The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Wanawake Zanzibar Wataka Uwakilishi Baraza la Maulamaa: ‘Hatuko Huru Kueleza Shida Zetu kwa Wanaume’

Wanawake wanalalamika kushindwa kueleza masaibu yao mbele ya waamuzi wanaume, wakitaka uwepo wa wanawake kulinda haki zao.

subscribe to our newsletter!

Zanzibar. Hamida* hakuwa mwanamke wa kwanza kushindwa kutoa utetezi wake mbele ya jopo la maulamaa alikokwenda kwa ajili ya kumshinikiza mume wake ampatie talaka baada ya kulalamika kutelekezwa, akilazimika kulea watoto watatu peke yake bila ya msaada wowote kutoka kwa mzazi mwenzake huyo.

Hamida, mfanyabiashara ya uji huko Fuoni, nje kidogo ya mji wa Zanzibar, ameishi kwa muda wa miaka mitatu sasa katika hali hiyo ya kutojijua kama ni mke wa mtu au la, na alikwenda mbele ya maulamaa hao akiwa na nia ya kuifikisha mwisho hali hiyo. Lakini kulikuwa na tatizo kidogo.

“Tulipoitwa, waliokuwepo kusikiza shauri wote [walikuwa] ni wanaume,” alikumbuka Hamida wakati akizungumza na The Chanzo. “Walikuwa viongozi watatu pale Ofisi ya Kadhi na aliyekuwa mume wangu. Sasa sikuweza hata kuzungumza, maana wote ni wanaume. Basi wakasema turudi pale siku nyingine nikiwa tayari kuzungumza.”

Ulamaa ni mwanachuoni wa elimu ya dini ya Kiislamu ambaye ameaminiwa kutoa fatwa, au uamuzi, kuhusu masuala mbalimbali kwa mtazamo wa dini ya Kiislamu, kama vile ndoa, mirathi, na kadhalika. Visiwani Zanzibar, Baraza la Maulamaa, lililochini ya Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar, na Ofisi ya Kadhi, ndizo zilizokabidhiwa jukumu la kutoa fatwa kwenye masuala yanayohusiana na Uislamu.

Lakini wadau wamekuwa wakizikosoa vikali taasisi hizo kwa kukosa uwakilishi wa wanawake, hali inayolalamikiwa na wanawake wengi kuwakosesha haki zao, hususan zile zinazohusiana na masuala ya ndoa, ambapo wanawake hao hujikuta wazito kueleza masaibu yao mbele ya jopo la wanaume watupu.

Zanzibar inatajwa kuwa na kesi nyingi zinazohusisha ukatili katika ndoa, hali inayowasukuma wanawake wengi kutamani kutengana na waume zao. Lakini imekuwa ngumu kwa wanawake visiwani humo, ambako suala la ndoa linaendeshwa kwa mujibu wa dini ya Kiislamu, kufanikisha azma yao hiyo kwani mamlaka wanazopaswa kupata msaada huo hazina uwakilishi wa wanawake.

SOMA ZAIDI: Ukatili Kwenye Ndoa Watajwa Kuchochea Talaka Zanzibar

Wanawake na wanaharakati mbalimbali waliozungumza na The Chanzo walieleza kwamba kukosekana kwa wanawake kwenye Baraza la Maulamaa, chombo kikuu kinachoweza kuvunja ndoa fulani, kwa mfano, kunawafanya wanawake wengi wasijiamini kwenye kujieleza, hali inayowafanya washindwe kupata haki zao.

Naonekana nina hasira

“Toka mwaka 2020 sikwenda tena maana kwanza walikuwa wananitizama tofauti na walivyokuwa wanamtizama mume wangu,” Hamida anaeleza. “Nilijiona kama siko sehemu sahihi pale. [Sasa hivi] nimekaa tu hapa, sina talaka na hayo matunzo [mume] anatoa siku akitaka, lakini kule sikurudi tena.”

Mariam* ni mwanamke mwingine ambaye aliwahi kutafuta msaada wa Baraza la Maulamaa kuvunja ndoa yake na mume wake ambaye anadai kumpiga na kumnyanyasa, lakini kukosekana kwa wawakilishi wanawake kwenye chombo hicho kilimpelekea kushindwa kufanikisha azma yake hiyo.

“Tulipofika humo ndani ni masheikh wawili [wa kiume] na huyo bwana [mume wangu], basi tumekaa, naambiwa, enhe, eleza haswa shida ni nini? Hata sijaanza kusema, mume wangu akaanza kuniambia haya sema maana huna haya,” Mariam, ambaye ni mwalimu kitaaluma, anasimulia. “Niliona aibua na kushindwa kujua hata naanzaje kueleza.”

“Roho yangu haina imani kwamba nitaweza kusaidiwa,” Mariam, mama wa watoto wawili, aliongeza. “Maana wanaume wenzake nahisi kama watamtetea, lakini pia inaonekana kama mimi nina hasira tu.”

SOMA ZAIDI: Dhuluma Baada ya Kuachika Inavyowasukuma Wanawake Zanzibar Kutaka Kumiliki Ardhi Kisheria

Watetezi wa haki za wanawake visiwani humu wanaamini kwamba kunahitajika kufanyika kwa marekebisho ya kisheria ili kuwezesha uwakilishi wa wanawake kwenye Baraza la Maulamaa, huku Jamila Mahmoud, Mkurugenzi wa Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), akisema kwa sasa sheria haziko wazi kuhusiana na takwa hilo.

Mahmoud, ambaye shirika lake liko mstari wa mbele kupigania ukombozi wa mwanamke visiwani humu, anataja Sheria ya Mahakama ya Kadhi ya mwaka 2003 na Sheria ya Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar ya mwaka 2021 ambazo amezitaka zifanyiwe marekebisho kuweka ulazima wa uwakilishi wa wanawake kwenye Mahakama ya Kadhi na Baraza la Maulamaa.

Takwa la kijinsia

“Ukitizama [Sheria ya Mahakama ya Kadhi] unaona inatizama madhehebu ya mtu kwenye kupata haki [ya kuteuliwa kuwa hakimu],” anasema Mahmoud. “Sasa, ikiwa sheria imeangalia suala la madhehebu, lakini haijagusia kabisa suala la jinsia, hapa ni mtihani, na usawa wa maamuzi ni mtihani kupatikana.”

Mahmoud amesema kwenye Sheria ya Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar, takwa la mtu kuteuliwa kuwa ulamaa ni mtu awe mwanachuoni wa Kiislamu, mwenye elimu ya kutosha ya fani mbalimbali ya dini ya Kiislamu na lugha ya Kiarabu, kukiwa hakuna takwa la kijinsia.

“Sheria zinapaswa kufanyiwa marekebisho ili zitamke kwamba kutakuwa na idadi hii ya mahakimu [wa Mahakama ya Kadhi] na maulamaa [kwenye Barazala la Maulamaa], na kati ya idadi hiyo, idadi fulani itakuwa ni wanawake na idadi fulani itakuwa ni wanaume,” Mahmoud anachambua. “Vinginevyo, hakutakuwa na uwakilishi kwenye vyombo hivi.”

SOMA ZAIDI: ‘Siyo Uhuni’: Wanawake Jasiri wa Kizanzibar Walioingia Kwenye Sekta ya Uongozaji Watalii

The Chanzo ilimuuliza Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar, Haroun Ali Suleiman, endapo kama Serikali ina mpango wowote wa kufanyia kazi malalamiko na mapendekezo haya ya wanawake na wanaharakati ambapo Katibu wake alituelekeza tuzungumze na Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar.

Othman Mohammed ni Mkurugenzi wa Idara ya Mipango na Rasilimali Watu kutoka Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar ambaye aliiambia The Chanzo kwamba sababu kubwa kwa nini Baraza la Maulamaa halina uwakilishi wa wanawake ni kwa sababu “kuna kazi nyingine mwanamke hapaswi kuzifanya.”

“Ikiwa kuna kesi, au lalamiko, kwenye ofisi hii na linamuhusu mwanamke, basi kwa sasa kuna wanawake ambao wanafanya hiyo kazi na wanawasaidia,” alisema Mohammed. “Pia, hao wanawake ambao ni maulamaa tunakuwa nao pamoja na tunashirikiana pale mchango wao unapohitajika kwenye masuala ya kijamii.”

Ulamaa mwanamke?

Swali kama je, mwanamke anaweza kuwa ulamaa au la limekuwa likijadiliwa kwa hisia tofauti mbalimbali visiwani humu, huku makundi mbalimbali yakitumia Kurani na maandiko mengine mbalimbali ya dini ya Kiislamu kutetea na kupinga uamuzi huo.

Novemba 27, 2019, kwa mfano, mjadala mkali uliibuka wakati wa kujadili Mswada wa Marekebisho wa Sheria ya Kuanzishwa kwa Afisi ya Mufti Na. 9 ya Mwaka 2001 ndani ya Baraza la Wawakilishi, chombo kikuu cha utungaji sheria visiwani humu, kuhusiana na swali hilo, huku kikao kikimalizika kwa Serikali kuahidi kuhakikisha uwakilishi wa wanawake kwenye Baraza la Maulamaa.

SOMA ZAIDI: Shauku ya Kujitegemea Yawasukuma Wanawake wa Kizanzibari Masokoni

Lakini miaka takribani mitano baadaye, uwakilishi wa wanawake kwenye chombo hicho nyeti unakosekana, huku Serikali ikishindwa kutoa majibu ya dhati kwa nini imeenda kinyume na ahadi yake. 

Rashid Makame Shamsi alikuwa Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni (Chama cha Mapinduzi – CCM) ambaye alitetea kuwepo kwa uwakilishi wa wanawake kwenye Baraza la Maulamaa kwenye kikao kile cha Baraza la Wawakilishi kuhusu suala hilo, akisema “hakuna madhara” kwa wanawake kuwa maulamaa.

The Chanzo imemuuliza Shamsi, ambaye sasa siyo Mwakilishi tena, kwa nini anadhani imekuwa ngumu sana kwa Serikali kurekebisha sheria na kuruhusu uwakilishi wa wanawake kwenye Baraza la Maulamaa ambapo alisema ni watu kushindwa kuwa na uelewa mpana wa mambo.

“Hii inatokana na watu wenye mawazo mgando wanaofanya mambo kwa mazoea [na] hawataki kubadilika, na hawana hoja za msingi kwenye hilo,” Shamsi anasema. “Wito wangu kwa Serikali na watendaji wake katika Ofisi ya Mufti wabadilike na waone kuwa wanawake wanapata nafasi ya kushirikishwa kwenye vyombo vya ushauri, maamuzi na fatwa.”

Mfumo dume

Mahmoud kutoka ZAFELA anaamini kwamba mabadiliko yamechelewa kutokea kwa sababu jamii bado imeshikilia mawazo ya kale, yaliyojengeka kwenye mfumo dume, ambao bado haumuangalii mwanamke kama wakala wa mabadiliko, bali kama kiumbe dhaifu anayepaswa kufanyiwa mambo.

SOMA ZAIDI: Uhodari wa Mwanamke ni Zaidi ya Siku ya Wanawake Duniani

“Sheria ina mapungufu yake, kwamba haijaweka takwa la kijinsia, lakini wanaofanya maamuzi nao wanakubaliana na masuala haya,” alisema mwanaharakati huyo. “Huo ndiyo ukweli, na hivyo ni wakati wa kubadilika na kuona hawa wanawake wasomi wanapewa nafasi kwenye sehemu za maamuzi.”

Dk Mzuri Issa ni Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Zanzibar (TAMWA-Z), ambacho kimekuwa mstari wa mbele kupigania usawa wa kijinsia visiwani humu, amesema kwamba hali ni lazima ibadilike kuhakikisha wanawake wengi zaidi wanapata haki zao.

“Ni ukweli usiofichika kwamba wanawake wanakuwa huru kuzungumza na wanawake wenzao kuliko wanaume, hususani kwenye matatizo kama hayo ambayo yanayowakumba zaidi wanawake,” alisema Dk Issa. “Ikiwa wanawake wanakosekana kwenye vyombo vya maamuzi, basi hapo hakuna utekelezaji wa haki wala usawa, na inawavunja moyo wanawake.”

Amina Salum Khalfan, mwanaharakati wa haki za wanawake na msomi wa dini ya Kiislamu, amekuwa mstari wa mbele katika kuihamasisha jamii kubadili mtazamo kuhusu ushiriki wa wanawake kwenye uongozi, akisema hakuna sehemu kwenye Uislamu mwanamke amekatazwa kuwa kiongozi.

“Kuna madhara makubwa endapo kama wanawake hawatapata nafasi kwenye sehemu [za maamuzi] maana dini haijasema wanawake wasiwe viongozi,” anasema Khalfan. “Waliowengi wameshikilia dini na kukosa maarifa ya hiyo dini, lakini zaidi ni mitazamo yao binafsi [kutokuwa na viongozi wanawake]. Uislamu hausemi hivyo.”

*Siyo jina lake halisi.

Najjat Omar ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Zanzibar. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni najjatomar@gmail.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *