The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Malipo ya Wenza wa Viongozi Yatakiuka Katiba, Kuathiri Ujamhuri wa Taifa

Muswada unaolenga kutengeneza sheria ya kuwalipa wenza wa viongozi mafao baada ya viongozi hao kustaafu, unataka kuwalipa wenza hao malipo ya kazi ipi?

subscribe to our newsletter!

Baada tu ya Uhuru wa Disemba 9, 1961, iliyokuwa Tanganyika haikulala kwa sababu bendera yake ilipepea angani. Zilipotamatika tu sherehe za uhuru, Watanganyika waliendelea na madai mapya ya kutaka nchi yao kuwa Jamhuri.

Kwa sababu uhuru ulimaanisha kujitawala, lakini Jamhuri ingemaanisha kuwaondolea watu nafasi za kiutawala, hadhi ama haki na stahiki zozote zile ambazo wangezipata kwa sababu ya nasaba, jadi ama urithi wao.

Mwaka mmoja baada ya sherehe za uhuru, yaani Disemba 9, 1962, iliyokuwa Tanganyika ikawa Jamhuri ya Tanganyika.  Mwingine angeuliza kwani kuwa huru kuna tofauti gani na kuwa Jamhuri? Majibu yake ni mepesi tu. Tutaitumia nchi yetu kama mfano wa utofauti kati ya kuwa huru na na kuwa Jamhuri.

Wakati Uhuru wa mwaka 1961 ulimfanya Mwalimu Julius Nyerere kuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika na Mkuu wa Serikali ya Tanganyika, Ukuu wa Nchi ya Tanganyika, hata baada ya uhuru, ulisalia mikononi mwa Malkia wa Uingereza.

Kwa lugha nyingine, uhuru wetu haukufuta ukuu wa Malkia wa Uingereza juu ya nchi yetu hadi mwaka mmoja baadaye, yaani Disemba 9, 1962, tulipoamua kuwa Jamhuri.

Ujamhuri wetu hakuishia kurefusha jina letu kutoka Tanganyika hadi Jamhuri ya Tanganyika, la hasha! Ujamhuri wetu ulimaanisha mamlaka kamili ya kujitawala kwa sababu uliondoa nafasi ya Malkia wa Uingereza kama Mkuu wa Nchi ya Tanganyika na kumpa nafasi hiyo Mtanganyika mwenzetu, Mwalimu Nyerere.

Nyerere, ambaye baada ya Tanganyika kuwa Jamhuri alichaguliwa katika uchaguzi kuwa Rais, ambaye, kwa mujibu wa Katiba, akawa pia Mkuu wa Nchi, Mkuu wa Serikali na Amri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama.

Ujamhuri ulimaanisha hata baada ya Nyerere kuachia madaraka, Mkuu wa Nchi ya Tanganyika atakuwa Mtanganyika na atapatikana kwa kuchaguliwa na Watanganyika wenyewe.

Ujamhuri wa Tanganyika ungekuwa wakibaguzi kama ungeishia kufuta vyeo vya urithi vya wazaliwa wa familia ya kifalme ya Uingereza pekee na wenza wao huku ukilinda utaratibu kama huo ndani ya mipaka ya Tanganyika.

Ujamhuri wa Tanganyika ulimaanisha kufuta vyeo, haki na hadhi za kurithi za Wazungu wa Uingereza na Waafrika wa Tanganyika. Ndiyo maana mwaka huohuo, yaani 1962, Tanganyika ilipitisha sheria ya iliyoenda kufuta vyeo, hadhi na mamlaka ya Machifu wa Afrika.

Miaka miwili baadaye, yaani mwaka 1964, iliyokuwa Jamhuri ya Tanganyika iliungana na iliyokuwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Muungano wa zilizokuwa Jamhuri mbili bado uliunda taifa jipya lenye kuheshimu misingi ya Jamhuri.

Wenza wa viongozi kulipwa

Kwa nini nimelazimika kujadili yote hayo? Ni kwa sababu ya Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali, Namba 8B, wa Mwaka 2023. Muswada huo, pamoja na mambo mengine, unakusudia kurekebisha Sheria ya Mafao kwa Hitimisho la Kazi kwa Viongozi ya Mwaka 1999, (Sura Namba 225 ya Sheria za Tanzania).

Marekebisho hayo yanakusudia kuwapa stahiki za kisheria wenza – mume, mke au wake – wa viongozi wetu, mathalani Rais, Makamu wa Rais, na Waziri Mkuu, ili walipwe pesa mara baada ya wenza wao, yaani viongozi wetu, kustaafu utumishi wao Serikalini, ama kufariki dunia wakiwa madarakani, ama wakiwa wameshastaafu.

SOMA ZAIDI: Mabeyo: Jeshi Lilisimama Kidete Kuilinda Katiba Baada ya Kifo cha Rais Magufuli

Kwa mujibu wa vifungu 43, 45 na 48 vya Muswada huo, wenza wa viongozi wetu, yaani Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu, watastahili malipo sawa na asilimia 25 ya jumla ya malipo yote ambayo viongozi wetu wamewahi kulipwa kama mshahara wa kazi yao tokea siku waliyoapa kushika wadhifa husika hadi siku waliyomaliza muda wao mmadarakani.

Ni maoni yangu kwamba malipo hayo ya wenza wa viongozi yanaathiri Ujamhuri wetu kama taifa. Jamhuri maana yake ni kwamba nafasi za uongozi katika taifa zinapatikana kwa kupendekezwa na raia wenzako na si kwa sababu ya jadi, urithi au nasaba.

Kwa hapa kwetu Tanzania, Katiba yetu inataka uzipambanie nafasi hizo kwenye majukwaa ya kisiasa, uteuliwe toka kwa waliozipambania nafasi hizo majukwaani na wakaungwa mkono na wananchi wengi. Na teuzi hizo ziwe kwenye mipaka ya Katiba na sheria za nchi.

Katiba yakiukwa

Viongozi waliowekwa na walipa kodi ndiyo huongoza walipa kodi na hulipwa fedha za walipa kodi kama mishahara ya utumishi wao. Muswada unaolenga kuwalipa watu mafao kwa sababu ni wenza – wake ama waume – wa viongozi wetu unakiuka misingi ya Katiba yetu na unabatilisha jina letu kama Jamhuri.

Ibara ya 23(1) ya Katiba yetu inasema kuwa kila mtu anayo haki ya kupata malipo yanayoendana na kazi yake. Hivyo, kulipwa ni matokeo ya kazi. Hivyo basi, swali la msingi ni je, huo Muswada unaolenga kutengeneza sheria ya kuwalipa wenza wa viongozi mafao baada ya viongozi kustaafu, unataka kuwalipa wenza hao malipo ya kazi ipi?

Je, kuwa mwenza wa kiongozi ni kazi kwenye Utumishi wa Umma kwa mujibu wa sheria na Katiba ya nchi yetu?

SOMA ZAIDI: Rais Samia Ingilia Kati Uvunjifu wa Katiba Unaofanywa na Spika Ndugai

Urais, Umakamu wa Rais, na Uwaziri Mkuu ni ajira katika Utumishi wa Umma na ndiyo maana una malipo yanayolindwa na sheria. Lakini ndoa na kiongozi siyo ajira, ni suala la kijamii na ni suala binafsi la kiongozi mwenyewe aliloamua kulifanya kwa hiari yake. Na pia, kuoa ama kuolewa siyo kigezo cha Mtanzania kupata ama kukosa nafasi ya uongozi.

Malipo kwa wenza wa viongozi yatakiuka misingi ya usawa wa binadamu pia. Ibara ya 12(1) ya Katiba yetu inasema kuwa watu wote ni sawa. Malipo ya wenza wa viongozi yatawafanya wenza hao kuwa tofauti na wenza wa Watanzania wengine ndani ya Utumishi wa Umma kwa sababu wao hawatolipwa licha ya kuwa wao nao ni wenza kama walivyo wenza wa viongozi wetu.

Aidha, malipo kwa wenza wa viongozi wetu yatakiuka masharti ya usawa mbele ya sheria. Ibara ya 13(2) ya Katiba yetu inasema kuwa ni marufuku kwa sheria iliyotungwa na mamlaka yoyote, ikiwemo Bunge, kuweka sharti la ubaguzi wa dhahiri ama kwa taathira yake.

Iwapo Bunge litaufanya Muswada huo, kama ulivyo, kuwa sheria, litakuwa limekiuka Katiba kwa kupitisha sheria inayowapa watu malipo watu pasi na kufanya kazi yoyote inayotambulika kwenye Utumishi wa Umma.

Kwa kufanya hivyo, Bunge litakuwa limetunga sheria yenye masharti ya kibaguzi kati ya Watanzania fulani dhidi ya Watanzania wengine.

Ujamhuri mashakani

Kama hiyo haitoshi, malipo kwa wenza wa viongozi wetu yatakiuka misingi ya Ujamhuri wetu kama inavyolindwa na Ibara ya 29(3) ya Katiba yetu inayosema kuwa raia yoyote wa Jamhuri ya Muungano hatokuwa na haki, hadhi ama cheo maalumu kwa misingi ya nasaba, jadi ama urithi wake.

Iwapo wenza wa viongozi wetu watalipwa kwa sababu tu wameoa, ama wameolewa, na viongozi tutakuwa tumewapa wenza hao hadhi na cheo maalumu na haki ya kupata malipo ya fedha kwa sababu tu wao ni wenza wa viongozi.

SOMA ZAIDI: Serikali Yaondoa Mapendekezo ya Kurekebisha Sheria Kwa Ajili ya Miradi ya Kuendeleza Bandari

Kufanya hivyo ni kukiuka Ibara ya 29(4) ya Katiba inayosema ni marufuku kwa sheria yoyote kutoa hadhi, haki ama cheo maalumu kwa raia yoyote wa Jamhuri ya Muungano kwa misingi ya nasaba, jadi ama urithi.

Kwa lugha rahisi ni kuwa Bunge linakatazwa na Katiba kutunga sheria itakayowapa wenza wa viongozi haki ya kupata malipo kwa sababu ya wao kuoa ama kuolewa na viongozi wetu. Hayo ni masharti ya Katiba ambayo kila mbunge aliapa kuilinda na kuitetea.

Kwa nini urithi ama hadhi maalumu katikati ya mjadala huu? Ni kwa sababu viongozi wetu wanalipwa mishahara na Serikali.

Fedha wanazolipwa ni zao, na ikitokea wakafariki pasi na kuandika wosia, wenza wao ni warithi wao kisheria. Kama wenza wa viongozi wetu ni warithi wao, basi Katiba yetu, Ibara ya 29(3) inakataza vyeo, hadhi, na haki zitokanazo na urithi.

Siyo malipo halali

Ni dhahiri kuwa malipo ambayo muswada unataka wenza wa viongozi walipwe siyo malipo halali kikatiba kwa sababu siyo malipo ya kazi yoyote inayotambulika kwa mujibu wa sheria za Utumushi wa Umma.

Aidha, Katiba yetu, Ibara ya 64(5), inaeleza kuwa, “Iwapo sheria nyingine yoyote ile, zikiwemo sheria zinazotungwa na Bunge, inakinzana na Katiba, basi sheria hiyo itakuwa batili kwa kadiri inavyokinzana na Katiba.”

Kwa lugha nyingine ni kuwa sheria kinzani itaanguka na Katiba itasimama. Katiba inakataza haki ya kupata malipo kwa misingi ya urithi, ikiwemo ndoa kwa sababu ndoa huwafanya watu kuwa warithi wa wenza wao. Kama Katiba inakataza malipo hayo, kwa nini Serikali iwasilishe Muswada wa aina hiyo?

SOMA ZAIDI: Mvutano Kati ya Mungu na Shetani Unaweza Kueleza Hali ya Sasa Tanzania?

Aidha, Katiba yetu, Ibara ya 26 (1), inasema ni wajibu wa kila mmoja kufuata na kulinda Katiba na Sheria za Jamhuri ya Muungano. Ni kwa msingi huo, naishauri Serikali kuondoa muswada huo kwani una kiuka masharti ya Katiba ya nchi yetu.

Na iwapo Muswada huo utajadiliwa bungeni, nalishauri Bunge kutopitisha muswada huo kwa sababu ileile ya kukinzana na Katiba ya nchi.

Kama ambavyo ni wajibu wetu kulinda Uhuru wetu, na kama ambavyo ni wajibu wetu kulinda Muungano wetu, vivyo hivyo ni wajibu wetu kulinda Ujamhuri wetu.

Bahati mbaya sana taifa letu linaadhimisha kumbukumbu ya Uhuru wake kila Disemba 9, na pia Muungano wake kila April 26, lakini tumekuwa tukisahau kutilia mkazo maadhimisho ya Ujamhuri wake.

Tuadhimishe Ujamhuri

Tulipaswa kuisherekea Disemba 9 kama maadhimisho ya Uhuru lakini pia kama kumbukumbu ya Ujamhuri wetu. Ni ushauri wangu pia, tukiona vyema, tuiongozee nguvu Disemba 9 kwa kuitangaza kuwa siku ya maadhimisho ya Uhuru na Ujamhuri wa Tanganyika.

Pengine kwa kufanya hivyo kutatukumbusha Ujamhuri wetu. Kutatutafanya tuelewe kuwa Ujamhuri wetu ni tunu kama ulivyo Uhuru na Muungano wetu hivyo unapaswa kulindwa kwa wivu mkubwa.

Lile neno ‘Jamhuri’ kwenye jina la nchi yetu ndiyo linaloitofautisha Tanzania na nchi kama Morocco, Lesotho, Eswatini, Denmark, Ubelgiji, Uholanzi, Uingereza, Norway, Sweden na Uhispania.

SOMA ZAIDI: Rais Samia, Tunaomba Utuachie Kitabu Chenye Hadithi Nzuri

Nchi hizo zikiamua kuwalipa mishahara, ama mafao, wenza wa viongozi wao haitokuwa tatizo kwa sababu wao siyo Jamhuri, hivyo kumuoa au kuolewa na kiongozi kunamfanya mtu kupata cheo, hadhi na haki zote, ikiwemo malipo ya fedha za walipa kodi.

Nihitimishe kwa kusema kwamba nchi yetu ni Jamhuri.  Neno ‘Jamhuri’ halikuishia kufuta nafasi ya Malkia wa Uingereza kama Mkuu wa Nchi ya Tanganyika bali pia lilifuta utawala wa babu zetu waliokuwa Machifu wenye himaya na miliki zao walizorithi kwa mujibu wa tamaduni zetu za Kiafrika.

Kama tulisimamia Ujamhuri wetu mwaka 1962 kwa kuifuta nafasi ya Malkia wa Uingereza na wateule wake wote juu yetu, na tukafuta tawala za kichifu za mababu zetu ndani ya mipaka yetu wenyewe, basi tuna wajibu leo wa kusimamia Ujamhuri wetu kwa kutopitisha Muswada wa kuwalipa mafao wenza wa viongozi wetu.

Hatua hiyo itatusaidia kulinda usawa kati ya wenza wa viongozi na wenza wa Watanzania wengine wasio viongozi, lakini pia kulinda Ujamhuri wa Tanzania yetu.

Clay Mwaifwani ni mwanasheria na mdau wa usimamizi dumivu wa rasilimali za maliasili. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia +255 758 850 023 au claymwaifwani09@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Maelezo yako ya kisheria ni vema.Aidha,kwa mtazamo wa hali yetu ya uchumi wa jamii yetu;raia wa nchi rafiki kupitia makanisa wanajinyima na kujichangisha na kuonyesha huruma yao kwetu na kututumia michango hiyo kwa ajili ya chakula,mavazi ya watoto wetu ambao wazazi wao hawana mapato ya kutosha kuwatunza shuleni(compassionately).Pia,katika jamii yetu tunayo makundi ya raia wanaopata fedha za mkopo kutoka Benki ya dunia(TASAF),kwa kuwa mapato yao ni kidogo kumudu mahitaji muhimu ya binadamu kuishi.Sasa,viongozi wakuu wa nchi ndiyo wanapata malipo ya kazi yao makubwa kabisa.Hawashitakiki.Wanayofanya katika kazi zao kwa taarifa za CAG yanajulikana.Mantiki ya kuwaongezea malipo zaidi katika familia zao kutoka kwa walipa kodi hawa wanaopata mapato yao ya kuhurumiwa au kukopeshwa na wageni ni kuķosa huruma na upendo kwa raia wema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *