Mifuko ya hifadhi ya jamii, kama vile Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Mfuko wa Pesheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), ni moja ya njia muhimu za kuhakikisha usalama wa kifedha kwa wanachama wanaochangia.
Wanachama wa mifuko hii wanalipa michango yao kwa muda mrefu ili kuhakikisha kwamba watakuwa na uhakika wa kupata mafao katika siku zijazo, hususan wakifika uzeeni.
Hata hivyo, kumekuwa na malalamiko ya siku nyingi kutoka kwa wanachama wa mifuko hii, kubwa ikiwa ni kucheleweshwa kupata mafao yao pale wanapoyahitaji kwa sababu mbalimbali, iwe ni kukosa ajira au kustaafu.
Katika makala hii fupi, nitajaribu kujadili sababu za kawaida zinazosababisha wanachama kufuatilia mafao yao kwa muda mrefu na hatua wanazoweza kuchukua ili kupata faida kamili ya mifuko ya hifadhi ya jamii.
Sababu ya kwanza ninayoiona ni mwanachama kutofuatilia michango yake kama ni kweli anachangiwa na muajiri wake.
Tukumbuke kwamba ni haki ya kila mwanachama kuangalia taarifa za michango yake ili kuhakiki kama muajiri wake anamchangia pesa, ili kuepuka usumbufu wakati wa kudai mafao.
Pia, kuna tatizo la kukosa uelewa juu ya nyaraka zipi na sababu zipi zinahitajika pindi unapokwenda kudai mafao. Hii ni muhimu kwani kila fao lina sifa zake na nyaraka muhimu zinazohitajika pindi unapokwenda kulidai.
Watu wengi wamekuwa hawajui ni sifa zipi na nyaraka zipi zinahitajika wanapokwenda kudai mafao yao. Kwa mfano, fao la kukosa ajira nyaraka ya kwanza unayotakiwa kuwa nayo ni barua ya kufukuzwa kazi au ukomo wa mkataba.
Sababu nyingine ni ofisi za NSSF/PSSSF kuwa mbali na makazi ya watu. Watu wanaofuatilia mafao yao husafiri umbali mrefu kwenda ofisini kudai mafao, baadhi wakiwa wanasafiri kutoka wilaya moja kwenda nyengine.
SOMA ZAIDI: Kwa Nini Ni Muhimu Kufungamanisha Bima ya Afya na Hifadhi ya Jamii?
Baadhi ya watu wamelazimika kuacha kufuatilia mafao yao kutokana na gharama wanazotumia kufuatilia haki zao.
Changamoto hii inaweza kutatuliwa kwa mifuko kuzifanya ofisi zao kupatikana kila wilaya au kuanzisha mfumo kwa wanachama kudai mafao yao kwa njia ya mtandao.
Kutokuaminiana
Pia, kuna hali ya kutokuaminiana kati ya wanachama wa mifuko na wafanyakazi wa mifuko hiyo.
Kuna wakati wanachama wanakosa imani na wafanyakazi wa mifuko ya hifadhi ya jamii na wanahofia kuwa huenda mafao yao yakachelewa au kutopatikana kabisa.
Hali hii inaweza kutatuliwa kwa kuwa na mifumo thabiti ya uwajibikaji kwa wafanyakazi wa mifuko ya hifadhi ya jamii ili kuhakikisha kuwa huduma zinatolewa kwa ufanisi na uwazi.
Michakato mirefu ya kudai mafao pia ni sababu nyengine inayowafanya watu kutumia muda mwingi kufuailia mafao.
Kuna wakati michakato ya kudai mafao inakuwa mirefu na yenye usumbufu kwa wanachama. Kwa mfano, baadhi ya mafao yanahitaji nyaraka nyingi na za kina kuthibitisha hali ya mwanachama.
Hii inaweza kuwafanya wanachama kukosa motisha ya kudai mafao yao. Hali hii inaweza kutatuliwa kwa kuweka michakato rahisi na ya haraka ya kudai mafao ili kusaidia wanachama kupata mafao yao kwa urahisi na haraka.
Sababu nyengine inaweza kuwa ni kupungua kwa uaminifu kwa mifuko ya hifadhi ya jamii. Kuna wakati mifuko ya hifadhi ya jamii inakumbwa na matatizo ya kifedha, au uendeshaji, ambayo huathiri uwezo wa mifuko hiyo kulipa mafao kwa wanachama wake.
Hali hii inaweza kusababisha wanachama kupoteza imani na mifuko hiyo na hivyo kusita kujiunga au kuendelea kuwa wanachama.
Hili linaweza kutatuliwa kwa kuhakikisha kuwa mifuko ya hifadhi ya jamii inaendeshwa kwa uwazi, ufanisi na kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo.
Kwa kumalizia, mifuko ya hifadhi ya jamii kama NSSF na PSSSF ina jukumu kubwa katika kutoa mafao kwa wanachama wake, lakini kuna changamoto kadhaa ambazo zinaweza kuzuia wanachama kupata faida kamili ya mifuko hii.
Kutokana na sababu zilizotajwa hapo juu, ni muhimu kwa wanachama kufuatilia michango yao, kuwa na elimu ya kutosha juu ya mchakato wa kudai mafao, kuhakikisha taarifa zao za kibinafsi ziko sahihi, na kutumia mifumo mbadala ya kudai mafao.
Hizi ni hatua muhimu zinazoweza kusaidia wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii kupata mafao yao kwa urahisi na bila usumbufu wowote.
Thomas Ndipo Mwakibuja ni ana shahada ya sayansi kwenye hifadhi ya jamii kutoka Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM). Kwa maoni, anapatikana kupitia thomasmwakibuja@gmail.com au +255 767 879 281. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Unataka kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelekezo zaidi.
7 responses
Hili jambo la kudai mafao limekuwa jambo gumu kweli utadhani ni hisani kumbe ni haki yako, utasikia mifuko haina pesa eti ilikopesha…michango ya watu inakopeshwa bila ridhaa ya wenye michango, halafu wakihitaji pesa zao, ni usumbufu.
Maoni yangu, hizi fedha za mafao hazitakiwi kuwa kudaiwa, bali wahusika wanapaswa wapewe haki zao immediately baada ya kukamilisha taratibu za kupata fedha hizo.
Lakini pia walio ikopa mifuko hii warejeshe fedha hizo na wasiruhusiwe kukopa tena kwani wanakopa bila ridhaa ya wenye michango na hatimaye kusababisha usumbufu wakati wa kupatiwa mafao yao.
Umeambiwa hii ni nchi ya Madarali. Kwaiyo Taasisi zake pia za kidarali. Ukisikia wameweza kukopesha hela za wanachama bila ridhaa ya wenye hela jua kuwa wanaomilikipesa si wanachama bali ni waliozitoa ili zizalishwe. Mbona hawakopeshi wanachama ??
Ivi ni kwanini mnatunyima uhuru na pesa zetu?kwanini mashariti yanakua makubwa kupata pesa ambayo ni yangu? Kwanini napangiwa matumizi ya pesa eti hadi nezeeke? Me naona ingekua bora kila mwisho wa mwaka kila mwanachama aweze kutoa pesa zake warau nusu hakuna anaye ijua kesho.binafsi kupangiwa matumizi ya pesa yangu ukweri naumizwa na mifuko hiyo.watu wanakufa nakuacha pesa zaoo.ni vile wanachama hatuna sehemu ya kusemea.
Kweli kabsa
Enx for de bext knowledge!!
Ninahitajika kua na viambatamisho gani ninapohitaji kuanza kufuatilia mafao yangu baada ya kuachishwa kazi?
My advice, ondoeni kikokotoo, ni aina unyanyasaji wa kisaikolojia