The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Watanzania Tunahitaji Intaneti Kwa Bei Tutamudu

Tushindane na wale waliotuzidi kwa unafuu wa bei badala ya kubweteka na kujiliwaza kuwa tunafanya vema kwa kigezo cha tuliowazidi.

subscribe to our newsletter!

Kuna tofauti kubwa ya kuhitaji na kutaka. Wananchi wa Tanzania tunahitaji intaneti. Kitu kikiitwa hitajio maana yake hatuwezi kuishi bila hicho. Kama ilivyo kwa mahitaji kama ya nguo, chakula, makazi basi vile vile intaneti inaingia humo.

Wapo wanaotafsiri hitajio kama kitu ambacho ukikosa utakufa lakini hiyo si tafsiri sahihi. Kwani tukikosa mavazi tutakufa? Kwani hakuna wasio na makazi na bado wanaishi? Usipoenda shule utapoteza uhai? Licha ya kutosababisha vifo, mavazi, makazi na elimu ni mahitaji muhimu ya mwanadamu.

Kwa msingi huo, tukikosa intaneti pia tutaishi lakini maisha yatakuwa maisha magumu. Intaneti ni hitajio kwa sababu ni huduma muhimu katika kutuwezesha kuzifikia mahitajio mengine muhimu na haki zetu kadhaa za msingi.

Tunaidai Serikali itupatie intaneti bure au kwa bei tunayoweza kumudu kwa sababu ni wao ndiyo walioifanya intaneti iwe hitajio muhimu la maisha yetu ya kisasa. Serikali imetuunganisha katika mifumo ambayo hatuwezi kupata baadhi ya mahitajio yetu ya msingi  na taarifa muhimu bila intaneti.

Chukulia mfano kwenye elimu, vijana wanatakiwa kuomba nafasi ya kusoma vyuoni kupitia mtandao na wakishaingia vyuoni wanahitaji intaneti kufanya tafiti zao. Hata maombi ya mikopo vyuo vikuu, ambayo kimsingi inalenga kukomboa watu maskini, ni kupitia mitandao.

Vijana wetu waliomaliza elimu za vyuo, asiyekuwa na intaneti atapitwa na fursa nyingi mno. Hata ajira za serikalini zinaombwa mtandaoni!

SOMA ZAIDI: Namna Kuzimwa Kwa Intaneti Kulivyoathiri Wafanyabiashara  Wanawake

Kwa watumishi wa Serikali, huduma nyingi zinatolewa kupitia mtandaoni, ikiwemo vibali vya usafiri wa nje, huduma ya kupata hati ya mshahara (salary slip), na hata kujaza fomu za tathmini pia hufanyika mtandaoni. Siamini kama ofisi za Serikali nchi nzima, hadi vijijini, zina huduma ya intaneti ya bure kwa watumishi.

Katika sekta nyingine, ukitaka hati ya kusafiria, huduma ya usajili wa vizazi na vifo,  maombi ni mtandaoni. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wana huduma nyingi mtandaoni kuanzia usajili wa Namba ya Utambulisho wa Mlipa Kodi (TIN) hadi minada.

Ukipotelewa na kitu, toa taarifa polisi kupitia mtandao. Huduma za Serikali mtandaoni ni nyingi mno zikilenga wananchi,  wanafunzi, wafanyabiashara, watumishi na hata ndani ya Serikali yenyewe kwa yenyewe.

Hapo tumetaja huduma za Serikali pekee lakini hata kwenye sekta binafsi huduma nyingi – kwenye benki, bima, hoteli, usafirishaji, burudani, michezo – siku hizi zinatolewa mtandaoni.

Kuna kundi kubwa la wafanyabiashara hivi sasa wanategemea mitandao siyo tu kutangaza bidhaa bali hata kuuza. Anakutana na mteja Instagram, anachagua bidhaa, analetewa hadi mlangoni na kuilipia hapo.

Sekta ya sanaa na burudani imepata msukumo mkubwa kwa sababu ya intaneti kiasi cha kuwapa wasanii kiburi cha fedha zinazoingia kupitia mitandao (streaming). Hii ni kwa sababu bei za intaneti zilikuwa zikihimilika kwa waburudikaji wanaosikiliza hiyo miziki.

SOMA ZAIDI: Watanzania Kili Paul, Neema Wapongezwa na Waziri Mkuu wa India kwa Uwezo Wao wa Kuimba Nyimbo za Kihindi

Kwa baadhi ya watu, mitandao ni sehemu muhimu ya kujisahaulisha matatizo yao kupitia umbea, vichekesho, vita ya chawa wa watu maarufu mitandaoni, mapambano ya timu za wasanii, mbwembwe za wakina Mandonga nakadhalika.

Mitandao na demokrasia

Serikali inaweza kuona aibu kukiri lakini ukweli ni kuwa mitandao imetoa fursa kubwa ya demokrasia katika kujieleza, kujadili na kukosoa. Serikali imepata fursa kubwa ya kujua maoni ya umma kuhusu masuala mbalimbali kupitia mitandao na hatimaye kuchukua hatua sahihi.

Kupitia mitandao wananchi wanaonesha hasira zao, wanafoka na kupata nafuu kwa walau kutoa ya moyoni na kusikika. Wakati mwingine, harakati za mitandaoni zimesaidia kufanikisha mambo makubwa.

Huwezi kutaja mapatano yanayoendelea sasa kati ya vyama au kukubali kwa Serikali kufufua mchakato wa Katiba Mpya bila kutaja michango ya mbinyo kutoka kwa wanaharakati wa mitandaoni.

Kwa misingi hii, utaona kuwa intaneti ni kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na biashara, kijamii, michezo na kadhalika. Hivyo basi, kwa namna maisha yetu yanavyotegemea intaneti, ni muhimu mno huduma hiyo ipatikane bure au kwa bei ambayo wengi tunaweza kumudu ili kusijengeke matabaka kati ya wenye taarifa juu ya fursa na uwezo wa kuzifikia dhidi ya wale ambao wapo gizani.

SOMA ZAIDI: Ushauri Watolewa kwa Wanawake Wajasiriamali Mtandaoni

Serikali iliyotuingiza kwenye mifumo ya mitandao isijitoe sasa kwenye wajibu wa kutupatia intaneti bure au kwa bei tunayoweza kumudu. Serikali isijichanganye kwa upande mmoja kuhimiza matumizi ya mitandao na upande mwingine kudhibiti kwa kuruhusu bei isiyohimilika na wengi. Sera na mahubiri yaendane na vitendo.

Nikumbushe, kwa mfano, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye akiongea kwenye kipindi cha Power Breakfast on Saturday cha Clouds TV Agosti 20, 2022, alikiri kuwa katika ulimwengu wa sasa wa kidijiti huduma nyingi zinapatikana kwa njia ya mtandao, hivyo kuifanya huduma ya intaneti kuwa muhimu na ya msingi katika kuendesha shughuli za uzalishaji na upatikanaji wa huduma za kijamii.

Naye Waziri wa Fedha na Mipango Mwigulu Nchemba katika hotuba yake ya bajeti alitaja matumizi ya mifumo ya TEHAMA kama chaguo namba moja katika utekelezaji wa shughuli za Serikali ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kubana matumizi yasiyo ya lazima.

Mwigulu alitaka ofisi za Serikali zianze ‘paperless operations’ kwenye shughuli zake kwa maana kila shughuli zifanyike kwa mtandao. Alitaka kumbi za mikoa na wilaya zote ziwe na miundombinu ya mikutano ya njia ya mtandao (virtual meeting).

SOMA ZAIDI: Tozo za Laini na Miamala ya Fedha Zinafuta Maana ya Tanzania ya Kidigitali

Alitaka utaratibu wa kuitana wakuu wa mikoa nchi nzima, wakuu wa idara, wakuu wa wilaya, wakurugenzi watendaji wa halmashauri sehemu moja ukome kwani ni mzigo kwa walipa kodi.

Kutokana na umuhimu wa mtandao, Serikali ikaunda kabisa Mamlaka ya  Serikali Mtandao, taasisi ya umma iliyoundwa kwa Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya mwaka 2019 kuratibu, kusimamia na kukuza jitihada za Serikali Mtandao.

Mwisho wa siku walengwa wa kupokea huduma za Serikali, wananchi, nao wanapaswa kujengewa mazingira ya kushiriki katika huduma mtandao kwa Serikali kuhakikisha wanamudu gharama za vifurushi vya intaneti, ambayo kwa upande wao,  pia inawasaidia kuokoa muda na gharama za kusafiri  hususani kwa wale wanaoishi maeneo yasiyo fikika kwa urahisi.

Bei inayohimilika

Katika mahojiano na Clouds TV, Waziri Nnauye hivi karibuni alikunukuliwa akisema kuwa kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa na taasisi za kimataifa, Tanzania inashika nafasi ya sita kwa Afrika na nafasi ya 50 duniani kwa kuwa na gharama za chini za bando ‘vifurushi’  vya intaneti.

SOMA ZAIDI: Jinsi ‘Tweet’ ya Mkurugenzi wa Asas Diaries Ilivyozua Gumzo Mitandaoni

Hili ni jambo jema lakini unafuu wa bei upimwe siyo tu kwa viwango vya fedha lakini uwezo wa wananchi wa nchi husika. Sawa bei ya data kwa wastani wa 1GB ni $1.71 sawa na Sh3990 ni nafuu kulinganisha na nchi nyingine, lakini suala la muhimu hapa ni je, wananchi wengi wanamudu?

Nashauri tushindane na wale waliotuzidi kwa unafuu wa bei badala ya kubweteka na kujiliwaza kuwa tunafanya vema kwa kigezo cha tuliowazidi. Kila nchi ina jambo lake linaloifanya iwe ya kipekee, na kwa Tanzania ni uhuru wa mitandao uliokuwa unatokana na unafuu wa bei.

Waziri Nnauye amesema Serikali inaendelea kufanya michakato ili kuangalia namna ya kushusha bei. Hatutaki michakato, tunataka bei ya vifurushi inayohimilika sasa. Muda hauwasubiri vijana ambao hivi sasa wanaomba vyuo, wanatafuta kazi, na huduma nyingine nyingi kupitia Intaneti.

Njonjo Mfaume ni mwandishi wa habari na mchambuzi wa masuala ya kisiasa. Kwa mrejesho, wasiliana naye kwa meseji kupitia +255 735 420 780 au mfuatilie Twitter kupitia @njonjoOKAY. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelekezo zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts