Wazazi huwa tunakuwa na mawazo kadha wa kadha pale tunapodhamiria kuongeza idadi ya watoto katika familia. Tukiwaza kwamba sasa mtoto, au watoto, wetu wanakwenda kupata mdogo wao, na kupata mwenziye wa kuchezanae. Je, watakuwa marafiki na ndugu wa kutegemeana? Watapendana?
Ukweli ni kwamba watoto waliozaliwa kwenye familia moja, hasa wanaofuatana, huwa ni changamoto kubwa katika malezi kwani mara nyingi huwa na ugomvi wa hapa na pale, huku wanachogombea mara nyingi huwa hakionekani wala kueleweka.
Kwa mfano, watoto wanaweza kugombania vitu vidogo ambavyo wanavipenda, au wanavyotamani, kama kifaa cha kuchezea ambacho kila mtoto anataka kukitumia, hii inaweza kusababisha ugomvi kati yao. Wanaweza kushindana kwa sauti ili kila mmoja apate kumiliki kifaa hicho, au kukitumia, kwa muda mrefu zaidi kuliko mwingine.
Wanaweza kujaribu kumvutia, au kumshawishi, mzazi au mlezi kuwapa kipaumbele kwa kudai kuwa wao wanastahili zaidi, au kwamba wanahitaji kitu hicho kuliko mdogo wao.
Wataalamu wa malezi wanaamini kwamba watoto wenyewe wakipewa nafasi pasipo wazazi kuingilia, wanaweza kujenga heshima, upendo, kuaminiana na kutegemeana ki ndugu. Kwa mfano, unapomuona mtoto mkubwa anamsukuma, au kumnyang’anya kitu mdogo wake, usiwe mwepesi kukemea.
SOMA ZAIDI: Kwa Nini Mzazi Anashauriwa Amnyonyeshe Mtoto kwa Miaka Miwili?
Mpe fursa ya kujifunza na kumjali mdogo wake ambaye mara nyingi atapaza sauti kutaka ujue kaonewa. Namna hii, kaka, au dada, mtu atalazimika kumbembeleza mdogo wake na muda mchache baadaye watacheka pamoja. Hapa wanajenga mahusiano na ushirikiano.
Mfano mwingine ni mara tu unapokuwa umempata mdogo mtu, watoto wengi hujenga ‘chuki’ kwani ghafla mapenzi ya wazazi huamishiwa kwa mdogo. Namna nzuri ni kumshirikisha mtoto toka ujauzito kwa kumueleza kwamba nyote mnatarajia kupata ujio wa mdogo wake.
Mara tu anapozaliwa mfanye sehemu ya malezi kwa kumpa majukumu madogo madogo, huku ukitumia kauli jumuishi, kama vile, mtoto wetu analia, atakuwa anataka kunyonya, au mdogo wako analia atakuwa anataka kunyonya, au unapaswa kuwa mlinzi wa mtoto wetu, au mdogo wako, na kadhalika.
Hii itamfanya mtoto mkubwa ajisikie sehemu ya familia na kwamba kumbe huyu ni ndugu yake na ni moja ya wanafamilia.
Fursa nyingine ni wanapokuwa wametimiza umri wa kwenda shule. Mara nyingi mkubwa huanza kujua kusoma kabla ya mdogo wake . Mpe fursa kaka, au dada, mtu kuwa mwalimu wa mwenzie kwa kumfundisha namna ya kushika kalamu, kumsomea hadithi na hata kuimba nyimbo za kiada pamoja.
SOMA ZAIDI: Kwa Nini ni Muhimu kwa Wazazi Kujifunza Kuhusu Huduma ya Kwanza?
Namna hii unawafundisha kutegemeana na kuimarisha mahusiano yao kama mtu na mdogo wake.
Vilevile, unaweza kuwajengea mazingira ya kushirikiana katika kazi kwa kuwapangia kufanya usafi, kufua, kuosha vyombo, na kadhalika, kwa kushirikiana. Namna hii watajifunza kutekeleza majukumu kwa pamoja kama familia.
Ingawa wataendelea kuonesha kuudhiana kama vile wakati wengine wanafanya kazi, zoezi hili pia litakupa fursa ya kuzipata taarifa za namna wanavotekeleza majukumu yao ili uweze kuwaasa na kuwakanya juu ya utegeaji kazini.
Watoto wakikua kwa kutegemeana hata changamoto baina yao na marafiki zao zitatatuliwa mara nyingi na kwa amani bila hata wewe kushirikishwa.
Pia, kwa kuacha watoto wajifunze kusimamia utatuzi wa migogoro yao wenyewe, tunawapatia fursa ya kujifunza kujieleza, kusikiliza, na kuheshimu maoni na hisia za wengine. Namna hii unaandaa binadamu makini wenye uwezo mkubwa wa kutatua matatizo yao wenyewe na kwa kushirikiana.
SOMA ZAIDI: Mambo ya Kuzingatia Kabla ya Ujauzito Kama Una Ugonjwa wa Kudumu
Tutakosea tukikuaminisha kwamba baada ya kufanya mambo haya basi watoto watapendana.
Licha ya juhudi zetu za kuwaelimisha na kuwasaidia kujenga mahusiano mazuri, bado watoto wataendelea kukumbana na changamoto na migogoro ya hapa na pale kama kupigana, kufinyana, na kadhalika, lakini bado upendo baina yao utajengeka.
Kumbuka kwamba malezi ya familia ni safari ya muda mrefu. Tunachojifunza hapa ni kwamba kumbe hata watoto wenyewe wakipewa fursa ya kuhusiana bila ya sisi wazazi kuwa mahakimu kila wakati, wanaweza kujenga mahusiano mazuri tu.
Tena kwa kufanya hivi itakupa hata wewe mzazi nafasi ya kupumua toka katika kiti chako cha maamuzi.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, na kupitia barua pepe yao www.sematanzania.org.