The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tuache Kuwadhulumu Watoto kwa Kuwafukuza Shule za Umma kwa Kukosa Ada

Iwapo wanafunzi wengine wataondolewa kwenye shule ya mtaani kwao, kwa kuwa hawawezi kulipa ada katika mfumo wa elimu bila ada, ina maana kwamba shule imebinafsishwa kwa wanaolipa ada hii.

subscribe to our newsletter!

Eti shule haijauzwa, nani kasema? Iwapo wanafunzi wengine wataondolewa kwenye shule ya mtaani kwao, kwa kuwa hawawezi kulipa ada katika mfumo wa elimu bila ada, ina maana kwamba shule imebinafsishwa kwa wanaolipa ada hii. Si lazima bepari mmoja, au shirika fulani, wanunue. 

Imenunuliwa na wazazi ambao wako tayari kulipia elimu ya watoto wao katika shule ya Serikali, ndiyo maana watoto wasioweza kujiunga na kundi la wanunuzi wataondolewa, wakae palipo na kulia na kusaga meno kabla ya kulazimika kwenda mbali zaidi kutafuta shule.

Ndivyo ilivyo na siyo Ubungo tu. Shule nyingi za Serikali, shule zilizotegemea kodi zetu, zinageuzwa shule za wenye uwezo wa kulipa. Baada ya kuruhusu tabaka la juu kuwaondoa watoto wao na kuwapeleka shule za bei mbaya, sasa tunawaruhusu tabaka la kati nao wapate shule zao ili mradi wawe na pesa za kulipia. 

Tunabaki na shule za tabaka la kata!

Nawaelewa wazazi

Lakini sina budi kukiri kwamba nawaelewa wazazi hao walioshinikiza kupiga msumari mwingine kwenye jeneza la elimu ya umma. Tuache suala la lugha kwanza. Kama huwezi kutamba na Mavii 8, basi angalau upate gari la Toyota IST. Si afadhali kuliko bodaboda au baiskeli? Na ukijua kuendesha vizuri IST, unaweza kuvuruga Mavii 8 kwa utundu wa kuchepuka, kutanua, na kujipachika!

Hali ya elimu nchini Tanzania inasikitisha. Kwa muda mrefu sasa, wazazi wamekuwa wanapiga kura ya kutokuwa na imani na shule zetu za umma. Za umma zaumiza. Na si wakubwa tu. Wazazi wengi sana wanajinyima, wanatafuta kila senti, hata za ndugu zao, ili mtoto asomeshwe shule nyingine. 

SOMA ZAIDI: Richard Mabala: Je, Kupata Nafasi ya Shule Ni Kupata Nafasi ya Elimu?

Nawafahamu hata wauza mahaba, wanaouza haya ili watoto wasome shule isiyo ya umma. Hili ndilo tatizo. Zipo shule nzuri za umma, wapo walimu wazuri sana katika shule za umma, lakini, kwa ujumla, kiwango cha elimu kinachotolewa katika shule za umma kiko chini. 

Matokeo ya mitihani ya taifa yasitumike kama kipimo maana ugumu wa mtihani na kiwango cha kufaulu vinapangwa, na mitihani si kipimo cha kiwango cha uelewa na uwezo wa kufikiri wa wanafunzi, la hasha!

Kwa sasa, mitihani ni kipimo tu cha uwezo wa kukariri majibu “sahihi,” na kutotumia fikra tunduizi ndiyo maana kila mwaka wa mtihani wa taifa, wanafunzi hawasomi tena, hawapanui maarifa yao na uwezo wao wa kufikiri, bali wanafanya mazoezi ya kujibu mitihani tu.

Ndivyo hivyo. Wananchi wengi hawana imani na mfumo wetu wa elimu. Na bila shaka hawataki watoto wao wajichanganye na wasio na uwezo. Hivyo, wameshinikiza, na wamefanikiwa katika shinikizo lao, kujenga matabaka ya wazi ndani ya mfumo wa umma. 

Hii nayo haishangazi maana hali hii ipo tayari katika jamii yetu. Tuchukue afya, kwa mfano. Kuna wodi za kulipia ndani ya hospitali za umma. Watu wasiporidhika na huduma za wote, wanahangaika kupata huduma za upendeleo, hivyo wanatafuta pesa kwa udi na uvumba ili kupata upendeleo huu. 

SOMA ZAIDI: ‘Elimu Isipomkomboa Maskini, Basi Ndoto Yake ni Kuwa Mnyonyaji’

Upande wa elimu, nani hataki mwanaye asome katika shule yenye walimu wa kutosha na waliobobea, vitabu vya kutosha, madawati imara, sehemu nzuri ya michezo, na kadhalika? Sote tunataka. 

Na yawezekana wazazi wengine wanatafuta mambo hayo ya lazima kwenye elimu, si lugha tu. Kumbe, ili kupata mambo haya ya msingi ya elimu, inabidi tuwe na hela ya ziada.

Kwa hiyo, ni lazima kukiri sasa kwamba nchi yetu ni nchi ya matabaka ya wazi. Na kwamba elimu ni silaha kubwa zaidi ya kujenga matabaka haya; walionacho watapata walichokitaka wakati wasionacho walie tu. 

Maana ninao uhakika kwamba hata walimu wanaoonekana ni wazuri zaidi watatolewa huko walikokuwa na kupelekwa kwenye shule hizi za walionacho kiasi. Labda hatua itakayofuata ni kuwa na madarasa ya kulipwa ndani na shule zote. 

Wenye kutoa pesa kidogo watasoma kwenye madarasa bora ndani ya shule hiyohiyo. Msishangae. Nani alitegemea matabaka ndani ya shule za umma?

Silaha ya kitabaka

Na tusidanganyanye. Lugha ya kufundishia na kujifunzia pia ni silaha ya kitabaka. Kuwa na mfumo wa mitihani wa Kidato cha Nne ambao unawaweka pamoja waliotumia Kiingereza kama lugha ya kujifunzia kuanzia chekechea na waliotumia Kiswahili hivyo hadi mwisho la darasa la saba tayari inawahukumu walio wengi kuwa raia wa daraja la pili. 

Bado najiuliza hawa wa Ingilishi Medium wakiingia Kidato cha Kwanza na wenzao waliosoma kwa Kiswahili, mwalimu atafundishaje? Upande huu, wako wanaoelewa sana na wanacheleweshwa kupata maarifa zaidi. Upande ule, wako walio wengi ambao hawamwelewi mwalimu hata ukiweka wiki sita au 12 ya Kiingereza mwanzo wa Kidato cha Kwanza. 

SOMA ZAIDI: Je, ‘English Mediums’ za Serikali Zinakinzana na Sera ya Elimu Bila Ada?

Sikatai, wapo ambao watatoboa. Ikifika kama Kidato cha Tatu au cha Nne watawafikia ‘Waingereza’ na hata kuwapita kutokana na juhudi zao. Lakini walio wengi hawawezi kutokana na usuli na muktadha yao, na kwa nini walazimike hivyo? 

Tayari tunazidi kuwagawa watoto wetu katika matabaka. Wapo walionacho na zaidi … tabaka la walioukata, walionacho cha kujitafutia kwa nguvu, tabaka la kati, na wasionacho, tabaka la kata.

Sijui lini tutatambua kwamba kwa njia hii tunavunja mikataba ya haki za binadamu na ile ya haki za watoto. Haki ya kufikia elimu haiishii tu kwenye haki ya kukaa darasani. 

Haki ya kupata elimu ina maana kwamba watoto wanaelewa wanachofundishwa, wanaweza kushiriki na kuchangia darasani, wanaendeleza stadi zao za ubunifu na fikra tunduizi. 

Hii ndiyo elimu, sio uwezo wa kuimba lugha ya kigeni. Nimeongea na wanafunzi wengi sana wa sekondari na walio wengi wangependa kusoma kwa lugha ya Kiswahili. Kwa nini? Wanataka kuelewa tunachofundishwa.

Na usinichoshe na propaganda ambazo zimetumika kuwadanganya wazazi. Ndiyo, kwa sasa lugha ya Kiingereza ni muhimu ili kufikia maarifa mengi, na hatimaye hata kufikia ajira mbalimbali. Ili watoto walio wengi, na si tabaka dogo, kufikia hayo, kwa nini hatufundishi lugha kitaalamu? 

SOMA ZAIDI: Kwa Kung’ang’ania Kiingereza, Rasimu ya Sera ya Elimu Imeshindwa Kuzingatia Maslahi ya Wengi

Kitaalamu, kutumia lugha ambayo wanafunzi walio wengi hawaimudu kama lugha ya kujifunzia ni kuvuruga kabisa uwezo wao wa kuelewa lugha hii pamoja na masomo yote. Ni njia bora ya kuwanyima walio wengi elimu na lugha. 

Ndiyo maana nchi zote duniani ambazo hazikutawaliwa na Waingereza, au Wafaransa, wanatumia lugha yao ya taifa katika elimu, halafu wanakuwa na walimu wazuri kabisa waliobobea kufundisha lugha ya Kiingereza kama somo. Hapo watoto wao wanapata elimu na pia wanapata lugha.

Visingizio

Mara oooh, nchi jirani. Huko shule za kata na ukata za nchi jirani, watoto hawaelewi pia. Tunaowaona wanatamba wametoka shule za tabaka la juu. Mara ooh, mbona wanafeli Kiswahili pia? Hata asilimia 30 ya Waingereza wanafeli Kiingereza. 

Kuna tofauti ya lugha kama somo na lugha kama chombo cha kuelewa masomo mengine. Tofauti kubwa kabisa. Hivyo, wale asilimia 30 ya Waingereza wanaofeli Kiingereza wanafaulu mitihani mingine.

Mara ooh, kwa nini tusifundishe kwa kutumia Kiingereza tangu chekechea? Usinichekeshe! Hadi sasa ni shida kupata walimu wa masomo yote kufundisha kwa lugha ya Kiingereza katika shule za sekondari, iweje shule za msingi? Malaki ya walimu wenye Kiingereza kizuri!

Mara ooh, mbona mimi nilifaulu. Hongera sana, ulitoboa, lakini inategemea ulikaa katika muktadha gani, muktadha ulio na Kiingereza kiasi, ulikuwa na walimu gani, na uwezo wako wa kutoboa. 

Tusisahau kwamba huko nyuma mchujo ulikuwa mkali na walio wengi walitupwa palipo na kulia na kusaga meno. Sasa, tunawaruhusu wote kuingia mahali patakatifu pa shule na kuwatupa tena kwa sababu ya lugha.

Kwangu mimi, na akili yangu mbovu, jibu ni rahisi sana. Waache watoto wasome na kufanya mitihani katika lugha wanayoielewa angalau hadi Kidato cha Nne, ambacho sasa kinahesabiwa kama elimumsingi. Kisha tufundishe lugha ya Kiingereza kitaalamu, badala ya kiholela. 

Hapa, watapata elimu na lugha, na tutakomesha unfair advantage ya kitabaka!


Richard Mabala ni mdau wa masuala ya elimu, mshairi na mwandishi wa vitabu. Anapatikana kupitia rmabala@yahoo.com au X kama @MabalaMakengeza. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Je, ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts