Mtafiti maarufu wa malezi nchini Poland, Jozef Augustyn, aliwahi kueleza kuwa, “Baba wengi hufikiri kuwa wao ni wazazi bora kwa sababu wanatafuta pesa kwa ajili ya familia.” Lakini hilo ni mojawapo tu ya majukumu ya baba.
Ukweli ni kwamba watoto hawamthamini baba tu kulingana na kiasi cha pesa alizonazo, au thamani ya zawadi anazowapatia; watoto pia hutaka upendo na muda wa kutosha kutoka kwa baba yao.
Kimsingi, ushiriki wa baba katika malezi huleta usawa ndani ya familia na kuimarisha uhusiano mzuri kati ya wazazi wote wawili na watoto wao. Kwa lugha rahsi, malezi ya watoto siyo jukumu la mama peke yake.
Uhusika wa baba katika malezi husaidia kujenga uhusiano mzuri na mtoto. Upendo na ukaribu uliopo kati ya mtoto na mama huwa ni wa moja kwa moja tangu mtoto anapozaliwa tofauti na upande wa baba.
Pia, uwepo wa baba humjengea mtoto uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali. Mara nyingi mtoto mwenye mahusiano mabaya na baba yake huwa na msongo wa mawazo na kuhisi upweke.
SOMA ZAIDI: Kwa Nini ni Muhimu kwa Wazazi Kuwashirikisha Watoto Kwenye Kupika?
Japo mama yupo lakini anapoona wenzie ambao wanalelewa na wazazi wote mtoto hujiona kwamba yeye si mkamilifu, na mara nyingi anaweza kuiga tabia zisizofaa mitaani, kama vile matumizi ya madawa ya kulevya, pombe na vilevi mbalimbali ili kuepukana na msongo huo wa mawazo.
Fahamu kwamba, kama baba, unaweza kuwa mlezi kamili na mzuri. Unaweza kumpatia mwanao malezi kamili kama mwenza wako afanyavyo. Hivyo, akina baba msisite kutimiza majukumu yenu kwa kufanya kazi za kujikimu pamoja na kuwatunza watoto, wenza wenu na wengine ndani ya familia.
Usiache imani za kijinsia juu ya malezi ziathiri dhamira na uwezo wako wa kumtunza mwanao, malezi ya mtoto na changamoto zake yamekuwa yakiaminiwa kuwa ni jukumu la mwanamke peke yake, jambo ambalo huwanyima wazazi wa kiume nafasi ya kutoa mchango wao katika malezi na makuzi ya mtoto.
Tafiti zimeonesha kuwa, ushiriki wa baba kikamilifu katika malezi una mchango mkubwa katika afya na ustawi wa mtoto.
Shiriki sawa na mwenza wako katika shughuli zote za malezi ya watoto wenu. Usiogope kutumia muda wako vizuri na mwanao wa kike, au wa kiume, na kufanya kazi zote kama vile kupika, kufanya usafi, kucheza nao na kuwabembeleza wanapolia.
SOMA ZAIDI: Usafi ni Muhimu Sana Katika Makuzi ya Watoto Wetu, Tuuzingatie
Watoto siku zote hukumbuka matendo haya na hivyo kujenga upendo na amani kati yenu. Ni vyema kuhamasishana wake kwa waume ili kila mmoja ajione ana uwezo wa kutekeleza majukumu ya malezi na kutafuta pesa kwa pomoja.
Baba, wajengee wanao uwezo wa kutekeleza majukumu bila kujali mipaka ya kijinsia. Wapende wanao na uwakubali walivyo, usitumie nguvu kuwabadli. Jitahidi kuwapa malezi yenye kuondoa mila potofu na kuleta usawa wa kijinsia katika majukumu kwa wewe kuwa mfano.
Vilevile, jijengee heshima na upendo kwa watoto wako na siyo nguvu na umangi-meza. Kila mtu hufurahia kupenda na kupendwa na unaweza kupata upendo wa watoto wako kwa kuwapenda na si kwa kuwaonesha ukali na umangi-meza. Ukali na ubabe unaambulia nidhamu ya uoga na siyo heshima na utii wa kweli.
Ni vyema kwa wazazi wa kiume kuonesha upendo, heshima na uwajibikaji kwa watoto, mwenza wako na familia kwa ujumla. Kumbuka kwa kufanya hivi unajenga msingi wa tabia za mwanao unayemtaka kwa miaka kadhaa ijayo.
Baba, yakupasa kuishi kama mfano wa kuigwa kwa watoto wako kwa kupitia malezi unayowapa, matendo unayotenda kwa familia, jinsi unavyotatua migogoro baina yako na mwenza wako, lugha unayotumia, na kadhalika.
SOMA ZAIDI: Tunawezaje Kujenga Mahusiano Mazuri Kati ya Watoto Ndugu?
Mabinti na vijana wakimuona baba yao katika hali ya utu, heshima, asiyetumia ukatili na mwenye mahusiano yenye usawa huiga na kurithisha usawa katika vizazi vyao vijavyo.
Kuwa baba ni zaidi ya kucheza na mwanao. Kuwa baba na kutekeleza jukumu la malezi huanza mtoto angali tumboni. Huhusisha ushiriki wako katika kutunza mimba, kumsaidia mwenza wako katika kipindi hiki na kumuonesha upendo kwa kumsaidia majukumu ya malezi.
Ingawa kucheza na mwanao ni muhimu, vivyo hivyo kushiriki kazi za nyumbani na malezi ya watoto, hujenga ari ya kujituma na kuleta usawa wa kijinsia kwa watoto wa kiume na kumjengea mtoto wa kike uwezo wa kujitegemea na kujiamini.
Tafiti zimeonesha kuwa mabinti waliolelewa na baba wanaojihusisha na shughuli za nyumbani wana nafasi kubwa ya kuwa wachapakazi na kujikita katika ajira zenye maslahi makubwa.
Mazungumzo na mijadala ya wazi kati yako na mwenza wako ni nguzo ya malezi. Mara zote zungumzeni kuanzia mambo madogo na hata mipango mikubwa katika familia. Namna hii mnawasaidia watoto wenu kujua umuhimu wa kufikia maamuzi kwa mazungumzo.
SOMA ZAIDI: Kwa Nini Mzazi Anashauriwa Amnyonyeshe Mtoto kwa Miaka Miwili?
Kuna kuteleza na kuanguka katika kutekeleza jukumu la malezi. Usikatishwe tamaa na chanagamoto unazokumbana nazo, au makosa yanayojitokeza katika jitihada zako za kulea. Kulea hakujawahi kuwa rahisi lakini tunajifunza siku hadi siku.
Kama tunakubaliana na ukweli kwamba mtoto hawezi kuzaliwa bila ya baba na mama, basi tukubaliane pia kuwa mtoto hawezi kulelewa kikamilifu bila baba na mama. Nafasi ya baba katika malezi haiwezi kulinganishwa na kitu chochote kile!
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, na kupitia barua pepe yao www.sematanzania.org.