The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Nioneshe Chama Kilichotayari Kurithi Mikoba ya CCM Kama Chama Tawala ‘Tanzania’

Siasa za vyama vya upinzani zenye kuashiria chuki dhidi ya kikundi fulani cha wananchi ni zawadi kwa CCM inayoiwezesha kuendelea kubaki madarakani.

subscribe to our newsletter!

Mara yangu ya kwanza kupiga kura ilikuwa ni mwaka 2015, nikichelewa kwa miaka mitano kutimiza wajibu wangu huo wa kiraia. Mara yangu ya kwanza ilipaswa iwe mwaka 2010, lakini kipindi hicho nilikuwa mdogo kiasi, nilikuwa Kidato cha Nne, na sikuwa na mwamko wa kifikra niliokuwa nao miaka mitano baadaye.

Uchaguzi mkuu wa 2015 ulinikuta nikiwa chuo kikuu, mwaka wangu wa pili, na lazima niweke wazi kwamba mimi sikuvutwa hata kidogo na upepo wa John Magufuli aliyekuwa akipeperusha bendera ya Chama cha Mapinduzi (CCM), akipambana na Edward Lowassa wa CHADEMA, akiungwa mkono na vyama vingine vya upinzani, kugombea urais wa ‘Tanzania.’

Kwenye uchaguzi huo, kura zangu zote – urais, ubunge na udiwani – zilienda kwa wagombea wa upinzani, hali iliyojirudia kwenye uchaguzi mkuu wa 2020 ambapo hakuna kura niliyopiga kwa wagombea wa CCM. Hapa ilikuwa tayari Magufuli ameshatuchachafya kwa miaka mitano, na nilitamani sana Tundu Lissu, wa CHADEMA, amtoe madarakani, na kuhimiza wenzangu wafanye hivyo.

Mwenendo wangu wa kupigia kura upinzani hata haujawahi kushawishiwa na sera, au hoja, za wagombea kutoka upande huo wa kisiasa. Kusema ule ukweli, niliwapigia kura Lowassa na Lissu licha ya ukweli kwamba sikuwa nakubaliana na baadhi ya sera zao, ambazo nyingi zilikuwa hazieleweki kwa wananchi, na wala baadhi ya hoja zao zilikuwa hazinishawishi hata kidogo.

Uwajibikaji

Msukumo mkubwa ni imani yangu kwamba ili kupata Serikali inayojali kweli maslahi ya umma ni lazima yawepo mazingira ambayo yatakifanya chama kilichopo madarakani kujua kwamba kinaweza kutolewa madarakani; yaani, kuwepo kwa mazingira ambayo wananchi kweli wanaweza kukiadabisha, na kukiwajibisha, chama tawala kwenye uchaguzi.

SOMA ZAIDI: Labda Suluhu ya Serikali Kudharau Maoni ya Wananchi ni Kuacha Kushirikiana Nayo?

Mazingira kama hayo yana faida nyingi sana ambapo, mbali na kukifanya chama kinachokabidhiwa madaraka kuenenda kulingana na matakwa na maslahi ya wapiga kura, wananchi wengi pia wanaweza kuona mantiki ya kushiriki kwenye chaguzi, wakifahamu kwamba kweli kura zao zinaweza kuleta mabadiliko wanayoyataka. Kumbuka, ni wananchi wachache sana hujitokeza kupiga kura ‘Tanzania,’ na sababu zimewekwa hadharani.

Msukumo mwingine ni imani yangu kwamba CCM imeshakaa sana madarakani kiasi ya kwamba imesahau kwamba Tanzania ni jamhuri na siyo nchi ya kifalme. CCM pia imeshakaa sana madarakani kiasi ya kwamba haina mawazo na fikra mpya za kutatua matatizo mapya yanayoibuka kila siku katika nchi yetu, pamoja na yale iliyoyasababisha yeye yenyewe.

CCM, na kabla yake TANU na ASP, inaweza kuwa imetoa mchango mkubwa kwenye kujenga, au kuharibu, kimsingi, Tanzania tunayoiona leo hii, na muda umefika wa kuiambia kwamba imetosha na inahitaji kuondoka. CCM inahitaji kuchukua likizo ambayo itaiwezesha kutafakari baadhi ya makosa ambayo imekuwa ikifanya na kupelekea kutolewa madarakani.

Pengine CCM kinaweza kuwa chama kizuri, chenye kutumikia wananchi, lakini naamini hiyo labda inawezekana endapo tu kama kitakaa nje ya madaraka hata kwa nusu muongo na kupata wasaa wa kuitafakari safari yake na kuona wapi ilijikwaa. Binadamu tunahitaji wasaa wa kutafakari maisha yetu, na nadhani hata taasisi, kama vyama vya siasa, vinahitaji wasaa huo pia.

Kama ambavyo iko kwa mwanadamu kwamba hawezi kufanya tafakuri pana kuhusu maisha yake akiwa sehemu yake ya kazi, akishauriwa kufanya hivyo wakati wa likizo ndefu, ndivyo hivyo hivyo kwa CCM, kwamba haiwezi kufanya tafakuri ikiwa itaendelea kuwepo madarakani. Kazi hiyo itafanyika kwa ufanisi pale tu chama hicho kitakapokuwepo nje ya madaraka.

Muda mrefu

Hata hivyo, nikiri kwamba kuitoa CCM madarakani inaweza kuchukua muda mrefu zaidi kuliko vile nilivyokuwa nategemea hapo awali. Ukiachilia mifumo ambayo CCM imejijengea na kuifanya iwe ngumu kutoka madarakani, kama vile kuvunja mpaka kati yake na dola, kiasi ya kwamba sasa dola ni CCM na CCM ni dola, kuna makosa vyama vyetu vya upinzani vinayafanya na kuipa CCM ushindi rahisi, hususan kwenye mitazamo ya wananchi.

SOMA ZAIDI: Tunahitaji Makavazi Mengi Zaidi ya Kidijitali Kama Lile la Salim Ahmed Salim

Maana, sisi bado ni Watanzania, tuliotokana na Muungano wa nchi mbili huru, Tanganyika na Zanzibar. Tunaweza kuwa na maoni tofauti kuhusiana na jambo hili, kama ilivyo kwa mambo mengine mengi tu, lakini ukweli unabaki kwamba sisi, mpaka muda wa kuchapisha makala haya, ni Watanzania, na umoja wetu wa kitaifa unazingatia ukweli huo.

Na umoja wa kitaifa, taifa la ‘Tanzania,’ kumbuka, ni suala muhimu na nyeti sana ambalo ungetegemea chama chochote cha siasa chenye lengo la kuunda Serikali ya ‘Tanzania,’ yenye uungwaji mkono kwenye iliyokuwa Tanganyika na Zanzibar, kingelichukulia kwa umakini sana. Katika pointi hii, lazima niseme kwamba, kwa masikitiko makubwa, CCM inavipita vyama vingine vya siasa hapa nchini, na silisemi hili kirahisi-rahisi.

Chuki

Katika nyakati mbalimbali, na za hivi karibuni kabisa, vyama vyetu vikuu viwili vya upinzani nchini, CHADEMA na ACT-Wazalendo, kupitia viongozi wao na wanachama wao waandamizi, vimekuwa vikitoa matamshi yenye kuacha maswali mengi kuhusu umakini na udhati wao kama vyama vyenye lengo la kuunda Serikali ya ‘Tanzania’ siku moja. 

Matamshi haya ni yale yenye kuashiria chuki dhidi ya watu wa upande mmoja wa Muungano na yenye lengo la kuwagawa Watanzania kulingana na maeneo yao wanayotoka; ni matamshi yenye lengo la kuwachonganisha watu wanaokandamizwa kutoka iliyokuwa Tanganyika na Zanzibar ili wapigane wao kwa wao na kuwaacha huru watesi na wakandamizaji wao.

Mnamo Juni 7, 2023, kwa mfano, akielezea msimamo wa chama chake kuhusiana na mkataba tata kati ya Tanzania na Serikali ya Dubai kuhusu ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uendelezaji wa bandari za bahari na maziwa makuu, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alitumia Uzanzibari wa Samia Suluhu Hassan, siyo kama Rais wa Tanzania, kuikosoa hatua tata ya Serikali yake kukubali masharti ya mkataba huo.

SOMA ZAIDI: Tutawezaje Kubuni Katika Mazingira ya Uhuru wa Mashaka?

Ilikuwa ni kauli iliyowashangaza wengi kwani Mbowe angeweza kuukosoa mkataba huo bila ya kutoa kauli iliyoashiria kujenga chuki dhidi ya watu wa Zanzibar. Kilichoshangaza zaidi ni kumuona Mbowe aking’ang’ania msimamo wake, akionesha kutotambua kabisa hatari inayoweza kuletwa na matamshi yake, akisema hapo Julai 21, 2023, kwamba “hajutii” chochote kuhusiana na kauli hiyo.

Katika hali iliyoonesha kutokujifunza kabisa kutokana na makosa hayo ya kiongozi mwenzake, mnamo Aprili 26, 2024, akihutubia mkutano wa hadhara mkoani Manyara, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA (Tanzania Bara), Tundu Lissu, alifuata nyayo za Mbowe kwenye kutumia Uzanzibari wa Samia katika ukosoaji wake wa hatua ya Serikali kunyanyasa jamii za kifugaji katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Na kama ilivyokuwa kwa Mbowe, kufuatia ukosoaji mkubwa ulioelekezwa kwenye matamshi yake hayo, Lissu alijitokeza hadharani, wakati wa mkutano wa hadhara mkoani Dodoma hapo Aprili 29, 2024, akitoa kile ninachoweza kukiita utetezi usiyokuwa na utetezi, akikataa kukiri kwamba alikuwa amekosea kwa kutoa matamshi yake hayo.

Moja kati ya mambo haya matatu linaweza kuwa kweli kuhusiana na hatua za viongozi hawa wawili waandamizi wa CHADEMA. Moja ni kwamba wanawachukia Wazanzibari. Pili ni kwamba suala la umoja wa kitaifa siyo kipaumbele kwao kama chama. Tatu ni kwamba viongozi wetu hawa wanakosa umakini kwenye hotuba zao kiasi ya kwamba muda mwingine hujiruhusu kutekwa na mhemko na kutoa kauli hatari kama hizi.

Wapo baadhi ya watu ambao hawaoni tatizo lolote na kauli hizi, wakiuliza, kila wakati mtu anapozikosoa, kwani Samia siyo Mzanzibari? Mara nyingi nimekuwa nikiwataka watu hawa watoe neno ‘Mzanzibari’ kwenye matamshi ya wanasiasa hawa na waweke neno ‘Muislamu’ au ‘Mwanamke’ halafu waseme je, wangekuwa na msimamo huohuo? Maana Samia ni Mzanzibari kweli, lakini pia ni Muislamu na Mwanamke. Je, tungeruhusu mtu atumie Uislamu na Uanauke wake kumkosoa?

SOMA ZAIDI: Eid Al Fitr Ikawe Chachu ya Kukoleza Mapambano Yetu Dhidi ya Aina Zote za Ukatili 

Lakini si viongozi kutoka kwa iliyokuwa Tanganyika tu ambao wamekuwa wakitoa kauli zenye kuashiria chuki dhidi ya Wazanzibari kwa siku za hivi karibuni; viongozi wa kisiasa kutoka Zanzibar na wao hawako nyuma katika kutoa matamshi yenye kuashiria chuki dhidi ya Watanganyika, huku tukishuhudia wakipata uungwaji mkono na Wazanzibari wenzao waliowengi tu.

Kiongozi wa hivi karibuni kabisa kufanya hivyo ni Mbunge wa Konde (ACT-Wazalendo), Mohamed Said Issa, aliyezungumza Bungeni hapo Aprili 23, 2024, kuhusiana na haja ya visiwa vya Zanzibar “kulindwa” dhidi ya “wahamiaji” kutoka iliyokuwa Tanganyika, anaohofia “kuijaza” Zanzibar, akipendekeza utaratibu wa watu kutoka sehemu hiyo ya Muungano kuingia Zanzibar kwa hati za kusafiria urejeshwe!

Ingawa Issa hashikilii nafasi yoyote ya uongozi ndani ya ACT-Wazalendo, ukimya wa chama hicho mshirika kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) Zanzibar unaashiria kutokukasirishwa na matamshi ya mwakilishi huyo wa wananchi kupitia tiketi ya chama hicho. Kama ACT-Wazalendo inalichukulia suala la umoja wa kitaifa kwa uzito, ingejitenga na kauli ya mwanachama wake huyo na hata kumkaripia. 

Kaka mkubwa?

Mbali na kauli hizi za waziwazi, ni nadra sana pia kwa vyama hivi vya upinzani kusikika vikihimiza umoja wa kitaifa wa ‘Kitanzania’ miongoni mwa wanachama wao, vikiiachia CCM nafasi ya kujibaragua kwenye eneo hilo, hali inayokifanya kionekane kama kaka mkubwa ndani ya nyumba, anayezingatia maslahi ya kila mmoja, kwenye macho ya baadhi ya Watanzania.

Bila shaka CCM haijali umoja wa kitaifa, kama inavyojidhihirisha kwenye kunajisi michakato ya kidemokrasia, kama vile chaguzi, ili kulinda maslahi yake finyu ya kisiasa. Lakini kwenye siasa uhalisia, au reality, wa mambo haujalishi sana; kinachojalisha ni mtazamo, au perception, tu wa wapiga kura, na kama CCM itaamua kuuza mtazamo huo kwa wananchi, ukweli ni kwamba hakutakuwa na uchache wa wateja.

SOMA ZAIDI: CCM Hawako Tayari kwa Mageuzi Lakini Suluhu Siyo Kususia Uchaguzi

Nihitimishe safu hii kwa kusema kwamba natamani vyama vyetu vya upinzani vingefanya vizuri zaidi ili kujitanabahisha kama mbadala wa kweli wa CCM. Viongozi, na wanachama, na hata wafuasi wa upinzani, wanapaswa kuwa makini na matamshi yao ili wasichangie kwenye kuwagawa wananchi katika misingi ya maeneo wanayotoka na hivyo kupandikiza chuki miongoni mwao.

Matendo yote ya vyama vya upinzani yanayoweza kujenga mtazamo hasi kwenye akili na mawazo ya wananchi ni hasara kwa vyama hivyo na faida kwa CCM ambayo, lazima niseme, imedhamiria kutumia njia zozote, za halali na zile za haramu, kubakia madarakani kwa gharama kubwa ya ustawi na uhuru wetu kama wananchi.
Khalifa Said ni mwandishi na mhariri wa The Chanzo. Unaweza kumpata kupitia Khalifa@thechanzo.com au X kama @ThatBoyKhalifax. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Mada nzuri, ila nina ombi, unaweza badili muonekane wa maandishi, usiwe concentrated katikati tu (center) uwe wa mwanzo hadi mwisho ili iwe rahisi kusoma na kutochosha kuhamisha macho kwenda mstari wa pili kila baada ya maneno mawili 🙏 natumain utalifanyia kazi na hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *