Mwanza. Mkutano wa kitaifa wa kutafakari na kujenga uelewa wa pamoja juu ya sheria za uchaguzi zilizopitishwa umemalizika Alhamisi, Mei 9, 2024, na kutoa azimio mahususi kwamba, ili chaguzi zijazo ziwe huru na za haki ni lazima mabadiliko ya Sheria yaliyofanyika yaende sambamba na mabadiliko madogo ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Aidha, wadau wametaka uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu 2924 usisimamiwe na Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na badala yake jukumu hilo liwe chini ya Tume Huru ya Uchaguzi, ambapo ili kufanikisha hilo Serikali imetakiwa kupeleka haraka bungeni muswada wa sheria ya usimamizi uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Hayo yote yamebainishwa kwenye mkutano huo uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kwa siku mbili kuanzia Mei 8, 2024, ukiandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), ukiwakutanishwa wadau mbalimbali kutoka kwenye vyama vya siasa, asasi za kiraia, mabalozi pamoja na waandishi wa habari.
Sheria ambazo wadau hao walikuwa wakizitafakari ni pamoja na Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani namba moja ya mwaka 2024, Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi namba mbili ya mwaka 2024, Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa namba tatu ya mwaka 2024 na Sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali namba nne ya mwaka 2024.
SOMA ZAIDI: Wadau Waingiwa Hofu Kuelekea Uchaguzi 2024, 2025
“Jambo mahususi la kwanza ni mabadiliko madogo ya Katiba ili kutanua wigo wa maoni na maboresho yanayotakiwa kufanyika wakati huo huo bila kusahau kuhuisha tena mchakato wa Katiba Mpya,” anasema Baruani Mshale ambaye ni Mkurugenzi wa Mafunzo kutoka shirika lisilokuwa la kiserikali la Twaweza, wakati akiwasilisha maazimio ya mkutano huo.
“Kufanya mabadiliko haya madogo kutawezesha yale mapendekezo katika hizi sheria za uchaguzi ambayo hayakuzingatiwa yaweze kuzingatiwa. Kwa sababu hoja zilitolewa ni kwamba mapendekezo hayo yanakinzana na yanakiuka vifungu mbalimbali vya Katiba.”
Kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa kusimamiwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mshale ameeleza kuwa sheria iliyounda tume hiyo, kifungu cha 10(1)(c) kimetanabaisha kuwa tume inaweza kufanya hivyo, lakini jambo hilo linatakiwa kutungiwa sheria.
Hata hivyo, ikiwa imesalia miezi minne kuelekea kufanyika kwa uchaguzi huo bado Bunge halijatunga sheria hiyo, jambo linaloonesha kwamba uchaguzi huo utafanyika chini ya TAMISEMI kwa kanuni za waziri mwenye dhamana na wizara husika.
Mkutano huo pia umeazimia kuwa kabla ya kufanyika kwa chaguzi zijazo, ipo haja ya kuboreshwa au kuandikwa upya kwa daftari la mpiga kura kwa sababu kuna hofu ya kuwa dafatri hilo kuwa na mapungufu tangu uchaguzi uliopita.
“Sisi tunasema daftari la mpiga kura ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha uchaguzi unakuwa, huru, haki na wa kidemokrasia,” Mshale anaeleza. “Katika chaguzi za huko nyuma tumesikia kwamba daftari la mpiga kura limeibua changamoto nyingi, kuna wanaosema kwamba lilivurugwa, lilichezewa. Sasa tunayofursa ya kuboresha ama kuliandika upya.”
SOMA ZAIDI: Je, Miswada Mipya ya Sheria za Uchaguzi Imekidhi Matarajio ya Wananchi?
Matumizi ya teknolojia nayo hayajaachwa nyuma, washiriki wa mkutano huo wametaka pia iwekwe wazi ni kwa namna gani teknolojia itatumika kwenye chaguzi ili kuondoa hali ya sintofahamu iliyopo sasa, kwani Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, kifungu cha 166 kimeeleza tu kuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi inaweza kutumia teknolojia.
Wadau wameshauri kuwa tekinolojia inaweza kupunguza mapungufu na gharama ambazo zipo wakati wa uchaguzi kwa kuwawezesha watu kupiga kura, kuhifadhi nyaraka na taarifa za uchaguzi na kutumika wakati wa kuandikisha na kuboresha daftari la kudumu la mpiga kura.
Azimio jingine mahususi ambalo washiriki hao wametaka lifanyiwe kazi ni suala la elimu ya mpiga kura. Suala hilo limeetakiwa kufanyiwa kazi kwa sababu mifumo ya sheria iliyopo sasa hivi imedaiwa kudunisha uwezo wa kutoa elimu hali inayopelekea jamii kuwa na hofu kutokana na kuwa na huo ufahamu mdogo kuhusiana na masuala ya uraia na masuala ya kupiga kura.
4R ziendelee kutumika
Mtazamo wa Rais Samia Suluhu wa kuliunganisha taifa kupitia falsafa yake ya R nne, ambayo ni maneno ya Kiingereza yanayomaanisha kujenga maridhiano, ustahimilivu, mageuzi na ujenzi mpya wa taifa umetakiwa pia kuendelea kutumika na vyama vyote vya siasa ili kufanikisha azma ya kuwa na demokrasia ya kweli.
SOMA ZAIDI: Maswali Fikirishi Kuhusu Falsafa ya 4R ya Rais Samia
“Tuendelee kuitumia hii fursa ya R nne iwezi kutuongoza katika ujenzi wa demokrasia yetu. Tunatofauti zetu ni nyingi ndiyo, lakini hizo tofauti zetu tuzitunie kama chachu ya ustawi wa demokrasia yetu na isiwe kama chanzo cha mifarakano baina yetu.”
“Tunaanza kuzisahau hizi R nne,” Mshale anasisitiza. “Na hapa ni vyema kusema kwamba inawezekana watu ambao labda hawatokei katika Chama cha Mapinduzi wasijisikie vizuri tukisisitiza matumizi ya falsafa ya R nne, wakiona kwamba wanaotokea vyama vingine waone kwamba hatuwatendei haki, lakini hii falsafa nadhani ni muhimu kwa vyama vyote katika mustakabali wa kujenga demokrasia yetu.”
Akizungumza wakati wa kufunga mkutano huo Mwenyekiti wa TCD, Profesa Ibrahim Lipumba, ameeleza kuwa kitu kilichofanyika kwa siku hizo mbili kimefanikiwa kwa kiasi kikubwa na yale waliyoadhia watahakikisha wanayafikisha kwa wahusika ili yaweze kufanyiwa kazi na kuleta tija haa nchini.
“Nasisitiza kweli mkutano huu umekuwa na mafanikio makubwa, watu wameweza kutoa fikra zao,” amesema Profesa Lipumba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF).
“Imeelezwa hapa kwamba maamuzi ya sisi wenyewe ni muhimu sana katika masuala haya. Kuna wakati watu wakitaka kuamua kufanya mambo mazuri inawezekana kuweza kuyatekeleza.”
Matonyinga Makaro ni mwandishi wa The Chanzo kutoka mkoani Mwanza. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia matonyingamakaro@gmail.com