Dar es Salaam – Mnamo Aprili 23, 2026, Rais Samia Suluhu Hassan alipokea ripoti kutoka kwa Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Ghasia na Uvunjifu wa Amani Yaliyotokea Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Ifuatayo ni hotuba Rais Samia aliitoa kwenye hafla iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, punde baada ya Mwenyekiti wa Tume, Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman kuwasilisha matokeo ya uchunguzi wake, ambayo, pamoja na mengineyo mengi, ni matokeo kwamba kilichotokea hayakuwa maandamano bali ghasia.
Angalizo la Mhariri: Maudhui yafuatayo yamehaririwa kuboresha usomaji mzuri:
Waheshimiwa viongozi na ndugu wananchi, sisi sote tuliokusanyika hapa, na Watanzania wote, hatuna budi kuungana kwa pamoja kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai na siha njema, na kutuwezesha kushuhudia tukio hili la leo kwa mustakabali wa taifa letu. Hili ni tukio muhimu kwa kuwa sote tulilisubiri ili tuelewe uhalisia wa matukio ya Oktoba 25 na mwelekeo wetu kama taifa.
Ndugu wananchi, niliunda Tume hii kama ilivyo kawaida ya taifa letu kuunda vyombo vya uchunguzi yanapotokea mambo mahsusi yanayohitaji kuangaliwa kwa kina. Hii ni Tume ya sita, au ya saba, katika historia ya nchi yetu. Katika Awamu ya Pili iliundwa Tume ya Uchunguzi wa Vurugu na Vifo Katika Kiwanda cha Sukari Kilombero ya mwaka 1986, iliyoongozwa na Jaji David Chipeta.
Awamu ya Tatu: Tume ya Uchunguzi wa Kifo cha Luteni Jenerali Imran Kombe ya mwaka 1996 iliyongozwa na Jaji Barnabas Samatta. Tume ya uchunguzi wa tafrani baada ya uchaguzi kisiwani Pemba mwaka 2001 iliongozwa na Brigedia Jenerali Hashim Bita, na baadaye mimi mwenyewe nikawa mjumbe kwenye kamati ya maridhiano ya tukio lile.
Awamu ya Nne: Tume ya Uchunguzi wa Mauaji ya Wafanyabiashara wa Madini yaliyofanywa na polisi wa mwaka 2006 iliyongozwa na Jaji Kipenka Musa. Tume ya Uchunguzi ya Uvunjifu wa Haki za Binadamu na vifo wakati wa Operesheni ya Wafugaji kutoka bonde la IHEFU na changamoto zake ya mwaka 2007, iliyoongozwa na Jaji Othman Chande, huyu huyu tuliyemtumia.
Tume zote hizi matokeo yake hayakuwa bayana. Lakini katika Awamu ya Sita, kama mnavyojua, tuliunda Tume ya Kuangalia Mfumo wa Haki Jinai na Haki za Wananchi, kujadili mwenendo wa kesi za jinai na haki za wananchi. Pia, tume hii ambayo imechunguza Matukio ya Vurugu Kabla na Baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025, ya Jaji Othman Chande, tuliitangaza bayana na leo imetupa matokeo ya uchunguzi bayana.
Ndugu zangu, kwa muktadha huo, nitumie fursa hii kukupongeza sana Jaji Mkuu Mstaafu, Mheshimiwa Mohammed Chando Othman, makamishna, pamoja na sekretariate ya tume, kwa kazi kubwa mliyoifanya kwa juhudi, uweledi, na uzalendo mkubwa. Mmefanya kazi katika mazingira magumu, mmeweza kuvuka viunzi vyote, na kudhihirisha uwezo wa nchi yetu kushughulikia changamoto zake wenyewe, kwa kutumia mbinu (methodolojia) na viwango vya kimataifa.
Aidha, naungana na mwenyekiti wa tume katika kuwashukuru sana wananchi waathirika wa matukio ya Oktoba 2025, sambamba na wawakilishi wa makundi maalum na asasi za kiraia, viongozi wa serikali waliopo kazini na wastaafu, na viongozi wa vyama vya siasa waliojitokeza mbele ya tume. Ushirikiano wenu kwa tume umedhihirisha utayari wenu kushiriki safari hii ya kutibu majeraha yaliyolisibu taifa letu.
Vilevile, naishukuru jumuiya ya kimataifa na nchi marafiki kwa kuonyesha kusikitishwa na changamoto hii kubwa katika historia ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alimtuma mjumbe maalum, Mheshimiwa Balozi Parfait Onanga-Anyanga. Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola alimtuma mjumbe maalum, Rais Mstaafu wa Malawi, Mheshimiwa Dk Lazarus McCarthy Chakwera.
Vilevile, Umoja wa Viongozi Wanawake wa Afrika, ukiongozwa na mwenyekiti wake, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Liberia, Mheshimiwa Ellen Johnson Sirleaf, walikuja nchini kufuatilia yaliyotokea. Wote hao tumefanya nao mazungumzo na mashauriano yenye kulinda na kujenga hadhi ya nchi yetu. Wote wametuhakikishia utayari wao wa kushirikiana nasi katika hatua yoyote ambayo tutaona tunahitaji msaada and ushirikiano zaidi.
Nawashukuru pia wadau wote waliokubali kukutana na wajumbe hao maalum, wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa. Kwa upande mwingine, wapo waliotumia matukio ya Oktoba 2025 kutusimanga na kutunyooshea vidole. Hatushangai sana kwa sababu mitazamo ya wanadamu haifanani, na kulikuwa na upotoshaji mkubwa wa habari za tukio lile uliofanywa na vyombo vya habari, hususan vya nje ya nchi na vya kimataifa. Kwa desturi ya waungwana, linapotokea jambo la hasara na kuumiza mioyo, matarajio ni kufarijiwa badala ya kuzodolewa.
Kwa vyovyote vile, walioumizwa na tukio lile ni sisi Watanzania. Ni sisi tuliopoteza watoto wetu, ndugu zetu, jamaa na marafiki zetu. Kwa hali yoyote ile, walioathirika ni Watanzania kwa ujumla wetu. Haiwezekani mtu mwingine asiye Mtanzania awe na uchungu zaidi kuliko sisi Watanzania. Haiwezekani! Lau kungekuwa na uwezekano, tunatamani siku zirudi nyuma, yaliyotokea Oktoba 2025 yawe hayakutokea, na historia ijiandike upya ili tuweze kufuta doa tuliloingia.
Hata Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, amewahi kusema katika moja ya hotuba zake kuwa wakati tunapata uhuru, tulichoachiwa na wakoloni halikuwa taifa, bali mkusanyiko wa makabila. Lakini kwa dhamira na utashi wa waasisi wetu, waliamua kujenga taifa moja imara, lisiloendeshwa kwa misingi ya kidini, kikabila au hadhi, na ambapo lugha yetu adhimu ya Kiswahili inatumika kama nyenzo ya kutuunganisha pamoja na kudumisha na kuimarisha utaifa wetu.
Mwaka 1991, pale Mwalimu Nyerere alipojitokeza mbele ya Watanzania kujenga hoja ya taifa kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi vya siasa, lengo lake lilikuwa kuweka mazingira ya kupambanisha fikra na si kuleta vurugu.
Pamoja na hayo, kipekee kabisa, narudia kuwashukuru sana wananchi kwa kutoendeleza vitendo vya uvunjifu wa amani licha ya hamasa zilizokuwa zinafanywa hususan kupitia mitandao ya kijamii. Nawashukuru tena kwa utulivu wenu na imani yenu kwa serikali wakati tukisubiri taarifa hii ya tume. Asanteni sana Watanzania.
Ndugu zangu Watanzania, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haikutokea kwa bahati bali ilijengwa na waasisi wetu kwa maono na matendo yao. Na kama ilijengwa, ni wazi ipo misingi iliyoifanya nchi hii yenye zaidi ya makabila 126 kusimama kama taifa moja lenye mshikamano.
Ndugu viongozi na ndugu wananchi, Hayati Kwame Nkrumah alipozungumzia umajumui wa Afrika, mara nyingi alisema, “Ukitaka kumla tembo, lazima umkate vipande vipande,” akimaanisha haiwezekani kuinyonya Afrika ikiwa imeungana. Kwa bahati mbaya, ndoto yake ya kujenga taifa moja la Afrika, yaani The United States of Africa, haikutimia. Hadi leo Afrika ingali vipande vipande na bado haijajikomboa kiuchumi.
Hapana shaka falsafa hii inazihusu pia nchi moja; kwamba nchi ikiwa na umoja na mshikamano, itakuwa vigumu kuinyonya na kuitawala kisiasa au kiuchumi. Mataifa mengi yenye rasilimali nyingi yamehujumiwa na kuingizwa kwenye migogoro ili kurahisisha uvunaji wa rasilimali zilizomo kwenye nchi hizo. Na kwa hakika, moja ya sababu kubwa ya umaskini wa Afrika ni migogoro ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, ambayo ukifuatilia kwa karibu, aliyewapiganisha yupo nje na anaendelea kufaidika na rasilimali za nchi hiyo. Ndugu zangu Watanzania, umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Niwaombe sana tuendelee kuimarisha umoja na mshikamano wetu ili tusitoe nafasi ya kuvurugwa na maadui wa nchi yetu.
Waheshimiwa viongozi na Watanzania wenzangu, katika nukta hii ninaelekea sasa kuzungumzia matokeo ya Oktoba 29, 2025. Tutakuwa tunajidanganya tusiposema ukweli kuwa yaliyotokea wakati ule yalitikisa taifa letu. Kwa kweli yalitutikisa. Waswahili tunasema, “Kupotea njia ndio kujua njia.” Tumegusa kaa moto na tumejifunza.
Tume imetueleza kwamba uchunguzi umebaini kuwa ghasia zilizotokea zilipangwa, ziliratibiwa, zilifadhiliwa, na kutekelezwa na watu wenye mafunzo na vitendea kazi vya kufanyia uhalifu na uharibifu. Hali kadhalika, imebaini kuwa malengo ya wahusika hao yalikuwa ni kuvuruga uchaguzi na kutengeneza omve la uongozi ili nchi isitawalike, na ndiyo maana ghasia zilianza siku ya uchaguzi.
Ili kutimiza azma hiyo, tumeelezwa kuwa wahusika walilenga miundombinu muhimu na kuvuruga mfumo wa huduma za jamii ili kuathiri uchumi na kuidhoofisha Serikali. Wataalamu wa sayansi za siasa mliopo hapa nasi, na yoyote mwenye uelewa wa masuala ya uongozi wa nchi, mnaweza kutafakari nini kingetokea endapo malengo ya wahusika wa ghasia au vurugu zile yangefanikiwa. Bila shaka, jitihada za vyombo vya ulinzi na usalama kudhibiti ghasia na vurugu zile ndiyo imefanya Tanzania iwe leo ilivyo.
Vinginevyo, tungekuwa tunazungumza hadithi nyingine. Lakini hapa, Mwenyekiti, haimaanishi kuwa kwa wale ambao tutabaini wamekiuka sheria na taratibu za kazi zao, hatutawajibisha; tutawajibishana.
Waheshimiwa viongozi na Watanzania wenzangu, kufuatia ghasia zile, kumekuwa na taarifa nyingi zilizotolewa bila usahihi. Makundi mbalimbali na baadhi ya watu mmoja mmoja walikuwa wakitoa takwimu za vifo na walioathirika bila ya kuwa na uhakika. Takwimu hizo ama zilikusudia kufifisha, au kuzidisha kwa kutia chumvi kiwango cha madhara yaliyotokea.
Wazee wetu walisema, “Kweli ikidhihiri, uongo hujitenga.” Leo tumepokea takwimu zilizochambuliwa vizuri na Tume hii. Tume imewasilisha taarifa yake inayotokana na uchunguzi wa kitaalamu, na ukweli umebainika.
Takwimu za idadi waliokufa, waliojeruhiwa, na waliopata madhara mbalimbali zimechambuliwa na tume, na tumezisikia. Aidha, tumeelezwa kuhusu uwepo wa madai ya baadhi ya wananchi ambao hawajaweza kuwaona ndugu zao au jamaa zao baada ya vurugu zile.
Niwaahidi kuwa, kama tume ilivyopendekeza, serikali itaendelea kufanya uchunguzi wa kina na wa kitaalamu ili tujue mambo haya kwa usahihi wake. Pendekezo la Tume tumelipokea na tutalifanyia kazi na hatutachelewa.
Ndugu zangu, katika kuwakumbuka na kutoa heshima kwa waliotangulia mbele ya haki, ninaomba tusimame kwa dakika moja. Tumuombe Mwenyezi Mungu azipishe roho zao mahali pema peponi. Kila mtu kwa imani yake. Amin.
Kwa masikitiko makubwa, nitoe tena pole kwa wazazi wenzangu waliopoteza vijana wao, na kwa Watanzania wote tuliopoteza ndugu na jamaa zetu. Katika hatua nyingine, ninawashukuru Wizara ya Afya na wadau wengine wa afya, zikiwemo hospitali za umma na hospitali binafsi, kwa kufanya kazi usiku na mchana, tena katika mazingira magumu, ili kuokoa maisha ya waliojeruhiwa.
Ndugu wananchi, tangu uhuru na hata baada ya muungano, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliamua kufuata mfumo wa kidemokrasia. Kwa nyakati tofauti tumekuwa na demokrasia ya chama kimoja au vyama vingi vya siasa. Kuanzia mwaka 1992, tumeamua kufuata siasa za demokrasia ya vyama vingi. Katika mfumo huu tunaendelea kujifunza na kukuwa katika mwelekeo huo.
Nakumbuka Mwalimu Nyerere katika hotuba yake ya Juni 1991 akiwa jijini Rio de Janeiro kule Brazil alisema, na hapa nanukuu, “Demokrasia sio chupa ya Coca-Cola ambayo unaweza kuiagiza. Demokrasia inapaswa kuendelezwa kulingana na nchi yenyewe.” Mwisho wa kunukuu.
Kwa maneno mengine, demokrasia haina budi kujengwa kwa kuzingatia mazingira ya nchi na muhimu zaidi, mila na tamaduni za nchi husika. Sasa nasi kama nchi, tuachwe tujenge demokrasia yetu kwa misingi yetu, mila na desturi zetu.
Ndugu zangu, mliponikabidhi dhamana ya kuongoza nchi hii, nilibaini kuwepo kwa changamoto katika mfumo wa demokrasia na siasa za vyama vingi hapa nchini. Kulikuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wadau wa siasa na wadau wengine kuhusu kunyimwa kwa uhuru wa kisiasa, uhuru wa kujieleza, na changamoto katika mifumo ya uchaguzi.
Kupitia falsafa ya 4R (Maridhiano, Usahimilivu, Mabadiliko na Kujenga Upya), nilichukua hatua kadhaa, ikiwemo kuundwa kwa Kikosi Kazi cha kushughulikia masuala ya kidemokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini; kufanya majadiliano na wadau wa siasa yaliyosababisha kufanyika kwa marekebisho ya sheria kadhaa zinazohusu uchaguzi zetu, lakini pia zinazohusu vyama vyetu vya siasa na msajili wa vyama hivyo.
Hatua nyingine zilizochukuliwa ni pamoja na kuruhusu na kupanua wigo wa kufanya shughuli za siasa na kukuza uhuru wa vyombo vya habari. Pamoja na hayo, bado kuna mambo kadhaa ya kufanyiwa kazi katika mawanda ya siasa, ikiwemo suala la mabadiliko ya katiba.
Kama mnavyofahamu na kama nilivyoahidi, tumepanga kukamilisha mchakato huu katika kipindi hiki cha pili cha Awamu ya Sita, na ni suala la kipaumbele kwenye ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi.
Kwa upande mwingine, tume imebaini kuwepo kwa malalamiko yanayohusu uwajibikaji wa baadhi ya viongozi na watumishi wa umma katika kushughulikia changamoto na kuwahudumia wananchi. Aidha, zipo tuhuma zinazohusu maadili ya viongozi, ikiwemo rushwa, badhirifu, na matumizi mabaya ya rasilimali za umma. Suala la ajira kwa vijana, kuweka mazingira rafiki ya biashara, na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi nayo yameibuliwa.
Ripoti pia imegusia kazi ya udhibiti wa vurugu na urudishaji wa hali ya usalama nchini iliyofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama. Vile vile, zimebainishwa changamoto zilizojitokeza na kupendekezwa hatua za kuchukuliwa ili kuongeza ubora wa kazi za ulinzi wa nchi na usalama wa raia wetu.
Waheshimiwa viongozi na ndugu wananchi, kwa hakika katika safari yoyote ya maendeleo, changamoto haziepukiki, na hatuna budi kuzikabili kwa nguvu ya pamoja. Kimsingi, dhana halisi ya maendeleo ni kuzikabili na kuzitatua changamoto ili tuweze kusonga mbele. Hili ni jukumu letu sote; upande wa serikali, sekta binafsi, na wananchi wote kwa ujumla wetu. Si jambo la busara hata kidogo kuzigeuza changamoto hizi kuwa ni sababu ya kufanya vurugu, uharibifu, na uhalifu.
Changamoto kama hizi na zaidi ya hizi zipo kwenye nchi nyingi duniani, hata nchi zilizoendelea. Lakini vile vile, changamoto za aina hizi ziko katika nchi zinazotuzunguka, lakini wananchi wao hawajazitumia kama sababu ya kuharibu miundombinu na kudunisha chumi zao au kuzifanya chumi zao kuwa duni.
Ni ukweli pia kwamba yaliyotokea Oktoba 2025 hayakuondosha wala kupunguza changamoto zetu. Vurugu zile na ghasia zile hazikuondosha changamoto zetu bali zimeongeza changamoto. Na kama nilivyoeleza hapo awali, kama ghasia zile zisingedhibitiwa, nchi ingepata hali kubwa zaidi na ingetuchukua miaka mingi kuinuka tena.
Nawasihi Watanzania wenzangu tutambue kuwa ni rahisi kupoteza amani lakini si rahisi kuirejesha. Ni rahisi kuibomoa nchi, lakini ni vigumu kuijenga upya. Hata hapa, nataka sote tufahamu kuwa hatima ya Tanzania ipo mikononi mwa Watanzania wenyewe. Nguvu ya ushawishi wa makundi ya nje inasaidia kuvunja amani, kuvuruga usalama na kubomoa nchi.
Lakini kurudisha amani na usalama na kuijenga upya nchi yetu hufanyika kwa misaada yenye masharti magumu ya kisiasa, kiuchumi na kibiashara. Kwa hiyo, tuwe makini kwamba Watanzania ndio wajenga Tanzania. Tunapoibomoa, hatuna mjomba wa kutusaidia.
Tutapata mikopo yenye masharti ya kiuchumi na kisiasa ili tuweze kujenga upya. Lakini wakati wa kubomoa, tunaweza tukapata msaada kirahisi kabisa. Hivyo basi, mambo haya magumu na ya hatari tuliyoyapitia yatupe funzo ili tuendelee kwenye mwelekeo sahihi.
Ipo nukuu maarufu ya Nelson Mandela inayosema, “It always seems impossible until it’s done,” ikimaanisha ili tuweze kukuwa, hatuna budi kujifunza kutokana na matukio yanayofurahisha na yasiyofurahisha pia. Nasi tumejifunza kutokana na mapito haya magumu, na tushirikiane ili tuweze kuimarika zaidi.
Waheshimiwa viongozi na ndugu wananchi, tumesikia masuala yaliyobainishwa na tume pamoja na mapendekezo kwa muktasari. Mmeshuhudia ripoti niliyokabidhiwa na mavitabu yale yaliyoko pale. Hii ni ripoti ya Rais. Aliyeunda tume ni Rais, na ripoti yote hii ni ya Rais. Kwa hiyo wasitokee watu wengine wakadai ownership ya ripoti hii; ni ripoti ya Rais. Nilisema tume za huko nyuma zilikuwa zinabanwa kimya kimya. Mimi nimeamua tuambizane, lakini ripoti ni mali ya Rais.
Nataka niwahakikishie Tume kwamba tumepokea mapendekezo yote yaliyowasilishwa, na tutakayoyasoma kwenye makabrasha yale, na tutaanza kuyafanyia kazi mara moja. Katika hatua hii, nitoe wito kwa Watanzania wenzangu tuungane kwa pamoja kulirejesha taifa letu kwenye misingi yake. Katika kuhakikisha mapendekezo ya taarifa ya tume, serikali itachukua hatua za haraka zifuatazo:
1. Upelelezi wa Kina: Kwanza, tutakwenda na mapendekezo ya tume kufanya upelelezi wa kina wa yale ambayo tume wameyabainisha.
2. Kuunda Tume ya Maridhiano: Katika muda mfupi ujao, tutaunda Tume ya Maridhiano ikijumuisha wadau wote muhimu. Itakayosimamia na kuongoza majadiliano na maridhiano ili kuziba mianya na migawanyiko iliyopo na kurejesha umoja na mshikamano wa kitaifa. Naomba nikumbushe kuwa nia ya kuwa na Tume ya Maridhiano ilikuwepo hata kabla matukio ya Oktoba 25, na ni moja ahadi zangu nilizoziahidi kutekeleza ndani ya siku 100 za kuanza. Hata hivyo, kwa bahati mbaya, ghasia zilizotokea Oktoba 25 zimechelewesha utekelezaji wa ahadi hiyo, kwa kuwa hata hadidu za rejea za tume ile ambazo nilitayarisha sasa zitapaswa kubadilika kuendana na mazingira yaliyopo sasa.
3. Mchakato wa Katiba: Baada ya Tume ya Maridhiano kuwasilisha ripoti yake, maoni na mapendekezo yatakayowasilishwa ndiyo yatakayoelekeza kwenye mchakato wa kurekebisha Katiba ya nchi.
4. Chombo Maalum cha Upelelezi wa Jinai: Kwa kuwa ripoti imebainisha kuwepo kwa viashiria vya jinai kuhusu matokeo yale, tutaunda chombo maalum cha upelelezi (criminal investigation) kwa ajili ya kufanya kazi iliyopendekezwa na tume. Chombo hicho kitaangalia masuala yaliyobainishwa na kubaini waliohusika katika kupanga, kuratibu, na kufadhili matukio ya ghasia au vurugu. Vile vile, watajielekeza kubaini wahusika wa matukio ya uhalifu, kwa sababu kuna vurugu na kuna uhalifu. Kuna wale wote ambao walikuwa wanavunja maduka, kuvamia, na kuiba. Kwa bahati nzuri, picha zipo zitatuongoza kwenye mambo hayo. Tume ya uchunguzi pia itaangalia kwa undani vifo vya watoto na kushughulikia suala la madai ya miili ambayo haijapatikana. Tume itajielekeza pia kwenye masuala ya wanaodaiwa kutekwa na ambao taarifa zao hazijapatikana, vile vile walioathirika nje ya eneo la vurugu. Chombo kitaangalia maeneo yote hayo.
5. Gharama za Matibabu na Msaada: Serikali itaweka utaratibu wa kugharamia matibabu ya majeruhi wa ghasia ambao bado wanahitaji matibabu. Vile vile, itagharamia vifaa saidizi na viungo bandia kwa waliopata ulemavu wa kudumu ili waweze kuyamudu mazingira yao ya kila siku. Natambua na kama ilivyosemwa hapa kwamba wapo wafanyabiashara ndogo ndogo ambao kwa uwezo wao hawawezi kuingia bima kubwa za kuweza kuwalipa, basi nao tutaangalia hasara waliyoipata na kuangalia faraja tutakayoweza kuwafariji.
6. Uimarishaji wa Ulinzi na Usalama: Navielekeza vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea kutekeleza majukumu yake ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa salama.
7. Maombi na Umoja wa Kitaifa: Ghasia zile za Oktoba 25 zimegharimu maisha ya Watanzania wenzetu, raia na askari. Vifo hivyo vimetuumiza sana. Tuelekeze mioyo yetu kwa Mola wetu. Tuendelee kuwaombea ndugu zetu waliotangulia mbele za haki. Aidha, tuliombee taifa letu ili Mwenyezi Mungu aendelee kuliponya na kuliimarisha. Tusimame na maneno ya Mwenyezi Mungu katika kitabu cha pili cha Mambo ya Nyakati sura ya saba, aya ya 14, ambayo yanasema, “Ikiwa watu wangu walioitwa kwa jina langu watajinyenyekesha na kuniomba na kunitafuta uso na kuziacha njia zao mbaya, basi nitasikia toka mbinguni na kuwasamehe dhambi zao na kuiponya nchi yao.” Vile vile maneno ya Mwenyezi Mungu katika Qur’an Tukufu, Sura Al-A’raf, aya ya 23, yanasema, “Mola wetu, tumejidhulumu nafsi zetu na usipotusamehe na kuturehemu, hakika tutakuwa miongoni mwa waliopata hasara.” Tusiendelee kuwa miongoni mwa waliopata hasara. Niwaombe sana viongozi wa dini wa madhehebu yote nchini msimame kwenye nafasi yenu ya kuliponya taifa letu.
Waheshimiwa viongozi na Watanzania wenzangu, wakati nikielekea kuhitimisha, nataka nikiri kwamba mimi binafsi sikutarajia kadhia hii ingetokea kwenye nchi yetu kipindi hiki nikiwa kiongozi mkuu wa nchi. Jambo hili limenitwisha mzigo mzito mabegani kwangu. Lakini nataka niwahakikishie, kadri Mwenyezi Mungu atakavyoniongoza na kunijalia, nitaubeba mzigo huu kwa ujasiri, kujiamini, na tahadhari kubwa.
Kwa mara nyingine tena, nihakikishie Tume kwamba serikali imepokea taarifa hii na mapendekezo yake, na kwa pamoja sisi na nyinyi wanatume tutakwenda kuyafanyia kazi. Mapendekezo mliyoyatoa ni dawa ya kuliponya taifa letu. Na kwa ladha yoyote iliyo dawa hiyo, lazima dawa inywewe ili tupoe. Mapendekezo hayo tutayafanyia kazi ipasavyo.
Tutafanya marekebisho ya mambo yaliyobainishwa kuwa na dosari. Tutaimarisha pale penye udhaifu, bila kuacha kuwajibika pale penye ulazima wa kuwajibishana. Katika hili, serikali inahitaji msaada wenu ndugu zangu Watanzania. Tuweke juhudi za pamoja, kwa nguvu na ujasiri, na kusema ‘never again’ yasijirudie.
Ndugu wananchi, wakati nafuatilia uwasilishaji wa ripoti hii, nilisikia sentensi inayosema, “Tunamtaka Samia wetu tunayemfahamu,” kama vile nilipoingia nilikuwa Samia mwingine na sasa ni Samia mwingine. Nataka niwahakikishie Watanzania, mimi ni Samia yule yule wa 4R, ni yule yule wa 4R.
Ninachoomba ni ushirikiano wenu katika kutekeleza hizo R. Nasema, “kidole kimoja hakivunji chawa,” au “It takes two to tango.” Kwa hiyo, mkimtegemea Samia peke yake afanye, hayaendi. Lakini mkinipa ushirikiano mkubwa, ndugu zangu, tutafika tunakoelekea.
Niwaombe tuungane sote kuamua hatima ya mustakabali mwema wa nchi yetu kwa manufaa ya kizazi hiki na vizazi vijavyo. Ninawasihi Watanzania tusikubali kurubuniwa kuharibu nchi yetu. Tusikubali kuchochewa, iwe na wanasiasa, wanaharakati wahalifu, au watu wenye chuki na wenye maslahi binafsi, kwa njia yoyote ile kuvuruga tunu ya amani yetu.
Tusimame imara na kwa umoja, tulijenge taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tanzania ndipo kwetu. Hatuna pengine katu. Kwa hiyo, tukijenga nchi yetu, tutakaa kwa raha. Tukivuruga nchi yetu, tutaendelea kukaa jinsi tunavyokwenda, tutakuwa na matatizo yasiyoisha.
Baada ya kusema hayo, niwatakie nyote neema na baraka za Mwenyezi Mungu. Tumuombe Mwenyezi Mungu aibariki nchi yetu, awabariki viongozi wetu. Tujaliwe hekima na umoja na amani, ambazo ndiyo ngao zetu Watanzania. Ibarikiwe Tanzania.
Tubarikiwe watoto wa Tanzania, kama tunavyoimba kwenye wimbo wetu wa taifa. Amin.
Amina, na asanteni sana kwa kunisikiliza!