The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

CCM Hawako Tayari kwa Mageuzi Lakini Suluhu Siyo Kususia Uchaguzi

Mageuzi ya kweli ya kisiasa ni kifo kwa CCM, na viongozi wa chama hicho tawala wanalifahamu hilo vizuri sana.

subscribe to our newsletter!

Ifike mahala kama taifa tuukabili ukweli mchungu uliopo mbele ya macho yetu na ambao mpaka sasa tumeendelea kujifanya kama vile hatuuoni: kwamba hakuna mageuzi ya kweli yanaweza kutokea kwenye nchi hii kwa baraka, hiari na utayari wa chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM).

Kimsingi, ni kutojitendea haki, kama watu wenye uwezo wa kufikiri sawasawa, kudhani, au kuamini, kwamba CCM inataka mageuzi, au ina maslahi kwenye mchakato huo mzima. CCM, kama chama chenye dola kilicho na malengo ya kulishikilia dola hilo, itafaidika nini na mageuzi? Hakuna. Badala ya kufaidika, itadhurika kwa kukoma kuwa chama tawala.

Mifano ya CCM kutokuwa tayari kutekeleza mageuzi yoyote ya msingi na yenye manufaa kwa nchi imejaa tele kwenye historia ya miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania kiasi ya kwamba inanipa huzuni nikijua kwamba wapo watu miongoni mwetu wanaohadaika na laghai zinazoendelea zinazoitwa za kuleta mageuzi nchini.

Hivi tujiulize, lipo jaribio kubwa la kutaka mageuzi ya msingi ya kisiasa hapa nchini kwetu zaidi ya lile la kuundwa kwa Tume ya Nyalali ambayo, pamoja na mambo mengine mengi mazuri, ilipendekeza mabadiliko makubwa ya kisheria, kikanuni na kitaratibu ili kuendana na mfumo wa vyama vingi vya siasa uliorejeshwa nchini mwaka 1992? 

Ripoti ya tume hii, iliyoundwa na Rais wa awamu ya pili, hayati Ali Hassan Mwinyi, na iliyofanya kazi yake kwa uadilifu na weledi mkubwa sana, ipo kwenye makabati na makabrasha ya idara za Serikali, huku wahusika wakijitia hamnazo kwa kujifanya kama vile ripoti kama hiyo haikuwahi kutolewa na hatujui suluhu za matatizo lukuki yanayotukabili!

SOMA ZAIDI: Miswada ya Uchaguzi Iliyopitishwa na Bunge Inakinzana na Nia ya Rais Samia ya Kuleta Mageuzi ya Kisiasa Tanzania

Vipi kuhusu mchakato wa mabadiliko ya Katiba? Ukiasisiwa kwa mbwembwe nyingi na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Mrisho Kikwete, mchakato huu pia haukuharibiwa na mtu mwingine yoyote yule isipokuwa CCM wenyewe na mpaka leo tumebaki tukidanganywa na kupigwa kalenda wakati tunajua kwamba hakuna popote tunapoenda. 

Mbali na ufujaji mkubwa wa fedha za walipa kodi unaotokana na uendeshwaji wa michakato hii ambayo haishii popote, nadhani ni dharau kubwa sana kwa Watanzania wanaoombwa kujitokeza kutoa maoni yao, wakiacha sulubu zinazowaingizia kipato, halafu hakuna chochote kinachofanyika baada ya kufanya hivyo.

Tabaka tawala, kote duniani, halijawahi kuvutiwa na tabaka tawaliwa, lakini hapa kwetu hali imefurutu ada kwa sababu dharau hizi hutokea mara kwa mara bila ya watawala kupata ukinzani wowote kutoka kwa wale inaowatawala na kuwadhalilisha.

‘Mageuzi’ ya Samia

Ndiyo maana haishangazi kuona kila Rais anayeingia madarakani anaweza kucheza na fedha, muda na akili za walipa kodi halafu akaendelea na maisha kama kawaida kama vile hakuna kitu kimetokea. Imetokea hivyo kwa marais wote na sasa inatokea kwa Rais Samia Suluhu Hassan, kiongozi anayependa kujitambulisha kama ‘mwanamageuzi.’

Kwanza ni lazima niweke wazi kwamba kwangu mimi, Samia ni kiongozi bora ukilinganisha na yule tuliyekuwa naye kabla yake, John Magufuli. Pengine hiyo ni bahati yake na anapaswa ajivunie nayo. Nikimlinganisha na mtangulizi wake, simuoni Samia kama kiongozi katili na muovu kama mtu. Ningemhukumu tofauti kama asingekuwa mrithi wa Magufuli.

SOMA ZAIDI: Tumechelewa Kupata Katiba Mpya Kabla ya Uchaguzi, Basi Tuboreshe Hii Iliyopo

Mbali na hapo, simuoni Samia akiwa na utofauti wowote na viongozi wengine wote ambao tumewahi kuwa nao kama taifa kupitia CCM. Viongozi wote hawa wanafanana kwenye sifa yao moja tu: kufanya lolote linalowezekana kuhakikisha CCM inabaki madarakani kwa kuminya uhuru wa watu na kuweka mifumo inayokipendelea chama hicho.

Kwa hiyo, binafsi hainishangazi nikimuona Samia akifanya yale yale yaliyowahi kufanywa na watangulizi wake yenye kuashiria dharau kubwa kwa wale anaosema anawaongoza. Chukulia, kwa mfano, uamuzi wake wa kuunda Kikosi Kazi cha kukusanya maoni ya wadau ili kuboresha demokrasia ya vyama vingi nchini, halafu jiulize ni nini mpaka sasa kimeshatokana na mchakato huo? Hakipo.

Kimsingi, Serikali ilishindwa kuzingatia maoni mengi ya wadau hata kwenye sheria za uchaguzi zilizozipitishwa na Bunge hivi karibuni na ambazo sasa zinasubiri sahihi za Rais ili kuanza utekelezaji. Kumbuka kwamba Kikosi Kazi kilikuwa ni cha Rais Samia mwenyewe na sheria zilizotungwa zilitokana na miswaada ambayo Serikali yake ilipeleka bungeni. 

Matendo hasi

Kuna namna nyingi tunaweza kuonesha kwamba Rais Samia hana nia ya dhati ya kuleta mageuzi ya msingi nchini kwa kuangalia sera, sheria na kanuni ambazo Serikali imekuwa ikiweka kuisaidia CCM kwenye chaguzi. Ubaya ni kwamba kukosekana huku kwa utashi hakuishii kwenye sheria tu bali unakwenda pia kwenye matendo ya CCM na watendaji wengine wa Serikali.

Angalia kwenye chaguzi ndogo za udiwani zilizofanyika hapo Machi 20, 2024, ambapo CCM ilitangazwa mshindi kwenye kata zote 23 zilizoshiriki kwenye zoezi hilo nchi nzima. ACT-Wazalendo, chama cha upinzani kilichoshiriki chaguzi hizo, kimelalamikia rafu zilizochezwa na CCM na watendaji wengine wa Serikali, wakiwemo polisi, zilizowazuia wananchi kushiriki kikamilifu kwenye chaguzi hizo.

SOMA ZAIDI: Falsafa ya CHADEMA ya ‘Nguvu ya Umma’ na Itikadi ya Ujamhuri: Je, Upo Ulinganifu?

Malalamiko ya kura feki, au kushikiliwa na polisi kwa wagombea au wasaidizi wao, ilitegemewa kwamba yawe ni mambo ya kale tangu Rais Samia atangaze mchakato wake wa maridhiano, mchakato ambao umempatia sifa kitaifa na kimataifa. Lakini hapana, malalamiko hayo yalitawala kwenye chaguzi hizo ndogo.

Rais Samia ni mtu mzuri na naamini kwamba anamaanisha anachokisema. Hata hivyo, kiongozi huyo wa kwanza mwanamke wa taifa hili amejikuta sehemu mbaya. Manukato, hata yawe mazuri kiasi gani, hayawezi kuipiku harufu ya shombo. Kimsingi, hakuna anayetaka mchanganyiko wa manukato na shombo kwani hayo hayatakuwa manukato tena!

Mtu anaweza kusema kwamba kama Rais Samia akiamua kuleta mageuzi ya kweli, hakuna atakayemzuia kwani yeye ni Rais, mwenyekiti wa CCM na Amiri Jeshi Mkuu, sifa zinazompa mamlaka ya kufanya chochote na chochote kisimtokee. Lakini swali la msingi ni hili, Samia yuko tayari kuwa Rais wa mwisho wa CCM? Maana mageuzi ya kweli yanatishia hatari hiyo, na sidhani kama Samia yuko tayari kwa hilo.

Mapambano

Tunafanya nini kukabiliana na hali kama hii? Kwanza ni kujaribu kuielewa na kukubaliana nayo. Hutakuwa ukivunjika moyo sana endapo kama utakuwa na matarajio hafifu kutoka kwa mtu au taasisi fulani. Tukishajua kwamba CCM haiwezi kutupa mageuzi tunayoyataka, hatutavunjika moyo tukiona wagombea wanaenguliwa kwa sababu za kitoto au vyombo vya ulinzi na usalama vikiingilia kati kuikoa CCM kwenye uchaguzi. 

Pia, hatuwezi kukabiliana na hali hii kwa kususia chaguzi zinazofanyika. Kufanya hivyo kutatuweka kwenye hatari zaidi ya vile tunavyofikiria. Kwanza, kama hatutashiriki hizi chaguzi, kama wanasiasa au wananchi, hatutakuwa na haki, au mamlaka, ya kuzilalamikia. Unawezaje kulalamikia ukali wa pilipili usiyoila? 

SOMA ZAIDI: Uchaguzi Umekuwa Kichocheo Kikubwa cha Marekebisho ya Katiba Tanzania

Pili, kususia chaguzi kutazuia uwezo wetu wa kudhihirisha maovu ya CCM kwa wananchi wenzetu na kwa dunia pia, dunia ambayo ndiyo imekua mlengwa nambari moja wa matamko ya Serikali kuhusiana na ‘megeuzi’ ya kisiasa nchini Tanzania. Watawala wanapozungumza kuhusu ‘mageuzi,’ hadhira yao lengwa siyo Watanzania bali dunia inayotoa misaada, ruzuku na ‘neema’ zingine.

Mwisho, kususia kungekuwa ni suluhu kama kungekuwa na namna nyingine ambayo wananchi wangeweza kutumia kuiondoa CCM madarakani. Ukweli ni kwamba, angalau kwa sasa, hiyo njia haipo na kususia chaguzi itakuwa ni sawa na kujipiga wenyewe risasi za miguu na kudhani kwamba bado tutaweza kukimbia.

Kila aina ya mapambano ni muhimu katika mchakato mzima wa kuleta mageuzi tunayotaka kuyaona katika nchi yetu. Kwenye uchaguzi tushiriki kama wapiga na wapigiwa kura; maandamano tufanye; matamko tutoe; tuchapishe kwenye mitandao ya kijamii na tuzungumze Clubhouse; pamoja na mbinu zingine zote za mapambano.

Tutafanya kosa, hata hivyo, tukiamini kwamba CCM imedhamiria kweli kuleta mageuzi ya kisiasa Tanzania. Kwa CCM kufanya hivyo ni sawa na kujinyonga na sikioni chama hicho, au viongozi wake, wakiwa tayari kutekeleza aina hiyo ya uhalifu, angalau siyo kwa sasa.

Khalifa Said ni mwandishi na mhariri wa The Chanzo. Unaweza kumpata kupitia Khalifa@thechanzo.com au X kama @ThatBoyKhalifax. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

2 responses

  1. Ccm inacheza na akili za wapinzani. Ikiona imekabwa koo inabuni kitu cha kufanya ikiwemo kuwaita Ikulu na kukaa meza moja. Ilufanya hivyo kipindi cha Kikwete, na sasa inafanya hivyo wakati wa Samia. Ni mabingwa wa propaganda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts