Dodoma – Kwa Marietha Jonas, miaka 24, kwenda hospitalini kutafuta matibabu si jambo rahisi. Mbali na kusubiri kwa muda mrefu, anakabiliwa na changamoto ya kueleza hali yake kwa wahudumu wa afya kutokana na ukosefu wa wakalimani wa lugha ya alama katika vituo vingi vya kutolea huduma za afya.
Marietha, ambaye ni mjasiriamali, alipoteza uwezo wa kusikia akiwa na umri wa miaka minne. Anasema mara kadhaa amejikuta akihisi kutengwa anapokwenda hospitalini, hasa anapoona wagonjwa wengine wanaweza kuwasiliana na wahudumu wa afya kwa urahisi huku yeye akishindwa kueleza mahitaji yake.
“Nilikaa muda mrefu kusubiri zamu yangu, lakini waliokuwa wanasikia walikuwa wanaingia na kutoka. Nilijihisi labda mimi si binadamu,” anasema Marietha katika mahojiano na The Chanzo.
Kwa mujibu wake, changamoto hiyo haiishii katika kuchelewa kupata huduma, bali inaweza kusababisha mgonjwa kutofanyiwa vipimo vinavyostahili au kupewa matibabu yasiyoendana na hali yake.
“Unapofika hospitalini na kuzungumza na daktari, hamuelewani. Kuna wakati hupati huduma au unapata huduma isiyostahili. Ili upate vipimo sahihi, ni lazima uwe na mkalimani anayeweza kukusaidia kuwasiliana na kupata huduma inayofaa,” anasema.
Uzoefu wa Marietha unaakisi changamoto inayowakabili watu wenye ulemavu wa kusikia nchini Tanzania, ambao licha ya kuwa na haki ya kupata huduma za afya bila ubaguzi, bado wanakumbana na vikwazo vya mawasiliano vinavyoweza kuhatarisha afya na maisha yao.
Kifungu cha 26(1) na (2) cha Sheria ya Watu wenye Ulemavu Na. 9 ya mwaka 2010 kinatambua haki ya watu wenye ulemavu kupata huduma bora za afya bila ubaguzi na kinazitaka taasisi za afya kuchukua hatua zinazofaa kuhakikisha huduma hizo zinapatikana.
Hata hivyo, kwa baadhi ya viziwi, utekelezaji wa haki hiyo bado ni changamoto.
Ally Jumanne Malacha, miaka 40, dereva wa bodaboda, mwenye usikivu hafifu, alipoteza uwezo wa kusikia vizuri akiwa na umri wa miaka sita baada ya kuugua malaria. Anasema alipopelekwa hospitalini na kuchomwa sindano ya dawa ya Kwinini, alipoteza kabisa uwezo wa kusikia.
Ally anasema anapokwenda hospitalini, mara nyingi hukumbana na kutoelewana na madaktari anapojaribu kueleza hali yake.
“Ukimuambia daktari kwamba husikii vizuri, anakuuliza, ‘Mbona nimeongea na unasikia?’ Wakati mwingine anaanza kugonga meza na kukushutumu kuwa unajifanya,” anasema.
“Nabaki namuangalia tu kwa sababu hajui kwamba tatizo lipo ndani ya mwili wangu.”
Kwa Ally, uwepo wa wakalimani ni muhimu, lakini anaamini pia kuwa madaktari wanapaswa kujifunza lugha ya alama ili kurahisisha mawasiliano na kulinda siri za wagonjwa.
SOMA ZAIDI: Mfumo wa Haki Jinai Tanzania Unawaangusha Walemavu wa Akili
Anatoa mfano wa mtu anayekwenda kupima virusi vya UKIMWI, akisema kulazimika kumtafuta mkalimani kunaweza kuathiri faragha ya mgonjwa.
“Unakuta kiziwi anaenda kupima UKIMWI, lakini anahitaji kutafuta mkalimani. Mkalimani anapoanza kutafsiri, maana yake siri ya mgonjwa inakuwa inajulikana kwa mtu mwingine,” anasema.
Ally pia anasikitishwa na mitazamo hasi ya baadhi ya watu kuhusu lugha ya alama, akisema wengine hudhani lugha hiyo inatumiwa na watu wenye matatizo ya akili.
“Lugha yangu imeonekana kama imetengwa. Mimi ninatumia lugha ya alama; nisipoweza kuwasiliana na wewe, nitawezaje kupata huduma? Kiziwi asipokuwa na mawasiliano mazuri hospitalini ananyimwa haki yake ya kupata huduma,” anasema.
Takwimu zilizotajwa kutoka Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 zinaonyesha kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma ina watu takribani 11,500 hadi 13,000 wenye ulemavu wa kusikia.
Aidha, ripoti ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ya mwaka 2025 kuhusu haki ya uhai na afya kwa makundi maalumu inaeleza kuwa viziwi wanakabiliwa na hatari ya kufa iliyo mara mbili zaidi wanapofikishwa hospitalini wakiwa katika hali mahututi, ikilinganishwa na watu wanaosikia.
Kwa Emmanuel Ntandu, miaka 40, mjasiriamali na baba wa watoto wawili, ukosefu wa wakalimani umemlazimu kutumia njia mbadala ili kueleza matatizo yake ya kiafya.
Anasema wakati mwingine hulazimika kuandika dalili zake kwenye karatasi ili daktari aweze kumwelewa.
“Viziwi tunapata shida sana. Tunatamani Serikali iweke wakalimani hospitalini, lakini bado upatikanaji wao ni changamoto,” anasema Emmanuel alipokuwa katika Kanisa la Bethel Baptist Deaf Church of Tanzania, lililopo Nkuhungu, Dodoma.
Hata hivyo, kuwasiliana kwa maandishi si suluhisho la uhakika kwa kila mgonjwa, hasa pale maandishi yanapokuwa magumu kusomeka au mgonjwa anapohitaji kueleza dalili kwa undani.
Yusuph Mloli, miaka 46, Mwenyekiti wa Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA), tawi la Mkoa wa Dodoma, ambaye pia ni mwalimu wa watoto wenye mahitaji maalumu, anakumbuka alivyokwenda katika hospitali binafsi akiwa na mkalimani wake, lakini daktari akamtaka mkalimani atoke nje.
Daktari alimwelekeza awasiliane kwa maandishi, lakini walishindwa kuelewana na hivyo Mloli akaondoka bila kupata huduma siku hiyo.
“Tulishindwa kuelewana, nikaenda hospitali nyingine na siku hiyo sikupata huduma,” anasema, akiwataka madaktari kujifunza lugha ya alama na kuboresha njia za mawasiliano na wagonjwa.
Changamoto nyingine ni namna watu waliofunzwa lugha ya alama wanavyotumika katika taasisi mbalimbali. Mazengo Wilium, Mwenyekiti Mstaafu wa CHAVITA Mkoa wa Dodoma, anasema baadhi ya taasisi zimefadhili mafunzo ya lugha ya alama, lakini wahitimu hawabaki katika maeneo ambayo wanahitajika kutoa huduma.
Anazitaja taasisi zilizowahi kutoa mafunzo hayo kuwa ni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ambako takribani watu 10 walipata mafunzo; Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, watu takribani 20; na Hospitali ya Benjamin Mkapa, takribani watu watano.
Mazengo anasema Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma ilikuwa na wakalimani waliowarahisishia viziwi kupata huduma, lakini hali ilibadilika baada ya baadhi ya wafanyakazi kuondolewa katika zoezi la kushughulikia wafanyakazi hewa.
SOMA ZAIDI: Sababu Zinazowanyima Watu Wenye Ulemavu Haki za Kidijitali Tanzania Zatajwa
“Tangu wakati huo, hakuna anayejua lugha ya alama. Kiziwi akifika mapokezi anakwama kwa sababu hakuna mtoa huduma anayeweza kuwasiliana naye kwa lugha hiyo,” anasema.
Athari za changamoto hiyo zinaweza kuwa kubwa zaidi kwa wanawake wanaohitaji huduma za uzazi.
Nassriya Ally, Mbunge wa Viti Maalumu anayewakilisha watu wenye ulemavu Tanzania Bara na Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi(CCM), anasema mawasiliano duni yanaweza kusababisha wahudumu kutafsiri vibaya dalili za mgonjwa na kutoa matibabu yasiyofaa.
Anatoa mfano wa mwanamke aliyemtaja kwa jina moja la Joyce, mkazi wa Tabata, Dar es Salaam, ambaye aliripotiwa kupoteza mtoto baada ya kutokea changamoto ya mawasiliano wakati wa kupata huduma za uzazi.
“Alikuwa na shida ya uzazi, lakini nesi alielewa tofauti. Matokeo yake mtoto alizaliwa akiwa amefariki. Nilipokutana naye aliniomba niongozane naye hospitalini kwa sababu ninaweza kuzungumza naye na akanielewa,” anasema Nassriya.
Kwa mujibu wa Nassriya, Joyce alipata matibabu na kupona, akapata ujauzito mwingine na sasa ana mtoto mwenye umri wa miaka sita.
Anasema viziwi pia hukosa taarifa muhimu za afya zinazotolewa kupitia televisheni katika vituo vya afya, ikiwemo elimu ya afya ya uzazi. Wakati wa janga la COVID-19, anasema, ukosefu wa wakalimani uliwafanya wengi kupata ugumu wa kuelewa taarifa muhimu za afya.
Mchungaji Kalebi Muhawi, Mwenyekiti wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu Dodoma (CHAWATA), anasema kulazimika kutafuta mkalimani binafsi kunaweza kuathiri usiri wa mgonjwa na kuwafanya baadhi ya viziwi kukosa ujasiri wa kwenda hospitalini.
Anashauri taasisi zote zinazotoa huduma kwa umma kuweka mifumo ya mafunzo ya lugha ya alama ili wafanyakazi waweze kuwahudumia viziwi bila vikwazo vya mawasiliano.
Justus Ng’wantalima, Katibu wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu (SHIVYAWATA), Mkoa wa Dodoma, anasema baadhi ya viziwi wamekuwa wakiepuka kwenda hospitalini kwa sababu wanatarajia kupoteza muda wakitafuta mtu wa kuwasaidia kuwasiliana.
Anaitaka Serikali kuhakikisha wakalimani wanapatikana katika hospitali na vituo vya afya ili kundi hilo lipate huduma kwa wakati na kwa usiri unaostahili.
Kwa upande wake, Daktari Edmond Mgeni, Mkuu wa Kitengo cha Kusimamia Ubora wa Huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, anakiri kuwa idadi ya wataalamu wa lugha ya alama haitoshelezi mahitaji.
“Huduma hiyo tunayo, lakini wataalamu ni wachache. Mpango wetu ni kuendelea kuwajengea uwezo wataalamu wengine kupitia mafunzo ili waweze kusaidia, kwa sababu wateja ni wengi,” anasema.
Anasisitiza kuwa hospitali zinahitaji kuongezewa wataalamu ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wagonjwa wenye ulemavu wa kusikia.
Aisha Msantu, Mbunge wa Viti Maalumu na Mkurugenzi wa Shirika la Glaring Future Foundation (GFF), linalosaidia makundi maalumu yakiwemo watoto, vijana na watu wenye ulemavu, anasema ukosefu wa ajira kwa waliofunzwa lugha ya alama ni sehemu ya tatizo.
Anasema wengi wa waliofunzwa lugha hiyo wameelekezwa katika ualimu, huku nafasi za ajira katika sekta nyingine zikiwa chache.
Aisha anaitaka Serikali kutenga nafasi za ajira kwa wataalamu wa lugha ya alama katika kada za afya na maeneo mengine yanayotoa huduma kwa umma.
SOMA ZAIDI: ‘Nimeamua Kuacha Kesi, Nibaki na Binti Yangu’: Masaibu ya Waathirika wa Udhalilishaji Walemavu Zanzibar
Serikali imewahi kueleza hatua zinazochukuliwa kuendeleza taaluma hiyo. Juni 2, 2025, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma, aliliambia Bunge kuwa wakalimani 300 wa lugha ya alama walikuwa wamejisajili katika kanzidata ya taifa ya wakalimani.
Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Stella Ikupa, kuhusu mkakati wa kuifanya lugha ya alama kuwa lugha rasmi ya mawasiliano, Mwinjuma alisema Serikali inatambua umuhimu wa lugha hiyo katika mawasiliano ya watu wenye changamoto za usikivu.
Alisema Serikali imeandaa muundo wa utumishi wa kada hiyo na inapanga kuimarisha mafunzo ili wakalimani wawe na weledi unaowawezesha kufanya kazi ndani na nje ya nchi. Pia, waliohitimu na kukidhi vigezo wanatarajiwa kuwezeshwa kujifunza lugha ya alama ya kimataifa.
Jackline Kuwanda ni mwandishi mwandamizi wa habari wa The Chanzo, aliyepo mkoani Dodoma. Anaweza kupatikana kupitia jaquelinevictor88@gmail.com.