Dar es Salaam. Ipo haja kwa Tanzania kutunga sheria mahususi itakayoruhusu na kusimamia upelelezi binafsi nchini, Tume ya Kuangalia Jinsi ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai Tanzania imemshauri Rais Samia Suluhu Hassan.
Tume hiyo imesema sheria hiyo ni muhimu kwani itaainisha mamlaka itakayosimamia na kuratibu upelelezi binafsi, masharti ya usajili, aina ya upelelezi unaoweza kufanywa na wapelelezi binafsi, mipaka ya upelelezi binafsi, maadili na wajibu wa wapelelezi binafsi kwa Ofisi ya Taifa ya Upelelezi (OTU), Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya kiuchunguzi.
Ushauri huo umetokana na maoni ambayo tume ilipokea kutoka kwa wadau muhimu wa haki jinai nchini kuhusu umuhimu wa kuwepo kwa upelelezi binafsi kwa ajili ya kukidhi mahitaji binafsi katika sekta ya upelelezi na uchunguzi.
Pamoja na huduma hii kutolewa hapa nchini, tume imebaini kuwa, ipo changamoto ya uendeshaji wa huduma hii inayotokana na kutokuwepo kwa sheria mahususi inayoweka masharti mbalimbali kuhusu upelelezi binafsi.
SOMA ZAIDI: Tume Yaitaka Serikali Kuacha Kuanzisha Taasisi Zenye Taswira ya Kijeshi
“Kwa sasa, zipo kampuni na watu binafsi wanaojihusisha na huduma ya upelelezi binafsi hasa katika taasisi za kifedha, mashirika ya bima na kampuni za mitandao ya simu,” tume hiyo iliyofanya kazi yake chini ya uenyekiti wa Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman ilisema kwenye muhtasari wa ripoti yake.
“Kupitia huduma hizi, yapo mafanikio mbalimbali yaliyowezesha kubainika kwa uhalifu, kuwaunganisha ndugu na familia zao, kutatua migogoro ya kijamii hasa ya kifamilia, kibiashara na kisiasa,” ilisema tume hiyo. “Hivyo, ni muhimu suala hili likawekewa utaratibu rasmi ili sekta ya upelelezi binafsi iweze kurasimishwa katika mfumo wa kisheria.”
Kwa mujibu wa kifungu cha 5 cha Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma Saidizi, Sura ya 322, Jeshi la Polisi ndiyo chombo kikuu cha upelelezi hapa nchini.
SOMA ZAIDI: Tume Yataka Uchunguzi Mali Zilizotaifishwa Chini ya Utaratibu wa Kukiri Kosa
Aidha, taasisi nyingine zenye mamlaka ya kisheria kufanya upelelezi na uchunguzi ni TAKUKURU chini ya vifungu vya 7(e) na (f) na 10 vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329 na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa ya Kulevya chini ya kifungu cha 4 cha Sheria ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, Sura ya 95.
Tume imefanya uchambuzi wa maoni na mawasilisho ya wadau na kuangalia uzoefu wa nchi nyingine kama vile Australia, Canada, Kenya, na Uingereza ambazo zina sheria mahususi zinazoratibu uchunguzi binafsi.
Kwa mujibu wa tume, uzoefu huo umebainisha faida mbalimbali za upelelezi binafsi kama vile kusaidia kupata taarifa ambazo ni muhimu zinazohusiana na mashauri ya jinai, kukutana na ndugu waliopotea na kupata taarifa za uhakika za watu unaotarajia kuingia nao katika mkataba.
SOMA ZAIDI: Tume Yataka Mkakati wa Kitaifa Kubaini, Kuzuia Uhalifu Tanzania
Pamoja na faida zake, tume pia imebainisha kwamba upelelezi binafsi unapaswa kuwekewa masharti mahususi katika utekelezaji wake.
Masharti hayo yatajumuisha: mpelelezi binafsi kutohitaji au kutumia taarifa za siri za Serikali; kujifanya ni askari polisi; na kutotumia vibaya taarifa binafsi za mtu au kampuni au kuingia kwa jinai katika maeneo ya watu.
Tume imebainisha kwamba wapelelezi binafsi wanatumika katika Mfumo wa Haki Jinai kwa kuwa wamekuwa ni sehemu ya msaada kwa vyombo chunguzi vya umma katika kubaini, kuzuia na kupambana na uhalifu.
“Sifa mojawapo ya mpelelezi binafsi ni ubobevu katika eneo la uchunguzi,” tume imebainisha.
“Aidha, nafasi ya upelelezi binafsi katika mfumo wa Haki Jinai, inaweza kuangaliwa kwa mtazamo kuwa, watu wengi wanachunguzwa kutokana na vitendo vya jinai lakini hawafikishwi katika mfumo wa Haki Jinai kwani mashauri husika humalizwa kwa maelewano ya pande zinazokinzana,” imeongeza tume hiyo.
SOMA ZAIDI: Wakuu wa Mikoa, Wilaya Wasiwe na Mamlaka ya Kukamata Watu, Tume Yashauri
Hata hivyo, tume pia imebaini kuwa ili mfumo wa matumizi ya wapelelezi binafsi uweze kufanya kazi vizuri ni lazima kuwe na mfumo wa kisheria utakaoweka masharti ya watu na sifa za kufanya kazi ya upelelezi binafsi, vigezo vya kupata leseni na sharti la ushirikiano na vyombo vya utekelezaji wa sheria.
“Nia kubwa ni kuhakikisha haki na faragha zinalindwa,” tume imesisitiza.
Tume imetolea mfano wa Tume ya Kurekebisha Sheria ya Australia ambayo katika taarifa yake kuhusu Sheria ya Faragha na Utekelezaji ilibainisha kuwa wapelelezi binafsi ni tofauti na vyombo vya utekelezaji wa Serikali kwa kuwa hawawajibiki moja kwa moja kwa Serikali au chombo cha ombudsman ambacho kinaweza kuchunguza malalamiko na kutoa fidia kama ambavyo kinafanya kwa vyombo vya serikali.
Tume hiyo ya Australia ilipendekeza umuhimu wa masharti magumu ya leseni ili kusimamia haki ya faragha ya mtu.