The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tumeanza Vibaya AFCON 2025 Lakini Hatujuti

Lazima TFF na watu waliopewa dhamana ya benchi la ufundi wajue tunakoelekea kunahitaji uwajibikaji mkubwa zaidi ya ule wa ndani ya mpira wa miguu

subscribe to our newsletter!

Timu ya taifa ya soka ya Tanzania, Taifa Stars imeanza vibaya harakati za kusaka tiketi ya kucheza fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kulazimishwa kwenda sare ya bila kufungana na Ethiopia kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Si matokeo ya mechi hiyo yaliyowakosesha raha wapenzi wa mchezo huo maarufu nchini, bali hata jinsi timu ilivyocheza kuanzia kimbinu hadi kiufundi, ikiwaacha wageni wakitawala sehemu kubwa ya mchezo na kuonekana kama wao ndio wenyeji.

Ndio, usingetegemea Ethiopia icheze tofauti na ilivyocheza mechi hiyo kwa sababu mchezo wa kumiliki mpira ndio staili yao kubwa na silaha yao, lakini kitendo cha Stars kucheza kama walipania kujilinda zaidi kiliwanyima raha mashabiki na kukosa matukio ya kushangilia.

Viungo wawili, Himid Mao na Novatus Dismas, walipewa jukumu la kuilinda ngome upande wa kulia na kushoto, huku mchezaji ambaye ni beki asilia wa pembeni, Nickson Kibabage akipangwa kuanza kama mshambuliaji wa pembeni, ilikuwa ni kama kucheza kimkakati kujilinda zaidi kuliko kutafuta ushindi muhimu nyumbani na katika mechi ya kwanza.

SOMA ZAIDI: Ubashiri Hatma ya Samatta Stars Haukutakiwa Kuwepo

Kocha Hemed Suleiman “Morocco” hakuonekana kuchukulia au kukubali kuwa mkakati huo ulikuwa ni kosa kubwa wakati alipoongea na waandishi baada ya mechi. Badala yake akasema walijaribu kupitisha mipira katikati na baadaye pembeni, lakini hawakufanikiwa.

Alichoshangaza zaidi, kocha huyo, ambaye bado anasaka mafanikio katika ngazi ya klabu na taifa, akasema timu yake ni mpya na iko katika mabadiliko na hivyo mashabiki waivumilie na kuipa muda kabla ya kuanza kuikosoa.

Lakini hakuzungumzia mkakati huo wa kutumia viungo wawili kucheza nyma pembeni ya mabeki na mlinzi asilia wa pembeni kucheza kama winga, ulikwama wapi na sababu hasa za kuutumia kwenye mechi hiyo ya nyumbani ya kwanza ya mashindano na ambayo ushindi ulikuwa kitu muhimu cha kwanza kuliko sare, hasa unapocheza na timu ambayo viwango havipishani sana.

Ni kama alizungumza kutimiza wajibu na si kuwapa mashabiki majawabu mashabiki kuhusu kile walichokiona kuwa hakikuwa kimekwenda vizuri.

SOMA ZAIDI: Bodi ya Ligi Iondoe Hisia Hasi za Udhamini

Na tangu wakati wa maandalizi ya mechi niliona tabia ya Morocco kutowajibika kwa Watanzania akionekana kudhani kuwa anawajibika zaidi kwa viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) tu ambao hata waingie wote uwanjani, hawawezi kujaza sehemu ndogo ya jukwaa la wageni maarufu.

Alitangaza kikosi kwa kutuma taarifa kwa waandishi wa habari na hakuwa na maelezo mengine kuhusu timu aliyoiteua, wachezaji walioachwa na mategemeo yake au ushauri wake au umuhimu wa mashabiki kuelekea mechi hiyo.  Sikushangaa nilipoona uwanja mtupu kwa kuwa mashabiki hawakuwa na sababu ya ziada ya kuwasukuma kwenda uwanjani.

Kwa hiyo, siku hiyo ya mechi ilikuwa ni mbaya kwa mashabiki wachache walioenda uwanjani na wengi waliofuatilia mechi hiyo katika runinga. Hakukuwa na matukio ya kutosha ya kuwafanya mashabiki walipukwe kelele za shangwe kwa kuwa Wahabeshi ni kama walishika kila idara, na hasa sehemu muhimu ya kiungo.

Kwa hiyo, ukifikiria mechi zijazo dhidi ya Guinea na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), huoni matumaini zaidi ya kutegemea bahati na hivyo ile hamu ya mashabiki kujitokeza kwa wingi uwanjani kuishangilia timu yao, pia inafifia.

SOMA ZAIDI: Olimpiki Itupe Mtazamo Mpya Kwenye Michezo

Haya yanatokea wakati Tanzania ikijiandaa kuwa mwenyeji wa fainali za Mashindano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) mwishoni mwa mwaka huu, na fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) zitakazofanyika hapa nchini, Kenya na Uganda mwaka 2027.

Kocha Morocco na TFF wanashindwa kuchukulia uzito huo wa uenyeji wa fainali hizo na kuutafsiri kwa vitendo, kwa kuchukulia mashindano haya ya sasa kama sehemu ya muhimu ya maandalizi na pia fursa ya kuwafanya mashabiki wawe nyuma ya timu yao.

Baada ya kucheza mechi mbili zilizoandaliwa na Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA), maarufu kama FIFA Series, usingetegemea Stars iingie mechi ya Ethiopia kwa lengo la kutaka ivumiliwe kwa kwa kuwa ni mpya. Upya ungeshughulikiwa katika mechi hizo za kirafiki nje ya nchi. Kwanza upya huu ulianza lini wakati miezi kadhaa iliyopita ilishinda mechi muhimu ya ugenini dhidi ya Zambia ikiwa na karibu kikosi chote kilichocheza na Ethiopia?

Watanzania wanaambiwa upya huu baada ya sare ya nyumbani? Kwa nini wasingeambiwa mapema na kuhamasishwa kuiunga mkono timu yao wakijua kwamba ni mpya?

SOMA ZAIDI: Kulihitaji Utafiti Ligi Kuu Kutumia Uwanja wa Amaan

Unawezaje kuanza kuijenga timu bila ya wachezaji wazoefu kuwepo kikosini kwa ajili ya kuwagawia uzoefu? Mbwana Samatta, Simon Msuva, Muzamil Yasin, Shomari Kapombe na wengine waliokuwa muhimili wa timu na ndio wana uzoefu wa kutosha ambao unaweza kuwa mfano mzuri kwa wachezaji wapya ndani nan je ya uwanja, hawakuwepo!

Mbali na sababu zilizotolewa na Morocco, bado kocha mwingine wa Stars amekuja na lake kwamba sababu kubwa ni TFF kuruhusu wachezaji wageni 12 na kwamba eti Simba na Yanga zikitumia wageni nane kila moja na wazawa watatu, ni vigumu kupata timu ya taifa.

Inawezekana ikawa kweli, lakini ukweli huo umekuja baada ya sare ya nyumbani? Wakati makocha wanapewa timu, hawakujua kuwa kanuni inaruhusu wachezaji 12 wageni?

Tunaendaje CHAN na Afcon 2027 kwa staili hii?

Kingine kilichoshangaza ni benchi la ufundi kurundikwa watu wasio na stadi tofauti.  Juma Mgunda, Jamhuri Kihwelo na Amri Kiemba ni makocha waliofuzu walioongezwa benchi hilo kwa sababu zinazoonekana kuwa za kisiasa; kuweka taswira ya uzawa, kuweka taswira ya ujumuishaji au ushirikishaji na kuepuka kukosolewa na vyombo vya habari.

Ungetegemea kunapokuwepo na jopo kubwa kama hilo, labda Mgunda angekuwa kocha wa kikosi cha kwanza, mara nyingi kwenye ngazi ya klabu, labda Kiemba angeshughuilika na washambuliaji na Julio angeshughulika na mabeki kwa kuwa tayari kuna kocha wa makipa. Leo ukiulizia sababu za makocha hao kuwepo, utaambiwa ni kuongeza nguvu.

Lazima TFF na watu waliopewa dhamana ya benchi la ufundi wajue tunakoelekea kunahitaji uwajibikaji mkubwa zaidi ya ule wa ndani ya mpira wa miguu. Jasho la wananchi linalotoa kodi ndilo litatumika kuandaa fainali za CHAN 2024 na Afcon 2027.

Viwanja vinakarabatiwa, mwingine unajengwa mkoani Arusha, vyombo vya ulinzi na usalama vitatumika kuhakikisha fainali zinafanyika kwa amani na usalama, watumishi wa umma watatumika zaidi ya majukumu yao ya kawaida. Hawa wote watalipwa kwa kodi za wavuja jasho wa nchi hii.

SOMA ZAIDI: Lini Tutapunguza Kukimbilia Wachezaji wa Kigeni?

Kwa nini wahusika wasionyeshe kujali hilo? Kwa nini wahusika watoe majibu yasiyoakisi kuwajibika kwa Watanzania? Kwa nini kusionekane hamu na hamasa ya kufanya vizuri kuakisi mkakati wa serikali ya wananchi hao kuridhia michezo hiyo kufanyika Tanzania?

Ni muhimu TFF na benchi la ufundi kutambua kuwa mashindano ya kufuzu kwa Afcon 2025 na mengine ni fursa muhimu na haina budi kutumiwa kikamilifu. Hivyo ni lazima wahusika wakubali kwamba tumeanza vibaya mashindano ya kufuzu Afcon 2025 na kuonyesha kujutia ndipo tutajua tusahihishe wapi. Tukijiandaa kutoa visingizio, hatutajua tulikosea wapi.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts