini na hata nje licha ya vikwazo vingi kujitokeza. Teknolojia ilikuwa duni na vifaa vya kisasa vya kurekodi havikuwepo. Mfumo wa usambazaji wa kazi za sanaa haukuwa wazi wala rafiki, na uhifadhi wa kazi hizo ulikuwa mbovu. 

Pia, kulikuwa hakuna mikataba rasmi inayoeleza namna wasanii wanavyogawana mapato ya ubunifu wao na kwa kweli hata kinachoitwa Record Label kwa wakati huo.

Miaka 30 ya Bongo Flava

Miaka 30 na zaidi ni mingi na mambo mengi yamebadilika. Wazazi wengi waliokuwa wakiikataa sanaa kama kazi halali sasa hawashangai tena kuona watoto wao wakiacha ajira rasmi na kuingia kwenye sanaa. 

Sababu ni kwamba wapo wasanii, hata kama ni wachache, waliobadilisha maisha yao kupitia Bongo Flava na kubadiliasha mtazamo wa wazazi kuwa sanaa ni uhuni kwani sasa sanaa ya muziki ni ajira.

SOMA ZAIDI: Waandishi Bunifu Tanzania Tukisahaulika Sasa, Tutakumbukwa Lini? 

Teknolojia pia imebadilisha uzalishaji na usambazaji wa muziki. Wadau wanasema kwamba enzi hizo kurekodi wimbo mmoja lilikuwa zoezi gumu lililohitaji jitihada kubwa na muda mwingi lakini leo hii, kazi hiyo imekuwa rahisi maradufu. 

Matokeo yake ni kwamba watayarishaji, wasanii na wafanyabiashara katika tasnia wameongezeka, na tasnia yenyewe imekua na inalipa kama ajira rasmi. Pamoja na maboresho yatokanayo na teknolojia, kazi nyingi za watu zimepotea kwa kutokuhifadhiwa vyema na historia za watu muhimu katika ujenzi wa tasnia pia hazijulikani. 

Kwa sasa, bila uwepo wa wahusika ama watu wa karibu wa wahusika hao, ni ngumu kujua, mathalan, wimbo uliorekodiwa miaka 20 iliyopita ulifanyika katika studio gani, ama mtayarishaji alikuwa nani, ilhali nyimbo za mtu kama Dk Remmy kumbukumbu zake bado zipo.

Upekee mkubwa wa zama hizi unaonekana kwenye maisha ya wasanii. Angalau baadhi yao wana ahueni kubwa kimapato kuliko ilivyokuwa zamani, na jamii inashuhudia mabadiliko hayo. Hali hii ni tofauti na ile aliyoiimba II Proud wakati huo (Sasa Sugu au Taita) katika wimbo Hapo Zamani kutoka katika albamu ya Itikadi aliomshirikisha marehemu King Kiki.

Kasi ya teknolojia

Tasnia ya burudani inabadilika kwa kasi kubwa duniani kote. Teknolojia inakua haraka, na ladha za wasikilizaji zinabadilika vilevile. Kwa hiyo, wasanii wa Bongo Flava hawana budi kuchukua hatua madhubuti ili kwenda sambamba na mabadiliko haya. 

Wasipofanya hivyo, wanaweza kukumbwa na yaliyowakuta wanamuziki wa dansi na taarab. Wanamuziki hao walishindwa kwenda na kasi ya mabadiliko ya tasnia na mahitaji ya wasikilizaji wao.

Miaka ya karibuni, waandaaji kadhaa wamekuja na matamasha ya kuuenzi muziki wa Bongo Flava. Joseph Mbilinyi, ama SUGU kama anavyofahamika kisanii, ana jukwaa la “BongoFlava Honors” ambalo linakwenda na kauli mbiu ya “Heshima kwa Wakongwe,” huku Hamadi Said Juma, kwa jina la kisanii Madee, akiongoza tamasha maarufu kwa sasa kwa jina la “Miaka 30 ya Bongo Flava.”

Uendeshaji wa BongoFlava Honors ya SUGU ulianza kwa kufanya tamasha la msanii husika angalau mara moja kwa mwezi kwa muda kabla ya mabadiliko ambayo kwa sasa tamasha husika hufanyika kila baada ya miezi mitatu. 

BongoFlava Honors ina takribani miaka minne tangu kuanzishwa na inaendelea kufanya vyema katika eneo lake.

Mwaka huu wa 2026, tamasha la Miaka 30 ya Bongo Flava likazaliwa, mpaka makala hii inaandaliwa, tayari matamasha yameshafanyika Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza na Arusha na mipango inaendelea kwenda Zanzibar hapo katikati mwa mwezi Oktoba.

Shamrashamra za miaka 30 ya Bongo Flava zinaendelea. Maadhimisho haya ni zaidi ya kumbukumbu, kwani yamekuwa fursa kwa wasanii kujipatia kipato kupitia kazi zao za zamani na za sasa. 

Wadau wa muziki wanasema tunahitaji majukwaa mengi ya aina hii ili wasanii wetu wasije kuwa mfano mbaya wa tasnia isiyo na tija kwa nchi. Mashabiki wengi, mimi nikiwemo, wanasema ni vigumu kusema kwa uhakika kwamba Bongo Flava ina miaka 30 kamili, na huenda ina miaka zaidi ya hapo. 

Maeneo ya kuboresha

Lakini hiyo si hoja kubwa, ili mradi tumeamua kuupa muziki wetu siku ya kuzaliwa na kuuenzi. Yawe ni maadhimisho ya miaka 31 au mwendelezo wa miaka 30 katika mikoa mingine, yapo mambo matatu ambayo yakiangaliwa upya yanaweza kufanya tamasha na sherehe nzima kuwa tamu zaidi.

Kama maadhimisho haya yatafanyika kila mwaka, ni muhimu kuboresha namna kamati ya maandalizi inavyopanga na kutekeleza shughuli zake.

Mosi, kuna umuhimu mkubwa wa kuwashirikisha zaidi waasisi, au nguli, walioubeba muziki huu tangu uchanga wake kufikia hapa ulipo. Bado kuna sura kadhaa ambazo hazijaonekana katika matamasha haya. 

SOMA ZAIDI: Ukiwa Mzembe, Vyombo vya Habari Vitakulisha ‘Matango Pori.’ Udadisi Utakusaidia Kulikwepa Hilo  

Ingependeza ushiriki wa watangazaji vinara kama Taji “Master T” Liundi na Mike Mhagama kama washereheshaji wakuu wa tamasha hili kama njia ya kuthamini mchango wao kwenye muziki huu.

Naelewa kwamba huenda kwa sababu za kimaslahi au za kiitikadi, kuna baadhi ya wasanii, ama wachonga barabara wa tasnia yetu, wameshindwa kuwepo katika maadhimisho haya, hivyo ni muhimu kwa waandaji kutafuta msingi wa pamoja ili maadhimisho yawe na maana zaidi. 

Ukweli ni kwamba kutokuwepo kwa baadhi ya wasanii au watayarishaji kunawanyima wakongwe hawa haki yao ya kutambuliwa na kujisikia kama sehemu ya muziki huu toka hapo mwanzo kabisa.

Pili, ubora wa maonesho na idadi ya wasanii ni jambo jingine linalopaswa kuzingatiwa. Hapa kuna mambo mawili, ikiwemo lile linalohusu ubora. Katika zama hizi za teknolojia iliyoendelea sana, ni uvivu kuwa na wasanii wasioweza kutumbuiza mubashara. Jukwaa lingependeza zaidi likijaa vyombo na ala mbalimbali, huku wasanii wakionesha ujuzi wao kwa kutumbuiza na “live” band badala ya “Playback.”

Pia, idadi na uteuzi wa wasanii. Inapunguza ladha kuwa na wasanii wengi ambao kila mmoja anaimba nyimbo mbili au tatu tu. Ingekuwa bora kuwa na wasanii wachache, waliochaguliwa kwa kuzingatia kanda walizofanya vizuri zaidi, na kupewa muda wa kutosha kuburudisha.

Tatu, ni hitaji la kuunganisha vizazi – vipya na vya zamani – ili kuleta burudani zaidi. Ingependeza pia kuwe na uwakilishi wa wasanii wa sasa, kama daraja kati ya kizazi kile na kizazi hiki. Kwa mfano, wasanii wa leo wangeweza kupewa nafasi maalum ili kuleta uwiano kati ya wakongwe na vijana.

Tunahitaji majukwaa mengi zaidi kama BongoFlava Honors na Miaka 30 ya BongoFlava ili kuwawezesha wakongwe kuendelea kutupa burudani na kuwaweka katika kumbukumbu. 

Wasanii wakongwe katika mahojiano kadhaa wamekiri kwamba matamasha haya yamewarudisha “kwenye ramani” na kuwawezesha kupata kipato. Maboresho yatazidisha faida hizi maradufu, kwa wasanii na sisi mashabiki.

Moruo King ni mpenzi na shabiki mkubwa wa muziki na michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia mtandao wa X @Moruoking au baruapepe mklomayani@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi. 

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×