The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Wananchi, Wawekezaji Wavutana Ulipaji Fidia Mradi wa Uchimbaji Mchanga Kigamboni

Watu wapatao 1,200 wanatakiwa kupisha mradi huo unaotekelezwa na kampuni ya Serikali ya Nyati Mineral Sands Ltd na ile ya Australia ya Strandline Resources Ltd.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Wananchi kutoka mitaa ya Madege, Sharifu, na Mwasonga, wilayani Kigamboni, jijini hapa wameelezea kusikitishwa na hatua ya Serikali kushindwa kutimiza ahadi yake iliyoitoa siku nyingi ya kufanikisha ulipaji fidia kwa ajili ya kupisha mradi wa uchimbaji madini ya mchango mzito wilayani humo.

Mradi huo unaopangwa kutekelezwa kwa ushirikiano kati ya kampuni ya Serikali ya Nyati Mineral Sands Ltd na kampuni ya madini ya Australia ya Strandline Resources Ltd unahusisha kuhamishwa kwa watu wanaokisiwa kufikia 1,200 kutoka maeneo hayo kupisha uwekezaji huo.

Hata hivyo, licha ya tathmini kukamilika mwaka 2020, iliyoambatana na zuio lililowataka wakazi hao kutokuendeleza shughuli yoyote ile, iwe ya kilimo au ujenzi, kwa kuahidiwa kulipwa fidia kabla ya Disemba 2022 ili wahame, fidia hiyo bado haijalipwa mpaka wakati wa kuandika habari hii, hali iliyolalamikiwa na wananchi kuwasababishia usumbufu mkubwa.

Baadhi ya usumbufu huo ni wananchi kushindwa kuboresha makazi yao, ikiwa ni kukarabati nyumba zao kwani kufanya hivyo siyo tu itakuwa ni kukiuka zuio lililowekwa bali pia ni kuingia gharama ambayo haitafidiwa kwani zoezi la tathmini tayari limekamilika. Wananchi pia hawawezi kufanya hata kilimo kidogo kama vile cha mbogamboga.

SOMA ZAIDI: CCM Yadaiwa Kupora Ardhi ya Wanakijiji Kilimanjaro

Ni katika mazingira haya ndipo mnamo Mei 30, 2023, wanavijiji zaidi ya mia moja walikusanyika mbele ya Ofisi ya Serikali ya Mtaa kuishinikiza Serikali hiyo iharakishe mchakato wa wao kulipwa fidia zao ili wajue hatma yao, wakisema mchakato huo umechukua muda mrefu sana kuweza kuvumilika tena.

Kutothaminiwa

The Chanzo ilikuwepo kwenye mkusanyiko huo ambao wanavijiji  na kushuhudia jinsi wanavijiji hao walivyokosa furaha, huku wengine wakihisi kutothaminiwa na kutelekezwa, wakiziangukia mamlaka husika kuingilia kati na kutatua kilio chao hicho cha muda mrefu.

Miongoni mwa wanavijiji ambao The Chanzo ilizungumza nao kwenye mkusanyiko huo ni Leornard Triphone, mkazi wa Sharifu, ambaye alizungumzia namna kuchelewa kwa fidia hizo kunavyopangua mipango yake ya maisha, akisema kuna muda anachanganyikiwa kwa kukosa kujua nini cha kufanya.

SOMA ZAIDI: Aidan Eyakuze: Ni Wajibu wa Wananchi Kusimamia Uwazi, Uwajibikaji Serikalini

“Mlango wangu wa mbele, wa chuma, ulishavunjika [na] siwezi kuurudishia kwa sababu tumeambiwa tusitengeneze chochote, hatuwezi kufanya chochote,” Triphone alilalama.  “Huko nyuma [ya nyumba], chemba za makaro yangu zimevunjika, siwezi kujenga.”

Baadhi ya wanakijiji walizungumzia namna ucheleweshwaji wa malipo hayo ya fidia unavyowalazimisha kuchukua hatua ambazo wanadhani si sahihi, kama ile iliyolalamikiwa na Benadeta Emili, mkazi mwengine wa Sharifu, aliyezungumzia usumbufu wa kuwalaza vijana wake wa kiume na mabinti zake kwenye chumba kimoja.

Sehemu ya makazi ya wanakijiji hao

“Nalazimika kulala na watoto wa kike ndani ya chumba kimoja, nalala na watoto wa kiume kwenye chumba kimoja hicho hicho,” Emili alisema, akibainisha kwamba zuio linamzuia kuongeza chumba cha pili. “Ina maana, mwisho wa siku, unasababisha mtoto wa kike na kiume wanalala sehemu moja, kitu ambacho siyo sahihi.”

Mwanakiji mwengine, Fatuma Athumani, alisema kwamba kama Serikali imeshindwa kulipa fidia hizo kwa wananchi, basi wananchi hao waruhusiwe kuendelea na maisha yao kama kawaida, ambayo yatajumuisha kujihusisha na shughuli zao za kilimo ili kujikimu kimaisha.

“Sisi wananchi tunaumia, hatuna hata sehemu ya kwenda kukaa kujificha, mabati [ya nyumba zetu] yametoboka [na] mvua hii [inayoendelea kunyesha], ni mafuriko, tunanyeshewa ndani na watoto, hatuwezi hata kununua bati kutokana na zuio,” alilalamika mwananchi huyo. “Kwa hiyo, tunaiomba Serikali, kama inatuona, kama inatusikia, itusimamie akina mama sisi ili tupate haki yetu.”

SOMA ZAIDI: Kuwaondoa Wananchi Ngorongoro ni Shambulio Dhidi ya Ufugaji wa Asili

Malalamiko haya ya wananchi yanakuja takriban miezi mitatu tangu Serikali iiagize kampuni ya Nyati kulipa wananchi hao stahiki zao ambapo mnamo Machi 9, 2023, Naibu Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa, alisema mchakato huo umechukua muda mrefu sana kukamilika.

“Malalamiko ya wananchi wanaotakiwa kulipwa fidia yameongezeka baada ya kuahidiwa kulipwa fidia mwaka 2020,” Dk Kiruswa alisema kwenye hafla iliyowakutanisha Serikali na kampuni hizo mbili za uendelezaji wa mradi huo. “Hadi sasa bado hawajalipwa na mwekezaji hajaeleza watalipwa lini.”

Bilioni 20 kutumika

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Katibu Mtendaji wa kampuni ya Strandline Resources Ltd, Jamie Cann, alisema jumla ya Dola za Kimarekani milioni 8.5, sawa na takriban Shilingi bilioni 20, zimetengwa kwa ajili ya zoezi hilo la ulipaji wa fidia.

The Chanzo ilimtafuta James Chialo, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Nyati Mineral Sands Ltd, na kumuuliza ni lini wataanza kutekeleza agizo la Serikali la kuwalipa wananchi hao fidia zao ambapo alijibu kwa ufupi, akisema zoezi hilo litaanza Juni 7, 2023.

SOMA ZAIDI: Serikali Wilayani Mbozi Yadaiwa Kuhamisha Wananchi kwa Nguvu Kupanua Hifadhi ya Kimondo

Sakata hili linalohusisha wananchi wa Madege, Sharifu, na Mwasonga na kampuni za Nyati na Strandline lilishawahi kufika mpaka bungeni, ambapo Mbunge wa Kigamboni (Chama cha Mapinduzi – CCM) Faustine Ndugulile aliitaka Serikali itolee ufafanuzi ucheleweshaji wa malipo hayo ya fidia kwa wananchi wake.

Hiyo ilikuwa ni Aprili 11, 2022, ambapo Serikali iliahidi bungeni kwamba zoezi hilo lingeanza Juni mwaka huo. Hilo halikufanyika, na mpaka sasa wananchi wameendelea kulalamikia kushindwa kulipwa stahiki zao.

Akizungumza na The Chanzo kuhusiana na sakata hili hapo Juni 3, 2023, Dk Ndugulile alisema ni muhimu kwa Serikali kuhakikisha wananchi hao wanapata stahiki zao, akisema suala hilo limechukua muda mrefu sana.

Kutaabika

“Wakazi ambao maeneo yao yaliguswa na mradi huu wamekuwa wakitaabika kwa muda mrefu, wakisubiri hatma ya malipo yao,” alisema Ndugulile. “Sasa hivi wengi wameshindwa kumalizia nyumba zao, na wengine ambao walikuwa na nyumba zao zinazohitaji marekebisho wameshindwa kuzirekebisha.”

“Mimi kama mbunge nimekuwa nikiendelea kuisisitiza Serikali, na hata mpaka wiki iliyopita, nimeendelea kuwasisitiza Serikali kuhakikisha kwamba wananchi hawa wanalipwa kwa wakati,” alisema mwakilishi huyo wa wananchi.

SOMA ZAIDI: Malalamiko Zaidi ya 7,000 ya Wananchi Yamfikia Mwinyi Kupitia App ya Sema na Rais

“[Wizara ya Madini] wameniahidi kwamba ndani ya huu mwezi [Juni, na mwezi] unaokuja [Julai], watakuwa wamekamilisha malipo, nasubiria kuona kama utekelezaji utafanyika kama walivyoahidi,” aliongeza Ndugulile.

Annagrace Rwehumbiza, Afisa Malalamiko katika mradi huo, aliiambia The Chanzo kwamba ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kwamba kila mwekezaji anayekuja nchini anafanya hivyo kulingana na sheria za nchi pamoja na zile za kimataifa.

“Lakini pia [Serikali] iweke watu ambao wanaweza kuwakumbusha hao wawekezaji kwamba hili [la kulipa watu fidia] ni takwa la kisheria na mnatakiwa mlitekeleze,” alisema afisa huyo.

“Ni muhimu pia kuwa makini kwamba [kwenye haya masuala ya uwekezaji] hufanyi wananchi wabaki kwenye mazingira ya umasikini,” aliongeza Rwehumbiza.

“Kwa sababu, tunataka kuwekeza kuleta maendeleo ndiyo, lakini maendeleo kama hayawanufaishi wananchi siyo maendeleo.”

Hadija Said ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anayepatikana mkoani Dar es Salaam. Unaweza kumpata kupitia hadijasaid826@gmail.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts