Dodoma. Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kimeitaka Serikali kuongeza kasi ya kulipa malimbikizo ya madeni ya mishahara, huku Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho Japhet Maganga akisema hatua hiyo itasaidia kuboresha ustawi wa walimu nchini.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Fedha iliyotolewa hapo Septemba 2022, watumishi wote wa umma wanadai malimbikizo ya Shilingi bilioni 318, huku Shilingi bilioni 178 zikiwa na zaidi ya miaka miwili. Taarifa hiyo, hata hivyo, haikuwa na takwimu mahususi za walimu.
Akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa CWT uliofanyika jijini hapa kati ya Disemba 15 na Disemba 16, Maganga alisema kwamba Serikali kuchelewa kuwalipa walimu malimbikizo hayo kuna athari ya moja kwa moja na ustawi wao.
“Athari ni kubwa, hususan kwa walimu ambao wamefikia umri wa kustaafu na wengine tayari wamestaafu kabla ya kulipwa madeni yao,” Maganga alisema wakati wa mkutano huo. “Hii inawawia vigumu [walimu] kuendelea kuidai Serikali wakiwa nje ya mfumo wa utumishi.”
Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2023/2024 uliotolewa mwezi huu kuhusu ulipaji wa madai ya malimbikizo ya mishahara kwa watumishi wa umma unasema katika kipindi cha kuanzia Julai 2021 hadi Juni 2022 madai ya malimbikizo yenye jumla ya Shilingi bilioni 131.1 yamelipwa kwa watumishi 76,866.
SOMA ZAIDI: Tumejifunza Nini Kutoka Mkutano wa Pili wa Urathi wa Maalim Seif?
Kati ya kiasi hicho Shilingi bilioni 124.3 zimelipwa kwa watumishi 74,798 ambao utumishi wao haujakoma na Shilingi bilioni 6.8 kwa watumishi 2,068 waliostaafu.
Hoja ya Maganga pia imeungwa mkono na baadhi ya wajumbe wa mkutano huo ambao wameiambia The Chanzo kwamba endapo Serikali itafanyia kazi ushauri wao huo, walimu watakuwa katika nafasi nzuri ya kufurahia utumishi wao.
Phinius Tuarila ni mjumbe wa mkutano huo kutoka Chalinze, mkoa wa Pwani, ambaye amesema kwamba malimbikizo ya madai hayo yanawaumiza kwa kiasi kikubwa.
‘Tunaumia’
‘’Unaweza ukakaa wakati mwingine hata miaka minne ndiyo unapata [malipo yako],” Tuarila ameiambia The Chanzo pembezoni mwa mkutano huo. “Unakuta [ulikuwa unadai] toka mwaka 2018, mtu anakuja kupata mwaka 2022.”
“Sasa unakuta mtu anaumia kwa sababu na yeye ana malengo yake,” aliongeza mtumishi huyo wa umma.
“Maana yake ni kwamba hela ile aipate afanyie kitu hiki na hiki. Lakini sasa kama mtu hukupata lazima usononeke na wakati mwingine hata utendaji wa kazi unashuka kutokana na hali hiyo.”
SOMA ZAIDI: Sifa Kedekede Zamwagwa Dunia Ikiadhimisha Siku ya Kiswahili
Mjumbe mwingine wa mkutano huo Mwalimu Faraja Dida kutoka Mbeya alisema kwamba ni haki ya mwalimu kupata fedha hiyo anayodai na kwamba inapokaa muda mrefu anatoka nje ya mstari kutokana na matarajio yake aliyo nayo.
“Ili matarajio yake [mwalimu] yawe ya tija, anatakiwa alipwe na asipolipwa madhara yake ni makubwa, kwanza anakuwa kila wakati anafikiria kwa nini yeye hajalipwa,” Dida alisema pembezoni mwa mkutano huo.
“Hii pia inapelekea utendaji kazi kushuka, sasa ili afanye vizuri kulingana na malengo yake ni lazima kusiwe na changamoto yoyote kwenye kichwa chake,” alishauri Mwalimu Dida.
Akizungumza katika mkutano huo ambao alikuwa mgeni rasmi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Profesa Joyce Ndalichako alisema kwamba Serikali inatambua malalamiko hayo, akibainisha kwamba tayari Serikali imeanza kuyafanyia kazi.
Walimu kupewa kipaumbele
Ndalichako alisema Serikali imekwisha kulipa madeni ya walimu 88,297 yenye thamani ya Shilingi bilioni 177.6, malipo ambayo yamefanywa kutoka mwaka wa fedha 2020/2021 hadi 2022/2023.
“Nafahamu zoezi la kupandisha vyeo na kulipa madeni ni endelevu,” alisema Profesa Ndalichako katika mkutano huo.
“Hivyo, nawasihi kuwa na uvumilivu na kuiamini Serikali kuwa ina nia njema ya kuona kwamba malimbikizo yote ya watumishi yanalipwa inavyostahili,” alishauri.
SOMA ZAIDI: Wadau wa Elimu Wahoji Ukimya wa Dira ya Taifa Katika Kutambua Nafasi ya Kiswahili Kwenye Elimu
Ndalichako aliongeza kwamba pamoja na hatua hizo, Serikali inachukua jitihada za makusudi kutoa kipaumbele kwa walimu ambao wanakaribia umri wa kustaafu.
“Wapo walimu wengi tayari wameshastaafu na wanahangaika kufuatilia madai yao mbalimbali kwenye halmashauri,” alisema Profesa Ndalichako, akitaka wakurugenzi wa halmashauri kuwasaidia walimu hao kupata stahiki zao.
“Kila siku [walimu hawa] wanapigwa dana dana za njoo leo, njoo kesho, njoo mwezi ujao nakadhalika,” alisema Ndalichako. “Hili kwa kweli hapana. [Wakurugenzi,] walipeni walimu madai yao yote ambayo ni halali kabla ya kustaafu.”
Jackline Kuwanda ni Mwandishi wa Habari wa The Chanzo anapatikana mkoani Dodoma unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com.