Tumejifunza Nini Kutoka Mkutano wa Pili wa Urathi wa Maalim Seif?

Dira yake ya kutaka kuigeuza Zanzibar kuwa ‘Singapore ya Afrika’ ilitawala mkutano wa kuenzi urathi wake kwenye elimu.
Najjat Omar24 October 20225 min

Zanzibar. Kwa mtu yoyote aliyekuwepo ukumbini, ilikuwa ni vigumu kujizuia asisimke kwa jinsi ambavyo watu mbalimbali walikuwa wakimzungumzia hayati Maalim Seif Sharif Hamad na maono aliyokuwa nayo kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Wakati wa mkutano huo wa pili wa kuenzi urathi wa Maalim Seif, aliyefariki hapo Februari 17, 2021, baada ya kuugua ugonjwa wa UVIKO-19, ilikuwa ni fursa ya Wazanzibari na wadau wake wa maendeleo kujadili mustakabali wao kupitia maisha na nyakazti za gwiji hilo la harakati za mageuzi nchini.

Ukifanyika chini ya mwavuli wa Wakfu wa Maalim Seif, taasisi iliyoanzishwa kwa ajili ya kuenzi na kutunza maono na dira ya Maalim Seif, aliyefariki akiwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, mkutano huo uliwakutanisha pamoja watu waliokuwa wakimfahamu mwanasiasa huyo katika hoteli ya Golden Tulip mjini hapa kutoka Oktoba 22 mpaka Oktoba 23, 2022.

Mkutano huo ulifanyika chini ya dhima isemayo Elimu na Ukuzaji wa Vipaji, Ubunifu na Uwezeshaji ukiwa na lengo la kujadili mawazo ya Maalim Seif, ambaye kitaaluma alikuwa ni mwalimu wa skuli kabla ya kuingia kwenye siasa, kwenye elimu na ukombozi wa kifikra wa mwanadamu.

SOMA ZAIDI: Maajabu ya Maalim Seif Akiwa Hai Yanaendelea Mpaka Akiwa Kaburini?

Othman Masoud Othman ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, nafasi aliyokabidhiwa baada ya kifo cha Maalim Seif, ambaye aliwaambia wahudhuriaji wa mkutano huo kwamba ilikuwa ni moja kati ya malengo aliyokuwa amejiwekea Maalim Seif kutatua “kitendawili” cha elimu visiwani hapa.

“Ndoto ya Maalim Seif [ilikuwa] ni kuleta mabadiliko kwenye elimu na namna pekee ya kuenzi maono yake ni kuhakikisha kwamba lengo hili linatimia,” alisema Othman ambaye chama chake cha ACT-Wazalendo ni sehemu ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar.

Mageuzi kwenye elimu

Maalim Seif, ambaye alifariki akiwa ni Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Taifa, hakuwa muumini wa kuweka viraka kwenye mfumo wa elimu wa Zanzibar ili kukabiliana na changamoto zinazohusishwa nao. Yeye alikuwa akitaka mfumo huo upinduliwe kabisa na uzaliwe mfumo mpya.

Baadhi ya matatizo yaliyokuwa yanamkera sana Maalim Seif yaliyokuwa yakihusiana na mfumo wa elimu ni pamoja na yale ya vijana wengi wa Kizanzibari kupata Divisheni 0 kwenye mitihani yao na skuli za Zanzibar kuongoza kwenye orodha ya skuli zinazofanya vibaya kitaifa.

Mnamo Januari 21, 2021, akiwa katika moja ya ziara zake za kuonana na wananchi, Maalim Seif alirudia kile ambacho amekuwa akibainisha takriban maisha yake yote kuhusiana na umuhimu wa kufanya mageuzi ya kimfumo kwenye elimu ya Zanzibar.

“Mfumo wote wa elimu unahitaji kukarabatiwa upya kabisa,” Maalim Seif, aliyezaliwa Oktoba 22, 1943, huko Mtambwe, kisiwani Pemba, aliwaambia wananchi. “Tukusanye wataalamu wetu wauangalie mfumo wetu wa elimu. Kama tunadhani wataalamu wetu hawatutoshi, tualike na wengine ili tupate mfumo mpya wa elimu Zanzibar.”

SOMA ZAIDI: Haya ni Lazima Yazingatiwe Ili Upangaji, Upanguaji Safu Katika Sekta ya Elimu Zanzibar Uweze Kuzaa Matunda

Na ingawaje Maalim Seif alikuwa akihusanisha tatizo hili la kimfumo la elimu ya Zanzibar na tatizo sugu la ajira linalowakabili vijana wa visiwa hivyo, Profesa Issa Shivji, mwanazuoni anayeheshimika nchini Tanzania, anadhani kwamba maono ya Maalim Seif juu ya elimu yalienda zaidi ya hapo.

“Maalim Seif alitaka, na alitamani, Zanzibar iwe sehemu ya kufundisha na kujifunza kama ilivyo Singapore,” alisema Shivji, gwiji la sheria nchini na Afrika. “Hivyo, ikiwa yeye alikuwa na maono hayo, basi ni vyema tukajua zaidi kuhusu huo mfumo wa nchi hio ili kuwa na elimu bora zaidi.”

Na kwa Profesa Shivji, sehemu muhimu ya mchakato huo ni kupinga mfumo wa elimu unaomezesha watu propaganda na kuhoji wimbo unaoimbwa kila siku na baadhi ya wanasiasa kwamba elimu ijenge uzalendo.

Kazi ya elimu

“Siyo kazi ya elimu kujenga wazalendo,” Profesa Shivji aliwaeleza wasikilizaji waliokuwa wakimsikiliza kwa makini. “Kazi ya elimu ni kuzaa vijana wenye kipaji na ustadi wa kudadisi dhana zote, pamoja na dhana ya uzalendo na utaifa, dhana ya utii na uwazi, dhana ya uongozi na utawala, dhana ya utajiri na umaskini, uzalishaji na ulimbikizaji [na dhana ya] ukweli na uongo.”

Kazi ya elimu ni kumfikirisha mtu na siyo kummezesha fikra, aliongeza Profesa Shivji, na kuendelea: “Kazi ya elimu ni kukuwezesha kutofautisha kati ya mahindi na mbakana. Kwangu mimi, elimu siyo nyenzo au kifaa cha kujitajirisha, au kujilimbikizia mali, au kupatia cheo cha kisiasa.”

SOMA ZAIDI: Inachoweza Kufanya Zanzibar Kuhakikisha Watoto Wanaorudishwa Skuli Hawarudi Mitaani

Rostam Aziz ni mfanyabiashara mkubwa nchini Tanzania ambaye pia amewahi kuhuduma kama mbunge wa Igunga kuanzia mwaka 1994 mpaka alipoamua kujiuzulu mwaka 2011 kupitia chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM).

Aziz, kulingana na maelezo yake aliyoyatoa kwenye mkutano huo wa siku mbili, alifanya kazi kwa karibu na Maalim Seif, hususan katika harakati za kutafuta muafaka wa kisiasa kati ya chama chake cha zamani CUF na CCM.

Aziz aliwaeleza washiriki wa mkutano huo kwamba mbali na kuvutiwa na haiba ya uongozi aliyokuwa nayo Maalim Seif, bilionea huyo pia alivutiwa na dira ya Maalim Seif ya kuigeuza Zanzibar kuwa “Singapore ya Afrika.”

“Katika kumuenzi Maalim Seif, ni muhimu sana kuwekeza nguvu kubwa katika ubora wa elimu ili kuwaandaa Wazanzibari kwa uchumi ambao yeye Maalim Seif akiamini unapaswa kufikiwa – ambao ni wa kuifanya Zanzibar kuwa Singapore ya Afrika – Kituo cha Biashara na Huduma katika Afrika Mashariki na Bahari ya Hindi,” alisema Aziz.

Ni ipi elimu bora?

Akichambua ipi ni “elimu bora” kwa mtazamo wake, mfanyabiashara huyo alisema kwamba “elimu bora” ni ile inayojikita katika kuwajengea watu uwezo wa kutambua fursa zilizopo mbele yao, vipi wazitumie fursa hizo, na vipi wafaidike kutokana na fursa hizo.

“Ni elimu itakayowafanya wahitimu wetu wawe watu wenye uthubutu wa kuhoji na kujihoji, wanaoweza kujitathmini, wawe na kiu isiyokwisha ya kujiongezea maarifa mapya katika ulimwengu unaobadilika kwa kasi kila uchao, wawe watundu na wabunifu na wawe na uthubutu na wanaojiamini,” alisema Aziz.

“Wakati umefika wa kuondokana na mfumo wa elimu ya kikoloni uliolenga kutuzalishia watumishi watiifu na waaminifu kwa mamlaka zao,” aliongeza mfanyabiashara huyo mashuhuri.

Kwa mujibu wa watu waliyomfahamu, bila shaka hii ndiyo ilikuwa dhamira ya Maalim Seif kama angepata nafasi ya kuwaongoza Wazanzibari, nafasi aliyoipigania kwa zaidi ya miaka 30 bila kufanikiwa.

Maalim Seif anaweza kuwa amefariki lakini kamwe siyo mawazo yake ambayo yataendelea kutoa mwongozo juu ya masuala kadhaa yanayoisumbua Zanzibar na Tanzania kwa sasa na kuwanyima usingizi wananchi wao.

Huu ndiyo mchango ambao Abdulrahman Kinana, Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara) ameuelezea kama ni “mchango mkubwa sana” na “ninaouthamini,” katika hotuba yake ya ufungaji wa mkutano huo wa siku mbili.

“[Maalim Seif] alikuwa ni kiongozi ambaye wakati wote aliweka mbele maslahi ya taifa kuliko maslahi yake binafsi,” alisema Kinana ambaye amewahi kuhudumu kama Katibu Mkuu wa CCM. “Amefanya hivyo hata wakati mwengine kwa kuwaudhi wenzake.”

Na kwa kuandaa mikutano ya kuenzi urathi wake, Kinana aliungana na Wakfu wa Maalim Seif katika kuamini kwamba hiyo ni njia pekee kiongozi huyo anaweza kuendelea kuwahudumia watu wake hata akiwa kaburini!

Najjat Omar ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka Zanzibar. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni najomar@live.com.

Najjat Omar

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

The Chanzo Black@300x

The Chanzo Initiative exists at the interface between advocacy and journalism. It is founded to uplift the voices of the underreported, vulnerable, and marginalized communities in Tanzania with the goal to make Tanzania the best place to live for everyone regardless of class, creed, sexual orientation and nationality.

Subscribe to Our Newsletter

The Chanzo Initiative, 2022 © All Rights Reserved