Dar es Salaam. Maelezo yanayofuata yametolewa kutoka sauti kwenda kwenye maneno kutoka kwenye mahojiano maalum ambayo The Chanzo imefanya na Dk Baruani Mshale, mtaalamu wa masuala ya maliasili na mabadiliko ya tabianchi. Uhariri umefanyika kuboresha usomaji.
Sasa hivi tulipofikia, na hasa katika taarifa ambayo imetolewa na jopo la wanasayansi ya hivi karibuni, taarifa ya sita ya utafiti wao wa uchambuzi wa tafiti zilizofanyika, hakuna ubishani tena kama mabadiliko ya tabianchi ni kweli yanatokea ama la. Hakuna ubishani tena.
Hiyo ni dhahiri kwamba mabadiliko ya tabianchi yanatokea na kitu kingine ambacho wanasayansi pamoja na watunga sera wameweza kufikia muafaka ni kwamba mabadiliko hayo siyo tu yanatokea [bali] yanatokea kwa kasi kubwa na kasi hii imesababishwa na shughuli za binadamu katika kujiletea maendeleo yake.
Kujenga maeneo ya makazi, kujenga viwanda, nakadhalika. Kwa hiyo, mabadiliko ya tabianchi yanatokea na yanatokea kwa kasi na kisababishi kikubwa ni shughuli za binadamu.
Maeneo ambayo pia kumekuwa na kuboresha uelewa wetu kuhusiana na mabadiliko ya tabianchi ni namna ambavyo jamii tofauti tofauti na sekta na mifumo tofauti tofauti itaathiriwa.
Kutokana na uhaba wa takwimu, kipindi cha miaka 10 [au] 15 iliyopita, ilikuwa ngumu kuweza kukadiria kiasi gani jamii za nchi zile masikini zaidi, nchi za kitropiki, ambazo hazina uwezo wa kukusanya takwimu za masuala ya hali ya hewa pamoja na mabadiliko ya tabianchi, ilikuwa ngumu kujua ni kwa kiasi gani zitaathirika.
SOMA ZAIDI: Mabadiliko ya Tabianchi Ni Nini? Mtaalam Afafanua
Lakini hilo ni eneo jingine ambalo sayansi imeweza kuboresha, [yaani] upatikanaji wa takwimu umeweza kuboreshwa kiasi kwamba sasa hivi tunafahamu namna ambavyo maeneo tofauti tofauti ndani ya nchi, kwa mfano katika ngazi ya Tanzania tu peke yake, ni kwa kiasi gani maeneo, labda maeneo ya kati, au maeneo ya nyanda za juu kusini, yataathirika tofauti na maeneo ya kaskazini au tofauti na maeneo ya magharibi.
Lakini kipindi cha nyuma ilikuwa ni ngumu kuweza kujua maeneo tofauti tofauti yataathirika vipi. Kwa hiyo, hakuna ubishani tena. Mabadiliko ya tabianchi ni dhahiri yanatokea na yanatokea kwa kasi kubwa kuliko kasi yetu ya kuweza kukabiliana nayo na kisababishi kikubwa ni shughuli zetu sisi wanadamu.
Tusishituke?
Hoja ya mwanzo [ya watu wanaopinga uwepo wa athari za mabadiliko ya tabianchi] ilikuwa ni kwamba hakuna mabadiliko ya tabianchi ya kutushitusha, kwa sababu mabadiliko ya tabianchi ni kitu ambacho kinatokea tu kiasili tangu dunia imeumbwa.
[Wanasema] kumekuwepo na kubadilika, kuna nyakati ambapo joto katika uso wa dunia liliongezeka na kuna nyakati ambapo joto katika uso wa dunia lilipungua. Na hiyo ni kweli, ndiyo, kumekuwepo na hayo mabadiliko ya tabianchi kwa miaka milioni, miaka ya elfu kadhaa iliyopita.
SOMA ZAIDI: Nini Hupelekea Mabadiliko ya Tabianchi?
Lakini kitu ambacho kinakubaliwa sasa hivi, kitu ambacho tunakubaliana na ushahidi upo, ni kwamba mabadiliko ya sasa yanatokea kwa kasi, yanatokea katika muda mfupi tofauti na mabadilko ambayo yalitokea kipindi cha nyuma.
Kwa hiyo, ile ya kusema kwamba mabadiliko haya huwa yanatokea tu kiasili, ama iwe kwa sababu ya radi, iwe kwa sababu nyingine zozote zile, tumeona kabisa kwamba ushahidi upo [unaopinga hoja hizo].
Miaka 100 mpaka 150 iliyopita ongezeko la gesi, hasa gesi ya hewa ukaa, ambayo imetokana na ongezeko la maendeleo ya viwanda, ndiyo imepelekea mabadiliko ya tabianchi ambayo tumeyaona sasa. Kwa hiyo, ile hoja ya kusema kwamba ni kitu cha asili kutokezea ile imeonekana kabisa kwamba haina mashiko
Dunia itaweza kujishughulikia?
Hoja yao nyingine ilikuwa ni kwamba hata yakitokea, dunia ina uwezo wa kukabiliana nayo, dunia yenyewe tu, au ulimwengu ulivyo, asili yake, una namna ya kukabiliana na mabadiliko kama hayo.
Walidai kwamba licha ya mabadiliko hayo, viumbe vitaweza kuishi, mimea pamoja na viumbe vingine vitaendelea kuishi na, kwa hiyo, tusihangaike nayo kwa sababu viumbe vitajua namna ya kukabiliana navyo, vitaweza kukabiliana navyo kama ilivyo tokea kipindi cha nyuma.
Hili nalo limeonekana kwamba halina mashiko kwa sababu mabadiliko haya yametokea kwa kasi tofauti na mabadiliko yaliyotokea kipindi cha nyuma. Na kasi hii ni kubwa kuliko uwezo wa viumbe pamoja mifumo mingine ya kiikolojia ya kuweza kukabiliana na mabadiliko haya. Yaani ile kuweza kuendana na haya mabadiliko kadiri yanavyotokea.
Mabadiliko yanatokea kwa haraka na ushahidi upo ambapo maeneo yamebadilika. Kuna viumbe hai ambavyo vimeanza kutoweka, kuna viumbe hai ambavyo idadi yake imepungua sana kutokana na mabadiliko ambayo yametokea.
Nadhani kwa watu wengi zimekuwa zikitumika taswira zile za wale dubu, jinsi ambavyo mapande yale ya barafu katika kizio cha kaskazini cha dunia yanavyokuwa yakiyeyuka na jinsi ambavyo wamekuwa wakiathirika.
Na ile inaonekana kabisa kwamba ni ule ushahidi unatokea kwamba haya mabadiliko yanatokea kwa haraka kiasi kwamba viumbe vile vinashindwa kukabiliana nayo. Lakini baadhi ya wadudu na baadhi ya ndege, wameshaanza kutoweka kwa sababu mabadiliko haya yametokea kwa haraka kuliko uwezo wa viumbe hivyo kuweza kuendana na mabadiliko hayo.
Kwa hiyo, hiyo ya kusema kwamba hata yakitokea dunia inaweza yenyewe kukabiliana nayo ikaendelea kuwepo, inaonekana kwamba haina mashiko.
Tulaumu water vapor?
Inapokuja kwenye nini visababishi, kuna wengine walikuwa wanasema kwamba visababishi vikubwa sivyo ambavyo tunaambiwa na wanasayansi. Wanasema, kwa mfano, uwepo wa ile water vapor, unyevuunyevu ule unaotokana na mvukizo, ndiyo unaosababisha joto kuongezeka.
Ni kweli, ule mvuke unaotokana na maji, unapokuwepo katika anga letu, ni moja wapo ya zile tunaita greenhouse gases na zinasababisha hilo ongezeko la joto duniani na mabadiliko ya tabianchi. Sasa wale waliokuwa wanasisitiza kwamba mvuke ndiyo tatizo kubwa zaidi kuliko hewa ukaa walikuwa na ajenda yao.
Ajenda yao ilikuwa ni kutetea vile vyanzo vinavyopelekea hewa ukaa ambavyo ni uchomaji wa mafuta kwa ajili ya usafirishaji, kwa ajili ya viwanda nakadhalika, matumizi ya makaa wa mawe, visiweze kuguswa, na kuonesha kwamba hiki ni kitu ni tatizo dogo tu na halisababishwi na vile ambavyo tunaambiwa vinasababisha.
Hii nayo haina mashiko kwa sababu licha ya kwamba mvuke wa maji ni moja wapo ya ‘greenhouse gases’ lakini ili kuweza kuona athari ya aina yoyote ile ya ‘greehouse gas’ [ni] lazima tuangalie ipo kiasi gani kwenye anga letu.
Na ni kwa kiasi gani inasababisha tatizo, na yenyewe inaweza kukaa kwenye anga letu kwa miaka mingapi kabla ya kubadilishwa na kuwa katika hali ambayo haileti athari.
Mvuke katika anga unakaa katika masaa machache mpaka siku na miezi kadhaa kabla haujaanguka tena kwa mfumo wa mvua. Wakati hewa ukaa, kama kabonidayoksaidi, inakaa kwa miaka elfu na maelfu.
SOMA ZAIDI: Nini Kinadhihirisha Athari za Mabadiliko ya Tabianchi Tanzania?
Na kabonidayoksaidi imeongezeka, imekuwa nyingi sana katika anga letu, kiasi kwamba kiasi chake kwenye anga, pamoja na kukaa miaka mingi bila kubadilika kuwa katika hali ambayo haina athari, ndiyo inayopelekea hasa kuleta haya mabadiliko ya tabianchi.
Na ushahidi [na] utafiti unaonesha kabisa kwamba maendeleo ya viwanda yanaendana na yanashabihiana na kuongezeka kwa kiasi cha hewa ukaa katika anga letu. Na yanashahabiana na mabadiliko ya tabianchi, kuongezeka kwa joto, kuongezeka kwa mvua, hali za upepo kubadilika nakadhalika.
Kwa hiyo, ile hoja yao ya kusema kwamba siyo hewa ukaa ambayo ndiyo tatizo kubwa na yenyewe imekuja kuonekana kabisa kwamba haina mashiko.
Tatizo la sasa
Wengine walikuwa wanajaribu kuleta ile hali ya sintofahamu kwa kusema kwamba hili tatizo litatokea miaka mingi sana ijayo, [kwamba] halitatokea sasa. Ndiyo mabadiliko haya yanatokea lakini athari zake tutaziona miaka mingi.
Ni kweli muda ambapo ile hewa ukaa, kwa mfano, inatoka katika kiwanda kufika kwenye anga na kusababisha mabadiliko ya tabianchi ni takribani miaka 20 mpaka miaka 30. Kwa maana hiyo ni kwamba, athari tunazoziona sasa zaa mabadiliko ya tabianchi ni kutokana na uzalishaji wa hewa ukaa na hewa nyingine zilizotokea miaka 20 mpaka 30 iliyopita.
Lakini katika kipindi hicho tumeendelea kuzalisha hewa ukaa nyingi zaidi. Na tayari hatuwezi tukasema kwamba hili ni tatizo la nyakati zijazo, ni tatizo ambalo tunaliona sasa.
Takwimu zinaonesha katika miaka 20, yaani ukisema kwamba uangalie miaka 10, yaani ile kumi bora, ambayo inaongoza kwa kiwango cha juu kabisa cha joto, unakuta kwamba sita, nadhani, ama zaidi ya sita kati ya hiyo kumi imetokea ndani ya miaka 20 mpaka 30 iliyopita kuonesha kwamba tatizo ni kubwa sana sasa hivi.
Matukio yale ya kama vimbunga, mvua kubwa maeneo mengi duniani yameenda yakiongezeka katika miaka hii 50 na hasa miaka 10 mpaka 20 iliyopita ukilinganisha na miaka mingi iliyopita.
Kwa hiyo, tayari tunaziona hizi athari. Hata hapa Tanzania tunaona kabisa kwamba hali ya ukame, mvua kunyesha nje ya msimu, imeongezeka zaidi katika miaka ya hivi karibuni kuliko kipindi cha nyuma. Kwa hiyo, hili si tatizo la nyakati zijazo tena. Ni tatizo ambalo liko sasa.
SOMA ZAIDI: Athari za Mabadiliko ya Tabianchi Huathiri Maisha, Uchumi wa Watanzania
Hoja hazina mashiko
Kwa hiyo, wale ambao walikuwa wakipinga kwa kiasi fulani haya mabadiko ya tabianchi na kusema hata yakitokezea miaka mingi ijayo tayari hiyo inaonekana kwamba haina mashiko tena kwa sababu haya mabadiliko na athari zake tunaziona sasa na zinaenda zikiongezeka.
Kwa hiyo, zile hoja zao za kusema kwamba kitu kinatokea kiasili, ushahidi unaonesha kwamba miaka 100 mpaka miaka 150 iliyopita ambapo shughuli za binadamu zimeongezeka ndiyo kumekuwa na mabadiliko ya tabianchi zaidi hiyo liko wazi.
Hewa gani zinazosababisha ni hewa ya ukaa na siyo mvuke kama ambavyo walikuwa wanajaribu kutuaminisha.
Kwamba dunia inaweza ikakabiliana nayo, viumbe vinaweza vikakabiliana nayo, ushahidi unaonesha kabisa kwamba mabadiliko yanatokea kwa haraka kuliko uwezo wa viumbe kuweza kuendana na hayo mabadiliko.
Na kwamba hili tatizo si sasa ni tatizo la baadaye, hiyo pia imeonekana kabisa kwamba hili tatizo ni la sasa, ushahidi upo, maeneo mbalimbali duniani yameshaathirika.