The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Je, Miswada Mipya ya Sheria za Uchaguzi Imekidhi Matarajio ya Wananchi?

Wakati inafurahisha kuona Serikali ikitimiza ahadi yake, miswada hii inahitaji marekebisho makubwa kukidhi kiu ya Watanzania.

subscribe to our newsletter!

Nimeipitia miswada yote mitano iliyowasilishwa Bungeni mnamo Novemba 10, 2023, kwa hisia mchanganyiko.

Kwanza, nimefarijika sana kwamba Serikali imetimiza ahadi yake ya kuleta miswada ya sheria kurekebisha sheria zinazohusu uchaguzi Tanzania kwa lengo la kupunguza malalamiko ya kutotendeka haki katika uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa, 2024 na Uchaguzi Mkuu, 2025. 

Ilipotolewa ahadi ya kuletwa miswada hiyo ya sheria, wadau wengi wa masuala ya siasa waliisubiri kwa hamu, huku wakieleza matarajio yao kuwa miswada hiyo ingejibu kiu ya muda mrefu ya kutaka kuwepo kwa mfumo unaotenda haki kwa kila Mtanzania wakati wa uchaguzi. 

Aidha, kwa sababu ambazo imeziona ni muhimu, Serikali imejiongeza na kuleta muswada unaoanzisha Sheria ya Uwekezaji wa Umma wa mwaka 2023 na pia Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali.

Hatimaye, Serikali imewasilisha jumla ya miswada mitano ya sheria bungeni. Kati yake, miswada mitatu ni mahsusi kwa masuala ya uchaguzi. Hapa kuna muswada mahsusi wa kuboresha masuala ya uratibu wa siasa za vyama vingi nchini na pia sheria zinazolenga kuimarisha mfumo wa usimamizi wa uchaguzi nchini. 

Nimefarijika sana

Kwa ujumla, mimi binafsi, kama walivyo Watanzania wengi, nimefarijika sana na kutimizwa kwa ahadi ya Serikali kukamilisha miswada hiyo na kuisoma Bungeni kwa mara ya kwanza.

SOMA ZAIDI: Uchaguzi Umekuwa Kichocheo Kikubwa cha Marekebisho ya Katiba Tanzania

Kwa desturi yetu ya utungaji sheria, miswada hii kwa sasa iko mikononi mwa Bunge la Tanzania na itasubiri utaratibu wa Kamati husika za Bunge – kutegemeana na miswada yenyewe – kuweza kuwaita wadau mahsusi kwa ajili ya kupokea maoni ya wananchi kuhusu maudhui ya miswada hiyo.

Kwa hakika, Bunge litakapoukaribisha umma kutoa maoni nitaweza kupeleka maoni yangu kuhusu miswada mitatu kwa kufika mwenyewe Dodoma, au hata kwa mtandao, kwa vile nina maoni mengi ambayo nimekuwa nayo kutokana na michakato ambayo nimeiratibu na kuiwezesha kwa miaka zaidi ya kumi sasa.

Miswada mitatu inayohusiana na uchaguzi iliyosomwa Bungeni ni pamoja na muswada wa sheria mpya inayoanzisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi inayopendekezwa kuitwa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Mwaka 2023.

Muswada mwingine ni ule wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, 2023 na Muswada wa Marekebisho ya Sheria zinazohusu Masuala ya Vyama vya Siasa, 2023, ambao umelenga kurekebisha baadhi ya vifungu vya Sheria ya Gharama za Uchaguzi, Sura ya 278 na Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258. 

Sheria ya Gharama za Uchaguzi ilitungwa mwaka 2010 kwa lengo la kudhibiti kufuru ya matumizi katika uchaguzi lakini wadau wanaona kuwa imeshindwa kutekelezwa kwa kiwango kilichokusudiwa. 

SOMA ZAIDI: Tumechelewa Kupata Katiba Mpya Kabla ya Uchaguzi, Basi Tuboreshe Hii Iliyopo

Kwa upande wake, Sheria ya Vyama vya Siasa, iliyotungwa kwa mara ya kwanza wakati wa kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992, pamoja na marekebisho yake kadhaa, ikiwemo marekebisho makubwa ya mwaka 2019, bado inalalamikiwa kwa udhaifu wa kushindwa kuvinyoosha vyama vya siasa katika mstari wa demokrasia ya vyama vingi nchini.

Umuhimu wa jina

Kwa upande wa Sheria Mpya ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Serikali imesita kuichagulia tume hiyo jina pendwa walitakalo wadau, ambalo ni Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi. 

Kwangu mimi, jina kamili la sheria hii linapaswa liwe ni Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya mwaka 2023. Aidha, kifungu cha kwanza cha sheria hiyo kinaeleza kuwa sheria hiyo itaanza kutumika katika tarehe ambayo waziri ataiteua. 

Hilo nalo ni jambo linalolalamikiwa kwa vile kumekuwa na ucheleweshaji wa mawaziri kuteua na kutangaza tarehe ya kuanza kutumika kwa baadhi ya sheria ambazo, kwa sababu moja au nyingine, Serikali haina haraka nazo. 

Kwa mfano, waziri mwenye dhamana ya Katiba na Sheria hajaweza kuteua na kutangaza tarehe ya kuanza matumizi ya Sheria ya Haki ya Kupata Taarifa ya mwaka 2016 ambayo Bunge liliipitisha miaka saba iliyopita sambamba na Sheria ya Huduma za Habari ambayo matumizi yake yalianza mara moja baada ya Rais John Pombe Magufuli kuitia saini.

SOMA ZAIDI: Yanayokera Kuhusu Katiba ya 1977 na Haja Yakuwa na Katiba Mpya Sasa

Kwa maoni ya wengi, sheria hii mpya ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imesubiriwa kwa miaka mingi sana na utekelezaji wake itafaa uanze mara tu baada ya Bunge kuipitisha mwakani 2024 na Rais kuitia saini.

Kwa sababu hiyo, napendekeza kuwa kifungu cha kwanza cha sheria hii kisomeke kuhusu kuanza kutumika kuwa sheria hii itaanza kutumika siku 30 tangu tarehe ya kusainiwa na Rais.

Muundo wa Tume

Sheria ya Taifa ya Uchaguzi ilitarajiwa ilete mageuzi kadhaa katika muundo na uhuru wa Tume ya Uchaguzi hapa Tanzania. Kwa mfano, muundo wa tume unapaswa kuwa ni ule unaoifanya iwe huru kiasi cha kutopokea maelekezo, au kuingiliwa na mtu, chombo au mamlaka yoyote. 

Juhudi zimefanywa kuongeza kiwango cha uhuru wa tume kisheria, kimajukumu na kibajeti. 

Kwa mfano, kifungu cha 6(1) kinaitamka bayana tume kama chombo huru kinachojitegemea na ambacho maamuzi yake hayataingiliwa na mamlaka, au kulazimika kufuata maagizo ya mtu yeyote, au idara yoyote ya Serikali, au maoni ya chama chochote cha siasa. 

SOMA ZAIDI: Mambo Muhimu Ukamilishaji wa Mchakato wa Katiba Tanzania

Hili ni jambo zuri sana kuliweka katika sheria. Aidha, muswada umejibu kiu ya Watanzania kutaka tume iwe na uwezo wa kushtakiwa endapo kutakuwa na haja ya kufanya hivyo. 

Katika kifungu cha 6(2)(b), tume itakuwa na uwezo wa kushtaki au kushtakiwa. Hii inaondoa kinga ya kisheria na kikatiba iliyokuwa imewekwa juu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kiasi cha kuifanya kujiona ipo juu ya sheria.

Upatikanaji wa wajumbe

Ni jambo ninaloliona jema pia kuwa, kwa mara ya kwanza, wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi watapatikana kwa kuomba wenyewe na kusailiwa na Kamati Maalum ya Usaili kwa kuzingatia sifa. Jambo hili lilisubiriwa sana!

Kifungu cha 9(1) kinatamka wazi kuwa wakati wote inapobidi kuteuliwa wajumbe wa tume, kamati ya usaili itaitishwa kwa kazi hiyo. Aidha, baada ya usaili, Muswada unapendekeza kuwa Kamati ya Usaili itawasilisha kwa Rais majina manne zaidi ya nafasi zinazohitajika kujazwa kwa ajili ya uteuzi.

Kwa masharti ya kifungu cha 10(2), Rais atalazimika kuteua wajumbe wa tume kutoka miongoni mwa majina yaliyowasilishwa kwake na Kamati ya Usaili. Kwa bahati mbaya, sharti hili halimbani Rais katika kuteua Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.

SOMA ZAIDI: Malipo ya Wenza wa Viongozi Yatakiuka Katiba, Kuathiri Ujamhuri wa Taifa

Hapa pana tatizo. Maoni yangu ni kuwa, Rais asiteue kabisa Mwenyekiti na Makamu wake bali ateue wajumbe saba wa tume ambao watakapokutana kwa mara ya kwanza baada ya kuapishwa watachagua Mwenyekiti na Makamu wao kwa kuzingatia Masharti ya Katiba na Sheria hii. 

Kanuni ya Uhuru wa Tume ya Uchaguzi inataka Rais asiwe na mamlaka ya kuamua nani aiongoze tume ili kuepuka hisia kuwa ataendelea kuwapa maelekezo hata baada ya kuwateua.

Sambamba na kutowateua wajumbe wa Tume ya Uchaguzi na Mkurugenzi wa Tume, Rais pia hapaswi kuwa na uwezo wa kuwaondoa kazini. 

Utaratibu wa Kimahakama

Kwa maoni yangu, kifungu cha 8(2)(e) kinachoweka uwezekano wa Rais kumuondoa kazini mjumbe wa tume kutokana na kupoteza uwezo wa kufanya kazi, tabia mbaya au kupoteza sifa ya kuteuliwa kuwa mjumbe ni kifungu kibaya kinachoweza kuleta hofu kwa wajumbe dhidi ya matamko ya kisiasa ya Rais kabla, wakati, na baada ya uchaguzi. 

Utaratibu mzuri ni ule uliopo kikatiba wa kunidhamisha majaji ambapo Ibara ya 110A ya Katiba inasema kuwa Jaji wa Mahakama Kuu hawezi kuondolewa kazini isipokuwa tu kwa sababu ya kushindwa kutekeleza majukumu yake kutokana na maradhi au tabia mbaya inayoathiri maadili ya kazi yake na ambapo kabla ya kufikia kuondolewa kazini itateuliwa tume, ikihusisha majaji kutoka nchi nyingine za Jumuiya ya Madola kuchunguza tuhuma zinazomkabili.

SOMA ZAIDI: Nia Ovu ya Wanasiasa Yahatarisha Kuwanyima Watanzania Katiba Mpya

Utaratibu huo unaweka kinga katika ajira za majaji na kuhakikisha haki inatendeka pale anapotokea kulalamikiwa na itafaa utaratibu kama huu uwekwe katika kushughulikia ajira na nidhamu ya wajumbe wa tume.

Kwa ujumla, ni mambo gani mengine yanapaswa kurekebishwa katika muswada mpya wa Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi? 

Je, vipi kuhusu miswada mingine miwili ya uchaguzi iliyosalia? Na mbona muswada wa mabadiliko madogo katika Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977, ambao nao ulitarajiwa, haupo mezani? 

Je, vipi kuhusu miswada ya kuhuisha Mchakato wa Katiba Mpya? Fuatilia makala zijazo kwa haya na mengineyo!

Deus Kibamba ni mtafiti anayefundisha utatuzi wa migogoro na uendeshaji wa mazungumzo ya amani katika Chuo cha Diplomasia. Anapatikana kupitia +255 788 758581 na dkibamba1@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Hao atakao wateuuwa mama samia uhuru wata kosa mana ugali kawapa yeye na yeye ndiye mgombea urais pia ana zingua bado hapo ndipo vituko vipo bado.nivilevile tuu. Bunge lingefanya kazi hiyo hakuna haki hapo uhuru haupo hapo walio teuliwa wana uhuru gani hapo lazima tuu michango iwepo kwa watakao teuliwa. pia mahama Inge husika kwenye maamuzi sahihi ya utoaji haki, wizi mtupu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *