Dodoma. Kamati ya Kudumu ya Bunge, Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) imekamilisha mchakato wa kupokea maoni ya wadau kuhusu Muswada wa Sheria ya Uwekezaji wa Umma ya mwaka 2023 siku ya Jumatano, Januari 10, 2023.
Muswada wa Sheria ya Uwekezaji wa Umma ulisomwa kwa mara ya kwanza Bungeni Novemba 10, 2023 ambapo Disemba 18, 2023 Ofisi za Bunge zilitangaza kuanza kwa zoezi la kupokea maoni ya wadau juu ya muswada huo.
Akiongea na waandishi wa habari jijini Dodoma, Mwenyekiti wa PIC, Deus Clement Sangu alisema, kusudio la muswada huo ni kwenda kufanya marekebisho makubwa kwenye Ofisi ya Msajili wa Hazina ambayo ndiyo inasimamia mashirika hayo.
“Kwa muda mrefu tangu kuanzishwa kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina kumekuwa na ombwe kwenye uendeshaji wa mashirika ya umma” alisema Sangu ambaye pia ni Mbunge wa Kwela.
SOMA ZAIDI: Serikali Yafuta Mashirika Manne,16 Yaunganishwa.Yawatoa Hofu Watumishi
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Msajili wa Hazina mpaka kufikia mwezi Juni mwaka 2023 kuna mashirika ya umma 304 yenye uwekezaji wa trilioni 76.8 ambayo yapo chini ya Ofisi hiyo.
Kulingana na takwimu hizo, Mwenyekiti wa PIC alisema tija iliyotegemewa kutokana na uwekezaji wa mashirika hayo bado ipo chini kutokana na mfumo mzima wa uendeshaji wa mashirika hayo.
“Matarajio ya Watanzania ni kuona uwekezaji wa namna hii unakuwa na tija kwenye maeneo mbalimbali,” alisema Sangu. “Kwanza, unakuwa kichocheo cha uchumi sababu Serikali ni mwekezaji anayeweza kuonesha uelekeo kwa wawekezaji wengi”
Mabadiliko Ofisi ya Msajili wa Hazina
Mabadiliko makubwa yanayotajwa katika Muswada huo ni kuanzishwa kwa Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma ambayo itakwenda kusimamia masuala yote ya uwekezaji ya Serikali ikiwemo mashirika ya umma.
SOMA ZAIDI: Tukitaka Maendeleo, Hatuwezi Kukwepa Uwekezaji Mkubwa Kwenye Tafiti
“Marekebisho mawili ambayo yanaenda kutokea kwenye muswada huu endapo Bunge litaridhia na kuupitisha tunaenda kufuta Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa maana ya majukumu,” alisema Sangu.
Majukumu hayo yataamishiwa kwa Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma ambayo itakuwa na majukumu mbalimbali ikiwemo kutoa ushauri kwa Serikali kuhusu uanzishaji au ufutaji wa mashirika ya umma na umilikishwaji wa biashara au mali yoyote katika mashirika ya umma.
Mamlaka pia itakuwa na jukumu la kufanya mapitio ya utendaji wa kifedha wa mashirika ya umma kwa lengo la kubaini mahitaji na kupendekeza kwa Kamati ya Uongozi njia bora za uwezeshaji wa kifedha.
Majukumu mengine ni pamoja na kufanya tathmini ya utendaji na ufanisi wa vyombo vya usimamizi vya mashirika ya umma na kupendekeza kwa Serikali hatua za kurekebisha au kuboresha kwa lengo la kuhakikisha matumizi sahihi ya fedha na mali za mashirika ya umma.
Pamoja na kuanzishwa kwa Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma pia Mfuko wa Uwekezaji wa Umma ambao unakusudiwa kuwa chanzo cha uhakika cha kugharamia uwekezaji mbalimbali unaofanywa na Serikali, kukwamua na kuwezesha mashirika ya umma yenye ukosefu wa mitaji na kugharamia uendeshaji wa Mamlaka.
“Ni jambo muhimu sana,”alisema. “Nchi zilizofanya kuwa na Mfuko wa Uwekezaji zimekuwa na ufanisi mkubwa sana. Muswada ukifanikiwa kupitia utakwenda kubadilisha utendaji,” alisisitiza Sangu.
SOMA ZAIDI: Je, Miswada Mipya ya Sheria za Uchaguzi Imekidhi Matarajio ya Wananchi?
Maoni ya wadau kuzingatiwa
Katika taarifa yake Mwenyekiti wa PIC amesema kamati yake imepokea zaidi ya maoni 50 ya wadau mbalimbali kwa lengo la kuboresha muswada huo.
“Wote kwa ujumla wake wamekuja na maoni ya kujenga,” alisema Sangu. “Sikuona mtu ambaye anasema hili jambo halifai. Kila mtu amekuja na mawazo ya kujenga, zaidi ilikuwa ni kupunguza na kuongeza kadiri muswada ulivyoletwa na Serikali.”
Hatua inayofuata sasa kwa kamati hii ni kwenda kuchakata maoni hayo na watakapokamilisha watatakiwa kuyawasilisha Bungeni.
Kiu ya Kuongeza Tija Kwenye Mashirika ya Umma
Chimbuko la mabadiliko haya, ni kiu ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akisisitiza mara kwa mara haja ya kufanya maboresho katika uendeshaji wa mashirika ya umma ili yawe ufanisi na tija.
Mwezi Julai mwaka jana wakati akifungua kikao kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Mashirika ya Umma, Hassan alisema, taasisi na mashirika mengi yamekuwa mzigo na tegemezi kwa Serikali na hivyo kunahitajika jitihada ya kubadili hali hiyo.
“Mashirika yaendeshwe kimashirika, tuache kuyaingilia kisiasa,” alisema Rais Samia. “Kama shirika ni la huduma litoe huduma. Kama shirika ni la biashara lifanye biashara”
Katika kufanya mabadiliko kwenye mashirika ya umma, ukiachana na muswada huu wa Sheria, Rais Samia hivi karibuni aliridhia mapendekezo ya Wizara ya Mipango na Uwekezaji ya kufuta na kuunganisha baadhi ya taasisi na Mashirika ya Umma.
Hatua hiyo ilitokana na mashirika na taasisi hizo kuingiliana na kushabihiana majukumu, hivyo kwa kitendo cha kuyaunganisha kinatajwa kitapunguzia Serikali gharama za uendeshaji na kuongeza ufanisi wa kiutendaji.
Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana mkoani Dodoma. Unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com