The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kabumbu Itusaidie Kujenga Utambulisho, Ufahari Wetu Kama Taifa 

Kushindwa kwetu katika michezo kunatokana na kushindwa kuoanisha tamaduni zetu na maendeleo tunayoyataka.

subscribe to our newsletter!

Kombe la Dunia limeisha na mshindi amepatikana lakini mpira, kama maisha, lazima uendelee kudunda. Wote tunajua kuwa mpira ni mduara kama dunia na dua zake. Na uduni, au ubora, wake unategemea na kuegemea mambo mengi sana.

Kwa hiyo, tunaweza tukasema kwamba mpira ni zaidi ya burudani na mchezo; mpira unahusisha na kuakisi mambo lukuki. 

Dimbani pamekuwa jukwaa la kusemea, na kusukuma, itikadi na bendera mbalimbali kama za kudai uhuru kamili wa Wapalestina, bendera za watetezi wa haki za LGBTQ+, kuonesha matabaka ya kijamii, imani, na tamaduni za watu mbalimbali.

Katika mwavuli na uvuli huu wa kibepari, mpira ni biashara inayolipa sana; mpira unaleta bashasha inayouza upande mmoja na kuliza upande mwingine. Mpira ni mashindano; ni michuano ya pande kama zile za jehanamu na paradiso. 

Kwa kifupi, ni mtanange wa aina yake, unaowasha na kuamsha shamrashamra, hisia, na mihemko mingi.

Nyuma ya pazia la mpira tunaweza kudadavua na kuielewa jamii au taifa husika; kujitambua yenyewe na kutambulika kwake mbele ya mataifa mengine, maana mpira ni ishara na kielelezo cha hulka ya kitaifa, national character, fulani. 

SOMA ZAIDI: Shangwe la ‘Mlete Mzungu’ Lina Harufu ya Ubaguzi wa Rangi

Ndiyo maana kushinda, au kushindwa, kwa vilabu vyetu Tanzania, au timu yetu ya taifa, kusiangaliwe tu juu juu, kiufundi, kipaji cha mtu binafsi au bahati fulani. Bali ufanyike uchambuzi yakinifu unaoangaza utamaduni na utambulisho wetu kama taifa.

Tabia, upekee na hulka yetu kama nchi inaonekana na kudhihirika waziwazi katika namna tunajitambua na kutambulika mbele ya jamii nyingine. Maana mbele ya wengine ndiyo tunajielewa vizuri zaidi. 

Kushindwa kwetu katika michezo, umaskini wetu na matatizo mengine mengi makubwa na ya kina yanatokana na kushindwa kuoanisha kati ya tamaduni zetu na maendeleo tunayoyataka. Kuna nyufa, au mpasuko, mkubwa hapo. 

Tunachukulia utamaduni kama kitu cha kale tu na kiufinyu sana kama kufanya maonesho fulani, au kucheza tu ngoma. Wazo la utamaduni kama kioo cha jamii na mahala pa kutia hamasa, kujituma, kuwa na ile collective imagination na ubunifu haipo kabisa au ipo kwa uchache sana.

Sipendi sana tabia ya kufanya mlinganisho na kuiga iga, lakini kama mtakumbuka katika hili Kombe la Dunia lililomaliza, moja ya timu za taifa zilizoshangaza dunia katika ufanisi kimpira ni timu za Asia, hususan zile za Wakorea na Wajapani.

SOMA ZAIDI: Je, Serikali Inaifahamu Dhana ya Utamaduni Anuai? 

Tukumbuke, mpira katika nchi hizi umepata umaarufu na ufanisi miaka ya hivi karibuni. Mafanikio yao siyo katika mpira tu bali hata katika maendeleo kwa ujumla, yanasukumwa na hali yao ya juu ya kujitambua kiutamaduni. 

Kwa mfano, tumewaona Wajapani kila baada ya kandanda walifanya usafi uwanjani, hiyo ni moja ya sifa yao. 

Lakini pia wana nidhamu ya hali ya juu mno; wana roho ya kujituma na kufanya sana kazi; kuwahi kwenye matukio na uaminifu mkubwa, hususan kwenye huduma za kijamii. 

Sisi huku mara nyingi tunabaki kushangaa, na hata kuwacheka, mhandisi wa Kichina anapojinyonga eti kwa sababu daraja alilolijenga limebomoka, au Wajapani wanapoachia ngazi eti kwa sababu wamesinzia bungeni. 

Tunacheka kwa sababu tumezoea kuwa na mediocrity na dishonesty. Aibu na adabu miongoni mwetu imepungua sana, kila mtu analinda tumbo lake na itikadi yake tu.

Hatima ya mpira na michezo yetu mbalimbali itategemea sana sera zetu za michezo; hilo ni pamoja na kuondoa siasa nyingi kwenye vilabu na michezo yetu. Mpira wetu unahitaji kwenda mbele na kuvuka ule ushabiki wa u-Simba na u-Yanga. 

Mpira siyo ushirikina, au bahati nasibu fulani, bali ni sayansi; nikuufanya utamaduni wetu, nidhamu na imani ya hali ya juu, ni muunganiko wa vitu vingi. 

SOMA ZAIDI: BASATA na Kupatwa kwa Sanaa na Wasanii Tanzania

Ndiyo maana, kwa nchi kama Brazil, mpira ni zaidi ya mchezo, ni utambulisho na fahari yao kama taifa. Ndiyo maana mara nyingi wanajiona wana haki-miliki ya kushinda na kuchukua Kombe la Dunia mara zote. 

Wabrazil hawaridhiki tu na kuuza nyama, au kahawa, na malighafi nyingine nje na nchi za mbali; wanatambua kuwa wajibu wao ni kusafirisha nje utamaduni, maarifa, na mpira wao. 

Hilo ndiyo limekuwa msukumo na siri kwao ya kushinda michezo mbalimbali. Matokeo ya timu hizi za michezo imekuwa ni kielelezo na kioo cha utendaji wao kama jamii. Na kwa kweli, maisha yetu binadamu ni kama uwanja wa mpira. 

Kuna siku tunacheza uwanja wa nyumbani siku nyingine ugenini. Tunapokezana mechi, ushindi na maumivu. 

Kuna kupanda daraja na kushuka. Kushinda na kupoteza. Kutesa kwa zamu, kuumia kwa zamu. Kila mtu kwa wakati na msimu na mhasibu wake.

Tujitafakari!

Isaack Mdindile ni mdau wa michezo na elimu. Kwa mrejesho, unaweza kumpata kupitia ezyone.one@gmail.com au Twitter kama @isaacMaverickjr. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts