The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Uchaguzi Umekuwa Kichocheo Kikubwa cha Marekebisho ya Katiba Tanzania

Marekebisho haya ya Katiba yaliondoa baadhi ya misingi ya kidemokrasia ambayo kwa sasa ndiyo inapigiwa chapuo iweze kurejeshwa.

subscribe to our newsletter!

Wakati tukijiandaa kushuhudia Muswada wa Marekebisho ya 15 katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, nimejaribu kufanya utafiti mdogo kuhusu historia ya Katiba tuliyonayo kwa lengo la kubaini sababu kuu ambazo zimekuwa zikisukuma marekebisho yake tangu ilipotungwa rasmi miaka 43 iliyopita. 

Kwa ujumla, nimebaini kuwa takribani mara zote, msukumo mkubwa umekuwa ukitokana na haja ya kubadilisha jambo moja au jingine linalohusiana na uchaguzi. 

Katika wakati mwingine, mabadilko ya Katiba yaliondoa baadhi ya misingi ya kidemokrasia ambayo kwa sasa ndiyo inapigiwa chapuo iweze kurejeshwa. 

Ni matumaini yangu kuwa makala hii fupi itachangia kutuangaliza kama taifa ili tusije tukarudia makosa ya miaka iliyopita katika kuondoa mema na kuweka yanayolalamikiwa.

Awali ya yote, vizazi vya sasa wanaweza wasijue kuwa Katiba tuliyonayo hivi sasa ni Katiba ya tano katika mtiririko wa Katiba ambazo Tanganyika – na baadaye Tanzania– iliwahi kuwa nazo. 

Katiba ya uhuru

Katiba ya kwanza ya Tanganyika iliitwa Katiba ya Uhuru ya mwaka 1961 na ilitungwa katika Bunge la Uingereza kwa azimio maalum la Bunge la nchi hiyo, au Order in Council kwa kimombo, mnamo Novemba 28, 1961. 

Katiba hiyo ilianza kutumika Disemba 9, 1961, na iliendelea kuwa na nguvu hadi Bunge la Tanganyika lenye wabunge 71 lilipopitisha Katiba ya pili ya Tanganyika ikiitwa Katiba ya Jamhuri ya Mwaka 1962. 

Kati ya wabunge waliopitisha Katiba hiyo ya Jamhuri walikuwamo Watanganyika wenye asili ya kiasia 11 na Watanganyika Wazungu 10.

SOMA ZAIDI: Tumechelewa Kupata Katiba Mpya Kabla ya Uchaguzi, Basi Tuboreshe Hii Iliyopo

Katiba ya uhuru iliendelea kuweka mamlaka ya nchi chini ya Gavana wa Tanganyika kwa niaba ya Malkia wa Uingereza ambaye, kwa mwaka mzima chini ya Katiba ya Uhuru, alikuwa Mkuu wa Nchi ya Tanganyika. 

Mabadiliko makubwa yaliyofanyika kupitia Katiba ya Jamhuri yalikuwa ni kuifanya Tanganyika kuwa huru na Jamhuri, ikimaanisha kuwa tangu Disemba 9, 1962, Rais wa Tanganyika alikuwa ndiye Mkuu wa Nchi na Mkuu wa Serikali. 

Aidha, Mwafrika huyo alikuwa pia ndiye Amiri Jeshi Mkuu, jambo ambalo lilikuwa jipya kwa Tanganyika. Baada ya miaka miwili yenye kashikashi za ugeni wa kujitawala, Tanganyika changa na Zanzibar changa zaidi ziliamua kuungana na kuwa nchi moja mwaka 1964.

Muungano

Kikatiba, hati za Muungano huo ndizo zinazochukuliwa kama mabadiliko ya tatu ya Katiba ya Tanganyika ambayo yalizaa Katiba ya Muungano ya mwaka 1964. 

Baadhi ya wachambuzi wanaweka bayana kuwa mambo yaliyokubalika kuwa ya Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar yalikuwa ni 11 pekee na siyo 22 yaliyomo kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivi leo. 

SOMA ZAIDI: Yanayokera Kuhusu Katiba ya 1977 na Haja Yakuwa na Katiba Mpya Sasa

Je, ni mambo gani yaliongezeka lini na kwa utaratibu upi? Hili linahitaji utafiti wa peke yake na ninaweza kuahidi kufanya hivyo siku za usoni. 

Yatosha tu kusema kwa sasa kuwa Katiba ya Muungano ilidumu kwa mwaka mmoja hadi ilipotungwa Katiba ya Mpito na kusainiwa na Rais wa wakati huo mnamo Julai 8, 1965. 

Ingawa Katiba hii ilikuwa iwe ya mpito wa mwaka mmoja kama jina lake lilivyoakisi, ilipita miaka 11 hadi kupatikana kwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo Aprili 26, 1977. 

Kwa kujua kuwa Katiba ya mwaka 1965 ilikuwa imeitwa ya mpito na ikaishia kudumu kwa miaka 12, waliokuwepo mwaka 1977 waliamua kuibatiza Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kama Katiba ya ‘kudumu.’

Hata hivyo, takribani miaka miwili tu baadaye, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilikosolewa vikali kiasi cha kufanyiwa marekebisho ya kwanza mwaka 1979. 

SOMA ZAIDI: Mambo Muhimu Ukamilishaji wa Mchakato wa Katiba Tanzania

Maudhui ya mabadiliko haya yalikuwa ni kujaribu kufikiria jinsi migogoro inavyoweza kutatuliwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania endapo, kwa mfano, kutakuwa na kuhitilafiana kati ya Tanganyika na Zanzibar. 

Ni kutokana na fikra hizo ndipo Mahakama ya Rufani ilianzishwa kwa marekebisho ya kwanza ya Katiba ya Tanzania mwaka 1979. Baadaye kidogo tu, ilionekana kuwa kuanzishwa kwa Mahakama ya Rufani pekee kusingemaliza Kero za Muungano. 

Katika kutaka kuimarisha zaidi Muungano, yalikuja marekebisho ya pili mapema mwaka 1980.

Uchaguzi

Aidha, katika hali ambayo siyo ya kawaida sana kwenye taaluma ya ujenzi wa Katiba, masuala ya kiuchaguzi yalipelekea marekebisho mengine ya Katiba ya Tanzania kabla ya kufunga mwaka 1980. 

Ni kupitia marekebisho haya ya tatu ya Katiba ndipo mfumo wa Uchaguzi wa Rais wa Zanzibar; mfumo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar; na Muundo wa Baraza la Wawakilishi ulishughulikiwa na kuwekwa sawa. 

Kwa wakosoaji, marekebisho mara tatu katika Katiba ya Tanzania ndani ya kipindi cha miaka mitatu ilikuwa ni ishara ya Katiba iliyoshindwa kukata kiu ya Watanzania mwaka 1977. 

SOMA ZAIDI: Malipo ya Wenza wa Viongozi Yatakiuka Katiba, Kuathiri Ujamhuri wa Taifa

Kwa kumbukumbu zangu, upepo wa mabadiliko ya kiuchumi na kisisa duniani, pamoja na machungu ya kimaisha kutokana na vita kati ya Tanzania na Uganda vilivyokamilika 1979, zilikuwa chachu ya wananchi kutaka mabadiliko ya Katiba ambayo yangeweka sawa mamlaka ya wananchi na kuboresha mfumo wa kiutawala, kisiasa, na kiuchaguzi.

Vilevile, Watanzania wengi walikuwa wakipigania ugatuzi wa madaraka ya umma ili yawe mikononi mwa wananchi wenyewe. 

Katika hali kama hiyo, Serikali iliona umuhimu wa kupeleka miswada ya sheria ili Bunge litunge Sheria za Serikali za Mitaa Na. 7 na Na. 8 mnamo mwaka 1982 ambazo ndizo zinatumika mpaka hivi leo. 

Wakati huohuo, kulionekana haja ya kurekebisha Katiba ya Tanzania ili kuboresha utaratibu wa uteuzi wa wakuu wa mikoa na viongozi wengine wa tawala za mikoa na Serikali za Mitaa.

Hilo lilitokea mwaka huohuo wa 1982 kupitia marekebisho ya nne ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Mabadiliko ya kidunia

Katika hali iliyoashiria kutoridhishwa na marekebisho madogo madogo, wananchi wengi walikilalamikia chama tawala na chama pekee cha siasa wakati huo, Chama cha Mapinduzi (CCM) na kukitaka kuleta mchakato wa Katiba Mpya ili kuandika Katiba itakayoendana na upepo mkali wa mabadiliko makubwa ya kisiasa na kiuchumi duniani uliokuwa ukivuma wakati huo kutokea ‘Mashariki na Magharibi.’ 

SOMA ZAIDI: Nia Ovu ya Wanasiasa Yahatarisha Kuwanyima Watanzania Katiba Mpya

Katika kuonesha usikivu wake, CCM kiliandaa mchakato wa kutafuta maoni kutoka kwa wananchi juu ya nini kinapaswa kubadilika katika Katiba ya Tanzania. Mchakato huo ulikabidhiwa kwa Timu ya Wataalamu wa Sheria na Rais Ali Hassan Mwinyi mwaka 1991. 

Kamati iliongozwa na Jaji Mkuu wa wakati huo, Francis Nyalali ambaye aliongoza kamati hiyo akiwa Mwenyekiti. 

Baada ya mchakato mrefu na mzuri, Jaji Mkuu Nyalali alikabidhi taarifa ya maoni kwa CCM ambao walitumia maoni hayo kuandaa marekebisho makubwa ya tano katika Katiba ya Tanzania yaliyoingiza tamko la Haki za Binadamu katika Katiba ya Tanzania kwa mara ya kwanza tangu Katiba ya kwanza mwaka 1961. 

Sehemu ya tatu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kama ilivyo hivi leo, iliingizwa kupitia marekebisho ya tano ya Katiba ya Tanzania mnamo mwaka 1984.

Baada ya sherehe za wadai haki za binadamu za miaka takribani sita, kelele zilirejea upya zikidai mabadiliko makubwa zaidi ya Katiba nchini. 

SOMA ZAIDI: Wadau Wapendekeza Marekebisho Muhimu Yafanyike Katika Katiba ya Sasa Kuruhusu Kujiandaa na Uchaguzi

Wakati huo, vuguvugu la mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi duniani lilikuwa limepamba moto, huku baadhi ya Watanzania waliokuwa wamefichwa, au kujificha, ndani na nje ya nchi walianza kusikika wakirejea katika ulingo wa siasa. 

Nikiwa masomoni Malangali na Tabora miaka ya 1990, niliwasikia watu mashuhuri ambao majina yao yalichafuka kisiasa miaka ya baada ya uhuru wakianza kutajwa tena kama watu mashuhuri. 

Baadhi yao ni akina Oscar Kambona, Chistopher Kasanga Tumbo, na Lifa Chipaka waliowahi kuwa na kesi za uhaini na mwanamajumui mashuhuri Abdulrahman Mohammed Babu. 

Baadaye kidogo tulianza kuwasikia wengine kama akina Bibi Titi Mohammed na watu wa kizazi kipya cha wanasiasa kama Mashaka Nindi Chimoto, Prince Bagenda, Masumbuko Lamwai, Bob Nyaga Makani na Amani Walid Kabourou ambaye baada ya kutumikia kama Katibu Mkuu wa Pili wa CHADEMA alikuja kurejea CCM na kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM mkoani Kigoma.

Usimamizi wa uchaguzi

Wakati huo, Serikali iliamua kuja na Marekebisho ya Sita ya Katiba ya Tanzania mwanzoni mwa mwaka 1990 mahsusi kwa ajili ya kuanzisha mfumo wa usimamizi wa uchaguzi ambao usingelalamikiwa hata kukija kurejeshwa vyama vingi vya siasa nchini. 

SOMA ZAIDI: Mchakato wa Katiba Mpya Tanzania: Yajayo Yanafurahisha

Ni mabadiliko haya ndiyo yaliyozaa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) tuliyonayo hivi leo!

Baada ya wajumbe wa mwanzo wa NEC kuteuliwa mnamo Januari 14, 1993, tume ilianza kazi polepole kwa kuanza kusimamia chaguzi ndogo chini ya mfumo wa vyama vingi vya siasa kufuatia kurejeshwa kwa mfumo huo kwa Sheria ya Vyama vya Siasa Sura ya 258 ya mwaka 1992. 

Moja ya majimbo ya mwanzo kabisa NEC kuandaa na kusimamia uchaguzi chini ya vyama vingi ulikuwa ni Kwahani mwaka 1993. Kabla ya kuanzishwa kwa NEC,masuala yote ya uchaguzi yalisimamiwa na CCM, wakati huo kikiwa ndicho chama pekee nchini.

Katika mwaka uleule wa 1990 kulifanyika pia marekebisho ya saba ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo utaratibu ulianzishwa wa kumpata mgombea mmoja wa urais kwa upande wa Zanzibar. 

Katika malalamiko ya baadhi ya Wazanzibari, ilionekana kuwa mfumo wa kumpata mgombea urais kwa upande wa Zanzibar ulikuwa unakosa uwazi. 

SOMA ZAIDI: Othman Masoud Ataka Haya Yazingatiwe Kwenye Mchakato wa Katiba Mpya

Na kama ilivyokwishabainishwa kulikuja mabadiliko ya Nane ya Katiba mwaka 1992 ambayo yalifuta rasmi mfumo wa chama kimoja nchini na kuanzisha mfumo wa vyama vingi. 

Hili lilifanywa na Serikali ya CCM bila kujali matokeo ya maoni yaliyokusanywa na Tume ya Jaji Mkuu Nyalali ambapo wananchi kwa wingi wa asilimia 80 walitaka mfumo wa chama kimoja uendelee na asilimia 20 ndiyo walitaka mfumo wa vyama vingi vya siasa urejeshwe nchini, wakijikumbusha kuwa wakati Tanganyika ikipata uhuru, kulikuwa na vyama vingi kama vile TANU, AMNUT, ANC and UTP.

Uchaguzi wa Rais

Miezi sita tu baada ya Marekebisho ya Nane katika Katiba ya Tanzania, kulikuja marekebisho ya tisa mwaka huohuo 1992 ambayo yalileta mabadiliko katika utaratibu wa Uchaguzi wa Rais wa Muungano nchini. 

Hapa pia, kulianzishwa utaratibu kwamba rais anaweza kuondolewa madarakani kwa kushitakiwa bungeni ambapo kura ya kutokuwa na imani naye inaweza kuanzisha mchakato wa kumsimamisha kazi na baadaye uchunguzi ambao, ukithibitisha makosa kwa upande wa rais, basi utaratibu wa kumuondoa utafuatia. 

Sambamba na hilo, marekebisho ya tisa yalianzisha pia Ofisi ya Waziri Mkuu kikatiba na kuweka utaratibu wa Bunge kuweza kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye na kumuondoa katika nafasi hiyo. 

SOMA ZAIDI: Twaha Mwaipaya: Rais Samia Hawezi Kukwepa Hitaji la Katiba Mpya

Aidha, marekebisho haya yaliweka masharti magumu kwa rais kuweza kulivunja Bunge.

Katika kipindi ambacho hakikufikia mwaka mmoja, kuliletwa marekebisho mengine ya kumi ya Katiba mnamo mwaka 1993 ambapo Uchaguzi wa Madiwani, ambao ulikuwa ni sehemu ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ulihamishwa na kuwa sehemu ya Uchaguzi Mkuu ambapo sasa diwani alichaguliwa sambamba na mbunge na rais. 

Mabadiliko haya yalimaanisha mambo mawili kuhusu uchaguzi wa diwani. Kwanza, madiwani walilazimika kuhudumu kwa miaka zaidi ya mitano ili kusubiri kuja kuchaguliwa tena mwaka 1995. 

Pili, kutokana na kuhamishiwa kwenye Uchaguzi Mkuu, Uchaguzi wa Madiwani sasa uliwekwa chini ya usimamizi wa NEC kuanzia mwaka 1995.

Kwenye marekebisho ya 11 ya Katiba yaliyofanyika mwaka 1994, mfumo wa Uchaguzi wa Rais ulikwenda sambamba na Uchaguzi wa Makamu wa Rais ambaye atatokana na mgombea mweza wa mgombea aliyeshinda uchaguzi. 

SOMA ZAIDI: Hatua Tano Muhimu Kufikia Upatikanaji wa Katiba Mpya Tanzania

Mfumo huu ulitokana na Mapendekezo ya Tume ya Jaji Mark Bomani iliyopewa kazi ya kuangalia namna ya kutatua changamoyo zinazoweza kujitokeza katika mfumo wa vyama vingi vya siasa. 

Tangu wakati huo, Rais wa Zanzibar aliacha kuwa Makamu wa Rais kama ilivyokuwa awali tangu kuungana kwa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964. 

Badala yake, Rais wa Zanzibar alibaki kuwa mjumbe katika Baraza la Mawaziri, jambo ambalo lililalamikiwa na baadhi ya Wazazibari kwa tuhuma kuwa lilimshushia hadhi Rais wa Zanzibar kutoka ngazi ya Umakamu hadi Ujumbe wa Baraza la Mawaziri katika Jamhuri ya Muungano.

Ulinzi wa Muungano

Siku chache tu kabla ya Bunge kuvunjwa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi mwaka 1995, kulipitishwa Marekebisho ya 12 katika Katiba ya Tanzania ambapo viongozi wakuu wa nchi, akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano, Makamu wake, Waziri Mkuu na Rais wa Zanzibar walilazimika kikatiba kula kiapo cha kuulinda Muungano mara tu watakapochaguliwa katika nafsi zao. 

Hii ilitafsiriwa kuwa ni kinga ya uwezekano wa kuvunjika kwa Muungano endapo chama tofauti na CCM kingeshinda kiti cha urais Zanzibar baada ya uchaguzi. 

SOMA ZAIDI: Ismail Jussa: Sikubaliani na Hoja Kwamba Mchakato wa Katiba Mpya Uanze Baada ya 2025

Aidha, marekebisho haya yaliweka ukomo wa utumishi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa ni vipindi viwili tu vya miaka mitano kila kimoja na si zaidi ya hapo. 

Kwa kuendelea kuheshimu masharti haya ya Katiba, Tanzania inasifiwa kuwa ni moja ya nchi chache zilizobaki na msingi huu wa ukomo wa vipindi vya urais katika ukanda huu wa Afrika. 

Maoni mapya ya wananchi yanalenga kuweka pia ukomo wa umri unaoruhusiwa kwa mtu kugombea nafasi ya Urais, Umakamu wa Rais na Ubunge ili kuondoa uwezekano wa mtu wa umri mkubwa sana kuomba kuchaguliwa kuwa Rais wa Tanzania.

Baada ya uchaguzi wa vyama vingi mwaka 1995, kulifanyika tafakuri juu ya mambo yalivyoenda katika uchaguzi na Serikali ikaleta marekebisho mengine ya kikatiba. 

Safari hii, marekebisho ya 13 katika Katiba ya Tanzania yalitua Bungeni mwaka 2000 kufuatia Mapendekezo ya Kamati ya Jaji Robert Kisanga ya mwaka 1998 ambayo mengi yake yalitupiliwa mbali na Serikali. 

SOMA ZAIDI: ‘Ni Muhimu Madai ya Katiba Mpya Yakawa ya Wananchi, Siyo Wanasiasa Pekee’

Badala yake, Serikali ilipeleka Bungeni hoja za kurekebisha Katiba ili kuondoa ulazima wa Rais kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura zote ili ndipo atangazwe kuwa ameshinda.

Jambo hili lilionekana kuwa linatokana na hofu ya Serikali kuwa inaweza kuja siku ambapo wagombea watashindwa kupata zaidi ya nusu ya kura zote zilizopigwa ambayo ingelazimisha duru ya pili ya uchaguzi kati ya wagombea wawili wenye kura nyingi zaidi. 

Mabadiliko haya ya Katiba pia yalimpa rais uwezo wa kuteua Watanzania wapatao 10 kuingia Bungeni kama aina moja wapo ya Wabunge wanaotajwa na Ibara ya 66 ya Katiba. 

Pia, kulikuwa na jambo lililosifiwa hasa na makundi ya watetezi wa usawa wa kijinsia kwa vile kiwango cha wabunge wa Viti Maalum wanawake kilipandishwa kutoka asilimia 15 hadi kufikia asilimia 20.

Marekebisho ya 14 na ya mwisho kufanyika hadi leo ni yale yaliyopelekwa Bungeni mwaka 2005. 

SOMA ZAIDI: ‘Harakati za Kudai Katiba Mpya Ziende Sambamba na Kudai Mabadiliko Kwenye Mfumo wa Elimu’

Haya yalisifiwa sana kwa kuboresha demokrasia katika maeneo kadhaa, ikiwemo usawa wa kijinsia bungeni kupitia Viti Maalum vya wanawake kuongezwa hadi asilimia 30 na kuongeza ulinzi kwa uhuru wa maoni, kuabudu, na uhuru wa habari. 

Pia, marekebisho haya yalipunguza vikwazo vya kikatiba vya kufurahia haki na uhuru mbalimbali, claw back clauses kwa kimombo, ambayo viko sana katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Kwa sasa, wengi tunajiuliza maswali, likiwemo la je, ni mambo gani yataletwa na Serikali katika marekebisho ya 15 ya Katiba ya Tanzania ambayo yamelazimika kuja kutokana na maeneo mbalimbali ya maboresho ya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi; Sheria ya Vyama vya Siasa; Sheria ya Ghrama za Uchaguzi; Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na Sheria ya Uchaguzi wa serikali za Mitaa ambazo zinapelekwa Bungeni kwa maboresho katika Mkutano wa Bunge unaoanza tarehe 31 Oktoba 2023?

Yetu yanabaki macho na masikio!

Deus Kibamba ni mtafiti anayefundisha utatuzi wa migogoro na uendeshaji wa mazungumzo ya amani katika Chuo cha Diplomasia. Anapatikana kupitia +255 788 758581 na dkibamba1@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *