Haji Manara, moja kati ya wadau muhimu wa soka Tanzania, aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram wiki hii tunayoimaliza kuwa mashabiki wa soka na klabu wasichoke kukemea makosa ya waamuzi yanayosababisha baadhi ya timu kukosa haki ya kupata matokeo mazuri.
Ni ushauri ambao kila mpenda maendeleo ya mpira wetu angeupokea vizuri kwa kuwa haulengi kuisakama timu moja, labda iwe na viongozi wajinga ambao hawajui hayo makosa yanaweza kuigeukia timu yao na kuiathiri kwa kiasi kikubwa kuliko awali yalipokuwa yanawanufaisha.
Hii ni baada ya mfululizo wa makosa yaliyoziathiri timu za Singida United, Azam FC, Prisons na hata Yanga kwenye fainali ya Ngao ya Hisani. Bahati mbaya sana makosa hayo yalizinufaisha timu chache na hivyo viongozi ambao ni hamnazo kuona kelele hizo dhidi ya uamuzi mbovu zimejaa wivu dhidi ya klabu yao.
Na wako mashabiki walioamua hata kurudisha video za miaka kadhaa nyuma zinazoonyesha makosa ya waamuzi yaliyozinufaisha timu zinazolalamika sasa.
Tatizo la kimfumo
Kwa muda mrefu nimekuwa nikiamini kuwa ukosefu wa uzoefu wa muda mrefu wa waamuzi wetu umekuwa ukichangia makosa ambayo wazoefu wangeyashughulikia bila lawama nyingi. Lakini nimeanza kuwa na wasiwasi dhidi ya mwendelezo wa makosa hayo kiasi kwamba sasa nahisi huenda ni ya kimfumo, kama yataangaliwa vizuri.
Wanaofanya makosa hayo ni walewale ambao wanafungiwa, na mara wanapomaliza adhabu hupewa tena michezo mikubwa, tena baadhi ya timu ambazo zilisababisha wafungiwe na wanaporudi wanafanya makosa mengine yanayozinufaisha timu zilezile. Hilo linawezekanaje kama si matatizo ya kimfumo, au kimtandao?
Na unapoona baadhi ya viongozi wanatetea makosa hayo wakati timu zao ndiyo zilinufaika na uozo huo, unapata hisia zaidi kwamba huenda ni mambo ya kutengenezwa ndiyo maana kwao si tatizo la kimpira, bali la klabu chache zilizoathirika.
SOMA ZAIDI: CAF Imetuonyesha Uamuzi Wetu ni Janga
Ni mambo ya hovyo sana kuona tuna viongozi na watendaji wa klabu wa aina hii. Nilitegemea viongozi wote wa klabu wakemee uamuzi mbovu ili bingwa apatikane anayestahili, lakini inavyoonekana si wote wanaoona kwamba kuna tatizo kubwa la kimpira, bali wale ambao timu zao zimeathirika tu. Hapa huwezi kuzungumzia maendeleo ya mpira, bali ujingaujinga tu.
Na kwa kuwa tunatumia falsafa ya kwamba “kosa moja huhalalisha kosa jingine,” basi kuna uwezekano mkubwa wa hawa waamuzi kutumika kutengenezea makosa yatakayozinufaisha kwa kiasi kidogo timu zinazolalamika, ili ionekane matatizo yako pande zote na hiyo wao kuendelea kunufaika zaidi.
Misimu miwili iliyopita, mabao ya Yanga na Simba dhidi ya timu nyingine yalikataliwa ndani ya muda wa siku saba. Lilikataliwa kwanza bao la Simba wakati mshika kibendera alipoashiria kuwa mpira wa kona ulitoka nje kabla ya kumfikia mfungaji wa Simba.
Siku chache baadaye bao la Yanga likakataliwa kwa hoja hizo hizo. Huoni hapo kosa moja lilitengenezwa kuhalalisha jingine?
Angalia mabao ya kuotea ya msimu huu. Ni kama yanatengenezwa kuhalalisha makosa mengine yaliyotokea au kutengeneza mazingira ya kuhalalisha makosa mengine kwa timu inayokusudiwa. Inawezekanaje? Ona malalamiko ya Azam FC na Singida Fountain Gate kama yanatofautiana.
SOMA ZAIDI: Simba, Yanga Hazina Haja Tena ya Kuhofia Yeyote Ligi ya Mabingwa
Angalia rafu zinazohitaji adhabu moja zinavyoadhibiwa kwa adhabu tofauti. Inawezekanaje mchezo hatarishi ukaadhibiwa kwa kadi ya njano kwa upande mmoja na kadi nyekundu kwa upande mwingine?
Kazi yetu ni kufurahia kuwa hata wanaolalamika nao walinufaika na makosa ya waamuzi. Kwa hiyo yaendelee?
TFF haikereki
Kibaya zaidi, hata Shirikisho la Soka (TFF) halionekani kukerwa na ongezeko la makosa ya waamuzi kwa kutoa karipio kali na kuahidi kuchukua hatua kali zaidi. Badala yake, linaingia kwenye falsafa ileile ya “kosa moja huhalalisha kosa jingine.”
Nilimsikia kiongozi wa juu wa TFF akisema eti, “Makosa ya waamuzi ni mengi lakini yakiwagusa wao ndiyo wanalalamika sana.” Hiki kitu kinatia kichefuchefu!
Yaani hata wenye mamlaka hawakerwi bali wanaona kwamba eti klabu fulani zimezoea kulalamika wakati makosa ya waamuzi yako pande zote! Ajabu sana!
Kwa kiongozi mwenye weledi anayekerwa na uamuzi mbovu au tuhuma za upangaji matokeo, ongezeko hili la makosa katika raundi tano tu za mwanzo angeshachukua hatua kwa sababu huenda ndani yake kweli kuna upangaji wa matokeo, kuna rushwa kwa waamuzi, kuna mtandao mkubwa wa kamari ambayo ni sumu kwenye michezo.
SOMA ZAIDI: Huu ni Wakati Muafaka Kuanzisha Wakala wa Viwanja Vya Michezo
Hatujui ni kwa kiwango gani ligi yetu, ambayo sasa ni ya tano kwa ubora Afrika, imeingizwa katika mikeka ya michezo ya kubashiri ndani ya Afrika na nje.
Wakati fulani nikiwa kwenye ziara ya kikazi nchini Ujerumani, mmoja wa watu aliokuwa katika safari hiyo ni mwandishi kutoka Singapore. Alikuwa akinieleza jinsi kamari inavyoathiri mpira. Nilishangaa kwamba hata Singapore ambako soka si maarufu sana, nako watu wanabashiri.
Akaniambia kuwa si mechi za Singapore peke yake, akiongea “Hata za kwenu.” Kumbe raia wa Singapore wanabashiri mechi za Tanzania?
Na mara nyingi, hawa wacheza kamari hutumia waamuzi kufanikisha mambo yao, kama ilivyokuwa kwa Robert Hoyzer, yule mwamuzi wa daraja la pili nchini Ujerumani aliyekiri kushiriki kupanga matokeo mwaka 2005, ikiwemo mechi iliyohusisha klabu ya Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga), Hamburger SV na klabu ya SC Paderborn iliyoshinda kwa mabao 4-2, huku timu hiyo ndogo ikipata penati mbili za mashaka.
Uzoefu kwengineko
Baada ya kashfa hiyo, ndipo kamati ya udhibiti ya Shirikisho la Soka Ujerumani (DFB) ilipoibuka na maazimio kadhaa kupunguza makosa ya waamuzi na upangaji wa matokeo.
SOMA ZAIDI: Kocha Singida Amedokeza Tatizo Kubwa la Soka Letu
Iliazimia kuwa hakutakuwa na mwamuzi atakayepandishwa kwenda kuchezesha mechi za ligi daraja la pili kutoka ligi za mikoa, ni lazima aangaliwe kwa kipindi cha miaka mitatu. Waamuzi wetu hata hawajachezesha mechi za madaraja ya chini kwa miaka miwili. Unastukia anapuliza filimbi Ligi Kuu!
Pia, DFB iliamua waamuzi wote watakaohusika kwenye tatizo ambalo limeonekana, watasimamishwa mara moja chini ya utaratibu maalum hadi tatizo hilo litakapopatiwa ufumbuzi, yaani kosa kudhihirika au kutodhihirika.
Pia, iliamua kutumia zaidi marudio ya video ya matukio ya uwanjani ili kubaini makosa. Ingawa hapo kunahitajika maendeleo zaidi ya kiteknolojia, ukitilia maanani kwamba kamera zinazotumiwa viwanjani ni chache sana.
Hata ule utamaduni wa Chama cha Soka Ulaya (UEFA) wa kuteua waamuzi siku mbili kabla ya mechi ulionekana haufai na kutafutwa mwingine.
Hizi ni hatua chache kati ya nyingi zilizochukuliwa na DFB kudhibiti makosa ya waamuzi. Hapa kwetu ni adhabu tu. Hakuna mkakati wowote unaowekwa kudhibiti uamuzi mbovu au kuwapiga msasa waliopo ili kuongeza ubora wao, zaidi ya zile programU za FIFA.
Ni muhimu sana TFF ikaona tatizo la waamuzi kuwa ni la mpira wa miguu na si la klabu chache zinazolalamika. Sumu ya mpira wa miguu ni uamuzi mbovu na upangaji wa matokeo. Hayo yasipoangaliwa, yataunda mtandao mkubwa ambao utavuruga kabisa soka letu!
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.