The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Ni Wakati Tuitendee Haki Kumbukumbu ya Maisha ya Siti binti Saad

Katika zama zetu, bado mwanamke anapingana na mfumodume kwa kiwango kikubwa lakini si zaidi ya vile ilivyokuwa kwa Siti.

subscribe to our newsletter!

Mwanadamu anayo nguvu kubwa ndani yake ya kubadilisha mwelekeo wa maisha yake. Kama kuna yeyote aliye na mashaka juu ya hilo, yampasa asome kuhusu maisha ya Siti binti Saad. Alizaliwa fukara na kuishi maisha ya chini sana; lakini mpaka mwisho wa uhai wake, hata jina lake lilibadilika.

Siti hakuzaliwa Siti. Alizaliwa Mtumwa binti Saad, na kujulikana hivyo kwa miaka 31 ya kwanza ya maisha yake. Kwa miaka 39 iliyobaki, na hata leo tunamfahamu kama Siti binti Saad, Siti ikiwa na maana ya Bibi, au jina la heshima kwa mwanamke. Japokuwa alizaliwa kijijini Fumba huko Unguja, wazazi wake walikuwa wametokea Tanganyika, sasa Tanzania Bara.

Baba Mnyamwezi alikuwa mkulima na mama Mzigua alikuwa mfinyanzi – kazi ambayo Siti pia aliifanya. Alizaliwa na nduguze tumbo moja, Musa, Mbaruku na Masika umbu lake. Hata hivyo, alipofika umri fulani aliamua kwenda mjini ‘kutafuta maisha.’ Na kweli, aliyapata. 

Shaaban Robert, kwenye kitabu chake Wasifu wa Siti Binti Saad, kilichochapishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1952, na kuchapishwa tena mwaa 2015 na Mkuki na Nyota, anasema kwamba maisha ya shamba yalimpa Siti mwanzo mwema sana. Alikuwa na moyo mkuu (uk. 24). Tena, alikuwa mnyenyekevu.

Umaarufu wa Siti

Pengine angekuwa hai leo, Siti angekuwa kwenye kila shughuli ya kiserikali, kwenye kila bango mtaani wakati wa Sauti za Busara, nyimbo zake zingepigwa kila redio Afrika Mashariki na hata aka trend kwenye mitandao ya kijamii; na bila shaka angekuwa amepokea Tuzo ya Kora kama mwanamuziki bora Afrika. 

Maana wakati wa uhai wake, vitu hivyo vilikuwa vya kawaida. Naviona tayari vichwa vya habari magazetini na kwenye mitandao – Kutoka Fumba hadi miisho ya ulimwengu: Siti Binti Saad; Malkia wa Taarab aitikisa dunia; #2024TaarabTour: Malkia Siti afika India; Mwanamke wa Kwanza kuimba Taarab huyu hapa, na vichwa vingine vya habari vinavyofanana na hivyo.

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Tunahitaji Kusoma Vitabu Vingi Zaidi vya Kiswahili?

Yawezekana mtu akasema, lakini taarab ya leo siyo ya jana. Utakuwa hujaelewa hoja yangu. Kwa hulka ya Siti, hata kama angeimba Bongo Flava bado angevuma sana. Nashangaa ni kwa nini mpaka sasa hakuna filamu inayomhusu yeye, si hapa nyumbani wala katika mitandao ya filamu ya nje kama Netflix, Amazon Prime, na kadhalika. 

Watu wengi wanaweza wasifahamu hili, ila Siti alirekodi na kampuni ya santuri – Columbia Records mwaka 1927 kama sehemu ya kampeni yao ya kurekodi watribu wapya wa kila taifa. Kwa Afrika Mashariki, Siti alituwakilisha. Alikuwa mwimbaji wa kimataifa!

Siti alikuwa si tu mwanamke wa kwanza kuimba taarabu, lakini pia mwanamuziki wa kwanza kuimba taarab kwa Kiswahili. Alikuwa mwanamke wa kipekee. 

Ni ngumu kuelewa yawezekanaje kuwa kabla yake hakukuwa na wanawake kwenye taarab kwani leo hii mtu akiwaza taarab, anawaona wanawake wamevaa madera wakimtuza mwimbaji pale mbele ambaye kwa asilimia kubwa atakuwa ni mwanamke. Hata hivyo, mbuyu nao ulianza kama mchicha.

Siti alikuwa tajiri na maarufu sana. Shaaban Robert anasema, “Katika wakati wake hapakutokea mwimbaji hata mmoja wa Afrika Mashariki aliyeweza kumshinda kwa kuimba, isipokuwa Umi Kulthum wa Misri.” (uk 25). 

Katika utajiri wake, wapo wajanja katika tasnia walionufaika kwa mgongo wake. Shaaban Robert anasema, “Mafundi wa sahani za santuri walimkimbilia wakapata fedha nyingi sana kuliko ile aliyopata yeye. Waliweza kupata shilingi elfu moja kwa kila shilingi moja alizoweza kupata yeye. Santuri yake ilienea katika santuri za ulimwengu.” (uk. 21)

Shaaban Robert anaelezea kuwa Siti alikuwa anaimba nyimbo ambazo hazikupungua 12 kwa saa moja kwa siku. Kwa mwaka, aliimba zaidi ya nyimbo 4,000. Jumla hii, yatosha kuwa kitabu cha maneno 100,000 kama kila wimbo ungekuwa na maneno thelathini. Na japokuwa alikuwa hajui kusoma na kuandika, alikuwa hodari wa kukariri. (uk 36)

SOMA ZAIDI: Laiti Kama Ningepata Nafasi ya Kumhoji Shaaban Robert

Shaaban Robert ananishangaza. Jinsi alivyomheshimu Siti kwa kuandika wasifu wake; jambo hili linazungumza mengi kuhusu yeye mwandishi. Anasema mwenyewe kuwa alipokutana naye ili kuandika wasifu wake ilikuwa Februari 1950 huko Unguja. 

Japokuwa alikuwa ni bibi wa miaka 70, ambaye nywele zake zilikuwa na miali michache ya mvi, kwake yeye Shaaban, alionekana kama mwenye umri wa miaka 40 tu! 

Mauti yalimkuta Siti miezi minne tu baada ya yeye kubahatika kumpiga picha na kufanya naye mahojiano. Shaaban Robert angeweza kuamua kuachana na mradi huu, akauweka kando. Lakini hakufanya hivyo. Daima tutamshukuru kwa uungwana wake.

Maumbile na uzuri

Shaaban Robert anatumia muda mwingi kuchambua suala la maumbile na uzuri wa Siti. Anasema, utotoni mwake hakuna aliyedhani kwamba “maumbile yalikuwa yamekusudia kumtoa katika giza la sahau na kumtia katika nuru ya umaarufu baadaye. 

Kadhalika, ilikuwa si watu wale tu, hata baba na mama yake walikuwa hawajui kabisa kwamba maumbile yalikuwa yamemwekea binti yao akiba ya umaarufu mkubwa wakati ujao.” (uk 6-7)

Sauti yake ndiyo iliyompandisha hata akaketi na wakuu. Lakini kuhusu maumbile yanayoonekana, Siti hakuwa na uzuri kwa viwango vya walimwengu. Wabaya wake, walitumia kigezo hicho kumkosoa kama msanii mahiri. 

SOMA ZAIDI: ‘Mhariri Msalabani’ Inatueleza Nini Kuhusu Historia ya Uhuru wa Habari Tanzania?

Lakini hawakuweza, kwani “Siti alijua kuwa riziki haikuletwa wala haikupingwa na sura nzuri au mbaya, [na kwa sauti yake] kila mtu alionekana kama kwamba alirogwa mbele yake (uk. 25).

Kwa nini hili lilikuwa na umuhimu? Siti hakutumia uzuri kuishi, aliitumia sauti yake. Hakuuza mwili wake, aliuza sauti yake. Na hilo lilimtofautisha. Mwandishi anachambua jambo hili na kusema: Malezi makubwa ya wanawake katika nchi hizi yalikuwa utawa. 

Utawa huu ulifuatwa na mashindano ya ndoa kwa uzuri wa sura. Malezi haya yalikuwa mazuri, lakini hayakuacha nafasi ya matukio yaliyoweza kutokea kwa mwanamke kwa ujane au talaka. 

Nje ya ndoa wanawake maskini walikuwa hawawezi kujitegemea. Kanuni hii ililazimu kuhidiwa. Kama Siti alikuwa na kusudi hili alipojitia katika kazi ya kuimba alikuwa mmoja wa wahidi wakubwa wa maendeleo ya wanawake katika Afrika Mashariki. (uk. 26)

Katika zama zetu, bado mwanamke anapingana na mfumodume kwa kiwango kikubwa lakini si zaidi ya vile ilivyokuwa kwa Siti. Pamoja na mitazamo ya jamii, na mifumo mbalimbali iliyowekwa ambayo ingeweza kumrudisha nyuma, bado aliinua kichwa chake na bado aling’aa.

Hakuwa katika ombwe

Kama simulizi nyingine yoyote ya mtu aliyefanikiwa, haikutokea katika ombwe. Sio kwamba Siti alifanikiwa kwa jitihada zake mwenyewe bila msaada wa mtu mwengine. Hapana. 

SOMA ZAIDI: Zubayda Kachoka Lakini Ally Saleh Anaendelea Kupambana Zanzibar

Alipofika mjini Unguja, alikutana na bwana mmoja jinale Muhsin Ali ambaye alimfundisha Siti kiarabu na kuimba. Japokuwa alikuwa na kipaji, alikuwa hajui jinsi ya kukikuza. Urafiki wao ulimjenga sana. 

Baadaye akajiunga na kikundi cha watribu waliokuwa maarafu wakati huo. Akazungukwa na wanaume tu! Hata hivyo, sauti yake na ujasiri wake ndivyo vilivyomwinua juu. Wao wakawa wanapiga vyombo, yeye anaimba. Na baada ya kujiunga nao, neema iliwashukia; mapato yao yaliongezeka maradufu.

Ndiyo, watu walimsaidia katika safari yake; ila Shaaban Robert anasisitiza tena na tena, kwamba Siti hakufanikiwa kwa sababu ya kipaji. “Alifaulu kwa sababu alishikilia kazi yake kwa bidii na kwa muda wa siku nyingi.” (uk 14). Hakukata tamaa, hakubweteka. 

Hakujiona mimi ni mwanamke, kwa hiyo ni duni au nahitaji nisaidiwe wakati wote, hapana.

Ninaguswa sana na jinsi Siti, mwanamke mcha Mungu, alivyobadilisha maisha yake na jinsi Shabaan Robert alivyompamba. Nafikiri kuwa hatuitendei haki kumbukumbu ya maisha yake. Bado hajakaa midomoni mwetu na mawazoni mwetu vya kutosha. 

Siti alikuwa mwanamke aliyeruka vihunzi vingi – umasikini, ugeni mjini, ugeni kwenye tasnia ya muziki wa taarab, maneno na husda za watu, na kadhalika – mpaka akafika katika umaarufu na sifa kuu aliyofikia. Tuna mengi ya kujifunza kutoka kwake.

Esther Karin Mngodo ni mwandishi na mhariri anayeishi Dar es Salaam, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia mtandao wa X kama @Es_Taa. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts