Azimio la Bunge, kimsingi, ni mkataba (Inter-governmental Agreement – IGA) wa mahusiano kati ya Serikali yetu na Serikali ya Dubai. Pamoja na kwamba IGA imesainiwa, Serikali yetu inaweza kuwasilisha kwa Serikali ya Dubai mapendekezo ya maboresho ya maeneo ya mkataba kutokana na maoni ya wananchi.
Wabunge walipaswa kutaka maboresho ya IGA na kuridhia baada ya hapo. Sasa, ni wajibu wa Serikali kuandaa jedwali la maboresho ya IGA na kupata ‘addendum.’ kwenye andiko hili fupi nakusudia kuainisha baadhi ya maeneo ya kutiliwa mkazo na kuyabadilisha katika addendum ya makubaliano ni pamoja na haya nitakayoyataja hapa.
Pia, kwenye andiko hili nazungumzia masuala mengine muhimu kuhusiana na suala hilo husika na mjadala ambao umeambatana nalo.
Kwanza, suala la muda wa mkataba utakaoingiwa kwa ajili ya uwekezaji ni muhimu kuwa wazi pamoja na vipindi vya kufanya marejeo, au contracts reviews kama tunavyosema kwa kimombo. IGA inapaswa iboreshwe katika eneo hili. Eneo hili limeleta mkanganyiko mkubwa sana miongoni mwa wananchi wetu katika jamii.
SOMA ZAIDI: Zitto Kabwe: Hili la Wamachinga Linanisononesha Sana
Mbili, suala la aina ya uwekezaji ni muhimu liwe wazi kwamba itakuwa ni Concession Agreement (CA). CA hii iwe na muda maalumu, kwa mfano, miaka 25, na kila baada ya miaka mitano kuwe na mapitio ya kuona kama malengo yamefikiwa.
Ni muhimu sana iwekwe wazi kwamba bandari haiwezi kuuzwa, na kimsingi haiuziki, wala kubinafsishwa, bali ni uwekezaji wa pamoja wa kuendeleza na kuendesha bandari.
Tatu, suala la kuvunjwa kwa mkataba pale pande mbili zikishindana liwe wazi kwenye IGA badala ya kuzuia kuvunjika kwa mkataba. Hii IGA imeliweka hilo jambo vibaya sana kana kwamba ni mkataba ambao hauna ukomo na wala hauwezi kuvunjika.
Nne, suala la umiliki wa kampuni ya uendeshaji, au port operator, itakuwa na hisa sawa kwa sawa kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai. Ni muhimu sana katika mazingira tuliyonayo kuhakikisha kwamba kampuni ya uendeshaji itakayoundwa iwe na umiliki wa 50-50 kati ya DP World na kampuni ya umma yenye hisa nyingi za Serikali.
Hii itasaidia kujenga uwezo wa Watanzania. Hili jambo pia litaondoa husda kabisa iwapo Serikali itakuwa na hisa katika kampuni ya uendeshaji.
Msajili wa Hazina aunde kampuni ya uwekezaji kwenye bandari ambapo Mamlaka ya Bandari (TPA) na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii iwe na hisa, na sehemu ya hisa ziorodheshwe katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) kwa ajili ya wananchi watakaotaka kuwa sehemu ya uwekezaji huo.
SOMA ZAIDI: Zitto Kabwe: Hatujaweza Kutumia Uhuru Wetu Kuleta Maendeleo ya Taifa Letu
Kampuni hii iunde ubia, yaani joint venture na mwekezaji DP World ili kuendesha bandari yetu.
Tano, suala la ulinzi wa bandari, kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vya Tanzania ndiyo pekee vitatoa ulinzi, liwe wazi kabisa katika IGA.
Sita, suala la eneo lipi la bandari ya Dar es Salaam litaendeshwa na kampuni binafsi na bandari zipi zitakuwa sehemu ya uwekezaji huu liwe wazi ili kuondoa sintofahamu ya bandari zote za Tanzania kuwa chini ya DP World.
Saba, suala la upekee, au exclusivity, wa kampuni binafsi itakayoendesha bandari kwamba nchi pia iwe na exclusivity dhidi ya kampuni hii kuwa na mikataba na bandari shindani na Tanzania.
Ni muhimu sana mjadala ukajikita kwenye kuongeza ufanisi wa bandari yetu ili kuongeza mapato ya Serikali, mapato ya fedha za kigeni kwa taifa, na Tanzania kutumia nafasi yake ya jiografia kukuza uchumi wake.
SOMA ZAIDI: Zitto Kabwe: Taasisi za Kimataifa Zina Nguvu Sana Tanzania Kuliko Watanzania
Tanzania haijatumia vizuri nafasi yake ya jiografia kiasi kwamba inapata 1/6 tu ya mapato ya fedha za kigeni inayoweza kupata. Hivi sasa, mapato ya fedha za kigeni kupitia bandari ni Dola za Kimarekani bilioni 1.9 tu.
Lakini bandari ikiwa na ufanisi, Tanzania inaweza kupata mpaka Dola za Kimarekani bilioni 12 ambazo ni sawa na fedha zote za kigeni tulizopata mwaka 2022 kwa bidhaa zote na huduma tulizouza nje ya nchi.
Bandari pekee inaweza kutupatia mapato ya fedha za kigeni mara nne ya mapato yote tunayopata kutoka kwenye dhahabu. Bandari peke yake inaweza kulipa mishahara ya watumishi wa umma na kuhudumia Deni la Taifa iwapo ikitumika ipasavyo.
Hivi sasa mapato ya kodi kutoka bandarini kwa ushuru wa forodha ni Shilingi trilioni 7. Kutokana na kukua kwa biashara, tunaweza kupata mpaka Shilingi trilioni 26 trilioni.
SOMA ZAIDI: Kilimo na Umasikini, Malaysia na Tanzania
Nitumie safu hii pia kurudia nasaha zangu kwa Watanzania kwamba tuepuke kugawanyika katika mazingira ya sasa. Viongozi tujiepushe kabisa kupandikiza chuki miongoni mwa watu wetu kutokana na kauli zetu.
Mjadala wa uwekezaji katika bandari ulenge haswa ufanisi wa bandari na namna nchi yetu inaweza kufaidika na nafasi yake ya jiografia.
Mwisho, nihimize haja ya watu kuwa huru kwenye kujadili masuala ya nchi yao bila bugudha. Wanaopinga wawe huru kupinga, wanaounga mkono wawe huru pia, na wanaotoa majawabu ya kwenda mbele wafanye hivyo.
Mijadala, kama ambavyo nimekuwa nikisisitiza kila mara ninapopata nafasi ya kufanya hivyo, ndiyo uhai wa taifa. Taifa lisilo na mijadala, kimsingi, ni taifa mfu. Serikali isikilize, iyabebe inayoona yanafaa, na kutimiza wajibu wake!
Zitto Kabwe ni Kiongozi wa ACT-Wazalendo. Unaweza kumpata Twitter kupitia @zittokabwe. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.
3 responses
Huyu ndio Zito Zuberi Kabwe ninye mjua mm. Hongera sana. Serikari hamna haja ya mawazo mapya. Tumieni hii akilo ya Zito Kabwe kila mwananchi atafaidika na mali asili ya mama Tanzania
Tatizo la Tanzania / Watanzania ni kama Waafrika wengine, tunasumbuliwa na kasumba ya kudharau vyetu na kuthamini vya nje, ikiwemo fikra na mawazo mbadala. Maneno haya Zitto wetu yangesemwa na “Mzungu” Serikali yote ingesimama wima na kutaka kuyafanyia kazi.
Mola wetu Mlezi Atuhurumie na Atuzindue Wabongo!🤲🏽
I am very impressed with Zitto’s flow of ideas. He seems a very able politician who can lead the country to a prosperous future