Dodoma. Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) umeandaa mafunzo ya siku mbili ya waandishi wa habari jijini hapa ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha vyombo vya habari vinaandika habari zitakazochochea ushiriki wa wanawake kwenye nafasi za maamuzi na uongozi.
TGNP, shirika lisilo la kiserikali ambalo limekuwa likijihusisha na harakati za kijinsia nchini tangu mwaka 1993, lilifanya mafunzo hayo katika wakati ambapo kumekuwa na malalamiko mengi juu ya ushiriki hafifu wa wanawake kwenye masuala ya uongozi, hali inayoibua wasiwasi kuhusu ustawi wa wanawake nchini na hatma ya taifa kwa ujumla.
Kwamba kuna ushiriki mdogo wa wanawake kwenye nafasi za uongozi wa nchi ni jambo ambalo watafiti wengi wameshalibainisha. Kwenye Bunge, kwa mfano, wanawake wanachukua asilimia 36.7 tu ya viti vyote kwenye mhimili huo wa utungaji sheria.
Kwenye uchaguzi wa Urais wa mwaka 2020, ni wanawake wawili tu ndiyo waliojitokeza kuwania nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa nchi – Cecilia Augustino Mwanga (Demokrasia Makini) na Queen Cuthbert Sendiga (Alliance for Democratic Change – ADC).
Watafiti wamekuwa wakihusisha hali hii na mfumo dume unaoongoza Tanzania, ambao unapelekea sheria na kanuni kutungwa kwa namna zinavyompendelea mwanaume lakini pia kuifanya jamii iamini kwamba mwanamke hawezi kuwa kiongozi.
SOMA ZAIDI: Nini Kitatokea Pale Wanawake Wengi Wakiwemo Kwenye Nafasi za Maamuzi?
TGNP inaamini kwamba ili kubadilisha hali hii, vyombo vya habari ni lazima vitimize wajibu wake sawasawa kwa kufanya habari ambazo siyo tu zitalenga maboresho ya kisheria na kikanuni, bali pia kuijengea imani jamii kwamba mwanamke ana uwezo sawa wa kuwa kiongozi kama ilivyo tu kwa mwanaume.
Catherine Mzurikwao, Mratibu wa Mafunzo kutoka TGNP, aliiambia The Chanzo kwamba mafunzo hayo yanatokana na imani yao kama shirika kwamba kama kuna mabadiliko yoyote yanayotakiwa yatokee kwenye jamii, basi ushiriki wa vyombo vya habari ni wa lazima.
“Waandishi wa habari wana nafasi ya kuwasemea wanawake ili kuwa na uwakilishi sawa kati ya wanawake na wanaume kwenye masuala mbalimbali ya uongozi,” alisema Mzurikwao.
“Waandishi wa habari wako sehemu nzuri sana ya kuhakikisha jamii inabadilika. Tunatamani waandike habari zenye mrengo wa kijinsia ziweze kumsemea mwanamke na kuwahamasisha kuchukua hatua za kugombea.
“Waandishi wa habari wako sehemu nzuri sana kuhakikisha kwamba wanawake wengi zaidi wanajitokeza kwenye vitongoji, vijiji, [na] mitaa ili tuwe na uwakilishi ulio sawa kati ya wanawake na wanaume,” alisema Mzurikwao.
SOMA ZAIDI: Fatma Taufiq: Wanawake Tunahitaji Ukombozi wa Kiuchumi
Licha ya kuongozwa na Rais mwanamke, Samia Suluhu Hassan, na wanawake wengine kushika nafasi kubwa za kiuongozi, kama vile kuwa na Spika wa Bunge mwanamke, Tulia Ackson, mitazamo ya kijamii dhidi ya wanawake bado inatajwa kuendelea kukwamisha ushiriki mkamilifu wa wanawake kwenye nafasi za uongozi.
Dk Ananilea Nkya, mwandishi wa habari wa siku nyingi, na mkufunzi kwenye mafunzo hayo, aliwaasa waandishi kwamba kubadilisha mitazamo hiyo ni kazi yao ya msingi kwenye majukumu yao ya kila siku kama wanahabari.
Hata hivyo, Dk Nkya, ambaye pia amekuwa akishiriki kikamilifu kwenye harakati za kupigania usawa wa kijinsia nchini, alisema hilo haliwezi kufanikishwa endapo kama waandishi wataendelea kuandika habari zinazotegemea matukio badala ya kwenda kwenye jamii na kukutana na watu na kupata uzoefu wao halisi.
“Ni lazima ziwe habari ambazo wananchi wanaeleza hali zao za maisha,” Dk Nkya alisema. “Habari zisiwe zile za kumchukua mtu mmoja, hata kama ni kiongozi wa juu [wa nchi] kazungumza. Mwandishi wa habari aje huku chini, ahoji watu wa chini, wanaume na wanawake.”
“Habari nyingi hazilengi kuchukua sauti za wanawake, yaani wanawake waweze kuzungumza,” aliongeza mwandishi huyo wa siku nyingi. “Labda wamefanya mambo gani katika nafasi zao kule kwenye jamii ili watu waweze kujua kumbe huyu ni kiongozi [mwanamke] ameweza kufanya hili na hili.”
SOMA ZAIDI: Sheria za Uchaguzi, Vyama vya Siasa Kufanyiwa Marekebisho?
Dk Ankya pia ameshauri waandishi kuacha kuandika habari zenye kunukuu viongozi tu, ambao mara nyingi wamekuwa ni viongozi wa juu na wanaume.
Wakiongea na The Chanzo pembezoni mwa mafunzo hayo, waandishi wa habari waliopata mafunzo hayo walisema kwamba yatasaidia kuboresha namna watakavyokwenda kufanya kazi zao wakiwa kwenye vyumba vya habari ili kubadilisha hali ya mambo ilivyo sasa.
Moja kati ya waandishi hao wa habari ni Asha Mwakyonde, mwandishi wa habari wa mtandao wa Ihojo, ambaye alisema mafunzo hayo yatamsaidia kubadilisha namna alivyokuwa anafanya kazi zake.
“Baada ya mafunzo haya nitakwenda kuandika habari za wanawake ambao wako chini kabisa kwenye jamii,” alisema Mwakyonde. “Kwa mfano, wale ambao wako kwenye VIKOBA, kuna viongozi wanawake lakini mimi sijawahi kuwaandika.”
Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari The Chanzo anapatikana Dodoma unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com.