Machi 19, 2023, ilitimia miaka ishirini kamili tangu majeshi ya Marekani na washirika wake yalipoivamia Iraq na kumpindua aliyekuwa Rais wa taifa hilo la Asia Magharibi Saddam Husssein.
Wanajeshi wapatao 173,000 walitumika katika uvamizi huo, huku asilimia 73 wakitoka Marekani, wakifuatiwa na Uingereza (asilimia 25), Australia (asilimia moja) na Poland (asilimia 0.1).
Matokeo yake ni kuwa katika muda wa miaka mitatu tu, Wairaq takriban 655,000 walipoteza maisha na wananchi zaidi ya milioni tisa wakakosa makazi.
Wamarekani 4,600 na Waingereza 179 nao walipoteza maisha. Serikali ya Marekani ilitumia Dola za Kimarekani bilioni 815 katika uvamizi huo.
Matokeo yake, Iraq ikagawanyika katika misingi ya kidini, kikabila, na kimajimbo. Washia, Wasunni, na Wakurdi wakaunda vyama vyao vya siasa na wakaishi katika maeneo “yao.”
Wakaanza kushambuliana wenyewe kwa wenyewe, huku Marekani ikidai inalinda usalama wao.
Wapiganaji wa Al-Qaïda wakapata mwanya wa kuingia Iraq na kutangaza utawala wao wa Kiislamu (ISIS au Daesh). Wakadhibiti asilimia 40 ya Iraq. Hii pia ikawapa Wamarekani kisingizio cha kubaki nchini Iraq.
Ndipo miaka ishirini imepita na bado wanajeshi wa Marekani wapatao 2,500 wangali wameikalia Iraq na wanakataa kutoka ingawa wananchi wanataka watoke.
Muda wote huo wanajeshi wa Marekani wamekuwa wakichoma takataka za kemikali na matokeo yake nchi hiyo inakabiliwa na magonjwa ya mapafu, saratani, nakadhalika.
Mnamo mwaka 2022, Rais wa Marekani Joe Biden aliidhinisha sheria ya kulipa fidia kwa wanajeshi wake walioathirika na magonjwa hayo.
Wananchi wa Iraq wamesahauliwa. Inasemekana Biden mwenyewe alilazimika kupitisha sheria hiyo kwa sababu mtoto wake Beau Biden Jr alikufa kutokana na saratani ya ubongo baada ya kuathirika alipokuwa jeshini nchini Iraq.
Vita ya udanganyifu
Wavamizi wa Kimarekani walidai eti lengo lao lilikuwa ni kuwakomboa wananchi wa Iraq na ndiyo maana uvamizi huo waliuita Operation Iraqi Freedom.
Wakabuni hadithi eti Saddam alikuwa akishirikiana na Al Qaeda na Rais George W. Bush akaitumia hadithi hiyo.
Vyombo vya habari vikaonyesha “uzalendo” wao kwa kurudia hadithi hiyo hadi ikaingia katika akili za Wamarekani. Wanahabari, walio wengi, badala ya kutafuta habari sahihi wakawa wapiga debe wa Ikulu ya White House.
Mwaka 2006, Kamati ya Inteligensia ya Baraza la Seneti ikaungama kuwa hadithi hiyo ya kusadikika haikuwa na ukweli wowote. Ukweli ukadhihirika kuwa Al Qaeda walipata mwanya wa kuingia Iraq baada ya uvamizi wa Marekani.
SOMA ZAIDI: Kwa Kuzipatanisha Saudia na Iran, China Imelamba Dume Kwenye Siasa za Kimataifa
Ndipo Osama Bin Laden alipomtuma msaidizi wake Abu Musab Al Zarqawi kwenda Iraq na kuanzisha tawi la Daesh huko.
Riwaya nyingine iliyotungwa ni kuwa Saddam alikuwa ni hatari kwa usalama wa Marekani kwani anaweza kuishambulia.
Ukweli ni kuwa Saddam hakuwa na ndoto wala uwezo wa kuishambulia Marekani ambayo iko kilometa 11,000 kutoka Iraq. Kama kawaida, Mwamerika akaaminishwa uongo huo na wapiga debe walio katika sekta ya habari.
Uwongo mwengine uliobuniwa ni kuwa eti Saddam ndiye aliyepanga mashambulizi ya kigaidi yaliyofanyika New York mnamo Septemba 11, 2001.
Vyombo vya propaganda vikaingia mitamboni na wananchi wakaaminishwa kuwa Saddam aliishambulia New York, na kwa hivyo lazima aadhibiwe.
Uongo mkubwa ni walipodai kuwa Saddam alikuwa amekusanya silaha za maangamizi za kemikali (WMD) na angeweza kuzitumia dhidi ya Marekani.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani wa wakati huo Colin Powell akalidanganya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) Februari 5, 2003, kwa kuonyesha “ushahidi” uliobuniwa ili kuthibitisha kuwa kuna WMD nchini Iraq.
Powell mwenyewe baadaye akaungama kuwa aliidanganya UNSC!
Hata Bunge la Marekani mwaka 2005 lilitoa ripoti iliyosema kuwa kabla ya kuivamia Iraq, Serikali ya Bush ilikuwa inaudanganya ulimwengu iliposema kuwa Saddam alikuwa na WMD na kuwa alisaidiana na Al-Qaeda katika kuishambulia New York. Ripoti ikaongeza kuwa idara ya upelelezi ilitoa habari hizo za uongo.
Asasi ya utafiti nchini Marekani iitwayo Center for Public Integrity imehesabu matamshi ya uongo yaliyotolewa na Rais Bush pamoja na mawaziri wake kuhusu Saddam na Iraq.
Wakagundua kuwa katika muda wa miaka miwili tangu mashambulizi ya New York walisema uongo angalau mara 935.
SOMA ZAIDI: ‘Kidole Kimoja Hakivunji Chawa’: Uchaguzi Mkuu wa Nigeria 2023 na Mambo Makuu ya Kujifunza Tanzania
Mnamo Aprili 2007, aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA), George Tenet alisema shirika lake halijawahi kuhakiki kuwa Saddam alihusika kwa namna yoyote katika mashambulizi ya New York au alikuwa akishirikiana na Al Qaeda.
Ni huyu huyu Tenet ndiye aliyemshauri Powell. Wakati Powell anaidanganya UNSC, Tenet alikuwa amekaa nyuma yake.
Dikteta Saddam?
Kisingizio kingine walichotumia kumshambulia Saddam ni kuwa yeye ni dikteta aliyekuwa akiongoza Serikali ya Sunni, wenzake walio wachache, kuwakandamiza Shia walio wengi pamoja na Wakurdi. Wapiga debe nao wakaeneza shutuma hizo bila ya kutafuta ukweli.
Na ukweli ni kuwa katika Serikali yake Saddam aliwateua mawaziri na viongozi waandamizi kutoka jamii za Wakristo, Washia, Wasunni, na Wakurdi.
Hii si kusema kuwa Saddam hakuwa dikteta au alikuwa mtawala mwadilifu.
Historia yake inaonesha alianza uongozi akiwa kibaraka wa Marekani akilipwa na CIA. Mnamo mwaka 1958, wanajeshi walimpindua mfalme wa Iraq. Nchi ikaongozwa na Abd al-Karim Qasim, ambaye akataifisha visima vya mafuta.
Al-Karim pia alitaifisha ardhi iliyokuwa ikimilikiwa na mfalme na mabwanyenye wenzake na kuwagawia wakulima wadogo.
Akajenga nyumba takriban 35,000 kwa ajili ya masikini. Akabadili Katiba na kuruhusu wanawake washike nafasi za uongozi.
Mwaka 1963, Al-Karim akapinduliwa na akauawa. Saddam akashika madaraka kwa msaada wa Marekani.
Saddam akapewa na CIA orodha ya majina ya makomredi wa Al-Karim naye akawauwa kwa kuwapiga risasi. Inakisiwa aliwaua watu 5,000.
SOMA ZAIDI: Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Miaka 63 ya ‘Uhuru wa Migogoro’
Hiyo ni kazi aliyoifanya Saddam kwa niaba ya Marekani. Lakini, kama wasemavyo mabeberu, wao hawana rafiki wa kudumu wala adui wa kudumu, bali wana maslahi ya kudumu.
Ndipo kibaraka Saddam hatimaye akawa adui wa Marekani; wakampindua na kisha akanyongwa!
Wakati huo Rais George W. Bush alitaka dunia nzima imuunge mkono katika uvamizi wake wa Iraq usiokubalika. Akatuambia “msiponiunga mkono mtakuwa mnaunga mkono ugaidi.”
Lugha hiyo hiyo imerudi chini ya Rais Joe Biden ambaye anasema ni lazima tumuunge mkono katika vita vya Ukraine.
Uhalifu wa kivita
Uvamizi wa Iraq ulikuwa ni uhalifu wa kivita. Haya yalisemwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa UN, Kofi Annan.
Na hivi karibuni aliyekuwa mkaguzi wa WMD nchini Iraq, Hans Blix, ametamka kuwa kimsingi Bush na Tony Blair wanastahili kufikishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).
Hata Rais mstaafu wa Marekani Barrack Obama amekubali kuwa uvamizi wa Iraq ulifanyika “kimakosa.”
Bush na Blair wanastahili wafikishwe ICC kwa sababu ya uhalifu wa kivita walioutekeleza huko Iraq kinyume na sheria ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na mauaji, utesaji, na udhalilishaji wa raia.
Ulimwengu ulishtushwa kuona jinsi katika gereza la Abu Ghraib walivyowavua nguo raia na kuwapanga mithili ya magunia huku wakiwapiga na kuwatesa.
SOMA ZAIDI: Marekani Yadaiwa Kukwepesha Mashtaka Dhidi ya Afisa Wake Aliyeua Mtanzania Kwenye Ajali ya Barabarani
Waliwalazimisha wafungwa wa kiume wavae nguo za kike. Wakawabaka kwa kutumia bunduki. Raia walishambuliwa katika makazi yao kwa kutumia mabomu ya kemikali kama urani na phosphorus.
Kwa mfano, mnamo Aprili 2004, katika maeneo ya Fallujah, wanavijiji 736 waliuliwa, wakiwemo watoto na wanawake.
Hapo hapo tena mnamo Novemba waliuliwa raia kati ya 581 na 670. Mauaji kama hayo yalifanyika pia katika mji wa Haditha na kwengineko mnamo Novemba 2005.
Uhalifu mwengine ni kuwa mara tu Marekani, Uingereza na washirika wao “walipoikomboa” Iraq kama wanavyodai, kampuni zao za mafuta zikaingia kwa nguvu, zikiongozwa na ExxonMobil, Chevron, BP na Shell.
Pia, iliingia kampuni ya Halliburton iliyomilikiwa na Dick Cheney aliyekuwa Makamu wa Rais wa Bush.
Mwaka 2011, BP ilichukua mapipa 31,000 ya mafuta kila siku. Mwaka 2015 ikazidi hadi mapipa 123,000 kwa siku. BP ikabandikwa jina la “Blair Petroleum” kwa vile ilikuwa ikilindwa na Waziri Mkuu Tony Blair.
Uhalifu wa kivita uliofanywa na Marekani na Uingereza huko Iraq siyo tu unakiuka sheria za kimataifa bali hata sheria za Marekani na Uingereza. Hata hivyo, imepita miaka 20 na hakuna Mmarekani au Mwingereza aliyewajibishwa.
Katika wakati ambao dunia imeonesha nia ya kuwaadhibu wahalifu wa kivita, huku ICC ikimfungulia mashtaka ya uhalifu wa kivita Rais wa Urusi Vladmir Putin kwa uvamizi wake wa Ukraine, kwa shinikizo la mataifa ya Magharibi, ikiwemo Marekani, je, tutarajie Bush na Blair nao kuburuzwa mahakamani kwa uhalifu wao dhidi ya watu na taifa la Iraq?
Nizar Visram ni mchambuzi wa siku nyingi wa siasa za kimataifa. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia +255 673 004 559 au nizar1941@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.
One Response
Tuna la kujifunza? Ndio
Mwandishi anasema kule Marekani kuna waandishi wapiga debe wa Ikulu ya white house
Nasi hapa Tanzania tuna wanaojiita wanahabari ambao kazi yao ni kurudia tu yanayosemwa na Ikulu. Badala ya kutafuta au kudadisi habari wazipokeazo wao kazi yao ni kurudufu tu press release za serikali
Si magazeti, si redio si TV hiyo ni kazi ya wapiga debe wetu hapa sawa na wale wa Marekkani