Wadau na wanaharakati wa masuala ya haki za kimtandao wana khofu kwamba wakati Watanzania wakielekea kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 2020 Serikali inaweza kuchukua hatua za kudhibiti matumizi ya intaneti, hususani mitandao ya kijamii, na hivyo kuhatarisha ukiukwaji wa haki za msingi za wananchi wake kama vile uhuru wa kujieleza.
Mitandao ya kijamii, hususani ile ya Facebook, WhatsApp, Twitter, na Instagram, imekuwa majukwaa mashuhuri kwa siku za hivi karibuni ambapo watu hutumia majukwaa hayo kuelezea hisia na maoni yao juu ya mambo mbali mbali yanayotokea katika nchi yao.
Inategemewa kwamba zaidi ya kipindi chochote kile, mitandao hii itachukua nafasi ya kipekee katika uchaguzi unaokuja hali ambayo imesababisha hofu miongoni mwa wafuatiliaji wa masuala hayo kwamba Serikali inaweza kushawishika kuchukua hatua zilizozoeleka kuchukuliwa na nchi zingine: kubana matumizi ya, au kuzima, intaneti.
Tanzania haina sheria inayoipa mamlaka Serikali kuzima intaneti. Hata hivyo, kanuni za maudhui mitandaoni zinaipa nguvu Mamlaka ya Mawasiliano (Tcra) kuwaamrisha watoa huduma kuziua au kuchuja baadhi ya maudhui kama Tcra itadhani kwamba maudhui hayo hayakubaliki, anasema Daniel Marari, ambaye ni mwanasheria wa haki za binadamu.
“[Namna kanuni] zinavyofanyakazi ni kwamba zimekasimisha nguvu za udhibiti na nguvu za kutoa maudhui mtandaoni kwa watoa huduma,” anasema Marari wakati wa mahojiano na The Chanzo. “[TCRA] inaweza kuwaelekeza watoa huduma za intaneti kuchuja, au kuzuia kabisa, baadhi ya tovuti au kuyatoa [mtandaoni] baadhi ya maudhui. Kama hawatotii, wanaadhibiwa. Hii ni njia isiyo ya moja kwa moja ya kuzuia upatikanaji wa baadhi ya maudhui au huduma.”
Hali hii inawapa watu wengi wasi wasi juu ya hatma ya uhuru wa intaneti tukielekea kwenye uchaguzi mkuu na moja kati ya watu hao ni Zaituni Njovu, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na kukuza uelewa miongoni mwa wananchi, hususani wanawake, juu ya suala zima la haki na usalama mtandaoni Zaina Foundation. Wakati wa mahojiano maalumu na The Chanzo yaliyofanyika ofisini kwake Kunduchi, Dar es Salaam, hivi karibuni, Njovu, 30, anasema uwezekano wa Serikali kuzima intaneti ni mkubwa mno kutokana na viashiria kadhaa ambavyo vimeonekana tayari katika kipindi cha hivi karibuni.
“Viashiria hivi ni kama vile kuminywa kwa uhuru wa kujieleza na haki zingine za mtandaoni,” anafafanua Njovu. “Tayari tumeshasikia malalamiko ya Serikali kwamba mitandao ya kijamii inatumika kusambaza habari za uongo. Kuwa na uzimwaji wa moja kwa moja wa intaneti ni ngumu kwani hii itaiathiri hata Serikali yenyewe. Lakini kinachoweza kufanyika ni hivyo kuzima mitandao ya kijamii.”
Ni katika muktadha huo ndiyo kampeni ya #KeepItOnTZ, au #NaiwakeIntaneti, ilizinduliwa kuhakikisha kwamba Serikali haichukui hatua yoyote ya kuzima intaneti kwani inaweza kuwa na madhara makubwa katika ushiriki wa wananchi katika uchaguzi unaokuja. (The Chanzo iliandikia Tcra kwa kutaka kupata ufafanuzi juu ya masuala haya lakini haikuweza kupokea mrejesho wowote kutoka kwao. The Chanzo pia ilimtumia ujumbe wa WhatsApp Mkurugenzi Mkuu wa Tcra, James Kilaba, kupata mtazamo wake juu ya jambo hili lakini haikuweza kupata mrejesho wowote, licha ya ujumbe aliotumiwa kuonesha alama mbili za blue, kuonesha kwamba ujumbe ulimfikia na aliusoma).
Yafuatayo ni sehemu ya mahojiano ambayo The Chanzo ilifanya na Njovu. Endelea…
The Chanzo: Kwanza asante kwa kutenga muda wako na kukubali kuongea na sisi, tunashukuru sana. Labda kwa ufupi tu, na kwa niaba ya wasomaji wetu, unaweza kutueleza Zaina Foundation ni nini na ipo kwa ajili ya kufanya kazi gani?
Njovu: Zaina Foundation tulianza rasmi mwaka 2017 na tulikuwa tukifanyia shughuli zetu Arusha. Mnamo mwaka 2019, moja kati ya wadau wetu akatushauri tuhamie Dar es Salaam kutokana na kazi zetu nyingi tunazofanya tunafanyia hapa.
Sisi kwanza kabisa tunashughulika na wanawake kwenye maeneo kama vile usalama wa kimtandao kwa makundi mbali mbali ya wanawake lakini haswa haswa kwa wanawake waandishi wa habari. Kuna miradi mbali mbali inaendelea kwa ajili wa waandishi wa habari, ikiwemo kuongeza uelewa wao juu ya masuala ya usalama wao mitandaoni.
Pia tunafanya kampeni mbali mbali kuhusu haki za kimtandao, kwa sababu kusema kweli Tanzania tuna changamoto nyingi sana kwenye eneo hilo. Kama sehemu ya kampeni yetu, tunatafsiri kwenda Kiswahili zana na maudhui tofauti tofauti zinazolenga kuongeza usalama wa mtu wakati wa kutumia intaneti kwani tuligundua kwamba zana na maudhui hayo kubaki katika lugha ngeni inafanya kuwa ngumu watu kuelewa thamani na matumizi yake.
Mpaka sasa tumeweza kuifanya app ya Signal kupatikana kwenye Kiswahili kwa watumiaji wa Android.
The Chanzo: Umegusia kwamba Tanzania ina changamoto nyingi linapokuja suala la haki na usalama wa kimtandao, tungependa tu utufafanulie kwa kina ni zipi haswa hizi changamoto?
Njovu: Tanzania kusema ukweli ni kwamba hatuko vizuri kwenye eneo la haki na usalama wa kimtandao. Uhuru wa kujieleza na uhuru wa watu kushiriki mitandaoni ni mdogo sana Tanzania [ukilinganisha na nchi zingine]. Kuna wadau wawili wa kulaumiwa kwa hali hiyo. Kwanza, ni mamlaka za Serikali ambazo zimekuwa zikiwanyima watu haki [zao za msingi] iwe ni kwa kuwatishia kwa maneno au kwa kutungwa sheria zinazokiuka haki hizo.
Mdau wa pili ni watoa huduma ya intaneti, au mitandao ya simu, ambao huminya ushiriki wa watu mitandaoni kwa kutoza gharama kubwa kwa watumiaji wa intaneti nchini. Gharama za vifurushi vya intaneti ni kubwa mno. Hiyo ni moja, pili ni kwamba hata hivyo vifurushi vyenyewe havifanyi kazi kama vile inavyotangazwa. Unaweza kuambiwa kifurushi ni cha wiki lakini kikamaliza ndani ya siku moja tu na hata matumizi yake hayaeleweki. Huna mahali pakuuliza, ikikutokezea ndo imeisha hivyo.
Kuna suala jengine pia. Unaweza kumudu gharama ya kifurushi na kweli kikabaki kama ulivyokusudia lakini mtandao ukawa unasumbua kiasi ya kwamba unashindwa kufanya shughuli zako ulizokusudia kufanya na kifurushi hicho. Hizi zote zinachangia kudumaza haki na uhuru wa watu wa kujieleza. Changamoto hizi na zingine zinakatisha watu tamaa kutumia haki zao za kuwa katika mtandao na zimechangia kuwa na hali tuliyonayo leo kama taifa.
The Chanzo: Hivi karibuni Serikali, kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano (Tcra), ilitoa kanuni iliyoelekeza kwamba mtu haruhusiwi kumiliki zaidi ya laini moja ya simu na kukaibuka mkanganyiko mkubwa miongoni mwa watumiaji wa simu. Kwanza tunaomba utuchanganulie mkanganyiko huu na pili unaielezeaje hatua hiyo katika mtazamo wa haki za kimtandao?
Njovu: Cha msingi ni kwamba Serikali inataka kila mtu awe na laini moja tu ya simu. Sasa hii kwanza inaminya uhuru wa mtu wa mawasiliano. Kwa sababu kama mimi naweza kumudu kuwa na laini tano [za simu] kwa nini nisiwe nazo?
The Chanzo: Unadhani ni nini kilimeishajihisha Serikali kuchukua hatua hii?
Njovu: Kuna kitu kinaitwa ‘surveillance and censorship,’ au uchunguzi na udhibiti kwa Kiswahili. Kwa sasa, hili ni tatizo kubwa sana nchini: kutazamwa kila wakati ili uweze kudhibitiwa. Kwa sasa Tanzania inatumia utaratibu kusajili laini za simu kwa kutumia alama za vidole, au ‘biometric registration’ kama wanavyooita kitaalamu. Lengo kubwa ni kwa ajili ya kufanya uchunguzi kwa raia wake. Kwa sababu hili ndiyo lengo, inakuwa ni rahisi kulifanikisha endapo kila mtu anatumia laini moja tu ya simu.
Serikali yenyewe inajitetea kwamba utaratibu huu unasaidia kuzuia uhalifu, kwa sababu uhalifu wa mitandaoni umekuwa uko juu, ikiwemo watu kudhulumiwa kwa kutumia [laini] simu. Lakini hiyo haindoi ukweli kwamba utaratibu huo unakiuka haki zetu kama raia, za kibinadamu na za kimtandao pia.
The Chanzo: Unaiamini Serikali inaposema kwamba inawachunguza na kuwadhibiti raia wake eti kwa sababu inapambana na uhalifu?
Njovu: Hapana. Ni kweli kwamba moja kati ya faida ya huu utaratibu ni kuzuia huo uhalifu. Lakini ujuwe kuna suala la faragha pia. Ukimfanyia mtu uchunguzi [kwenye mawasiliano yake] inakuwa umeingilia ile haki yake ya kuwa na faragha mtandaoni. Mimi ninapaswa kuwa na faragha yangu na mawasiliano yangu yabaki kuwa yangu na kusiwe na mtu wa kuyaingilia.
The Chanzo: Katika mazingira kama haya, unatathmini vipi uelewa wa Watanzania juu ya haki zao na usalama wao mitandaoni?
Njovu: Uelewa uko chini. Hii inatokana na ukweli kwamba eneo la usalama na haki za kimtandao linawadau wachache sana wanaolipigia chapuo. Zaina Foundataion wenyewe tunashirikiana sana na wadau kutoka Kenya na Uganda kwa sababu Tanzania ni wachache sana, takribani hakuna. Kinachohitajika kwa sasa ni kuongeza kupaza sauti na kuhamasisha wananchi katika mambo haya.
The Chanzo: Ungependa kuona Tanzania ya aina gani miaka 10 inayokuja katika eneo zima la usalama na haki za mtandaoni na unadhani ni wadau gani muhimu wanaweza kufanikisha dira hiyo?
Njovu: Kimsingi siyo miaka kumi ijayo, hivi sasa kwetu sisi kama shirika tunataka Tanzania ambayo watu wawe na uhuru kwanza wa kutumia intaneti. Tunataka ifike mahali ambapo kama mtu mmoja atashtumiwa kusambaza habari za uongo, mtu mwingine aje akanushe, au aliyetoa habari za uongo aamriwe asahihishe [na siyo kumkamata na kumfunga]. Serikali, makampuni ya simu, asasi za kiraia na jamii kwa ujumla, kama wadau muhimu sana katika kufanikisha hili, wanayo nafasi kubwa ya kuibadilisha Tanzania na kuwa nchi salama kwa watumiaji wa intaneti.